Na Mohammed Said
JOTO la siasa lilikuwa katika kiwango kama hiki wakati wajumbe kumi na saba wa TAA kutoka kwenye matawi majimboni na makao makuu walipokutana mjini Dar es Salaam tarehe 7 Julai, 1954, kujadili katiba mpya ya chama kipya cha siasa - TANU(Tanganyika African National Union).
Jimbo la Mashariki ambalo lilikuwa na wajumbe wawili liliwakilishwa na ndugu wawili, Abulwahid na Ally Sykes, Dossa Aziz, Tewa Said Tewa, Patrick Kunambi, Kasella Bantu, John Rupia, Julius Nyerere na C. O. Milinga; Jimbo la Kaskazini liliwakilishwa na na Joseph Kimalando na Japhet Kirilo; Jimbo la Ziwa liliwakilishwa na Abubakar Kilanga, L. M. Makaranga.
Katika wanachama kumi na saba waasisi tisa kati yao walitoka makao makuu, watano kutoka Jimbo la Ziwa, mmoja kutoka Jimbo la Magharibi na wawili kutoka Jimbo la Kaskazini.
Uwakilishi huu wa wajumbe kutoka kwenye majimbo na makao makuu unatoa picha ya hali ya harakati za siasa nchini Tanganyika kabla ya kuundwa kwa TANU.
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa TAA ulikuwa na agenda ndefu. Katika siku ya kwanza mkutano ulichukua masaa matano na nusu. Siku hiyo ilitumiwa kuondoa matatizo yaliyokuwa yakikiathiri chama.
Agenda ya kwanza ya mkutano huo ilikuwa kuthibitisha kufukuzwa kazi kwa Alexander Tobias aliyekuwa katibu mtendaji tangu Juni, 1953. Tobias aliyekuwa katibu mtendaji tangu 1953, alipoteza majalada na nyaraka muhimu sana za chama zilizokuwa chini ya mamlaka yake kama katibu mtendaji.
Kulikuwa na tetesi kwamba majalada hayo aliyakabidhi kwa Special Branch baada ya kupewa fedha. Ilikuwa katika siku ya pili ndipo wajumbe walikaa chini kuanza kazi hasa ya kujadili ya kuigeuza TAA kutoka vile ilivyokuwa na kukifanya chama cha siasa - TANU bila ya kuficha madhumuni yake na kutangaza dhamiri ya chama ya kuwatayarisha Waafrika wa Tanganyika kujitawala.
Julius Kambarage Nyerere, mwanasiasa mgeni katika TAA pale makao makuu akiwa amejiunga n uongozi wa chama miezi kumi na tano tu iliyopita, alichaguliwa rais wa kwanza wa TANU na John Rupia makamo wa rais.
Agenda ya kwanza kujadiliwa chini ya TANU tarehe 9 Julai ilikuwa lile suala la uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria. Katika mwaka 1950 itakumbukwa kuwa TAA chini ya uongozi wa Abdulwahid na Dk. Kyaruzi iliwakilisha memorandum kwa Gavana Twining kueleza mapendekezo yake juu ya mabadiliko ya katiba.
Ilishauriwa kwamba ili kufikia kiwango fulani cha maendeleo ya siasa, ilikuwa lazima Waafrika wapitie utaratibu wa maendeleo hatua kwa hatua kwa kushiriki katika kuitawala nchi yao.
Moja ya mapendekezo ilikuwa Waafrika waruhusiwe kuchagua wawakilishi wao wenyewe katika Baraza la Kutunga Sheria. Ilikisiwa kwamba haya mabadiliko ya hatua kwa hatua yaruhusiwe kuendelea kwa kipindi cha miaka kumi na tatu baada ya hapo Waafrika waruhusiwe kuunda serikali yao wenyewe iliyo huru. Hii ilikuwa agenda muhimu sana na Abdulwahid na Rupia ambao walikuwa wajumbe wa kamati ndogo ya siasa ya TAA iliyorasimu mapendekezo hayo walieleza mkutano kwa ufupi juu ya upinzani wa serikali katika kukubali mapendekezo hayo.
Ilikubaliwa na wote kwa pamoja kuwa suala la kuanzisha kanuni za kidemokrasia katika uchaguzi wa wajumbe kwenye Baraza la Kutunga Sheria lilikuwa muhimu sana na watu lazima wafahamishwe juu ya haki hii.
Agenda ya mwisho kujadiliwa ilikuwa nafasi ya Malkia juu ya Waafrika wa Tanganyika na mgogoro wa ardhi ya Wameru.
Itakumbukwa kuwa mwaka 1951 Ally Sykes, akiwa katibu wa TAGSA, alitoa maneno makali dhidi ya serikali ya Uingereza kama mtawala wa Tanganyika. Ally Sykes aliiandikia barua serikali ya kikoloni na kuiomba ijitoe katika utawala wa Tanganyika.
Mkutano ulisisitiza kuwa Waafrika wa Tanganyika si raia wa Uingereza na kwa hiyo Malkia hana mamlaka juu yao. TANU ilieleza kuwa inamtambua Malkia kama kiongozi wa serikali ya kikoloni inayoongozwa na Gavana Edward Twining.
Kwa mantiki hiyo basi TANU ilidai bendera ya UNO ipandishwe sawasawa na bendera ya Uingereza ili kuonyesha kuwa mamlaka hizo zote mbili kwa pamoja ndizo zinazoitawala Tanganyika chini ya udhamini.
Serikali ya kikoloni haikutaka kukubali kuwa Tanganyika ilikuwa chini ya mamlaka mbili. Mwisho wa mkutano Japhet Kirilo alieleza kuhusu mgogoro wa ardhi kule Meru na TANU iliitaka serikali ya kikoloni ama irejeshe ardhi hiyo kwa wenyewe au ilipe fidia.
Kipindi cha mpito kutoka TAA kwenda TANU pale makao makuu kilikwenda vizuri sana. Hakukuwa na matatizo ya migongano kati ya viongozi wa makao makuu ukitoa kikundi kidogo cha Waislamu wenye msimamo mkali waliokuwa wakipanga kumg'oa Nyerere kutoka uongozi wa TANU kwa kuwa alikuwa Mkristo.
Hii ilikuwa ni mara ya pili kwa suala la dini kuzuka tangu Nyerere achukue uongozi wa chama kwa mara ya kwanza mwaka 1953. Mkutano uliitishwa kuweka hali sawa kuhusu Ukristo ndani ya chama. TANU iliamua kuwa chama kitakuwa ni cha kisekula ili kunusuru na kuihifadhi umoja wa kitaifa.
Mkutano huu ulifanywa ndani ya nyumba moja katika mtaa wa Pemba na uamuzi wake uliungwa mkono na Mufti Sheikh Hassan Bin Amir, Sheikh Nurdin Hussein toka Lindi na Sheikh Abdallah Chaurembo wa Dar es Salaam.
Mkutano huu ulimfananisha na Yuda mwanachama yeyote yule ndani ya TANU atakayembagua Mwafrika mwenzake kwa sababu ya imani yake. 99 Jina la hili 'Yuda' lilikuwa ndilo lile jina la Yuda Iscariot katika Biblia, mfuasi aliyemsaliti Yesu kwa vipande thelathini vya fedha.
Matatatizo ambayo TANU ilipambana nayo yalikuwa hasa toka serikali ya kikoloni na yale yaliyotokana na Waafrika wenzao vibaraka waliokuwa wakitumiwa na wakoloni kuvunja nguvu harakati za chama. TANU ilipambana na tatizo kama hilo huko Moshi.
Joseph Kimalando na Japhet Kirilo walikuwa wajumbe toka Jimbo la Kaskazini katika ule mkutano mkuu wa 1954 wa kuunda TANU. Kumbukumbu za wakoloni zinamuonyesha Kimalando kama mtu aliyejihusishana siasa za African Association alipokuwa akifanya kazi mjini Dar es Salaam katika miaka ya 1930.
Kimalando akiwa mzee mwanaharakati, aliheshimiwa sana na vijana waliokuwa makao makuu kama ilivyokuwa kwa John Rupia. Kimalando alikataa kusajili TANU. Kimalando alikuwa mwanasiasa mkongwe toka enzi ya African Association katika miaka ya 1930, akishiriki siasa za wakati ule huku akifanya kazi Tanganyika Railways.
Aliporudi Moshi sasa akiwa mtu mzima, aliajiriwa katika ofisi ya wakili mwenye asili ya Kiasia. Inawezekana kabisa fikra za umri wake mkubwa baada ya kustaafu na kazi yake hii mpya ilimuweka katika hali ambayo haikumwezesha yeye kuijenga TANU ili kudai uhuru wa Tanganyika.
Aliwaza hali yake ya baadae zaidi kuliko siasa. Kwa ajili hii Kimalando alishindwa kuisajili TANU Moshi kama chama cha siasa. Hii ilikuwa pigo kubwa kwa kuwa Kimalando alikuwa hodari wa kuandika Kiingereza na kwa wakati ule ilidhaniwa kuwa kujua lugha hiyo kwa fasaha ni muhimu katika kuendesha mambo ya siasa na serikali.
Wakati sehemu nyingine zikihamasika na harakati za kudai uhuru Moshi ilikuwa katika usingizi. Uongozi wa TANU Arusha, chini ya Japhet Kirilo ulikuja Moshi pamoja na Rajab Chamshama na Robert Otieno kuja kuchunguza kwa nini TANU ilikuwa inachelewa kusajiliwa Moshi.
Viongozi hawa waliitisha mkutano wa uchaguzi Welfare Centre ambao ulihudhuriwa na watu takriban ishirini na tano mmoja wao akiwa Yussuf Ngozi. Mkutano ule ulimchagua Mzee Yussuf Ngozi kuwa mwenyekiti wa kwanza wa tawi la TANU Moshi mjini.
Taratibu Kimalando akawekwa pembeni. Katika halmashauri ya kwanza ya tawi lile alikuwapo msichana mdogo wa miaka ishirini na nne, Lucy Lameck ambae baadae alikuja kuwa waziri katika serikali ya wananchi. 101
Mmoja wa wanachama wa mwanzo shupavu na msomi kabisa kujiunga na TANU alikuwa Zuberi Mtemvu. Mtemvu alikuwa akiishi Somali Street jirani na akina Sykes. Baba yake Mtemvu, Mzee Mwinshehe Manga Mtemvu, alikuwa amejenga nyumba yake nyuma ya nyumba ya Kleist.
Kwa hiyo Mtemvu alimfahamu Nyerere mwaka 1952, Nyerere alipokuja kufahamiana na akina Sykes. Mtemvu alikuwa na kipaji cha kuzungumza kama alichokuwanacho Nyerere. Mtemvu alikuwa na kipaji cha kuweza kushawishi na kuwashirikisha watu katika harakati.
Takriban mwezi mmoja baada ya kuundwa kwa TANU Nyerere na Mtemvu walikwenda kuifanyia kampeni TANU huko Morogoro ambako ndiko ilipokuwa asili ya ukoo wa Mtemvu.
Baba yake Mtemvu, Mzee Mwinshehe, alikuwa ameongea na baadhi ya wazee wenzake kuhusu TANU mjini Morogoro. Ijapokuwa Nyerere alijaribu kwa uwezo wake wote kuwafikishia watu ujumbe wa TANU matokeo hayakuwa mazuri.
Katika barua ambayo Mtemvu alimwandikia Ally Sykes mnamo Agosti, 1954 aliwaelezea watu wa kabila lake kama 'wagumu'. Ndani ya barua hiyo Mtemvu alimjulisha Ally kuhusu mwanachama mpya wa TANU, msomi, Ally Mwinyi Tambwe.
Mtemvu alimjulisha Ally kwa Tambwe kukubali kuingia TANU lilikuwa 'jambo zuri sana'. Tambwe, Mngazija wakati huo alikuwa katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika. Tambwe alimwahidi Mtemvu kuwaingiza TANU wanachama wengine 'wanaounga harakati zile mkono'. Baadae kidogo, mweka hazina wa Al Jamiatul Islamiyya, Iddi Faiz Mafongo, akawa mweka hazina wa TANU.
Mtemvu alimuelezea Ally kwa ufupi juu ya mkutano wao na Nyerere Morogoro mjini na aliomba apewe mara moja kadi za TANU 200. Ally aliwaandikia na na kuwapa kadi za uanachama wa TANU, Mtemvu na Tambwe na akamwambia mdogo wake Abbas, awaalike wote wawili kwenye mkutano wa uzinduzi wa tawi la TANU la Dar es Salaam ambao ulikuwa unanyika Jumamosi inayofuata.
Wakati uongozi wa TANU unajitayarisha kwa mkutano wa uzinduzi, Ally Sykes alikuwa tayari amekabidhiwa barua ya uhamisho kutoka Dar es Salaam kwenda Korogwe. Kwa hakika hasa, Ally alipewa barua hiyo wiki mbili tu baada ya kuundwa kwa TANU. Hii ilikuwa mara ya pili Ally kupewa uhamisho kama adhabu yake ya kupambana na utawala wa kikoloni.
Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1951 kufuatia kuandikiana kwake barua na Chief Secretary, Bruce Hutt, kufuatia serikali kushindwa kufuatilia memorandum ya TAGSA kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa uliozuru Tanganyika.
Katika mgogoro huu rais wa TAGSA, Dk William Mwanjisi alipewa uhamisho toka Dar es Salaam kwenda Kingolwira na Kawawa aliyekuwa katika kamati ya utendaji ya TAGSA alihamishiwa Bukoba. Dk. Mwanjisi na Kawawa walikubali uhamisho lakini Ally Sykes alikataa uhamisho huo na akachukua hatua za kuupinga.
Serikali ilinuia kumpeleka Ally nje ya Dar es Salaam kama moja ya mbinu za kuidhoofisha TAA pale makao makuu. Kuwatupa wanasiasa waliokuwa wakipambana na serikali ya kikoloni sehemu za mbali ilikuwa jambo la kawaida. Ally alitaka kufanywa kama Dk Kyaruzi alivyofanywa mwaka 1951 alipokuwa rais wa TAA akaondolewa Dar es Salaam na kutupwa kwanza Kiongolwira na baadae Nzega. Tutakuja kuona jinsi Ally Sykes na Rashid Mfaume Kawawa na Dk. William Mwanjisi wakiwa viongozi TAGSA alivyopambana na utawala wa Waingereza hapo baadae.
Uhamisho wa Ally kwenda Korogwe ulielekea kupelekwa kasi, hakukuwa na jambo lolote ambalo mtu angeweza kufanya kuhusu uhamisho huo. Abdulwahid, Nyerere na Mtemvu walifadhaishwa na jambo hili.
Katika barua ambayo Mtemvu alimwandikia Ally Sykes, Mtemvu alimjulisha Ally kuwa alikuwa na majadiliano na Nyerere ikiwa wakate rufaa kwa Labour Commisioner, Molohan, dhidi ya uhamisho huo.
Mtemvu alimjulisha Ally kuwa Nyerere alikuwa na wasiwasi katika uamuzi huo isije aikathibitisha ile shuku ya serikali kuwa 'Ally alikuwa mtu muhimu na mwenye manufaa sana kwa TANU'. Nyerere alimwambia Mtemvu kwamba njia nzuri ya kutatua tatizo la Ally ilikuwa kwa kupitia 'njia ya kuzunguka, kumfikia Labour Commisioner kwa kupitia mtu anaemmudu.' Lakini ukweli ulibaki kuwa si watu wengi waliokuwa na ujasiri wa kusimama kidete dhidi ya utawala wa kikoloni. Hata Nyerere mwenyewe kwa wakati ule hakuwa na ujasiri ule. Si Nyerere wala TANU waliokuwa na nguvu za kutosha wakati ule kuinasihi serikali kwa niaba ya Ally Sykes, mtu mwenye sifa mbaya ya uchochezi dhidi ya utawala wa kikoloni.
Serikali ya kikoloni ilidhani kuwa kumtoa Ally Dar es Salaam kusingeiondolea tu TANU mwanaharakati sugu lakini vilevile kungekiondolea chama mmoja wa wafadhili wake na chanzo kikuu cha fedha. Katika barua ile Mtemvu alimjulisha Ally kwamba mara tu atakapokuwa nje ya Dar es Salaam asiwe na matumaini yoyote ya kurudishwa tena Dar es Salaam. Mtemvu alimaliza barua yake kwa kumtahadharisha Ally kuwa serikali itahakikisha hapandishwi cheo au kupewa kazi yoyote ya madaraka daima.
TANU ilinufaika sana kwa siasa za wastani za Nyerere, umakini wake na kipaji chake cha kuzungumza. Vilevile harakati kwa ujumla zilinufaika kwa ujasiri wa Mtemvu na Ally. Wao walitenda mambo kwa ujasiri zaidi. Hawakushughulishwa sana na nadharia katika maamuzi yao ya siasa. Ilikuwa katika kipindi hiki cha kuijengea TANU misingi imara ya uongozi ndipo Nyerere alimshauri Mtemvu aache kazi serikalini ajiriwe na TANU. Mtemvu alikubali ushauri ule na akaacha kazi. Mtemvu akawa katibu wa kwanza wa TANU.
Mtemvu na Mhando walijukana kama 'wakomunisti' na serikali lakini wao wenyewe hawashughulishwa na jina hilo. Hivi ndivyo ilivyokuwa Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu alivyokuja kuwa mmoja wa viongozi wa juu katika TANU.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |