Tusichague watoa rushwa

BAADHI ya watu wameifananisha rushwa na gonjwa hatari la ukimwi lisilo na tiba wala chanjo, gonjwa ambalo limekuwa tishio kwa maisha ya watu.

Rushwa ni adui wa haki. Wapenda haki daima huikimbia rushwa na wasiopenda haki huiambata na kuifanya rafiki ili kuwatimizia matakwa yao.

Rushwa hutumika kama kishawishi cha kubatilisha haki. Mtu anapoitoa au kudai madhumuni yake ni kununua haki kwa njia ya batili.

Kwa kutoa rushwa, mtu hushawishi ufanyikaji wa dhulma na kwa kudai rushwa kadhalika ni tamaa ya kutenda batili.

Mahali ambapo pameshamiri rushwa haki inakuwa haitendeki. Ni mahali ambapo wale wenye uwezo wa kutoa rushwa ndio hufanywa wenye haki siku zote na wanyonge wasio na uwezo huonekana hawana haki.

Baya zaidi katika utoaji rushwa ni pale inapotumika kama kishawishi cha kumpa wadhifa wa uongozi mtu asiyestahili na kumuacha anayestahiki.

Rushwa inaweza kuwa kipimo cha chama cha siasa kilicho makini. Kwa kuchelea hatari ya rushwa chama makini cha siasa kinakuwa macho kuziba mianya yote ya rushwa ili kuhakikisha kuwa kinatoa viongozi walio safi watakaounda serikali safi.

Chama makini ni kile kinachofahamu kwamba viongozi kama wabunge wanaochaguliwa kupitia chama hicho ni watu muhimu ambao watakuwa na majukumu makubwa ya kuwatumikia wananchi hivyo ili kuweza kubeba majukumu hayo. Mbunge ni lazima kwanza awe ni chaguo la wananchi utakaowatumikia na awe na uwezo wa kubeba majukumu hayo.

Mgombea anayepitishwa na chama ambaye si chaguo halali la wananchi wake ambaye aliyejisukuma kwa kutumia rushwa ambayo ni adui wa haki kumtoa mgombea huyo ili apigiwe kura ni kulisaliti taifa.

Kwani mara nyingi tumeona wanaogombea nyadhifa uwe wa ubunge, udiwani au wowote ule kwa kutumia rushwa ni watu wasio na uwezo na kwa kweli hawana sifa za kukubalika kwa wananchi hivyo hutumia rushwa kama kishawishi cha kukubaliwa.

Sasa ni juu ya kila mwananchi mpenda haki na maendeleo kuacha kumpigia kura mgombea wa aina hii katika uchaguzi unaotarajia na badala yake tuchague wagombea ambao ni safi.

Kwa ushahidi wa vyombo mbalimbali vya habari zoezi la upigaji kura ya maoni kuwatafuta wagombea Udiwani na Ubunge ndani ya CCM umeonesha mfano mbaya kwa chama cha siasa.

Magazeti yamedai mazoezi hayo yametawaliwa kwa kiasi kikubwa na vitendo vya utoaji rushwa ambapo wagombea wengi wamedaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kuwashawishi wapiga kura wawateue.

Wananchi mbalimbali wamekuwa wakijiuliza iwapo katika kura ya maoni tu vitendo vya rushwa vilivuka mpaka itakuwa vipi katika uchaguzi wenyewe?

Au kama CCM imeshindwa kudhibiti vitendo vya rushwa katika zoezi hilo, je itaweza kuvidhibiti katika serikali yake?

Hali hii ndani ya CCM imewajengea mawazo baadhi ya wananchi kwamba kugombea Udiwani au Ubunge kupitia chama hicho ni uwezo wa mhusika kumwaga fedha na sio uwezo wa kiutendaji.

Somo ambalo tunalipata ni kwamba upo uwezekano wa wagombea wengi kupata nyadhifa za Udiwani na Ubunge kupitia chama hicho kwa sababu ya umwagaji huo wa fedha uliokwishaanza kuonekana bayana lakini hawatakuwa wenye sifa zinazostahili japokuwa si wote.

Kwa mantiki hiyo tutakuwa na madiwani na wabunge wasio na uwezo wala moyo wa kuwatumikia wananchi bali waliojaa mawazo ya kurudisha fedha walizopoteza kuwahonga wananchi.

Ndipo hapa wananchi tunapolazimika kujiuliza manufaa ya baadaye ya kuwa na viongozi wa aina hii katika nchi yetu kwani miongoni mwa watu hao waliokuwa wakishindana kumwaga fedha kutatoka Mawaziri watakaounda serikali na Mameya.

Katika kusherehesha makala yangu hapa ninamnukuu Sheikh Ally Bassaleh wa jijini kama alivyoripotiwa na gazeti hili toleo la Agoti 1, 2000.

Akiongea jijini hivi karibuni na waumini wa Kiislamu, Sheikh Ally Bassaleh alisema kuwepo kwa taarifa za utoaji rushwa kwa baadhi ya wagombea Ubunge kupitia CCM ni aibu kwa chama hicho kinachojitangaza usafi na kupambana na rushwa.

Alisema rushwa ni adui wa haki na moja ya dhulma inayopigwa vita na vitabu vitakatifu vya Mwenyezi Mungu.

"Uislamu unapinga dhulma yoyote na rushwa ni miongoni mwa dhulma, hivyo hatuna budi kuipinga kwa kuwakatalia watoa rushwa kupata madaraka".

Alisema ikiwa watu wa namna hiyo watachaguliwa kuna hatari ya kupata viongozi watakaoendelea kuleta dhiki kwa wananchi kwa vile hawatakuwa na uadilifu.

"Kiongozi muadilifu hapatikani kwa rushwa bali uwezo wake na sifa zake hivyo tuwachague kwa vigezo hivyo badala ya milungura. Viongozi wa namna hiyo ni hatari kuliko petroli katika moto", alimalizia Sheikh Bassaleh.

Ndugu mwananchi mpenda haki na maendeleo Mwenyezi Mungu mkarimu amekupa macho unaona, amekupa masikio unasikia na amekupa akili unafikiri, itumie kura yako kwa uangalifu wakati utakapowadia.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook