Nani?!
Leo nalipiga goma, goma hili la mgambo,
Livume hadi Dodoma, na Tabora kwa Mirambo,
Lindi Mtwara Kigoma, Pangani kwa Mwinyi Kombo,
Wa CCM Mkapa, Lipumba nani zaidi?
Nani nauliza Kiko, apasaye hiki chombo,
Mwenye sera za mashiko, si kiburi majigambo,
Ya matapishi makoko, ayasafishe makombo,
Wa CCM Mkapa, Lipumba nani zaidi?
Nani mwenye nzuri sifa, za manukato si shombo,
Busara na maarifa, siyo mipasho mafumbo,
Mkweli hana kashifa, na maneno ya utumbo,
Wa CCM Mkapa, Lipumba nani zaidi?
Yupi nauliza mimi, mahiri mtenda mambo,
Asiyepinda ulimi, au kutufanya chambo,
Akuze wetu uchumi, siasa isende kombo,
Wa CCM Mkapa, Lipumba nani zaidi?
Yupi chamache na sera, zitung'arishe maumbo,
Kilimo na barabara, viwanda vyenye mitambo,
Ichanue biashara, ndani na nchi za ng'ambo,
Wa CCM Mkapa, Lipumba nani zaidi?
Nani awe kiongozi, aso tucharaza fimbo,
Mwenye ukweli uwazi, si wa kuimba vinyimbo,
Hodari mchapa kazi, asiyevimbisha tumbo,
Wa CCM Mkapa, Lipumba nani zaidi?
Nani limetimu swali, ni bei siyo kimombo,
Nijibuni Waswahili, kwa tungo zenye ulimbo,
Zinase kwenye akili, nisitatizwe kitambo,
Wa CCM Mkapa, Lipumba nani zaidi?
Idd Kikong'ona,
Morogoro.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |