KATIKA jamii nyingi za kijahili haki ya kutoa
talaka iko kwa mwanamume tu na mwanamke hana haki yeyote ya kumtaliki mume.
Katika sheria ya Kiislamu haki ya kutoa talaka iko kwa wote - mume na mke.
Haki ya Mume kutoa Talaka
Ilivyo katika kawaida ya maumbile mwanamume ndiye anayeanza kutoa posa au pendekezo la kuoana. Katika sheria ya Kiislamu, mwanamume pia ndiye anayepaswa kutoa mahari kumpa anayemtaka waoane, ndiye mwenye jukumu la kumlisha mkewe na kukidhi haja zake zote, na ndiye kiongozi wa familia. Kwa kuzingatia ukweli huu, Uislamu umempa haki ya kutoa talaka lakini iwe inapokuwa hapana budi na iwe ni kwa wema na kwa kutekeleza masharti yaliyowekwa na sheria.
Haki ya mke kumwacha mumewe
Ndoa katika Qur'an imeelezwa kuwa lengo lake ni kuleta upendo na huruma kati ya mume na mke - (Rejea Qur'an, 30:21). Endapo mwanamke ataona sababu za msingi ambazo, zinaifanya ndoa yao isifikie lengo hili, mwanamke anapewa uhuru wa kudai talaka kwa mumewe. Mumewe akimkatalia, anaruhusiwa mwanamke kwenda mbele ya vyombo vya Sheria ya Kiislamu na kudai talaka. Itabidi mume alazimishwe kutoa talaka iwapo vyombo hivi vya sheria vitashindwa kuwasuluhisha. Wakati mwingine, mwanamke anaweza kumtaliki mumewe bila hata ya kukubaliana naye au kupitia mahakamani. Inawezekana hivi kwa namna mbili:
Kama tangu mwanzo, katika kufunga mkataba wa ndoa mume alikubaliana na mkewe kuwa atakuwa na uhuru wa kuvunja ndoa, endapo mume atamfanyia au atafanya jambo fulani asilolipenda; basi atakapo vunja ahadi hiyo, mkewe atakuwa na uhuru wa kumwacha bila ya kudai talaka kwake au mahakamani. Kwa maana nyingine mwanamume tangu mwanzo katika mkataba wao wa ndoa, amempa mkewe haki ya kumtalakisha, endapo atafanya au atamfanyia jambo fulani asilolipenda. Talaka ya aina hii huitwa "Khula".
Kwa mfano, kama mume ametoa ahadi au amekubaliana na sharti alilopewa na mkewe katika makubaliano yao ya mkataba wa ndoa kuwahataoa mke wa pili, basi ndoa ya mke wa kwanza itavunjika mara tu atakapooa mke wa pili bila hata ya mume kutamka kuwa amemwacha au bila hata hukumu ya Kadhi.
Kama katika mkataba wa ndoa, mwanamume alitoa haki yake ya "kutamka" talaka na kumpa mkewe ili kumpa uhuru na uwezo zaidi wa kuvunja mkataba wa ndoa endapo ataona haifikii lengo lake.
Kuvunja ndoa kwa makubaliano ya mume na mke
Wakati mwingine, mume na mke wote baada ya kuona kuwa hawaishi kwa maelewano kama ilvyotarajiwa, wana uhuru wa kukubaliana kuachana kwa wema. Mahakama ya Kiislamu haitaingilia kati, labda itokee kuvunjwa kwa sheria nyingine kutokana na kuachana kwao huko. Aina hii ya Talaka huitwa "Mubarat".
Haki ya Mahakama ya Kiislamu katika kuvunja Ndoa.
Wakati mwingine, hata bila ya makubaliano ya mume na mke, mahakama ya Kiislamu ina uwezo wa kuvunja ndoa. Kwa mfano talaka ya aina ya "Li'aan" husimamiwa na Serikali.
Aina za Talaka na namna ya kuacha Kiislamu
Kuna aina nyingi za talaka ambazo ni vyema kila Muislamu kuzifahamu. kwani kwa kutojua talaka inavyopatikana mtu anaweza kukaa na mke aliyekwisha muacha kitambo. Kuna aina kubwa mbili za talaka zinazofahamika kwa wengi: (i) Talaka Rejea na (ii) Talaka isiyorejewa. Pia katika kipengele hiki tutaona aina nyingi za talaka.
Talaka Rejea
Talaka rejea nazo ziko za aina mbili:
Talaka Moja (Talaki-Ahsan)
Itakapofikia hatua kuwa mume na mke hawana budi kuachana baada ya jitihada zote za kuleta suluhu kati yao kushindikana, mume, akiwa na akili timamu na mbele ya mashahidi wawili waadilifu, wakati mkewe akiwa katika twahara atatamka kuwa amemuacha mkewe. Baada ya mume kutamka maneno ya kudhihirisha dhamira ya kumuacha mke kama vile kusema: "Nimekuacha", atalazimika kukaa na mkewe katika nyumba moja (ila atatengana naye katika malazi tu) na kukidhi haja zake zote kama kawaida, mpaka kiishe kipindi cha twahara tatu au miezi mitatu. utaratibu wa kutalaki unabainishwa wazi katika Qur'an:
Ewe Mtume (wa Mwenyezi Mungu)! Mtakapotoa talaka kwa wanawake toweni talaka wakati wa eda zao. (Yaani waacheni wakati wa twahara zao ambapo hamkuwahi kuwaingilia). Na fanyeni hisabu ya siku za eda zisije zikesha kabla hamjawarejea). Na mcheni Mwenyezi Mungu, Mola wenu. Msiwatoe katika nyumba asitoke katika nyumba hiyo, akae papo hapo kwa kulishwa na kuvishwa mpaka eda iishe), ila wakifanya jambo la ufasiki ulio wazi. Na hii ni mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na anayevuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui, labda Mwenyezi Mungu atatokeza jambo jingine baada ya haya (yaani jambo la kupatana).
Na wale waliokoma kutoka hedhi miongoni mwa wake zenu, ikiwa mnayo shaka, basi muda wa eda yao ni miezi mitatu, na (pia ndiyo eda kwa wale) ambao hawajapata hedhi bado. Na wanawake wenye mimba, eda yao mpaka watakapozaa. Na anaye muogopa Mwenyezi Mungu humfanyia mambo yake kuwa mepesi. (65:4).
Wawekeni humo humo mnamo kaa nyinyi kama mpatavyo (Ijapokuwa mumewaacha maadam eda yao haijaisha). Wala wasiwadhuru kwa kuwatia dhiki. Na kama wakiwa na mimba, wagharimieni mpaka wajifungue... (65:6).
Na wanawake walioachwa wangoje mpaka twahara tatu ziishe. Wala haiwajuzii kuficha (mimba) aliyoumba Mwenyezi Mungu katika matumbo yao, ikiwa wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na wanaume wana haki ya kuwarejesha katika muda huo kama wakitaka kufanya suluhu. Nao (wanawake) wanayo haki kwa sheria (kufanyiwa na waume zao)) kama ile haki iliyo juu yao kuwafanyia waume zao. Na wanaume wanadaraja zaidi kuliko wao. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye hikima. (2:228).
Katika aya hizi tunajifunza yafuatayo:
Baada ya mke kupewa talaka na mumewe mwenye akili timamu kwa matamshi au kwa maandishi kuwa "Nimekuacha" (au kwa maneno mengine yenye maana hiyo), atakaa eda - kipindi cha twahara tatu au miezi 3 - katika nyumba moja na mumewe na kila mmoja atawajibika kwa mwenziwe kama kawaida. Kama mke atakuwa amefanya jambo ovu sana lililowazi kiasi kwamba haivumiliki kumbakisha hapo nyumbani, itabidi akakalie eda kwa wazazi wake au nyumba nyingine mbali na mumewe.
Eda ya mwanamke mwenye mimba huisha pale atakapojifungua.
Endapo katika kipindi cha eda itadhihiri kuwa mke ana mimba, eda haitaisha mpaka atakapojifungua.
Pia tunajifunza kuwa hekima ya kuamrishwa kukaa eda ni:
Kuwapa wawili muda wa kufikiri zaidi na kuamua kurudiana. Hii ndio hekima ya amri ya kukaa katika nyumba moja na kila mmoja kumtekelezea mwenziwe haki zake kama zamani ila tu hawagusani (hawaingiliani). Katika kipindi hiki mwanamke anashauriwa ajipambe na "kujikwatua" zaidi. Kama mke ndiye aliyeomba talaka, mwanaume anatakiwa ajirekebishe kwa mkewe na aonyeshe upendo na mapenzi makubwa kwake.
Kumsitiri mwanamke anayeachwa asibadilishe maisha yake ghafla na kusononeka.
Kuthibitisha uhalali wa mtoto. Mtoto wa mume aliyeacha asije akafanya mtoto wa mume mwingine atakayemuoa huyo mke baada ya ndoa kuvunjika.
Kabla ya kipindi cha eda kuisha, mume na mke wanaweza kurejeana, endapo wanaahidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa wataishi kwa wema kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:
Na mtakapowapa wanawake talaka, nao wakafikia kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa wema au tokaneni nao kwa wema. Wala msiwaweke kwa kuwapa dhara mkaruka mipaka. Na atakayefanya hivyo atakuwa amejidhulumu mwenyewe. Wala amsizifanyie mzaha aya za Mwenyezi Mungu... (2:231).
Basi wanapofikia muda wao ima (warejeeni) muwaweke kwa wema au farikianeni nao kwa wema na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu. Na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Hivyo ndivyo anavyoagizwa yule anayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na anayemuogopa Mwenyezi Mungu, (Mwenyezi Mungu) humtengenezea njia ya kuokoka. (65:2).
Katika aya hizi, inasisitizwa kuwa uamuzi wa mke na mume kurejeana upitishwe kabla ya kipindi cha eda kwisha na warejeane kwa ahadi ya kuishi kwa wema. Isije mume akamrejea mkewe ili amkomoe. Huko ni kutomuogopa Mwenyezi Mungu na kuzifanyia mzaha aya zake. Vile vile kumuacha mke kwa mikiki-mikiki (kwa ukatili), pia ni kutomuogopa Mwenyezi Mungu na kuzifanyia mzaha aya zake. Kwa ujumla aya hizi zimesisitiza kumrejea mke kwa wema au kutengana naye kwa wema.
Baada ya kipindi cha eda kwisha, mwanamke atakuwa ameachika kwa talaka moja. Kitendo hiki cha kuachana kishuhudiwe na mashahidi wawili Waislamu waadilifu kama tunavyoamrishwa hivyo katika Qur'an, (65:2). Baada ya kuachika kwa utaratibu huu mwanamke sasa atakuwa huru kuolewa na mume mwingine yeyote anayekubalika katika sharia ya Kiislamu. Pia, wakipatana na mume wa kwanza kabla hajaolewa na mume mwingine, wanaweza kuoana tena kwa kufunga ndoa upya kama tunavyofahamishwa katika Qur'an:
Na mtakapo wapa wanawake talaka, nao wakamaliza eda yao, basi (nyinyi jamaa wa mke) msiwazuie kuolewa (na waume wengine au) na waume zao (wa mwanzoni) endapo wamepatana (kurejeana na kuishi) kwa wema. Hayo anaonywa nayo yule miongoni mwenu anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya mwisho. Hayo ni mazuri mno kwenu na safi kabisa. Na Mwenyezi Mungu anajua lakini nyinyi hamjui. (2:232).
Talaka mbili
Katika aina hii ya talaka, mume baada ya kushindwa kufikia suluhu na mkewe, huamua kumuacha kwa talaka mbili kwa kumuandikia au kumtamkia kuwa amemuacha katika twahara ya kwanza (kama tulivyoona katika talaka moja), kisha kumtamkia tena kuwa amemuacha talaka ya pili katika twahara ya pili au ya tatu. Pia inahesabiwa talaka mbili kama baada ya kutoa talaka moja, wawili walipatana na kurejeana kabla ya kipindi cha eda kwisha, halafu kisha wakakosana wakati mwingine kiasi cha kufikia hatua ya mume kutoa talaka nyingine. Vile vile kama wawili baada ya kuachana kwa talaka moja, watafikia maafikiano ya kuoana tena kisha wakagombana tena kiasi cha kupeana talaka, zitakahesabika talaka mbili.
Utaratibu mwingine wa kuacha kwa talaka mbili ni sawa tu na ule wa kuacha kwa talaka moja tuliouona. Hii nayo ni talaka rejea, kwa maana ya kwamba mtu anaweza kumrejea mkewe kabla ya kipindi cha eda kwisha. Pia baada ya kuachana mwanamume anaruhusiwa kufunga tena ndoa na mke aliyemuacha endapo wataelewana na akiwa bado hajaolewa na mume mwingine. Mke aliyeachwa kwa talaka zaidi ya mbili harejewi tena kama inavyosisitizwa katika Qur'an:
Talaka (unazoweza kumrejea mwanamke) ni (zile zilizotolewa) mara mbili. Kuisha naye kwa wema au kumwacha kwa ihsani... (2:229).
Talaka isiyorejewa
Talaka isiyorejewa ni ile ambayo mume hawezi kumrejea mkewe katika kipindi cha eda hata kama watasuluhishana, ila baada eda wakitaka wanaweza kuoana tena. Talaka zisizorejewa nazo zimegawanyika katika mafungu makubwa mawili: (a) Talaka tatu - talaka ambayo, mtu akishaitoa haruhusiwi kumuoa tena mke aliyemuacha mpaka aolewe na mume mwingine. (b) Talaka ambayo, mume anaruhusiwa kufunga ndoa upya na mtalaki wake watakapoamua kuoana tena na kuahidiana kuishi kwa wema.
Talaka Tatu
Talaka tatu zinapatikana kwa kutamka dhamira ya kumuacha mke mara tatu katika kila twahara katika twahara tatu za eda. Vile vile zitahesabika talaka tatu kama mume katika muda wa ndoa yao amewahi kutoa talaka rejea mbili kwa kipindi kimoja cha eda au vipindi tofauti ambapo walipatana na kurejeana. Pia kama mtu na mkewe waliwahi kuvunja ndoa mara moja kwa talaka mbili kisha wakaoana tena au kama waliwahi kuvunja ndoa mara mbili kwa talaka moja kisha mara zote hizo mbili walipatana kufunga ndoa tena watakapopeana talaka katika ndoa yao hii ya mwisho, talaka hiyo itahesabika kuwa ni talaka ya tatu.
Ni kinyume kabisa na sheria ya Kiislamu kutoa talaka tatu mfululizo katika kikao kimoja au katika twahara moja kwa matamshi au kwa maandishi. Wanachuoni wengi wamekubaliana kuwa talaka ya namna hiyo itahesabiwa kuwa ni talaka moja. Waislamu wanaofanya hivyo, wajue kuwa huko ni kuzifanyia mzaha aya za Mwenyezi Mungu na kuvuka mipaka ya Mwenyezi Mungu. "... Na anayeruka mipaka ya Mwenyezi Mungu basi amejidhulumu nafsi yake..." (Qur'an, 65:1). Uislamu umekataza vikali mchezo wa kutoa talaka tatu kwa mpigo kama tunavyojifunza katika hadithi ifuatayo:
Mahmuud bin Labiid ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alielezwa juu ya mtu aliyetoa talaka tatu mfululizo kwa mkewe. Kisha Mtume alisimama akiwa amechukizwa sana na akasema: "Unacheza na Kitabu cha Mwenyezi Mungu (s.w.) nikiwa bado tupo pamoja (nikiwa bado sijafa)?" (Mtume alikasirika) kwa kiasi ambacho mtu mmoja alisimama akauliza: Je, siwezi kumuua? (Nisai).
Hukumu ya talaka tatu ni kwamba baada ya mume kutamka talaka ya tatu hawezi tena kumrejea mkewe katika kipindi cha eda hata kama watapatana vipi. Baada ya kipindi cha eda kwisha, mkewe atakuwa ameachika kwa talaka tatu na atakuwa huru kuolewa na mume mwingine yeyote aliyehalalishwa kwake katika sheria ya Kiislamu. Lakini haramu mwanamke huyo kuolewa na mumewe wa kwanza mpaka aolewe na mume mwingine. Kisha, akiachika kwa mume wa pili kwa sababu za msingi au akiachwa mjane, ndipo itakuwa halali kwake kuolewa na mume wake wa mwanzo. Ndoa ya namna hii inajulikana kwa jina la "Tahliil". Qur'an inabainisha hukumu hii katika aya ifuatayo:
Na kama amempa talaka (ya tatu) basi (mwanamume huyo) si halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwingine. Na (mwanamume huyo mwingine) akimwacha, basi hapana dhambi kwao kurejeana (kwa kuoana tena), wakiona kuwa watasimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na hii ni mipaka ya Mwenyezi Mungu anayoibainisha kwa watu wajuao. (2:230).
Hukumu hii kali imetolewa ili Waislamu wasifanye mas-khara na talaka. Kuna baadhi ya Waislamu, wakikwaruzana tu kidogo na wake zao hutishia talaka au anatoa talaka kabisa. Mtu akiendelea na mchezo huu atajistukia ameshamuacha mkewe kwa talaka tatu na hana namna tena ya kumrejea. Ni katika mchezo huu wa kutoa talaka tatu bila kufikiri na kumuogopa Mwenyezi Mungu, baadhi ya Waislamu wameishia katika majuto. Baadhi ya Waislamu wanadiriki kumdanganya Mwenyezi Mungu kwa mtu kumuhonga mume mwingine amuoe mtalaki wake kwa lengo la kumuacha baada ya muda mfupi (na ikiwezekana asimguse) ili awe halali kuolewa na mume wake wa mwanzo. Huku ni kuzifanyia mzaha Sheria za Mwenyezi Mungu na ni Haramu ya uwazi. Ndoa za namna hiyo hazisihi mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.).
Talaka ya 'Ilaa
Aina hii ya talaka inapatikana kwa mtu kuamua kujitenga na mkewe zaidi ya miezi minne. Katika jamii za kijahilia palikuwa na tabia ya wanaume, kwa sababu mbali mbali, kuapa kutofanya tendo la ndoa na wake zao kwa kipindi kisichojulikana. uislamu unamruhusu mtu kutengana na mkewe kwa kipindi kisichozidi miezi minne.
Kwa wale wanaoapa kwamba watajitenga na wake zao (muda wao) ni kungojewa miezi minne. Na kama wakirejea (wakatangamana na wake zao) basi Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe (na) mwingi wa kurehemu. (2:226).
Baada ya miezi minne kupita bila ya mume kumrejea mkewe, ndoa itavunjika, bila hata ya kutamka kuwa amemuacha. kama atataka kumrejea tena mkewe itambidi afunge ndoa upya. Ni kwa mtazamo huu vile vile, mwanamke ana haki ya kudai talaka mbele ya kadhi endapo mumewe atakuwa amemsusa (amemuacha bila ya maagano yoyote) zaidi ya miezi minne. Mwanamke huyu atakuwa ameachika Kiislamu na atakuwa huru kuolewa na mume mwingine. hekima ya hukumu hii ni kuwapa wanawake haki zao na uhuru wao wanaostahiki.
Talaka ya Zihaar
Katika jamii ya Waarabu wakati wa ujahili, palikuwa na aina nyingine ya kumsusa mke kwa kumwambia: "Ninakuona kama mgongo wa mama yangu". Baada ya mume kutamka maneno haya hakuwa tena anamuingilia mkewe na kumtekekelezea vilivyo haki zake nyingine na wala hakuwa anamwacha ili apate kuolewa na mume mwingine. Uislamu umekataza desturi hii na kuwaadhibu vikali wale wanaofanya hivyo kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:
Mwenyezi Mungu amekwisha sikia usemi wa mwanamke yule anayejadiliana nawe sababu ya mumewe, na anashtaki mbele ya Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu anayasikia majibizano yenu; hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia, mwenye kuona.
Wale miongoni mwenu wawaambiao wake zao kuwa wanawaona kama mama zao (kwa hivyo wakajiepusha nao wasiwaingilie, wala wasiwape ruhusa ya kuolewa na waume wengine); hao si mama zao. Hawakuwa mama zao ila wale walio wazaa. Wanasema neno baya na la uwongo. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye msamaha, mwenye maghfirifa.
Na wale wawaitao wake zao mama zao, kisha wakarudia katika yale waliyoyasema (wakataka kuwarejea wake zao wakae kama kidesturi ya mke na mume), basi wampe mtumwa uhuru kabla ya kugusana. Mnapewa maonyo kwa haya. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda.
Na asiyepata (mtumwa) basi afunge saumu ya miezi miwili mfululizo kabla ya kugusana; na asiyeweza basi awalishe maskini sitini (kila maskini kibaba kimoja). (Mmeamrishwa) haya ili mumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu; na kwa makafiri iko adhabu iumizayo.(58:1-4).
Tunajifunza katika aya hizi kuwa, mtu akimsusia mkewe kwa kumwambia kuwa anamuona kama mama yake, anaharamishiwa mkewe na hawezi tena kumrejea kama mkewe mpaka atoe kafara kwa:
(a) Kumwacha mtumwa huru
(b) Kama hana mtumwa, kufunga miezi miwili mfululizo (bila ya kupumzika katikati).
(c) Kama hana uwezo wa kufunga kwa sababu za kisheria zinazomruhusu mtu kutofunga Ramadhani, atalisha maskini sitini.
Kama mtu hatatekeleza adhabu hii kwa hiari yake, mahakama ya Kiislamu itaingilia kati na kumlazimisha kufanya hivyo, ili mkewe awe halali kwake. Muda wa miezi minne ukipita kabla hajatekeleza adhabu hii, mkewe atakuwa ameachika kama ilivyo katika talaka ya 'Ilaa. Mkewe atakuwa huru kuolewa na mume yeyote aliye halali kwake. Pia mume anaweza kumrejea mkewe kwa ndoa mpya, endapo atamuwahi kabla hajaolewa na mwingine.
Talaka ya Li'aan
Talaka hii hupatikana kwa viapo viwili cha mume na mke. Ititokea kwamba mume au mke amemkamata mwenzie ugoni lakini hapana mashahidi wanne walioshuhudia kitendo hicho ila yeye mwenyewe itabidi, kama mume ndiye aliyemkamata mkewe ugoni, aape kwa kurudia mara nne kuwa anashuhudia kuwa mkewe ni mzinifu, kisha mara ya tano aape kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake ikiwa yeye ni miongoni mwa waongo. Mke naye ataapa mara nne kujitetea kuwa yeye hakufanya kitendo hicho kisha mara ya tano aape kuwa laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake kama mumewe ni miongoni mwa wasemao kweli. viapo hivi vinabainishwa katika aya zifuatazo:
Na wale wanaowasingizia wake zao (kuwa wamezini) na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushughulikia mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba: bila shaka yeye ni mmoja wa wanaosema kweli. Na mara ya ya tano (aape) kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake ikiwa ni miongoni mwa waongo.
Na (mke) itamuondokea adhabu kwa kutoa shahada mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba (huyu mume) ni miongoni mwa waongo. Na mara ya tano (aape) ya kwamba hasira ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake kama (mumewe) yu miongoni mwa wanasema kweli, (na yeye mke ndiye mwongo). (24:6-9).
Baada ya kuapizana hivi hapo hapo ndoa itakuwa imevunjika moja kwa moja kwani wawili hawa hawategemewi tena kurejeana na kukaa kwa furaha na amani.
Talaka ya 'Khul'
Hii ni aina ya talaka ambayo inapatikana kwa mwanamke kudai aachwe. Kama mwanamke atakuwa hapati furaha na amani katika ndoa ya mume aliye naye, kwa sababu zake mwenyewe ana haki ya kudai talaka kwa mumewe na itabidi mumewe ampe talaka kwa kufuata utaratibu wa kawaida wa kutoa talaka, na baada ya kipindi cha eda, mwanamke atakuwa ameachika. Kama mke amedai apewe talaka kwa sababu zake mwenyewe bila ya mumewe kumnyima haki yake yeyote, atalazimika kumrudishia mumewe mahari, ili iwe kikomboleo kwake. Hata hivyo, wanaume wanaweza kusamehe mahari hayo. Ilivyo kawaida mwanamume haruhusiwi kudai mahari kama ndiye aliyetoa talaka, kama inavyobainishwa katika Qur'an:
Wala si halali kwenu kuchukua chochote mlichowapa (wake zenu), isipokuwa (wote wawili) wakiogopa ya kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu (yaani hawataweza kuishi kwa wema). Basi mkiogopa kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu, hapo itakuwa hapana dhambi kwao (mwanamume wala mwanamke katika) kupokea (au kutoa) ajikomboleacho mwanamke. Hii ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu; basi msiiruke. Na watakaoiruka mipaka ya Mwenyezi Mungu, hao ndio madhalimu. (2:229).
Ilivyo katika sheria ni kwamba kabla mwanamke hajafikia kuomba talaka, atamshitaki mumewe katika mahakama ya Kiislamu au kwa Kadhi, endapo atakuwa anamtesa na kumdhulumu haki zake. Mwanamume atashauriwa kutekeleza wajibu wake kwa mkewe. Mwanamume akizidi kukengeuka, itabidi mke adai talaka mbele ya mahakama, kama mume amekataa kutoa talaka kwa hiari yake. Kwa hali hii, kwa kuwa mwanamke ndiye aliyekosewa, hatalazimika kurudisha mahari au chochote alichopewa na mumewe. Na mwanamume naye hatalazimika kumpa kitoka nyumba.
Wanawake wanaodai talaka kwa sababu zao binafsi zisizo za msingi, kwa sababu tu eti wanataka kubadilisha mazingira, wajue kuwa mchezo huo ni mbaya sana mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.) kama tunavyojifunza katika hadithi ifuatayo:
Shuuban ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Mwanamke yeyote atakaye dai talaka kwa mumewe bila kosa, hata harufu ya Pepo imeharamishwa kwake. (Ahmad, Tirmidh).
Talaka kabla ya Jimai
Mwanamume anaweza kughairi, na kuamua kumuacha mkewe ambaye ndio tu wamefunga ndoa lakini hawajakutana kwa jimai. Anaruhusiwa kutoa talaka na mkewe ataachika hapo hapo bila ya kukaa eda. Kama mwanamume alishatoa mahari hatadai chochote bali anatakiwa ampe mwanamke kiliwazo (kitoka nyumba) na ikiwa hajatoa mahari, atalazimika kutoa nusu ya mahari. Hukumu ya talaka ya aina hii inabainika katika aya zifuatazo:
Si dhambi kwenu kama mkiwapa wanawake talaka ambao hamjawagusa au kuwabainishia mahari (yao). Lakini wapeni cha kuwaliwaza (kitoka nyumba); mwenye wasaa kadri awezavyo. Matumizi hayo yawe kama ilivyosema sheria. Ndio wajibu wa wafanyao mema.
Na mkiwapa talaka kabla ya kuwagusa, na mmekwisha wawekea hayo mahari, basi wapeni nusu ya hayo mahari mliyoagana, isipokuwa wanawake wenyewe waache au yule (mume) ambaye kifungo cha ndoa ni mikononi mwake aache (haki yake ampe mahari kamili). Na kuacha ndiko kunakomkurubisha mtu sana na kumcha Mungu. Wala msisahau kufanyiana ihsani baina yenu; hakika Mwenyezi Mungu anayaona yote mnayoyatenda. (2:236-237).
Talaka ya Aliyerukwa na Akili na aliyetezwa nguvu
Talaka si jambo la kulifanyia mas-khara. Muislamu anatakiwa, kama imebidi atoe talaka, ahakikishe kuwa akili yake iko katika hali ya kawaida. Asitoe talaka akiwa katika hali ya kuchanganyikiwa-changanyikiwa. Talaka ya aliyerukwa na akili haisihi kama tunavyojifunza katika hadithi ifuatayo:
Abu Hurairah (r.a.) ameeleza kuwa Mtume wa Allah
amesema: "Kila talaka ni halali isipokuwa talaka ya punguani na mwenye
kurukwa na akili". (Tirmidh).
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |