KATIKA siku za mwanzo nafasi ya katibu mwenezi ilikuwa ikishikwa na viongozi mbali mbali baina ya Mtemvu, Denis Phombeah, Oscar Kambona, Iddi Faizi Mafongo na Stephen Mhando.
Mtemvu akiwa katibu mwenezi alikuwa na kazi ngumu ya kuwashawishi na kuwashirikisha watu kujiunga na kusajili matawi ya TANU. Ili kampeni ya kuwaingiza watu ifanikiwe na ujumbe wake uwafikie wananchi ilibidi TANU ifanye mikutano ya hadhara. Kwa bahati mbaya serikali ikawa haitaki kutoa kibali kwa TANU ili ifanye mikutano.
TANU ilijikuta katika hali ambayo haiwezi kuwasiliana na watu kuwatayarisha katika harakati za umma. Katika hatua kadhaa za ujasiri Mtemvu alifanya mikutano ya hadhara bila ya kupata kibali cha serikali.
Nyerere mtu wa hadhari hakutaka kuonekana anavunja sheria. Alifahamu kwamba vitendo kama hivyo vingesababisha matatizo kutoka serikalini. Jambo kama hilo lilikuwa sawa na kuikaribisha misukosuko bila sababu ambayo ingeathiri chama na uongozi wake wote.
Nyerere, kama rais wa TANU, alikuwa amepokea barua kadhaa kutoka kwa Chief Secretary, T. Griffith-Jones, kuhusu mikutano isiyokuwa na kibali aliyokuwa akiifanya Mtemvu. Lakini kwa hakika kwa TANU kunyimwa haki ya kuitisha mikutano ilikuwa sawasawa na kuifunga mikono.
Hakukuwa na namna nyingine TANU ingeweza kufanya ili iwasiliane na watu. Kuacha kufanya mikutano TANU ingebakia dhaifu na harakati zingekufa.
Mtemvu alikuwa akifahamu kuwa serikali ilikuwa imedhamiria kabisa kuiua TANU ingali bado changa. Akiwa bado amenaswa katika kitendawili hicho cha 'kibali cha kufanya mkutano', Mtemvu alipata nakala ya mkutano wa 674 wa Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa ambayo Attorney General, Gratten Below, alifafanua juu ya msimamo wa serikali kuhusu suala hilo.
Mwanasheria Mkuu aliarifu kwamba watu wanaweza kuanza shughuli za chama mara tu maombi ya usajili ya chama cha siasa yatakapowakilishwa; na wanaweza kuendelea na shughuli za siasa mpaka majibu kutoka kwa Msajili Mkuu yamepokelewa kwamba tasjili imekataliwa. Uongozi wa TANU katika makao makuu ulisisimka kwa taarifa hiyo iliyofukuliwa na Mtemvu.
Chama cha TANU kama vuguvugu la siasa kilikuwa katika fikra za Abdulwahid kwa miaka mingi na alijitahidi sana kufanya bidii kuona kuwa TANU inaundwa.
Chama ambacho kitawaunganisha wananchi wote bila ya kujali kabila au dini sasa kilikuwa hakizuiliki tena. Abdulwahid na uongozi wa TAA ndiyo waliopanda mbegu ya umoja. Ikiwa umoja huu ulikuja kuvunjwa mara tu baada ya uhuru wazalendo hawa waasisi hawana lawama.
Mkutano wa uzinduzi wa TANU ulihudhuriwa na kikundi kidogo cha takriban watu 20 miongoni mwao Julius Nyerere, Abdulwahid na Ally Sykes, Dossa Aziz, John Rupia, Mshume Kiyate, Makisi Mbwana, Jumbe Tambaza, Juma Waziri, Clement Mtamila, Rajabu Diwani, Schneider Plantan, Marsha Bilali, Rashid Ally Meli, Frederick Njiliwa, Iddi Faiz Mafongo, Iddi Tulio, Denis Phombeah na wengineo.
Kuna picha mashuhuri sana ya wanachama waasisi wa TANU. Katika picha hiyo wanachama watatu hawaonekani, Ally Sykes, Tewa Said Tewa na Kasella Bantu. Hawa walikuwa watumishi wa serikali na kwa kanuni za utumishi katika serikali ya Kiingereza, watumishi wa serikali walikuwa hawaruhusiwi kujihusisha na siasa.
Mwafrika yoyote aliyevunja amri hiyo kuu adhabu yake ilikuwa kufukuzwa kazi mara moja. Kwa hiyo picha hiyo ilipopigwa Ally, Tewa na Kasella Bantu walijondoa. Picha hiyo ilipigwa na Gomes mpiga picha maarufu sana wa Ki-Goa katika siku zile.
Abdulwahid alikuwa amepatana na Gomes aje makao makuu ya TAA kupiga picha hiyo ya historia. Kwa bahati mbaya Gomes alichelewa kufika ofisi ya TAA. Abdulwahid alikosa subira kwa hiyo, alimwomba mdogo wake Abbas kwenda kumchukua Gomes kutoka kwenye studio yake Acacia Avenue (siku hizi Samora Avenue) katikati ya mji. Chombo pekee cha usafiri walichokuwa nacho TAA ilikuwa baiskeli moja iliyochakaa.
Wakati Abbas ananyonga baiskeli kuelekea mjini kumchukua Gomes, Gomes alikuwa keshaondoka anakuja makao makuu ya TAA; kwa hiyo wakaipishana njiani. Hivi ndivyo Abbas Sykes akakosa kuwepo ndani ya picha hiyo mashuhuri.
Lakini picha hii maarufu haikuweza kuepuka mgogoro. Mkono wa mtu umechafua picha ile kwa kuingiza kwa ustadi uso wa Kasella Bantu ndani ya picha ile ili ionekane kama kuwa na yeye alikuwemo katika ile picha ilipopigwa. Uso wa Kasella Bantu umebandikwa katikati ya Abdulwahid na Chifu Patrick Kunambi kwa ustadi. Ingeweza kueleweka kama picha za Ally na Tewa zingeingizwa vilevile.
Hivi leo kuna picha mbili za kihistoria kwa kwa tokeo moja. Hivi sasa ipo ile nakala halisi isiyokuwa na wale wanachama watatu waasisi; na hii nakala mpya yenye kuonyesha uso uliobandikwa wa Kasella Bantu, lakini bila ya wale wenzake Ally na Tewa ambao hawakuwapo ndani ya picha toka awali.
Germano Pacha amefafanua kwamba, kama isingekuwa kwa picha ile kungekuwepo na wanachama wengi waasisi wa TANU kuliko wale 17 wa mwanzo waliokutana mjini Dar es Salaam tarehe 7 Julai, 1954.
Mchunguzi mmoja wa mambo ameandika kuwa:
'...uso wa (Bantu) katika ile picha ya kihistoria uliingizwa na kitengo cha upigaji picha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mnamo Mei, 1974, miaka 20 baada ya kupigwa (picha hiyo). Pili, dai lake (Kasella Bantu) kuwa ilikuwa yeye aliyeitisha mkutano mkuu linamuonyesha kuwa ni mtu aliyelewa njozi ya historia. Rais Nyerere alichaguliwa rais wa TAA mnamo Oktoba, 1953 badala ya Kleist Sykes. Alikabidhiwa kazi ya kuigeuza TAA kuwa chama cha kudai uhuru chenye nguvu. Dai la Kasella Bantu la kutaka sifa (kwa hayo anayosema ametenda) haliungwi mkono na historia'.105 (Tafsiri yangu).
Wakati maelezo ya hapo juu yamesaidia kuonyesha jinsi historia ya Tanganyika ilivyojaa matatizo, mtu yoyote mwenye kuifahamu vyema historia ya TANU hatashindwa kuona makosa kidogo katika maelezo hayo.
Julius Nyerere alichaguliwa rais tarehe 17 Aprili, 1953 na siyo Oktoba, 1953; na Nyerere hakuwa rais badala ya Kleist Sykes, isipokuwa badala ya Abdulwahid Sykes ambae in mtoto wa Kleist Sykes.
Kasella Bantu ndiyo mtu aliyempeleka Julius Nyerere kwa Abdulwahid kumtambulisha. Hii ilikuwa mwaka wa 1952. Bantu na Nyerere walikuwa wakijuana toka huko nyuma walipokuwa wakifundisha Tabora.
Chama hakiwezi kupinga ukweli kwamba Kasella Bantu alikuwa miongoni mwa wale wanachama 17 waasisi wa TANU. Halikadhalika chama hakiwezi, kupinga ule ukweli wa historia kuwa Kasella Bantu alishiriki katika 'kuandika' ile katiba ya TANU. Kasella bantu anakerwa sana na kupotoshwa kwa historia.
Kila alipopata fursa kuanzia alipokuwa ng'ambo uhamishoni na baadae baada ya kurudi nyumbani kutoka uhamishoni, Kasella Bantu ameeleza kuhusu mambo haya mawili ya kihistoria, kuwa 'aliandika' katiba ya TANU na ni mmoja wa waasisi wa TANU. Bantu kama waanzilishi wengine wengi anahisi kwamba mchango wake katika harakati za uhuru wa Tanganyika hazijathaminiwa. 108
Ally Sykes ndiye aliyechora kadi ya TANU na kuchagua rangi na nembo yake. Rangi alizochagua zilikuwa nyeusi ikiwakilisha taifa la Kiafrika na kijani kwa ardhi ya Tanganyika. Mfano wa kadi ya TANU ilitokana na kadi yake ya Tanganyika Legion. Baada ya kumaliza kuichora ile kadi, aliwaendea Tanganyika Standard Newspapers ili wamchapishie.
Kutoka mfukoni mwake mwenyewe alichapisha kadi 1000 za kwanza na akitumia fedha za TAGSA alichapisha kadi nyingine 2000. Kadi nambari 1 ilitolewa na Ally Sykes kwa rais wa TANU, Julius Kambarage Nyerere na Ally aliweka sahihi yake kama afisa aliyeitoa. Ilipendekezwa kwamba kadi chache za mwanzo lazima zipigwe mnada na fedha zitakazokusanywa zitiwe kwenye hazina ya chama. Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz, Rupia na wengine walipanda dau kununua kadi hizo. Ally alimshinda kaka yake Abdulwahid kwa bei akapata kadi ya TANU nambari 2; Abdulwahid alipewa kadi nambari 3; Dossa Aziz kadi nambari 4; Phombeah kadi nambari 5; Dome Okochi, mmoja wa wale wazalendo kutoka Kenya katika TANU alipata kadi nambari 6 na Rupia kadi nambari 7. Bibi Titi kadi nambari 16; Iddi Tosiri kadi nambari 25.
Mara baada ya kuundwa kwa TANU ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulikuja Tanganyika mnamo Agosti, 1954. Kamati kuu ya TANU iliwakilisha madai yake kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa uliokuwa ukizuru Tanganyika.
TANU ilionyesha katika madai yake kuwa kwa Waafrika wa Tanganyika suala muhimu sana kwao lilikuwa kutafuta uvumbuzi wa ule mgogoro wa ardhi ya Wameru kwa njia za amani. Uzito wa jambo hilo kwa TANU unaweza kuonekana katika maneno ambayo inasemekana yaliandikwa na Abdulwahid, Nyerere, Stephen Mhando na Earl Seaton. Lugha ya kisheria ya Seaton iko wazi katika fungu la maneno lifuatalo:
Tunatambua kutopingana kuliko bayana baina ya utekelezaji wa azimio hilo na heshima ya serikali. Lakini kwetu sisi hili si suala la heshima, ni la yote mawili suala la mwenendo mzuri na la kupata tunachodai. Kwa kadri uhusiano huo unavyohusika kanuni muhimu imevunjwa na hatukubali mpaka haki imepatikana.109 (Tafsiri yangu).
Msimamo wa TANU juu ya mgogoro wa ardhi ya Wameru haukupingana na msimamo wa TAA. Tatizo la ardhi na walowezi lilikuwa ni suala moja ambalo chama kipya cha TANU kisingeweza kudiriki kwenda kinyume na misimamo wa awali uliowekwa na TAA. Madai ya TANU kwa Umoja wa Mataifa yalikuwa, ujinga na maradhi kuwa ndiyo matatizo yaliyokuwa yakielemea sana Tanganyika.
Ndani ya madai hayo neno native 'mwenyeji' limetumika mara kadhaa likiashiria Waafrika. Hili lilikuwa neno la dharau likitumiwa zaidi na wanataaluma wa elimu ya wanadamu, anthropologists likimaananisha washenzi, yaani, mataifa yasiyokuwa Wazungu.
Neno hili lilitumika Tanganyika wakati ule kutofautisha baina ya Waafrika na Wazungu. Kasumba ya kikoloni iliingia ndani sana kiasi kwamba hata TANU haikuona ubaya kulitumia neno hilo la dharau ndani ya madai yake ya kwanza kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa. Madai hayo yaliyotiwa saini na Nyerere yanasema: 'Matatizo ya nchi hii kama wageni watukufu watakavyoona wao wenyewe ni mengi, lakini kwa wenyeji wa nchi hii makubwa sana ni mawili: Ujinga na Umasikini'.
Ukweli ni kuwa si kama uongozi wa TANU ulikuwa na imani yoyote kuwa ujumbe ule wa Umoja wa Mataifa uliokuwa ukizuru Tanganyika ulikuwa na uwezo wa kutatua matatizo yaliyokuwa yakiwakabili Waafrika wa Tanganyika, TAA ilikuwa na uzoefu wa kutosha wa kujua udhaifu wa ujumbe ule. Hata hivyo kile TANU kilichotaka kukionyesha kwa ule ujumbe ilikuwa ujumbe huo ulipokewa na chama halisi cha siasa na kilikuwa na Mwafrika mwenye elimu ya juu kama rais wake.
Taarifa ya ujumbe huo iliitambua TANU kama chama pekee cha siasa kinachowakilisha watu wa Tanganyika. Inashangaza sana kuona kuwa hii leo baadhi ya wanahistoria bila ya kufanya utifiti makini na wa kina wanajaribu kufifilisha mafanikio ya TAA na vongozi wake.
Wakati ujumbe wa umoja wa mataifa unafika Tanganyika, TANU ilikuwa bado haijasajiliwa na serikali. TANU ilipata tasjili yake tarehe 30 Novemba, 1954 baada ya kuzishinda hila nyingi na vizingiti vilivyowekwa na serikali za kupinga usajili wake. Ally Sykes anakumbuka siku moja adhuhuri, jua lilikuwa kali, wakati Nyerere alipokwenda nyumbani kwake Mtaa wa Kipata (sasa Mtaa wa Kleist) ambako yeye na kaka yake Abdulwahid walikuwa wakimsubiri atoke mjini alikokwenda kushughulikia tasjila ya TANU aje awape matokeo ya huko.
Alipofika Nyerere alionekana amechoka taabani na mwenye wasiwasi. Alizama ndani ya sofa akaufunika uso wake kwa mikono yake na alikaa kimya kwa muda. Abdulwahid na Ally walikuwa wakimsubiri azungumze. Nyerere alikuwa na habari mbaya. Serikali ilikuwa imekataa kuisajili TANU. Nyerere aliwaambia kuwa serikali imekataa kutoa usajili kwa sababu za kiufundi. Serikali ilidai kuwa TANU haikuwa na wanachama.
Baada ya kufahamu kuwa serikali imekataa maombi ya TANU kwa kuwa ati haikuwa na wanachama wa kutosha, mithili ya onyesho la mchezo wa kuigiza unaokwenda haraka, Abdulwahid alimuomba Said Chamwenyewe aende nyumbani kwao Rufiji, kusajili wanachama kwa ajili ya TANU. Rufiji ni sehemu ya Waislamu watupu. Kwa sababu hii TANU haikuwa na tatizo la kuwapata wanachama. Kwa hakika wanachama wa mwanzo wa TANU walikuwa kutoka Gerezani na Rufiji. Illife ameandika kuwa:
Mtiririko wa kuungwa mkono kwa TANU mjini Dar es Salaam unahitaji uchunguzi, lakini mapato ya fedha kwa mwaka 1958 yanaonyesha sehemu iliyo kubwa ya kuungwa mkono chama ilikuwa kutoka makazi ya Waafrika - Kariakoo, Ilala, Gerezani... hadi Septemba, 1955 Dar es Salaam ikiwa na watu kama 110,000 - ilichukua kiasi cha 25,000 kati ya 40,000 za kadi za uanachama wa TANU zilitolewa kote nchini. Huu ulikuwa ndiyo msingi ambao TANU iliteka Tanganyika.
Abdulwahid sasa akiwa na umri wa miaka 30, alikuwa amekamilisha lile lengo lake kubwa katika maisha yake, lengo ambalo lilianza kwa marehemu baba yake ambae miaka ishirini na moja iliyopita alipotabiri kuendelea kwa mapambano kati ya Waafrika wa Tanganyika na serikali ya kikoloni. Kleist Sykes alikuwa halikadhalika ametabiri jukumu la kizazi kijacho. Katika barua aliyomwandikia Mzee bin Sudi rais wa African Association, mwaka 1933, Kleist katika umri mdogo wa miaka ishirini na tisa, akiwa kijana mdogo sana aliandika maneno haya:
Tupambane kwa nguvu zetu zote kuelekea njia ya ustaarabu kama vilevile watu wa makabila mengine wanavyofanya. Haidhuru kitu ikiwa hatukamilishi kila kitu. Wale watakaokuja baada yetu watamaliza yatakayobakia.
Kwa hakika Kleist alikuwa mtu wa fikra. Kleist alizungumzia kuhusu 'ustaarabu' ambao hivi leo ungemaanisha 'kujitawala' na kuhusu makabila ambayo TANU imeyageuza kuwa taifa. Katika mwaka 1954 robo karne baadae katika jengo hilo hilo 25 New Street ambalo Kleist alisaidia kulijenga kwa njia ya kujitolea, kizazi kipya nchini Tanganyika kilikuwa kikiigeuza African Association aliyoiunda katika mwaka 1929 kuwa chama cha siasa, lengo lake likiwa kuwatayarisha Watanganyika kujitawala. Miongoni mwa hao waliokuwa wakiongoza harakati za kudai uhuru zilizokuwa zikiibuka walikuwa watoto wake watatu, Abdulwahid, Ally na Abbas.
Inapendeza wakati mwingine mtu akakaa na kufanya tafakuri juu ya hatima. Mwaka 1954, Abdulwahid akihatarisha kazi yake kama Market Master, haikumjia hata kidogo kuwa siku itafika historia ya kudai uhuru itaandikwa na jina lake halitahusishwa na hiki kipindi muhimu katika historia ya utaifa wa Tanganyika. Vilevile mtu anaweza kukisia hii leo Nyerere angekuwa wapi katika siasa za Tanganyika kama mwaka 1951 Chifu Kidaha angekubali lile pendekezo la Abdulwahid la kumuomba kuchukua uongozi na kuwa rais wa TAA. Au nini ungekuwa mustakbali wa Tanganyika kama Abdulwahid na wenzake katika uongozi wa ndani wa TAA wangekubali lile pendekezo la Ivor Bayldon la kuunda chama cha siasa cha mchanganyiko wa mataifa mbali mbali. Hii ilikuwa ujanja uliopangwa na serikali kuwatia wazalendo katika siasa hizo na hivyo kuwatoa katika msimamo wao wa kutaka utawala wa Waafrika walio wengi. Kile serikali ilichokuwa ikitafuta kilikuwa kuunganisha uongozi wa TAA na utawala wa machifu ndani ya Baraza la Kutunga Sheria na kuunda kile ambacho kingeweza kudhaniwa kama uwakilishi halali wa serikali na Gavana akiwa mkuu wa serikali. Jambo hili lingedhuru harakati za utawala wa Waafrika wa Tanganyika.
Suali la kujiuliza ni kuwa, 'Je Nyerere angeweza kuunda chama chake mwenyewe cha siasa ama ndani ya TAA au kutoka chanzo kingine chochote? Je, chama chake kingejenga msingi wa nguvu yake kwanza toka kwa wakulima katika sehemu za kwao huko Musoma au angebahatisha kujenga msingi wake wa siasa Dar es Salaam kwa msaada ule ule wa Waislam alioweza kuupata katika TANU kupitia kwa watu kama Abdulwahid na Ally Sykes, Dossa Aziz, Sheikh Suleiman Takadir na watu wengine miongoni mwa watu wa mjini?'
Juu ya kuundwa kwa TANU Iliffe ameandika kuwa:
...Si taarifa hata moja zilizochapishwa hata zile za wanasiasa kama S.A. Kandoro au E.B.M. Barongo zenye kufichua hasa kumbukumbu za serikali zilizopo zina umuhimu kiasi gani katika kueleza kuundwa kwa TANU. Rais Nyerere katu hajaeleza wazi hadharani kuhusu hilo... Tatizo gumu sana katika yote ni kutathmini nafasi ya Nyerere mwenyewe katika utaratibu wa mageuzi ya siasa, hususan kile kiwango ambacho alikuwa anapanga kuunda chama cha siasa au aliongozwa kwenye chama hicho na wanasiasa wa pale mjini ambao tayari walikuwa wanahusika katika harakati za siasa.
TANU, kama chama cha siasa, kimekuwa ndani ya fikra za Abdulwahid katika maisha yake na alifanya kazi kwa uthabiti kuhakikisha kuwa anaunda TANU kikiwa chama cha kuwaunganisha Watanganyika wote bila kujali kabila au dini zao.
Kuundwa kwa TANU kwake yeye kulikuwa jambo lisilo na shaka. Abdulwahid na uongozi wa TAA ulikuwa umepanda mbegu za umoja wa wananchi wa Tanganyika, ikiwa umoja huo uliangamizwa mara baada ya uhuru kupatikana waasisi wa umoja huo hawapaswi kulaumiwa. Maisha ya siasa ya Abdulwahid hayawezi kutenganishwa na historia ya TANU wala historia ya taifa la Tanganyika.
Hakuna mwanasiasa yeyote anaeweza kujilinganisha na marehemu Abdulwahid kwa yale aliyoyafanya wakati wa ukoloni. Abdulwahid alitoa mwelekeo kwa chama cha wafanyakazi, aliunda chama cha siasa na alimweka Nyerere kwenye kiti cha madaraka.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |