KATIKA makala yangu iliyoishilia wiki zilizopita kuhusu usahihi wa maneno ya Kiswahili nilitoa ufafanuzi juu ya baadhi ya maneno yenye utatanishi katika Kiswahili.
Katika makala ya leo nitaeleza makosa yanayojitokeza katika matamshi ya herufi na silabi katika maneno.
Baadhi ya watu wanaozungumza Kiswahili hufanya makosa ya kubadili matamshi sahihi ya herufi na silabi wakati wanapotamka neno na badala yake kutumia matamshi yasiyo sahihi.
Makosa hayo si tu hufanya neno linalotamkwa kutokuwa sahihi bali pia hupoteza maana ya neno lenyewe.
Matamsihi ambayo yamekuwa yakipotoshwa ni ya herufi za R na L. Tamshi la R hutumika mahali pa tamshi la L na wakati mwingine tamshi la L hutumiwa mahali pa tamshi la R.
Kwa mfano, mtu anatamka, Ledio badala ya Redio au Arama badala ya Alama.
Hapa utaona tamshi la herufi R limegeuzwa kuwa la herufi L na tamshi la herufi L hugeuzwa kuwa la hefufi R.
Kadhalika wapo watu ambao hubadili matamshi sahihi ya silabi katika neno na hivyo kulitamka neno hilo kwa makosa.
Silahi hizo ni za dha dhe dhi dho na dhu na nyingine ni za tha the thi tho na thu.
Mara kwa mara tamshi la silabi dha hutamkwa za na tamshi la silabi tha hutamkwa sa.
Kwa mfano neno dhara hutamkwa zara na pengne neno thamani hutakwa samani.
Kwa kweli inakera sana na pengine kupunguza utamu wa Kiswahili pale sikio linaposikia tamshi la herufi ya L likitumiwa badala ya R au tamshi la herufi R hutumiwa badala ya L na vivyo hivyo kwa tamshi la silabi za kutumika badala ya dha.
Japokuwa makosa hayo yamezoeleka na kuonekana ni ya kawaida miongoni mwa watumiaji Kiswahili lakini yanatia dosari kubwa katika ufasaha wa Kiswahili.
Lakini mbali ya kutia dosari pia wakati mwingine huathiri mawasiliano pale neno lililokosewa linapochukua maana nyingine. Kwa mfano unapotamka samani wakati unakusudia thamani au uzi kwa kusudio la udhi unaweza kumchanganya msikilizaji akakuelewa vingine kwani neno ulilotamka limeshachukua maana nyingine.
Huu ni mfano mmoja tu unaoonesha umuhimu wa matumizi ya Kiswahili sahihi katika mawasiliano.Kwa mfano huo utaona kuwa upotoshaji wa maneno unaweza kuharibu mawasiliano.
Baya zai ni kuwa tatizo hilo wanalo pia baadhi ya Wahariri wa magazeti na watangazaji wa redio, watu ambao wanatakiwa kuwa mfano wa watumiaji sahihi na fasaha.
Wakati fulani Mhariri mmoja alinisahihisha katika makala yangu moja nilipoandika neno bilauli naye akabadili na kuandika bilauri. Nilipomuuliza kwanini alibadili neno hilo alijibu kuwa bilauri ndiyo neno sahihi wakati ukweli ni kuwa bilauli ndiyo neno sahihi.
Baadhi ya wataalamu wa Kiswahili wanadai kuwa makosa ya aina hii katika Kiswahili yanatokana na ndimi za wahusika kuathiriwa na lugha nyingine walizozoea kutumia tangu utotoni. Hapa Tanzania tuna lugha mbalimbali za kikabila ambazo hutumika vijijini na hata mijini.
Katika kujenga ufasaha mzuri wa Kiswahili inashauriwa kwa watu mbalimbali kuwa na tabia ya kujisomea vitabu na majarida ya Kiswahili mara kwa mara na pia kupendelea kufanya maongezi na watu wanaozungumza Kiswahili fasaha.
Kama nilivyoelezea hapo juu kuwa makosa ya aina hii hutokana na ndimi za wahusika kuathiriwa na lugha nyingine walizozoea kuzungumza tangu utoto, huenda wakosaji hawakusudii wanapotamka kwa makosa na pengine hawatambui kuwa wanatamka kwa makosa. Hao hukielewa Kiswahili kama wanavyokitamka.
Wajibu wetu ni kuelimishana ili tufike mahali ambapo Kiswahili kama lugha ya Taifa letu kinapozungumzwa popote pale kivutie masikioni mwetu kwa usahihi wa maneno na ufasaha wa ulimi.
Kiswahili tukikuze, lugha ya taifa letu,
Tukipambe kipendeze, kiwe ni hazina yetu,
Fasaha kisipoteze, akilinde kila mtu,
Wakirithi na wenetu.
KATIKA ukurasa huu, nami pia nimeonelea nitoe mchango wangu mdogo juu ya matumzi ya baadhi ya maneno ambayo yamekuwa yakitumiwa kimakosa na wazungumzaji walio wengi.
Ni jambo la kawaida kusikia watu wakisema, "wale ni wake zake fulani, wake za Mtume (s.a.w.) ..., watoto zangu, ng'ombe zake au zangu na kadhalika".
Ikumbukwe kuwa neno zake/zangu/zetu halitumiki kwa viumbe halitumiki kwa viumbe hai wajongeao bali latumika kwa vitu. Ni sahihi kwa mfano kusema 'kalamu zangu', nyumba zake, funguo zake, saa zake na kadhalika, na katika matumizi ya neno 'zake' huwa kumetanguliwa na neno jingine 'hizi', maneno ambayo huleta usahihi wa kinachozungumzwa.
Angalia mifano michache ifuatayo: Hizi ni kalamu zangu, hizi ni nyumba zake, hizi ni saa zake na kadhalika.
Kwa mfano huu huu, ikiwa tutasema wake zake, watoto zake au ng'ombe zake, itabidi tuwe na sentensi hizi:
Hizi ni wake zake, hizi ni watoto zake, na hizi ni ng'ombe zake na kadhalika. Matumizi ambayo mbali na kuwa si sahihi, bali hata matamshi yake hayapendezi. Usahihi hapa ni kusema: wake wake, watoto wake, ng'ombe wake na hivyo kufanya litumike naneo "hawa" mwanzoni, badala ya lile "hizi". Mifano ifuatayo inafafanua:
Hawa ni wake wake, hawa ni watoto/wana wake, hawa ni ng'ombe wake, hawa ni ndugu wake na kadhalika.
Matumizi mengine ya Kiswahili yasiyo sahihi ni yale ya kumwambia mtu aliye ndani ya kitu chochote kuwa "atoke nje" kwa kumaanisha kuwa aliye ndani anatakiwa kuwa nje. Kusema hivi si sahihi kwa sababu "kutoka" ni k uondoka mtu mahali alipo. Unaposema kwa mfano, "Fatma ametoka Tabora", maana yake ni kuwa ameondoka Tabora na hayuko huko. Kwa hivyo kusema "toka nje" maana yake sahihi ni "ondoka nje". Kwa yule aliye ndani ya nyumba tayari amekwisha toka nje na ndio maana yumo ndani na hayupo nje. Kumbe basi huyu aliye ndani aambiwe "toka ndani" au "toka nje" ikiwa hatakiwi kuwa ndani.
Mwisho tungalie tena matumizi yafuatayo:
Ni sahihi kabisa kusema "huyu ni mwalimu wangu" kwa kule kukufundisha, pia "huyu ni daktari/mganga wangu" kwa kule kukutibu. Lakini watu wengi tumekuwa tukitumia neno "fundi wangu" vibaya. Ikiwa kusema kwamba mtu fulani ni mwalimu wako ni kwa sababu anakufunza basi tuelewe hivyo hivyo kuwa kusema fulani ni fundi wako maana yake anakutengeneza wewe mwenyewe.
Tukumbuke kuwa ufundi si huduma ya moja kwa moja kwa mtu kama ilivyo kwa ualimu na uganga hivyo badala ya kusema kwa mfano kuwa "Mohammed ni fundi wangu", isemwe kuwa "Mohammed ni fundi wa Runinga yangu, ni fundi wa redio zangu, ni fundi wa gari yangu na kadhalika".
Nategemea walio wataalamu zaidi wa lugha yetu watatusaidia zaidi.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |