Baiskeli tegemeo la usafiri na uchukuzi Tanga

KUTOKANA na kupanda kwa gharama za usafirishaji na uchukuzi hasa kwa upande wa magari, baiskeli zimekuwa tegemeo kubwa la usafiri na uchukuzi kwa upande wa vijijini na hata mijini katika mkoa wa Tanga.

Hali ya kutegemea zaidi baiskeli kwa usafiri na uchukuzi imesababisha mji wa Tanga kuwa na baiskeli nyingi ukilinganisha na baadhi ya miji mingine.

Hata baada ya kuanzishwa kwa usafiri wa daladala na huduma ya uchukuzi wa mikokoteni, baiskeli bado zimekuwa na umuhimu wake kwa wakazi wa Tanga.

Hii imesababisha mji huo kuwa na maduka mengi ya kuuza baiskeli na spea za baiskeli na pia kuwa na gereji nyingi za mafundi wa baiskeli katika maeneo ya mijini na vijijini.

Kwa vile si kila mtu mwenye uwezo wa kumiliki baiskeli kuna vituo mbalimbali vinavyotoa huduma ya ukodishaji baiskeli.

Kwa upande wa uchukuzi, uchunguzi wa makala haya umebaini kuwa baiskeli ndizo zinazotegemewa kwa wingi na wakulima wadogo wadogo kuleta mazao yao mjini.

Baiskeli zinazotumika katika uchukuzi hufungwa tenga kubwa katika kiti cha nyuma ambalo hupakiwa mazao.

Nyakati za asubuhi kunakuwa na misafara mingi ya baiskeli zinazotokea vijijini zikiwa zimefungwa matenga yaliyobeba mazao mbalimbali kama vile nazi, mihogo na aina mbalimbali za matunda.

Wakulima hao hulazimika kusafiri kilometa nyingi kwenda na kurudi kwa kutumia baiskeli zao ili kuleta mazao yao kwenye masoko.

Mkulima mmoja Mashaka Maziku ambaye husafirisha mihogo kwa kutumia baiskeli kutoka kijiji cha Kirare kilichoko karibu kilometa 25 kutoka Tanga mjini alimueleza mwandishi wa makala haya kuwa hulazimika kutumia baiskeli kuleta mazao yake mjini ili kukwepa gharama kubwa za usafiri wa magari.

Anasema, huondoka kijijini kwake mapema asubuhi na kufika mjini saa mbili asubuhi ambapo baada ya kuuza mazao yake na kupata mahitaji mengine hugeuza na kurudi tena kijijini.

Anasema, matatizo yanayowakuta katika usafirishaji wa bidhaa kwa kutumia baiskeli, anasema, tatizo ni baiskeli kuharibika njiani huku wakiwa na mazao yanayotakiwa kuwahishwa kwenye soko.

Anasema, katika kukabiliana na tatizo hilo wakulima hao wanakuwa na vifaa kamili vya kutengeneza baiskeli zao zinapoharibika.

Kwa upande wa uchukuzi wa mjini siku hizi kuna wachukuzi wanaotumia baiskeli kubeba mizigo na kuifikisha inakotakiwa.

Katika maduka ya jumla jumla ya mjini hapa hutakosa kukuta wachukuzi wanaotumia baiskeli. Mfanyabiashara ya reja reja anapokwenda kununua bidhaa wachukuzi hao humbebea kwa kutumia baiskeli zao hadi katika mtaa lilipo duka lake.

Bidhaa hizo hubebwa kwa staili ya aina yake. Baiskeli moja huweza kubebeshwa mifuko hadi minne ya sukari ya kilo hamsini hamsini ambayo hufungwa kiufundi katika kiti kikubwa kilichopo nyuma ya baiskeli zao.

Wafanyabiashara wengi wadogo wadogo hupendelea kutumia uchukuzi wa baiskeli kwa vile ni rahisi kwao kuliko ule wa mikokoteni unaotumiwa katika baadhi ya maduka.

Hii ni kwa sababu mtu anayenunua mifuko minne ya sukari ni ghali kwake kukodi mkokoteni ambao huhitaji kuchukua mifuko kama hiyo zaidi ya kumi kwa safari moja.

Kwa upande wa usafiri wa kawaida baiskeli zimekuwa zikitumika kwa safari ndefu na fupi.

Kwa wale watu wasiomiliki baiskeli zao wenyewe hukodisha kwa wakodishaji waliotapakaa katika kila kona ya mji na kutumia baiskeli hizo kufanya safari zao mbalimbali.

Matumizi ya baiskeli yamekuwa yakipendelewa zaidi kwa vile yana gharama nafuu kuliko usafiri wa magari kama vile teksi au kupanda daladala.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook