KUTOKANA na hali ngumu ya uchumi katika miaka ya mwanzo ya 1980s ambapo bidhaa zote muhimu zilidimika na kusababisha watu wale unga wa njano na mchele mdundiko uliopatikana kwa foleni ndefu katika maduka ya kaya, watu walikuwa wakiuliza maswali mbali mbali yaliyokuwa dhidi ya serikali iliyokuwa madarakani.
Pamoja na hali ile ngumu ya uchumi iliyowapelekea Wananchi kuvaa nguo zenye viraka juu ya viraka, kuvaa viatu vya matairi ya gari maarufu "makatambuka", kufua nguo kwa sabuni zisizotoa povu au kwa maji matupu, sanda kwa kibali, uji wa chumvi au sukari guru iliyopatikana kwa magendo, kupitia milango ya uwani majumbani kununua vibaba vya sukari, unga wa ata badala ya ngano tena kwa bei ya kuruka wakati huo huo serikali ikiwasaka kwa nguvu zote "walanguzi" hao, hali ilikuwa shwari. Hapakuwahi kutokea ghasia.
Licha ya kuishi katika hali ya kuchoma vifuu na majani kama dawa ya mbu, kusafiri kwa malori, kukata tiketi za mabasi kwa kubuku, kutiwa mbaroni kwa kukutwa na Colgate au sabuni ya Lux, hapakuwepo na upinzani wowote dhidi ya serikali ukiondoa jaribio la Komandoo Tamim na wenzake mwaka 1982-1983.
Tofauti na nchi nyingine ambako bidhaa fulani inapopanda bei tu sio kuadimika watu huingia mitaani kuandamana, wananchi wa Tanzania waliendelea kujitokeza kwa wingi mabarabarani kuwalaki kwa shangwe watawala.
Badala ya kumzomea na kumpiga mawe, walimlaki kwa nyimbo na kofi. Kana kwamba hilo halikutosha, wananchi wakiitikia kwa nguvu pale iliposemwa "zidumu fikra za Mwenyekiti wa chama".
Hata hivyo mgeni asingeweza kujua siri ya hali ile ya mambo. Hakuuona mkono wa chuma ulivyokuwa ukifanyakazi.
Kwa sura ya kimataifa watawala walijitahidi kuonekana kama watu wenye huruma na ubinadamu kwa wenzao waliobanwa na makucha ya makuburu, kumbe kwa sura ya ndani nao walijenga mazingira kama hayo.
Utawala ulikuwa mbogo, hakuna aliyekohoa kuanzia mwananchi wa kawaida, afisa na hata kwa wale waliotumiwa kuendesha mkono huo wa chuma. Naambiwa bwana mkubwa mmoja alipomkosea mtawala alilazimika kutembea kwa magoti kuomba radhi!
Vyombo vya usalama vilikuwa makini kufuatilia hata minong'ono ya watu kila sehemu. Ungesemea wapi usisikike wakati ilivyokuwa katika kila watu watatu mmoja alikuwa "mwanahabari".
Kwa hali hiyo watu hawakuaminiana. Kila mmoja alikuwa akimuhofia mwenziwe. Na ilivyojengwa tangu nyuma, mtawala yule hakuwa na sifa ya kukosea, hivyo kila aliyethubutu kulaumu aliitwa lipyoto na akatafutiwa namna ya kudhibitiwa!
Nani angeweza kutoa fikra ya kimapinduzi katika mazingira hayo? Waliojaribu kufanya hivyo yaliwafika. Mzee Kasanga Tumbo alifungiwa kijijini kwao, akawa mchunga ng'ombe baada ya kuhoji "tumepigania nini kutoka kwa wakoloni na tulikuwa tunajenga nini"!
Mazungumzo yoyote dhidi ya serikali yalihesabiwa moja kwa moja kama ni uhaini kwani ungewezaje kuondoa serikali chini ya mfumo wa chama kimoja zaidi ya kupindua? Hata watu wawili walipokaa faragha kujadili jambo kwa muda, watu "wasiowafahamu" walianza kupita pita nyuma yao au kujifanya kusimama ghafla jirani nao wakijipapasa kuonesha wamesahau kitu fulani kumbe ni jitihada ya kutaka kusikiliza kinachoongelewa na watu hao mahali hapo.
Mzee mmoja, alipata kulazimika kuondoka nyumbani haraka baada ya bwana mmoja kusimama muda mrefu mkabala na nyumba yake.
Akihadithia tukio hilo huku akicheka alisema mtu mmoja mtanashati ambaye hakuwa akimfahamu alikuwa amesimama muda mrefu jirani na nyumba yake, hali hiyo haikuwa ya kawaida kwake akalazimika "kutoka kidogo", maana nchi hii inakuchimbana kweli!
Kwa ujumla ukachero na ushushu ulivunja kabisa mshikamano miongoni mwa wananchi, watawala wakafanya kila walilolitaka pasipo kuhofia nguvu ya watawaliwa.
Hata katika huo ulioitwa uchaguzi, mwananchi asingeweza kufanya chochote zaidi ya vile walivyovitaka watawala. Licha ya kufeli vibaya kwa serikali , bado mtawala aliweza kuibuka "mshindi" katika "chaguzi zote".
Angeshindwaje uchaguzi wakati mpinzani wake alikuwa kivuli. Na yeye na kivuli wote walitoka chama kimoja. Utake ndio huyo huyo, usitake ndio huyo. Kichwa chama hicho hicho, kivuli chama hicho hicho!
Mbali ya kuwa wagombea wote ni wa chama hicho hicho pia wasimamaizi wa kura na watangazaji wa matokeo ni wa chama hicho. Ulikuwa ni usultani wa kisiasa.
Hapakuwa na namna ya kumuondoa mtu madarakani kwa kura. Ndio maana ilifika mahali wananchi wengine hawakuona umuhimu wa kupiga kura. Ndio sababu leo hii inabidi ipigiwe mbiu kuwataka wananchi kujiandikisha kupiga kura.
Sasa Watanzania mnayo sababu ya kupiga kura. Wakati
ule wa mtu kushindana na kivuli hamkuwa na la kufanya lakini sasa ni mtu
dhidi ya mtu, mshindwe wenyewe iwapo hamtajiandikisha kupiga kura na kuwa
imara kusimamia kura zenu mpaka matokeo.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |