Ajenda ya siri isikiwamishe demokrasia

Na S. Hussein

UPO muelekeo unaojenga dhana kwamba ndani ya chama cha mapinduzi asiyekuwa mkiristo mkatoliki, Muislamu wa Bara au Mpemba hastahiki kushika madaraka ya Urais.

Mtu anaweza akahisi kwamba kuna uzoefu ndani ya Chama Cha Mapinduzi unaoonesha kutakiwa Rais Mkatoliki kwa upande wa Muungano na Muunguja kwa upande wa Zanzibar.

Pengine hisia kama hizo zilijengeka na kuimarika kwa vile awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi ilishuhudia Mkatoliki akikaa Ikulu kwa zaidi ya miongo miwili.

Kwa upande wa Zanzibar yawezekana ni kutokana na ukweli kwamba awamu zote tano za uongozi zimeshuhudia Waunguja watupu kupata fursa ya kuikalia Ikulu.

Baada ya awamu ya kwanza ya uongozi wa bara ambao ndio huo huo wa muungano, ndio sasa ikawekwa zamu ya miaka kumi kumi kwa kila upande wa muungano.

Akaanza Mzanzibari. Yawezekana kuingia kwake ilikuwa ni jambo la bahati tu. Lakini yawezekana pia ikawa kwamba ulikuwa mpango maalum. Vyovyote iwavyo awamu hii ilisaidia mambo mawili. Kwanza kuzima hisia za Wazanzibari juu ya nafasi yao katika muungano kwani wao 'wangejisikia'. Na pili, kuzima hisia za Waislamu ambao nao wangehisi kuwepo kwa uzalendo.

Ndio maana Rais aliyetangulia alipata taabu kubwa kumpa sifa kem kem kwamba huyu ni mwenzetu, anasifa 36 za kuwa Rais, nakadhalika.

Hii kisaikolojia ilisaidia kudumisha "mfumo Katoliki" uliojengeka katika kipindi chote cha awamu ya kwanza. Kwa kuongoza chini ya mfumo wa serikali mbili ni wazi pasingekuwa na uwezekano wa kuirejeshea Zanzibar hadhi yake iliyokuwa inadaiwa. Na kutoyaelewa mazingira ya siasa za bara, asingeliweza kuwasaidia chochote Waislamu pale walipodai kudhulumiwa. Vivyohivyo kumesaidia kujenga mazingira ya kuzuia Muislamu wa bara kushika madaraka ya urais kwa hoja ya kuwepo Muislamu wa Zanzibar.

Ndio maana, matatizo ya Wazanzibari yakabaki pale pale na ya Waislamu wa bara nayo halikadhalika. Sana sana, matatizo ya Waislamu yaliongezeka pale walipojikuta wakifungwa katika tukio la uvunjaji wa bucha za nguruwe zilizo kuwa zimewekwa kinyume na sheria.Katika tukio hilo Rais aliagiza waislamu waangushiwe rungu la dola.

Kwa hiyo zamu ya Rais huyu haikuathiri chochote zaidi ya kuonekana kwamba ilitumika kama 'mwavuli' wa kufunikia dhuluma dhidi ya Waislamu wa bara na hisia za Wazanzibari juu ya Uzanzibari wao.

Hivi karibuni Baraza kuu la jumuiya na Taasisi za kiislamu lilikutana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Lewis Makame, lilikuwa katika jitihada ya kutaka kujua ni bahati gani 'nzuri' iliyowaangukia Wakristo wakawa wao ndio asilimia kubwa ya wanaounda Tume hiyo na wasimamizi wote wa Kura. Jibu alilowapa kwa mujibu wa mjumbe mmoja aliyekuwemo kwenye ujumbe huo wa baraza, ni kwamba Yeye Jaji siye aliyeiteua hiyo Tume na wasimamizi wake bali ni Rais tena si Rais huyu ni yule wa awamu ya pili ambaye ni Muislamu kama wao!

Kiini cha matatizo ya Waislamu ni ukiukwaji wa katiba unaofanywa na serikali, na msingi wa matatizo ya Wazanzibari ni serikali mbili.

Yeyote asiyejua ajenda ya siri anaweza kupata tabu kuelewa kwa nini CCM, ambayo siku zote imekuwa ikikataa katakata serikali tatu katika muungano ambazo zingekuwa na maslahi kwa pande zote mbili.

Hakuna hoja ya msingi na ya wazi inayoweza kuhalalisha serikali mbili na kuharamisha tatu. Sana sana wahusika wanasema ni sera tu ya Chama Cha Mapinduzi!

Aidha, kutoielewa ajenda hiyo ya siri kwaweza kumpa shida mtu kuelewa kwanini Waislamu wananyimwa haki zao za kikatiba.

Kwa undani wake, serikali mbili na ukiukaji wa katiba ndio inaonekana kuwa mbinu ya kudhibiti madai na nguvu za waislamu. La sivyo, isingewezekana kwa nchi yenye Waislamu zaidi ya asilimia hamsini kufanywa uendeshaji wake udhibitiwe na Wakatoliki!

Ni wazi pia kuwa mfumo wa serikali tatu pasingekuwa na uwezekano wa kuzitumia serikali zote hizo kwa malengo ya kidini.

Serikali ya Zanzibar iwapo ingelikuwa na mamlaka yake kamili,hadithi ya "msitikise kiberiti kisha kikaonekana kumbe hakikujaa" isingekuwepo.Ndio maana wale waliotoa hoja ya serikali tatu walizimwa. Rais wa awamu ya pili wa Zanzibar alijikuta akipoteza nyadhifa zote. Na ndio maana mpaka leo inaonekana kuwa dhambi kubwa kuzungumzia sera ya serikali tatu.

Kwa maana hiyo basi, Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi amekuwa akitizamwa na baadhi ya wazanzibari kama mtu wa kukandamiza maslahi ya nchi yake. Inaposemwa Rais bora wa Zanzibar atatoka Chama Cha Mapinduzi au mchagueni mgombea atakayedumisha muungano, hufahamika kwa wazanzibari hao kuwa, kinachotetewa ni kile ambacho hakitaathiri utendaji wa mfumo Katoliki uliojichimbia ndani ya serikali mbili. Maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari hayapo hapo.

Kama Wazanzibari hasa wanaCCM watakuwa wamefuatilia mdahalo wa hivi karibuni kwa kutulizani bila ya kuweka mbele ushabiki wa kisiasa watakuwa wamegundua kitu katika mazungumzo ya Mheshimiwa Karume hasa katika kueleza mamlaka ya Zanzibar chini ya Muungano huu ambapo mara moja alitamka kuwa Zanzibar ina "mamlaka kamili" na mara nyingine akasema Zanzibar "haina Sovereignty"

"Katika barua iliyopelekwa Vatikano sababu mojawapo iliyotajwa ya kumuunga mkono Nyerere ilikuwa kwamba itakuwa faida kwa kanisa siku zijazo", ameandika Dk. Sivalon akifichua ajenda ya siri ya kanisa hilo katika kitabu chake Kanisa katoliki na siasa ya Tanzania Bara uk.26.

Katika mbio za Urais kupitia CCM mwaka 1995, watu wawili walikuwa miongoni mwa wale waliokuwa na nafasi kubwa ya kushinda, Bwana Mrisho akikwaa kisiki katika dakika za mwisho.. Na Bwana John Malecela 'akadhibitiwa' kibabe asiingie katika kinyang'anyiro kile.

Historia inonyesha kuwa umewekwa mkakati mahsusi wa kipropaganda dhidi ya waislamu.Propaganda hizo,kwanza huzima madai yao dhidi ya dhulma.Lakini,pili huwawekea vikwazo waislamu kuingia sehemu nyeti.

Neno "udini" hutumika kama silaha ya kumuua kisiasa. Hili liliwakuta akina Profesa Kighoma Malima. Si hivyo tu bali hata chama chenye mgombea Muislamu huitwa cha kidini japo kimepata tasjila kwa vigezo vya kisiasa kutoka kwa msajili wa vyama aliyeajiriwa na serikali iliyopo madarakani.

Sio kwamba mgombea huyo ataleta sheria za Kiislamu bali atairudisha nchi katika maadili ya uongozi kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Rais wa awamu ya kwanza hayati Mwalimu Nyerere,alikuwa muhimili muhimu katika kuudumusha mfumo huu.Na haishangazi kupewa kwake cheo kisicho kuwa na nafasi katika katiba ya nchi.

Katika kitabu "Umasikini sasa Basi Tanzania" kilichoandikwa na Heriel Naftali Kida, Mwandishi katika kiambatisho ameweka orodha ya viongozi wa kitaifa waliohudhuria Warsha ya Kitaifa ya kuondoa Umasikini na hifadhi ya mazingira iliyofanyika Dodoma.

Katika Orodha hiyo Viongozi wa kitaifa wametajwa kwa mfuatano akianza Mheshimiwa Baba wa Taifa, Mwalimu J.K. Nyerere akifuatiwa na Mheshimiwa Benjamin W. Mkapa, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kisha viongozi wengine kwa mfuatano wa nyadhifa za juu za kitaifa.

Orodha ya viongozi wastaafu waliohudhuria Warsha hiyo imewataja Mheshimiwa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Mheshimiwa John S. Malecela na Mheshimiwa Joseph Warioba.

Mwanasiasa mmoja alipata kusema mara baada ya kufariki dunia hayati Mwalimu Nyerere kuwa wale wenye kujua unyeti wa wadhifa wake nchi hii, ni kwa sababu hiyo waliimba kuwa kiza kimetanda, hawajui wakapate wapi ushauri.

Mantiki ya kuenzi aliyoyaacha ni kudumisha mfumo huo yaani kuendeleza serikali mbili na kutompa madaraka yeyote asiyeweza kuuenzi mfumo aliouasisi.Mfumo ambao muislamu anauliwa na isionekane haja ya kufikisha shauri mahakamani.Mwembechai imeyashuhudia haya.

Kwa ujumla mfumo kristo ndio kiini cha matatizo mbalimbali ya kisiasa na kidini. Mathalan kudumazwa kwa miji ya Waislamu, kuteuliwa Wakristo watupu katika Tume ya uchaguzi, kuvunjwa kwa jumuiya ya Waislamu (EMWS), kuundwa kwa BAKWATA, kukataliwa kwa OIC, kubaguliwa, kunyanyaswa, kukamatwa, kudhalilishwa, kushitakiwa, kufungwa na kuuawa Waislamu pale Misikitini Mwembechai na kupigwa marufuku kwa kitabu cha Mauaji ya Mwembechai.

Kinyume chake, Maaskofu kwa miaka yote, wamekuwa wakitoa maelekezo kwa dola na kujihusisha moja kwa moja na masuala ya kisiasa. Kuhusu uchaguzi wa mwaka huu wao wameandaa kitabu kabisa na kuikosoa serikali iliyopo.

Na kwa vyovyote vile hawawezi kuunga mkono chama kingine zaidi ya CCM. Ingawa wameishutumu kuwa ni kichaka cha wahuni na kuwa imeshindwa kutekeleza Ilani yake bado hatudhani wanaweza kuunga mkono "upinzani"

Wananchi wa kawaida , hawanufaiki chochote na mfumo huo. Badala yake wanateseka na matatizo mbalimbali.

Wananchi wamekwishang'amua kuwa upinzani hauhatarishi amani, umoja wa kitaifa wala muungano bali unahatarisha maslahi ya viongozi wachache wa dini na serikali na wale wanaowatumikia.

Iwapo demokrasia itapewa muelekeo unavyoonesha, patakuwa na maana mbili. Kwanza,kuleta maendeleo ya kiuchumi na pili kuiondoa nchi katika hatari ya kusambaratika kutokana na mfumo wa ubaguzi wa kidini usiojali hisia wala haki za wananchi.

Tanzania itakuwa nchi bora yenye amani na umoja wa kweli wa kitaifa iwapo itarudishwa katika katika maadili ya utawala wa uadilifu, ukweli,haki na usawa kwa wote ambao itaifanya nchi iwe ya watu wa dini zote.

Kwa kufanya hayo, matatizo ya Waislamu na Wazanzibari hayatokuwepo. Hivyo, wakati umefika nchi irejeshwe katika misingi hiyo imara ya utaifa badala ya utaifa wa propaganda uliopo sasa.

Wananchi, kama wapiga kura wana jukumu kubwa la kuliweka sawa Taifa lao kwa njia ya demokrasia. Waachwe huru kuchagua viongozi wawatakao.

Wimbi la kurundika maaskari vituoni, kuzuia baadhi ya watu wasijiandikishe, kusafirisha watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine wakajiandikishe haya kama yatakuwepo yatazidi kuimarisha ile dhana uhuru haki na uadilifu unaozungumzwa utakuwa umeishia kwenye midomo ya wanaotaka kudumisha mfumo ukandamizaji.

Maamuzi ya wananchi yasivurugwe kwa sababu ya dini au chama cha mtu. Ajenda ya siri isiwachagulie watanzania 'mtu' kinyume na demokrasia. Asibebwe mtu kwa sababu ya Udini wake na 'asiangushwe' mtu kwa sababu ya dini wala Upemba wake.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook