RIWAYA

Joka la Mdimu -18

BAADA ya kurejea ndani ya hoteli yake Gray Kwacha alijitupa kitandani akijutia nafasi aliyoikosa. Macho darini aliwaza hili na lile. Hatimaye aliondoka, akafungua kabati refu la kuwekea nguo na kuchukua bunduki ndani ya mfuko wa turubai. Aidha, alichukua darubini yake na kuitia ndani ya mfuko mwingine mdogo wa plastiki. Halafu alichomoa pochi yake kuangalia kiasi cha fedha zilizosalia. Noti kwa noti zilipangana ikawa vigumu kujua hesabu yake ila kukisia tu. Kila kitu tayari, alijiandaa kurejesha funguo za chumba chake kama ilivyokuwa kawaida kwa kila atokaye nje ya hoteli hiyo. Lakini wazo likamjia bora awache silaha zake hadi usiku.

Alizirejesha ndani ya kabati na kutoka. Kule chini ya hoteli aliingia ndani ya gari lake na kulipiga moto, akashika barabara ile iendayo hifadhi ya taifa ya Kwale. Aliiandama barabara hiyo kwa muda wa nusu saa kabla ya kushika njia ndogo ya kushoto. Huko alikwenda akipita msitu wa kadiri wa miti ya miiba na nyika.

Hakukuwa na kijiji kikubwa isipokuwa vijumba viwili vitatu vilivyoshikana pamoja kila baada ya hatua ndefu. Kinyume na vijiji vingi vya shamba, hivi havikuzungukwa na mashamba yoyote wala bustani. Alipishana na mtu mmoja mmoja tu akawaogesha vumbi zito jekundu lililotimuliwa na magurudumu ya gari lake. Kiasi cha dakika ishirini baadaye, huku msitu bado umeshonana, ghafla alitokezea kunako vibanda viwili vilivyojengwa kuelekeana.

Si mgeni sana na hapo alipunguza mwendo wa gari lake akaliingiza karibu na vibanda hivyo vilivyokuwa kiasi cha hatua kumi kutoka barabarani. Pote palikuwa kimya, pasisikike hata sauti ya kuku. Gray Kwacha akawa tayari kumlaumu Leila kwa kumletea ndege mbaya mintaarafu ya safari yake.

Aliukazia macho mlango wa kile kibanda cha kulia kilichojengwa kwa magogo matupu na kuezekwa kwa nyasi. Mlango wake ulikuwa wa mbao za msonobari.

Punde si punde mlango huo ulifunguliwa taratibu. Gray Kwacha akafunga pumzi zake kusubiri linalofuatia. Silka ya wasasi wote ilikuwa kuchukua hadhari na kutomwamini yoyote. Hodari wa kuwinda, nao waliwindwa nyikani, mwituni hadi nyumbani. Sura jasiri ya mwanaume wa makamu, ilitokeza kabla ya kuchomoza kiwiliwili chake chote nje ya mlango ule. Gray Kwacha alishusha pumzi yake, akapuna jasho lililofanya vijipele vya muda juu ya paji lake la uso.

"Karibu mzee!" mtu yule, mrefu, mwembamba, mweusi mno alisema akilisogelea gari huku kavalia suruali ya kaki na sweta nyekundu za zamani iliyokuwa na tundu katika bega la kushoto.

"Asante", Gray Kwacha alijibu huku akishuka kutoka ndani ya gari lake ambalo alilizima kitambo tangu afike pale.

"Habari za safari", yule bwana alimuuliza.

"Nzuri".

"Tulikutazamia jana".

Mwanamke yule habithi amevunja miadi yangu ya maana, Gray Kwacha aliwaza lakini akasema, "Niliwasili jana usiku, nikashinda nimelala kwa uchovu wa kuendesha gari kutoka Mindule hadi huku!"

"Doo! Kweli mzee!" yule bwana akasema huku akipitisha macho yake katika lile gari na kuyatuliza juu ya magurudumu. Akasema kwa upole, "Pole sana".

"Nishapoa".

"Karibu ndani".

"Sawa. Mwenzako yuko wapi?

"Amekwenda mjini leo alfajiri, atarejea mchana".

Kibanda kile kilikuwa na chumba kimoja na sebule ya kukalia ambayo iliwekwa viti viwili vya marimba na kimoja cha kulala ambacho katikati kiliwekewa gunia. Kwa ajili ya kutumika nadra, kilibaki kimekunjwa muda wote, usiku na mchana. Sebuleni hapo hapakuwa na dirisha, hivyo Gray Kwacha alipata muda kuviona vitu vilivyokuwemo mle kwa msaada wa mwanga hafifu uliopenya katikati ya magogo yale na mlango wa mbele uliofunguliwa kidogo mno.

Walizungumza mambo kadha kuhusu uwindaji kabla ya Gray Kwacha kuelezea, "Nilikuwa nataka kuja kuchukua mali usiku".

"Sawa, ziko pembe ishirini za faru na ishirini za ndovu. Unaweza ukazichukua zote, maana vitu hivi hatari".

"Vipi hali ya mawindo?"

"Sio nzuri. Ulinzi mkali, wawindaji wengi, na ndovu hasa faru wamepungua mno. Ndovu wamebaki wadogo tu. Inabidi tuingie hadi kwenye hifadhi ya wanyama wenyewe. Juzi tu wawindaji watatu walipigwa risasi na wengine wanne kukamatwa na walinzi", yule bwana alimueleza akimkazia macho Gray Kwacha ambaye alibwaga macho yake chini. Alibaki hivyo kwa muda mrefu akiwaza. Alitafuta maneno muafaka kukidhi risala kauli ile asiyapate, akaishia, "pole sana".

Mazungumzo baina yao yalikwisha. Gray Kwacha akasimama na kuaga. "Basi tutaonana usiku!" Alisema huku akitangulia kutoka nje. "Nikija nitakuleta bunduki nyingine nzuri zaidi".

"Vizuri".

******

Mchana wote Gray Kwacha alibaki amepumzika na kulala hotelini kwake hadi saa mbili ya usiku alikwenda Hunter's Hotel. Huko mazungumzo yalihusu zaidi shughuli za uwindaji na biashara ya vipusa, meno na ngozi za wanyama. Kitu kimoja kilichodhihirika katika maongezi ya juma ya pale ni kutoweka kwa faru pamoja na kupungua kabisa kwa tembo. Lakini hakuna aliyewaza lipi la kufanya dhidi ya hali hiyo. Kila mwindaji au mfanyabiashara hiyo aliwaza mbinu mpya za kupata vipusa kul hali. Na hiyo nayo ikabaki kinga iliyohifadhiwa mbali, chini kabisa ya chembe cha moyo cha kila aliyeshughulika na biashara ile.

Baada ya muda, maongezi hayo yalimchosha Gray Kwacha. Alipitisha macho huku na kule katika baa ya mle hotelini. Hatimaye alifanikiwa kumkaribisha msichana mmoja wa Kizungu ambaye baada ya mazungumzo ya muda mrefu waliondoka pamoja kuelekea hotelini kwake. Aliporejea alijitayarisha kuondoka. Nia yake ilikuwa kusafiri usiku kuepuka askari ili aingie Mindule alfajiri. Ingawa petroli ilikuwa ya shida zaidi Kwale kuliko Mindule, Gray Kwacha alihonga na gari lake lilijazwa petroli pamoja na matangi yake mengine ya akiba.

Saa nne kamili ya usiku alirejesha funguo hotelini, akaingia ndani ya gari lake.

Safari hii ya kwenda kwa yule mwindaji ilizizima zaidi kwa ukimya na kiza. Hakukuwa na kiumbe chochote ila chui mmoja ambaye mara moja alikatisha barabara upesi na kutokomea mwituni.

Yule bwana mwindaji alisaidiana na mwenzake kuvihifadhi vizuri vile vipusa wakavipakia ndani ya gari. Halafu waliingia ndani ambako Gray Kwacha aliichomoa ile bunduki mpya kutoka ndani ya mfuko wake, akamkabidhi yule bwana mwindaji huku akimuonesha namna ya kuitumia, pamoja na darubini yake. Pamoja nayo alimkabidhi risasi zake hamsini. Mwisho alichomoa pochi yake akawakabidhi wale mabwana vitita vya noti ilihali wamekenua meno kwa furaha.

Nje waliagana na Gray Kwacha akaanza safari ya kurejea Mindule.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook