KUFUNDISHA kunalenga ufikiwaji wa nyanja tatu za kitaaluma, katika kujenga au kubadili mwenendo wa mwanafunzi. Nyanja hizo ni utambuzi, stadi na mwelekeo.
Utambuzi hujumuisha maarifa, ufahamu, matumizi, uchambuzi, uundaji na tathmini katika upimaji wa mambo.
Kilicholengwa katika maarifa ni kuijenga taswira ya dhana, tukio au tendo liote mizizi kwenye sehemu inayohifadhi mambo iliyopo kwenye ubongo wa mwanadamu. Mwanafunzi anatakiwa aweze kukumbuka kile alichofundishwa na kutaja kwa kauli au maandishi. Vile vile mwanafunzi anatakiwa kubaini kile anachokijua pindi kinapokuwa katika mchanganuo.
Mathalan, utawala wa sheria ni kipengele kinachoonesha kuwepo kwa demokrasia. Hivyo mwalimu wa somo la Uraia anaweza kutumia mkanda wa mauaji ya Mwembechai ili kuwathibitishia wanafunzi kuwa katika Tanzania utawala wa sheria haupo, na hivyo hakuna demokrasia.
Mwanafunzi atakapokutana na swali linalomtaka ataje tukio la kuthibitisha kuwa Tanzania hakuna utawala wa sheria wala demokrasia, itamjia taswira inayoambatana na sauti ya askari anayesema "piga shaba!"
Kisha itafuata taswira ya mtu mwenye kofia nyeupe, kidevu na shati nyeupe ya mikono mirefu akipindua macho huku akisukuma miguu na mikono yake akiwa ameanguka baada ya kupigwa risasi. Ili kudhihirisha maarifa aliyoyapata mwanafunzi atataja tukio la Mwembechai kama ushahidi wa hoja yake.
Kipande cha pili, Utambuzi ni ufahamu. Hapa mwanafunzi anakusudiwa aweze kuyatumia maarifa katika kutafsiri, kusherehesha kwa muhtasari au kubashiri mustakabali kutokana na tukio au tendo.
Mathalan, mwanafunzi aliyeona mkanda unaoonesha mauaji ya Mwembechai anaweza akabashiri mustakabali wa Waislamu Tanzania. Kwamba endapo Waislamu wataendelea kuwaweka madarakani viongozi wa chama kisichojali haki za binadamu na utawala wa sheria, wataendelea kupigwa Misikitini, kukamatwa majumbani mwao na kufunguliwa kesi zisizo na ushahidi kwa lengo la kuwasotesha mahabusu.
Aidha, mwanafunzi anaweza kuonesha ufahamu wake wa somo la uraia kwa kutoa maelezo ya muhtasari ya tukio la Mwembechai kama kielelezo cha kutokuwepo kwa demokrasia ya kiutendaji.
Mbali ya ufahamu, katika nyanja ya utambuzi, kuna kipengele cha matumizi ya maarifa katika hali halisi. Mwenendo unaojengwa hapa ni ule uwezo wa mwanafunzi wa kutumia ujumbe, kanuni na fikra za maarifa ya ufahamu alionao katika mazingira halisi.
Kwa mfano, baada ya kujua umuhimu wa utawala wa sheria katika demokrasia, mwanafunzi aweze kutumia kura kutowapa madaraka viongozi wa chama waliokiuka katiba, na sheria na kuvunja haki za binadamu.
Sambamba na matumizi ya maarifa ya ufahamu, uchambuzi wa dhana, tukio au maarifa ni miongoni mwa kipengele muhimu cha kuonesha utambuzi. Moja kati ya malengo mahususi ya somo linapaswa kumuhamasisha na kumjenga mwanafunzi awe na uwezo wa kufanya uchambuzi wa mambo mbalimbali ya kimaisha.
Katika uchambuzi, ufundishaji ulenge kumuwezesha mwanafunzi kuchungua na kutaja uhusiano wa mambo. Hebu tutazame mfano ufuatao ili tuweze kuelewa vyema hiki kipengele cha uchambuzi.
Kuna kitabu kilichoandikwa na Dkt. John Sivalon jina la kitabu hicho ni "Kanisa Katoliki na Siasa Tanzania Bara". Mwanafunzi mchambuzi ataweza kuonesha uhusiano wa kipekee uliopo baina ya Kanisa na serikali kiasi cha kuathiri sera na utendaji wa viongozi.
Mauaji ya Mwembechai yalitanguliwa na kauli ya Paroko Lwambano iliyodai kuwa Yesu anatukanwa. Ikafuatia kauli ya kuomba radhi kutoka kwa Bwana Makamba na kuahidi atalishughulikia.
Yalipoahidiwa hayo, walikamatwa viongozi wa mihadhara ya Kiislamu akiwemo Bwana Magezi Shaaban. Haikutosha, askari walivamia Msikiti wa Mwembechai, wakavunja milango na kuingia na viatu kisha kupiga Waislamu. Kilele cha yote ni kule kuuawa Waislamu kwa kupigwa risasi.
Baada ya hapo viongozi wa chama na serikali wakapongeza kitendo hicho na kuwashambulia Waislamu kwa maneno ya shutuma. Naye Kadinali Pengo akahalalisha mauaji kwa kutoa kisa cha Daud na Goliath.
Kila kiongozi wa Waislamu aliyesimama kuihoji serikali kuhusu mauaji, alirundikwa mahabusu au kusakwa kama mhaini. Sheikh Ponda Issa Ponda alitafutwa kwa udi na uvumba. Simbaulanga, mhadhiri wa Kikristo alichiwa, lakini marehemu Sheikh Chata Abdallah Kidagaa akasota rumande na kufariki siku chache baada ya kutolewa.
Hata Waislamu walipomfikishia rasmi Mheshimiwa Rais Mkapa miongoni mwa madai kuwa mauaji ya Mwembechai yafanyiwe uchunguzi na ikibidi sheria iwakamate waliovunja sheria, malalamiko hayo yalipokewa na kutupiwa Waislamu baada ya kimya kirefu cha "Uchunguzi wa Kisayansi".
Kuna kitabu kilichochambua kisayansi namna Waislamu wanavyobaguliwa na kunyimwa haki zao za kiraia na uwananchi Tanzania. Kitabu hicho kiitwacho "Mwembechai Killings and the political future of Tanzania" kimetoa ushahidi wa kisayansi juu ya ukweli wa dhulma ya kuuawa Waislamu. Kitabu hicho kimepigwa marufuku kisiingizwe nchini.
Hivyo, katika utambuzi, ufundishaji ukusudie mwanafunzi aweze kuchambua mambo kama tukio la Mwembechai. Aweze kujiuliza ni kwanini madai ya Paroko yalitekelezwa bila ya uchunguzi wa kisayansi. Au inakuwaje serikali ikatae kuunda tume itakayotumia misingi ya kisayansi kuchunguza mauaji yale, badala yake inazuia uchunguzi wa kisayansi uliomo ndani ya "Mwembechai Killings and Political Future of Tanzania"?
Uundaji ni kipengele cha tano katika nyanja ya utambuzi. Hapa ufundishaji una shahaba ya kuichomoa akili ya mwanafunzi ifanye uvumbuzi au tafakari bunifu. Uundaji ni pamoja na kuandika jambo kwa namna ya kipekee, kugundua kanuni, kutengeneza mabunio mapya u kutoa jumuisho kama hitimisho la utafiti.
Serikali imetega sikio lake kuyakubali madai ya Kanisa hususan Kanisa Katoliki na kuyafanyia kazi bila ya kuyatazama kwa jicho la upembezi wa kisheria na kikatiba. Wakati huo huo sikio la serikali limeyapa ubatili madai yote ya Waislamu yanayoainishwa na katiba, yasiyo pingika katika mtazamo wa kisheria.
Ufundishaji uwe na shahaba kumfanya mwanafunzi agundue hali kama hii na kutoa maelezo ya mijumuisho yanayoonesha uzito wa hatari inayolinyatia taifa. Kisha apendekeze namna ya kuikoa jamii isifikwe kwenye janga la kumwaga damu za watu ionekane kuwa ni kawaida mithili ya kuchinja kuku.
Cha mwisho ni kipengele cha tathmini. Hiki kinakusanya yote. Yaani maarifa, ufahamu, matumizi, uchambuzi na uundaji. Kinachozidi hapa ni vile vigezo vinavyowekwa katika upimaji wa uhalali wa ubatili wa mambo. Kuangalia ukweli au uwongo wake, haki au dhulma na kushindwa ama kufanikiwa.
Taifa la Tanzania lina katiba na sheria ambavyo ndiyo vigezo vilivyowekwa kutoa hukumu ya uhalali au ubatili wa matendo ya maneno ya raia. Vigezo hivi pia vinauwekea mipaka utendaji wa serikali katika kurekebisha mwenendo batili wa wananchi. Kwamba rungu la dola litumike bila ya kukiuka haki ya mwananchi. Inapotokea viongozi kutumia nje ya mipaka, basi msumeno wa sheria urudishwe kinyumenyume uwakate hao wasaliti.
Hivyo, kwa kutumia vigezo vya sheria na katiba ya nchi, mwanafunzi aweze kutaja haki au dhulma ya polisi kumpiga risasi mwanafunzi Chuki Athumani. Aweze kubainisha ukweli au uwongo wa viongozi wa serikali wanaojinadi kuendesha nchi kwa kuzingatia sheria na katiba wakati Chuki Athumani anateseka kwenye kibaiskeli cha ulemavu bila wauaji waliompiga risasi kufikishwa mahakamani au kuacha huru kwa kusibu uchunguzi unaotakiwa kufanywa na Tume.
Kwa muhtasari, nyanja ya utambuzi inahusisha maarifa, ufahamu, matumizi, uchambuzi, uundaji na tathmini.
Nyanja ya pili inayokusudiwa kufikiwa katika ufundishaji ni ile ya mwelekeo. Ni hatua za mpandikizaji wa mambo ndani ya akili ya matendo ya mwanafunzi. Ni kummilikisha fikra, tabia, na vigezo vya kuthamini mambo.
Yaliyomo katika nyanja hii ni utayari wa kupokea, kushiriki, kuthamini, kujenga msimamo na kujizoesha. Hivi ni vipengele vinavyoyapa maana malengo ya ufundishaji yanayofikiwa katika nyanja ya utambuzi.
Utayari unaanzia pale mwanafunzi anapokuwa hadhiri juu ya jambo fulani. Kisha akaonesha nia ya kupokea kwa kujiweka sawa na kwa makini katika ufuatiliaji. Ni hatua ambayo mwanafunzi anakutana na fikra, dhana, au mazingira yaliyo kinyume cha alivyozoea.
Kwa mfano, Watanzania wengi hususan Waislamu walifanywa kuamini kuwa dini na siasa ni vitu visivyochanganywa pamoja. Dhana hii ilipandikizwa katika Tanganyika huru pale Waislamu walioasisi harakati za kuung'oa ukoloni walipotaka wapewe fursa za kielimu na uongozi walizonyimwa wakati wa ukoloni.
Kinyume cha matarajio ya kupata haki na usawa yaliyowasukuma kutoa nguvu, mali na muda wao, kuanzisha Chama cha TAA na baadaye TANU dhidi ya mkoloni. Waislamu hao walisambaratishwa kwa nguvu za dola na wengine kusota magerezani.
Kwa Makanisa, milango ya nchi ikapanuliwa kuruhusu ufanisi wa mawasiliano ya kiroho, uchumi na kisiasa. Wakati Kanisa Katoliki linasimika ubalozi wake toka Vatikani amao kwa mujibu wa kanuni yake ya Concordat linakuwa mshauri mkuu wa serikali, Jumuiya ya Waislamu ya Afrika Mashariki inapigwa marufuku.
Serikali ya Tanganyika huru haikuchukua jitihada za kuyawekea Makanisa kuwa na Baraza moja, lakini kimabavu Waislamu wakaundiwa BAKWATA kinyume cha matakwa na ridhaa zao.
Matukio haya na yale ya kuchomwa moto Qur'an, majaribio ya kutaka kuifanyia marekebisho Qur'an mwaka 1988, Waislamu kushambuliwa kwa mabomu Msikitini Morogoro na mengineo yakawafanya Waislamu kuwa hadhiri.
Waliposhtuka "bangi" la kutochanganya dini na siasa wanalazimishwa kulivuta ili haki na hadhi yao viendelee kuhodhiwa, mwaka 1991 Waislamu walikusanya nguvu zao ili kuisafisha BAKWATA inayodaiwa kuwa ni chombo chao. Serikali ikajitokeza kukinga kifua na baadaye kuikusanyia michango kutoka kwa Maaskofu chini ya usimamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani.
Kitabu cha "Kanisa Katoliki na Siasa Tanzania Bara" na kile cha "Development and Religion in Tanzania", tukio la mabucha ya nguruwe, mauaji ya Mwembechai na hatua ya serikali kuwapiga Waislamu walioandamana kupinga kauli za Wabunge waliopinga uvaaji wa hijabu mashuleni, vimewajenga Waislamu mwelekeo kwamba kutochanganya dini na siasa ni kukubali kudhulumiwa.
Kwa kifupi, nyanja ya mwelekeo hujihusisha na
utayari, ushiriki, kuthamini, msimamo, na mazoezi ya kitabia. Hujidhihirisha
pale mwanafunzi anapoonesha kuvutiwa, kupenda, kuchukia na kutangaza hoja
za msimamo wake kupitia mijadala, midahalo, tamthilia, vitabu na kadhalika.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |