MWENYEKITI wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba
ambaye yuko katika ziara ya kichama kanda za ziwa na magharibi ameamriwa
kusitisha ziara hizo mpaka muda wa kampeni utakapofikia.
Taarifa inayosemekana kutokea Tume ya uchaguzi ilifikishwa na polisi kwa Mwenyekiti huyo wa CUF jana akiwa mkoani Kigoma ambako ilikuwa afungue matawi ya chama chake na kuhutubia wananchi wa mkoa huo.
Kabla ya kuingia Kigoma hapo jana, Profesa Lipumba alikuwa wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera ambako imeripotiwa wananchi wengi waliihama CCM na kujiunga CUF baada ya kusikiliza hutuba zake.
Kwa mujibu wa taarifa hizo kulikuwa na jitihada za wazi zilizokuwa zikifanywa na vyombo vya Dola kujaribu kuzuia mikutano ya Mwenyekiti huyo ambaye hotuba zake zinazoelezea hali ngumu ya kiuchumi iliyopo nchini, zimekuwa gumzo kubwa la wananchi.
Mji wa Kigoma siku ya jana ulikuwa katika pilika pilika ya mapokezi ya Mwenyekiti huyo huku polisi wakiwa wamemwaga maeneo mbali mbali.
Jitihada za vyama vya CHADEMA na CUF mjini humo kukitaarifu chombo hicho juu ya mikutano ya Mwenyekiti huyo ziligonga ukuta badala yake alitakiwa kutofanya mkutano wowote mkoani humo.
Sababu ya polisi kuzuia mikutano hiyo imeelezwa kuwa ni taarifa waliyoipokea kutoka ngazi za juu zinazowataka wasiruhusu kufanyika mkutano wowote wa kisiasa mpaka hapo kampeni zitakapoanza rasmi.
Wananchi wa Kigoma walionekana kushangazwa na uamuzi huo wa jeshi la polisi ambapo wengine walikuwa wakishutumu na kuitafsiri hatua hiyo kama ni njama za kuwazuia viongozi wa upinzani wasiwasiliane na wananchi .
Profesa Lipumba ilikuwa ahutubie mikutano mitatu mjini Kigoma katika maeneo ya Mwandiga, Mwanga Centre na Ujiji kabla ya kuelekea Wilaya za Kibondo na Kasulu.
Hata hivyo, Profesa Lipumba alifanya mazungumzo ya ndani na viongozi wa CHADEMA na CUF akiwa na Katibu mkuu wa CHADEMA Dk. Amani Kaborou.
Anatazamiwa kuondoka mkoani humo leo kurejea Jijini.
MADAI ya kuwepo dosari katika uandikishaji wapiga kura, yametawala vituo vingi jijini Dar es Salaam.
Huko Manzese, baadhi ya wananchi wamedai kugundua kuwa wanaandikiwa namba zisizowiana na zile zilizo kwenye shahada zao.
Wamesema, ilivyo namba ya mwisho katika shahada ni lazima ifanane na namba ya kituo. Lakini wao wamekuwa wakipewa shahada zenye namba tofauti na ile ya kituo chao.
Hali hiyo imekuwa ikizua zogo katika vituo kadhaa ambapo wananchi wamekuwa wakidai kuwa zipo njama za kutia dosari shahada zao kwa makusudi ili wakose haki yao ya kupiga kura.
Mzozo mkali ulizuka huko Manzese na baadhi ya maeneo ya Tandale ambapo watu walikaribia kurushiana ngumi.
Bw. Almasi Shomari aliyekuwa akiongea kwa niaba ya wenzake alidai pia kuwa vipo vituo vya kuandikishia kura ambavyo havipo katika orodha.
Amesema, orodha ya vituo waliyopewa na msimamizi wa jimbo la Ubungo hakuna kituo kinachoitwa Manzese.
Bw. Almasi ambaye ni Katibu wa CUF Manzese amesema wananchi wanaojiandikisha kwenye kituo kinachoitwa Manzese wamekuwa na wasiwasi kuwa huenda siku ya kupiga kura kituo hicho kisiwepo.
Hata hivyo Msimamizi Msaidizi wa kata ya Manzese Bw. Abdallah amesema, kituo hicho ni halali na namba yake ni 218/E/...
Katika tukio jingine Mzee mmoja alizua mtafaruku pale alipodai ahakikishiwe jina lake limeorodheshwa kwenye kitabu.
Mzee huyo alifika katika kituo cha shule ya msingi Umoja Mabibo jana, na kudai ahakikishiwe kama alipojiandikisha Agosti 8, aliorodheshwa kwenye daftari la wapiga kura.
Hata hivyo mwandishi aliyejulikana kwa jina la Jesca alikataa kumfungulia kitabu kutoa wasiwasi wake.
Zoezi la uandikishaji wapiga kura lililoanza Jumanne, limetawaliwa na kutokuaminiana kati ya waandikishaji na wanaojiandikisha.
Baadhi ya watu wanaonekana kujenga dhana kuwa huenda pasiwe na uadilifu katika uandikishaji.
Wasiwasi huo umezidi baada ya kutokea madai kwamba badhi ya watu walipewa vipeperushi badala ya shahada.
Na wengine wakaandikishwa bila majina yao kuingizwa kwenye kitabu.
Matukio kama haya ndiyo yanayoimarisha wasiwasi kuwa baadhi ya waandikishaji wanaweza kutumiwa na baadhi ya vyama vya siasa kuhujumu vyama vingine.
Wakati huo huo, baadhi ya wananchi wameitaka Tume ya Uchaguzi iwe wazi katika maelekezo yake.
Wamesema haitoshi Tume hiyo kutoa makemeo ya jumla kwamba viongozi wa ini wasivifanyie kampeni vyama vya siasa.
"Tumesikia Askofu akisema CUF isichaguliwe, Mufti wa BAKWATA naye alikuwa ziarani mikoani akitoa ujumbe unaoipigia kampeni CCM", amesema Bw. Hamad na kuongeza; "wawataje kwa majina hawa wawakemee".
Tume ya Uchaguzi juzi ilitoa kauli inayopiga marufuku
viongozi wa kidini kuvifanyia kampeni vyama vya siasa.
HALI ya wasiwasi ilitanda hospotalini Bugando jana, baada ya Waislamu kumiminika hospitalini hapo kati ya saa 5 na saa 7 mchana.
Hali hiyo ilitokana na taarifa zilizowafikia waumini kuwa kundi kubwa la askari lilikuwa limeonekana hospitalini.
Waumini walipashana habari wakidhani kuwa askari hao walikuja kumchukua Ustadh Ilunga kumpeleka rumande.
Wasiwasi wao ulizidi kwa vile polisi hao walikuwa wadi Na. 6E iliyo jirani na Na. 6 C alipolazwa Ustadh.
Hata hivyo, iligundulika kuwa askari hao walimsindikiza kamanda wa polisi wa wilaya aliyekuwa na mgonjwa.
Jijini Dar es Salaam, Waislamu walikutana jana na kuamua kutuma ujumbe mzito Mwanza.
Ujumbe huo unafuatia mwingine ambao ushafika huko Mwanza na kuwasilisha salamu za awali.
Ustadh Ilunga alivamiwa usiku wa Jumatano ya wiki iliyopita na kukatwa mapanga. Mpaka leo polisi hawajachukua maelezo yake juu ya tukio hilo.
Badala yake wamemweka chini ya ulinzi wakidai wana kesi naye.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |