MAONI YETU

Rais Mkapa anafungia Mwembechai Killings, Kanisa launga mkono!

HABARI za kufungiwa kwa kitabu cha Mwembechai Killings and the Political Future of Tanzania na kwamba kinasomwa kwenye mtandao wa mawasiliano wa kimataifa kupitia kwenye kompyuta (Internet) zaelekea kuzua 'kiwewe' cha aina yake nchini.

Wananchi waliozungumza na AN-NUUR wameeleza kwamba wamesikitishwa na baadhi ya taarifa za habari na maoni ya baadhi ya watu kwamba badala ya kuzungumzia mantiki ya hoja na haja ya kufungia kitabu hicho, uzito unaelekezwa kwenye kutaka kupotosha hisia na mawazo ya wananchi.

Tunajua maadhali Mhe. Rais amekipiga marufuku, si ruhusa tena kukitangaza wala kuzungumzia maudhui yake.

Lakini tunadhani na sisi tuna haki ya kutoa maoni yetu juu ya kauli za baadhi ya watu kufuatia kupigwa marufuku kitabu hicho.

Mrengo wa habari zinazoandikwa kuhusu kitabu hicho zimejaa juhudi ya kutaka kupotosha mawazo na hisia za wanachi kwa lengo la kuchochea na kupandikiza mawazo ya baadhi ya watu wanaotaka kuona Waislamu nchini wanafanywa wananchi wa daraja la pili.

Kitendo cha kukiita kitabu hicho kuwa ni cha Waislamu kina lengo la kujenga dhana kwamba kila kitu kilicho cha Waislamu ni halali kunyimwa haki nchini. Dhana hiyo yaweza kuwa imejengeka kwenye vichwa vya baadhi ya watu wanaofaidika na dhulma ambazo Waislamu wamekuwa wakidai kufanyiwa nchini Tanzania.

Tunadhani Watanzania wangependa kujadili sheria za kupiga marufuku machapisho kama zinafaa kuendelea kuwepo nchini katika zama hizi za demokrasia, ukweli na uwazi kwa mwananchi kutoa maoni yake na wengine kupewa haki ya kuchambua maoni hayo ili kujua ukweli na uongo uliomo katika machapisho hayo.

Kutoa anwani potofu ya kukiita kitabu hicho kuwa ni cha "Waislamu" kunalengo la kuwatoa wananchi kwenye mada ya kujadili umuhimu wa kuwepo baadhi ya sheria miongoni mwa zile 40 ambazo Tume ya Jaji Nyalali iliona zimepitwa na wakati.

Tunaamini kwamba wanaopandikiza anwani hizo wanataka kupotosha fikra za Watanzania ili waamini kuwa jambo lolote la Waislamu, kuonewa ni sahihi.

Watanzania walio wengi hapana shaka wana mwamko na uwezo mkubwa wa kutambua propaganda za maonevu zenye lengo la kutaka kutugawa kwa misingi ya chuki za kidini.

Lakini linalotushangaza zaidi hatuoni ni vipi uongozi wa Kanisa Katoliki ujitokeze kuisemea serikali na uamuzi wa Rais Mkapa katika kukifungia kitabu hicho.

Katibu wa Kardinali Polycarp Pengo, Padri Andrew Luanda amealiambia gazeti moja kuwa "Waislamu hawana sababu ya kulalamika kwa sababu Rais amekipiga marufuku kitabu hicho kwa kutumia mamlaka aliyopewa kikatiba". Katibu huyo wa Pengo akanukuliwa akisema; "Sheria zetu ziko wazi na zinampa uwezo Rais kuchukua hatua fulani katika mambo kadhaa ilimradi mambo hayo yawe yanahatarisha usalama wa jamii".

Aliyepiga marufuku kitabu ni Rais Mkapa. Hata kama kungekuwa na watu wanaohoji uamuzi huo wa Rais, yeye Padri wa Kanisa Katoliki anahusika vipi? Au yeye ndiye pia Mwandishi wa Rais!

Mauaji ya Mwembechai yamechochewa na Padri wa Kanisa Katoliki, Lwambano.

Serikali ikaitikia uchochezi wake, polisi wakaua. Kardinali Pengo akahalalisha mauaji yale akidai hata jiwe linaua.

Leo Mhe. Rais anapiga marufuku maelezo ya Waislamu juu ya mauaji hayo, Padri Mkatoliki anasherehesha amri ya Rais!

Hii si hali ya kawaida. Na Mwandishi hakukosea kwenda kumhoji yeye. Anajua wapi pa kuthibitisha linalokubalika nchini hapa na lisilokubalika. Hakupata taabu kwenda kwa Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Ndani au wenye kitabu chao, bali kwa Pengo.

Amejisemea Dkt. Sivalon, Ukatoliki ulivyojikita katika siasa na serikali imekuwa kama kitu kimoja. Maamuzi na matendo ya serikali huonekana kama ya Kanisa.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook