Mwenye tumbo ni tumbole hata akifunga mkaja

WAHENGA wetu walikuwa wakitumia misemo na methali katika kutoa maonyo na mafundisho kwa jamii ya zama zao.

Tanzu hizi pia zilitumika kuwaarifisha watu walio waovu katika jamii na ambao wanaficha uovu wao na kujiwakilisha katika sura na umbo la wema; japo kwa undani wao ni wenye mwenendo usiokubalika na jamii inayohusika.

Kwa kawaida, methali na misemo hazichukui maana ya moja kwa moja ya maneno yaliyotumika. Vivyo hivyo katika methali hii, maneno 'tumbo' na 'mkaja' hayakutumika katika maana yake bali ni mafumbo yanayokusudia kueleza tabia mbaya ya mtu, ambayo imefichikana. 'Tumbo' limetumika kueleza tabia mbaya na 'mkaja' kuelezea kificho cha hilo tumbo. Wahenga wetu kwa busara zao waliepuka kutumia neno 'unafiki' na badala yake wakaliwakilisha kwa methali hiyo.

Ni ukweli usiopingika kuwa, yale waliyoyafundisha wahenga wetu, yawe ya misemo, nahau au methali, huwa ni yenye mafunzo yanayoendelea kwa nyakati na zama zote. Kilichokuwa kibaya na kilichokuwa kizuri katika zama zao huwa vivyo hivyo hata leo.

Hakuna Mtanzania mkalafu ambaye hajayasikia makemeo na maonyo ya viongozi wale wenye mamlaka juu yetu ambao hasa ni wale kutoka CCM na serikali yake; makemeo juu ya ubaya wa rushwa.

Mbali na kutahadharishwa juu ya viongozi wa CCM ambao ndio hao hao wa serikali, wamekuwa wakijinadi juu ya usafi na uadilifu walionao.

Wametangaza kwa mapana na marefu kuwa CCM ni safi na viongozi wanaotokana nao ni waadilifu na wamefanya kazi kubwa na kupiga hatua ya kuridhisha katika kutokomeza rushwa.

Darsa zao zimesikika hadi nje ya mipaka yetu mpaka wale wasiojua wakawadhania kuwa na hali ya kimalaika malaika. Masikini! Majigambo yao yamejidhihirisha kuwa walikuwa wakifunga na kukaza mikaja yao lakini matumbo yapo.

Kipindi hiki cha kinyang'anyiro cha uongozi miongoni mwa wana CCM ndani ya CCM yenyewe; na wakiwa wengi wao ndio hao hao viongozi wa serikali, na ambao walikuwa wakikemea rushwa, leo dira yao ya kuwaelekeza kwenye uongozi imegeuka kuwa ile ile rushwa waliokuwa wakiitushutumia wenzi wao.

Pamoja na kuwa vyombo vya habari vya CCM na serikali yake vimejifanya havioni yaliyokuwa yakitendeka lakini kwa hali ilivyokithiri hata yule asiyeweza kununua gazeti, habari hizi zimemfikia. Wengine wamefikia hatua ya kuuliza kuwa kile kibwagizo cha Radio Tanzania cha : "Rushwa ni mdudu mbaya" mbona hakisikiki tena?

Tabia ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Ikiwa ni mbaya au nzuri hata kama ataificha kiasi gani, iko siku itajitokeza bila ya yeye kutaka. Kutokana na hali iliyojitokeza ya rushwa na wizi wa kura katika kura za maoni za CCM, yuko ambaye bado atakuwa na uso wa kutoa kauli ya kukemea na kuelezea uovu wa rushwa? Tunadhani sasa wale waliokuwa wakijiuliza, "ni kwanini serikali ya CCM inashindwa kupunguza rushwa!" Sasa watakuwa wamepata jibu. Ukipanda mchongoma usitegemee kuvuna machungwa ila miba.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, hayati Mwalimu Julius Nyerere, alisema maneno yafuatayo: "Rushwa ni adui wa haki. Sitapokea wala kutoa rushwa". Wakati mmoja pia alisema: "Chama lege lege huzaa serikali lege lege". Masikini hayupo nasi tena. Angekuweko leo angeweza kutusaidia kutufahamisha kuwa chama kinachonuka uvundo wa rushwa kitazaa serikali ya aina gani! Angetusaidia hilo kutokana na kukithiri kwa rushwa na kupatikana kura za bandia.

Sasa inaeleweka kilichopelekea CUF kutahadharisha na mapema kuwa, mara hii hawatakubali ile sera ya "Ukipigwa kofi kuliani geuza na kushotoni", haitavumilika. Tunayo pia kila sababu ya kuwaunga mkono katika azma yao ya kulinda kura zao.

Ni vyema na ni wajibu wetu tuchukue fursa hii kuwatahadharisha wale wote wapendao amani na kutegemea mabadiliko kikatiba na kanuni za nchi, wajifunze kutokana na yanayojiri hivi sasa ndani ya chama tawala na vyombo vyake. Wajihadhari wasije kutumiwa wakatumika, wasijetegwa wakategeka. Hali halisi inavyoonekana lakini serikali, taasisi zake na hata ile ya kuzuia rushwa wameziba masikio, wamefumba macho. Vyombo vya habari vya chama na serikali vimeamua kuifichia CCM aibu inayoinyemelea. Hii ni ile ile tabia ya kufunga mkaja ili tumbo lisionekane. Wapenda haki kumbukeni kuwa, watoto wa wenye nchi hawapigwi virungu wala kutiwa rumande. Itakapofikia siku ya kinyang'anyiro baina ya CCM na mahasibu wao kila ovu litakalotokea sababu itakuwa ni nyinyi!

Pamoja na hilo jueni kuwa wapo ambao wamepandikizwa ndani ya vyama vyenu ili kuleta uharibifu humo. Mtawadhania wenzenu lakini wao ni katika wasiowatakia heri. Hayo ni mambo ya tungu zama za nyuma na hayana kificho kwa mwenye kuona. Katika kipindi cha Sauti ya Tanzania Zanzibar cha tarehe 22/7/2000 kijulikanacho kama "Kutoka Pemba", Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kama alivyotambulishwa na radio hiyo, ametuthibitishia hilo. Radio hiyo imemnukulu akisema: "Sisi (CCM) tuna majasusi wengi ndani ya CUF na tutaendelea kuwa nao". Kwa bahati nzuri tunaamini kuwa hilo CUF wanalijua na hao majasusi wanawajua kwa sura na majina.

Lenye kuhitajia tahadhari zaidi ni la wale ambao hawakupandikizwa katika vyama vyenu lakini wao hawana tofauti na hao majasusi wa CCM. Hawa ni wale ambao wameomba tasjili ya vyama, wakafungua ofisi na kupeperusha bendera,. Mtadhani wako katika upinzani kumbe ni mfano wa akina Abdallah Ibn Ubeid Salul ambaye alijinasibisha na wana Madina kuwanusuru wahamaji kutoka Makkah lakini nia yake ilikuwa kutia udhaifu katika kundi la wale waliofuata haki. Mnaonaje kama atawatahadharisha mmoja wenu kuwa hawa nao wameunda vyama kwa lengo hili? Wale tunaodhani kujitoa kwa akina Cheyo na Mrema katika muungano wa wapinzani ni jambo lilikuja bila kutazamiwa tunakosea.

Haya! Hali ndiyo hiyo! Hatupaswi kukaa tu na kushika tama. Kila maradhi yana dawa yake. Tunachotakiwa kufanya sasa, tena kwa nguvu zote, nyumba kwa nyumba na mtu kwa mtu, ni kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura. Kila mtu binafsi na kila anayemhusu na kila jirani awe amejiandikisha kupiga kura. Wasiojua kusoma na kuandika na watu wa zima kiumri wasaidiwe wapelekwe vituoni waandikishwe. Kumbukeni kuwa hii ndiyo nafasi pekee ya kujiamulia kiongozi unayemtaka. Tusiishie kuimba vibwagizo vya vyama vyetu, kupeperusha bendera na kuwasindikiza viongozi tu. Hapana! Tufanye hayo na kujiandikisha tufanye kwa hamasa kama hiyo.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook