KUTOKANA na kibano cha maisha kinachoendelea hivi sasa, wananchi wengi wanaonekana kuigopa miaka mitano ijayo kama moto.
Wanauliza, kama miaka hii mitano ya awali ya serikali ya awamu ya tatu, imekuwa migumu na kuonekana kama makumi matano yaani miaka hamsini, je miaka mitano ijayo itakuwaje kama utawala huu utarudi madarakani?
Lakini wakati wananchi wakiutafakari mustakabali wao, viongozi waliopo madarakani nao, kwa upande wao wanafikiria hali ya baadaye ya maisha yao itakuwaje kama watashindwa uchaguzi? Huenda wengine wanafikiria hata kuikimbia nchi! Ndio maana wamefikia kupigana mishale, risasi na utoaji wa rushwa ili warejee tena kwenye nyadhifa zao.
Kutokana na wasiwasi huo wa viongozi, ndio maana wapinzani wao wameelezea hofu yao kuwa wanaweza kushinda uchaguzi lakini wasikabishiwe madaraka. Hofu hii pia inatokana na kauli kadhaa wa kadhaa zilizotolewa na viongozi walio madarakani.
Mathalani, kiongozi mkuu wa nchi aliwahi kutamka kuwa, wao hawawezi kuwaachia nchi wapinzani ambao vyama vyao havina historia kama CCM. Na kwamba atatumia kila jinsi kuhakikisha chama chake kinaendelea kushika madaraka.
Nae kiongozi mmoja mwandamizi kule visiwani aliripotiwa kutamka kuwa serikali ya huko ilipatikana kwa njia a mapinduzi hivyo haiwezi kuondolewa kwa karatasi!
Kidemokrasia unapokataa kumkabidhi mshindi madaraka, humkomoi yeye, bali unakuwa umemdhulumu mpiga kura aliyemchagua mgombea huyo.
Kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura waliompa ushindi mgombea huyo dhulma hiyo yaweza kuleta mtafaruku mkubwa wa kijamii hali inayoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Kwa bahati nzuri au mbaya, tayari limekwishapatikana fundisho papa hapa nchini, katika uchaguzi uliopita, Kama si busara na hakima za viongozi waliosemekana kunyimwa ushindi huo, wananchi walikwisha kuwa tayari kudai haki yao kwa njia yoyote ile.
Wanachoaswa wanasiasa ni kuwa, kung'ang'ania kuwatawala watu waliokukataeni kwa kura zao kuna taathira mbili, moja, mazingira ya utawala yanakuwa magumu sana kiasi kwamba mnaweza kuona miaka mitano kama miaka hamsini.
Ugumu wa kuwatawala watu wasiokutaka waweza kupelekea kutumia mkono wa chuma.
Pili, kuwatawala watu ambao hawakukuchagua kunaweza kukaribisha uasi katika nchi. Siasa na uasi ni kama mkaa na moto, huo huo waweza kuwa mkaa na huo huo kugeuka moto.
Hivyo hivyo vinavyoitwa vyama vya kisiasa vyaweza kugeuka vikundi vya waasi pale vitakapohisi kudhulumiwa kisha kukosa namna ya kupata haki zao.
Lakini, kwanini tufike kule walikofika wenzetu wa Congo na Angola? Au kwanini tuingie kwenye migogoro itakayozorotesha jitihada zetu za kutokomeza umaskini? Badala ya kukaa vikao vya kujadili maendeleo, tukae vikao vya kutafuta suluhu!
Utamaduni wa kuipisha demokrasia ipite ndio utakaotunusurisha na hali hiyo, viongozi walio madarakani wanayo dhima ya kuheshimu utamaduni huo.
Dalili zinaonesha kuwa wananchi wengi wameelewa demokrasia na umuhimu wa kushiriki uchaguzi.
Ni vizuri serikali ikahakikisha kwamba vyombo vyake haviingilii na kukwaza haki hii ya wananchi.
Bali visaidie kuboresha mazingira ili wananchi
watakapopitisha uamuzi wao kupitia sanduku la kura, matokeo yawe ni yenye
kukubalika kwa walioshindwa halikadhalika walioshinda.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |