Waislamu Arusha zindukeni
Ndugu Mhariri
NI jambo la kushangaza kuona Waislamu wa mkoa huu wamesahau wajibu wao juu ya ahadi waliyoitoa kwa Mwenyezi Mungu (s.w.) kama anavyosema Allah "Na (kumbuka) Mola wako alipowaleta wanadamu kutoka migongoni mwa kizazi chao na akawashuhudishia juu ya nafsi zao (akawaambia) je, Mimi siye Mola wenu?" Wakasema: "Ndiye tunashuhudia ( kuwa wewe ndiye Mola wetu). Akawaambia Mwenyezi Mungu: Msije mkasema siku ya kiyama kuwa sisi tumeghafilika na hayo (hatuyajui)". (7:172).
"Au mkasema baba zetu ndiyo walioshirikisha zamani... (7:173)
Kinyume chake wamekuwa wakiuza ahadi hiyo kama anavyosema Mwenyezi Mungu: "Hakika wale wanaouza ahadi ya Mwenyezi Mungu na viapo vyao kwa ajili ya thamani ndogo ya kilimwengu hao ndio hawatakuwa na sehemu ya kheri katika akhera wala Mwenyezi Mungu hatasema nao (maneno mazuri) wala hatawatazama (jicho la rehma) siku hiyo ya kiyama wala hatawatakasa na madhambi yao, nao watapata adhabu iumizayo". (3:77).
Hivi tunang'ang'ania kumkumbatia mtu aliyewadhulumu haki aendeleze dhulma, kukandamiza na kuzuia kutekeleza yale waliyoamrishwa ikiwa ni pamoja na kutumia mwongozo wa Mwenyezi Mungu (s.w.).
Watoto wanaishi katika umaskini uliokithiri. Wengi wao wameishia darasa la saba au wengine hawakwenda shule kabisa. Watoto wa kike wakiwa wamezaliwa majumbani kwa wazazo wao au hata kuishi bila ndoa na wale wasiokuwa Waislamu.
Kutokana na kukithiri kwa umaskini Waislamu wengi mkoani hapa wamekuwa wakijishughulisha na dunia na kumsahau Mwenyezi Mungu (s.w.).
Enyi Waislamu Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'an: "Enyi mlioamini msiwafanye wasiri wenu watu wasiokuwa katika nyinyi hao hawataacha kukufanyieni ubaya wanayapenda yale yanayokudhuruni. (3:118).
Oh! Nyinyi mnawapenda maadui zenu hao hali hao hwakupendeni! .. (3:119). "Ikikupateni kheri huwasikitisha na ikikupateni shari wanafurahia ... (3:120).
Enyi Waislamu, sikilizeni redio juu ya dhulma wanazotendewa Waislamu wenzenu. Someni Qur'an mpate kujua dhulma mnazotendewa, rejea AN-NUUR la tarehe 7 - 10, Julai, mwaka huu uone Waislamu wanavyotumiwa na kuonewa. Si hayo tu, wangapi wameteswa kwa sababu ya dini yao? Wangapi wako jela kwa sababu ya dini yao?
Tembeeni masokoni na katika mitaa yenye maskini wengi ulize dini zao (wengi ni Waislamu).
Ngarenaro, Majengo na Unga Limited ni mifano hai juu ya kauli yangu. Fanyeni juhudi kuondoa dhulma hii.
Muislamu
Arusha
Ndugu Mhariri
NIMEPOKEA kwa masikitiko makubwa kitendo cha watendaji wa serikali ya awamu ya watu ya uwazi na ukweli tena inayojiita ya uadilifu ya kupiga marufuku kitabu cha Mwembechai Killings. Sielewi ni kitu gani kilichoogopwa kilichomo katika kitabu hicho.
Lakini nadhani uovu umefichuliwa sasa wanajitahidi kuuficha.
Nashukuru kuwa sasa sio jalada tu kitabu chote kipo kwenye INTERNET. Alhamdulillah!
Bakar Ali,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
KUMEKUWA na vijineno vya hapa na pale juu ya mustakabali wa nchi yetu baada ya uchaguzi hapo mwezi Oktoba.
Miongoni mwa vijineno hivyo ni kuwa wapinzani hawana miujiza ya kuboresha hali hii duni ya jamii yetu. Wanaosema hayo wanafikia hatua ya kuwakatisha tamaa wananchi kwa kusema kuwa hata wao wapinzani hawatofanya chochote. Mambo yatakuwa hivi hivi!
Maneno hayo ambayo yanatamkwa hata na viongozi wakubwa, yanapingana na historia yetu ya siasa katika kipindi cha takriban miongo minne.
Kila mtu anakiri kuwa kumekuwa na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kati ya awamu za uongozi wa nchi yetu.
Wakati hali ya kisiasa na kiuchumi ilikuwa mbaya na ngumu mno katika awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Nyerere, katika awamu ya pili ya Mzee Mwinyi, mambo yakabadilika. Pakawa na tahafifu ya kisiasa na kiuchumi.
Wakati wa awamu ya kwanza, kama mtu angekwambia kuwa Tanzania siku moja ingekuwa na vyama vingine zaidi ya CCM, vyombo vingine vya habari zaidi ya UHURU, Mzalendo, RTD, Daily News na Sunday News pamoja na uhuru wa kusema hata kuikosoa serikali, bila shaka ingekuwia vigumu kuamini.
Ungeshindwa pia kusadiki kama ungeambiwa siku moja watu binafsi wangemiliki vyombo vyao vya habari hasa hasa vituo vya Radio na Runinga. Na kwamba watu wangekuwa na majumba ya kifahari, magari yanayofanana na ya viongozi.
Ni wazi ungemuona jamaa anaota ndoto ya mchana kweupe au kachanganyikiwa. Yangewezekanaje mambo makubwa kama hayo ikiwa watu walikuwa hawana hata chakula, nguo wala viatu vya kuvaa?
Watu walilazimika kuamini kwa asilimia zote kuwa kama alishindwa Nyerere, nani angeweza? Tangu hapo watu wenyewe walijengewa hofu kuwa kama mzee huyo angeondoka madarakani kusingekuwa na Tanzania tena!
Lakini kumbe hayo yote yalikuwa mawazo finyu yaliyotokana na upeo finyu wa kuona mambo uliokomea katika mipaka ya Tanzania. Watanzania walikuwa wamefungwa katika gereza la kisiasa kiasi kwamba hawakuweza kuona dunia nyingine zaidi ya ile waliyoishi wao.
Baada ya Mzee Mwinyi kuleta mabadiliko, ndipo walipoamini kuwa kumbe avumae baharini si papa pekee, wapo wengine!
Leo hii Watanzania wanaishi katika dunia inayoshuhudia mabadiliko ya aina mbalimbali katika nchi kama hizi za wenzetu, vipi tena watu na akili zao waturudishe katika fikra za kale kuwa maadamu wao wameshindwa basi na wenzao hawatoweza! Propaganda!!!
Wananchi tunasema inawezekana kabisa, wakongwe kaeni pembeni muone!
Batuli Hussein,
128 Horton Hill
EPSOM - SURREY
KT 19 8 ST
Uingereza (UK).
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi ndogo nieleze machache kuhusiana na mdahalo wa BBC wa tarehe 6 mwezi wa nane.
Mdahalo ulikuwa kwa wagombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF na CCM, kwa Amani Abeid Karume na Seif Sharif Hamad.
Muulizaji mmoja alimtaka Bwana Amani atoe msimamo wake kuhusiana na Zanzibar kulazimishwa kujitoa OIC kwa ahadi ya Tanzania kujiunga yote badala yake.
Kwanza, Amani aliunga mkono kujitoa kwa Zanzibar kwa vile Zanzibar si "Sovereign State". Halafu akasema tayari Kamati iliyoundwa kufuatilia suala hilo, imeshatoa ripoti yake na kwamba Tanzania iko mbioni kujiunga OIC.
Ubabaishaji wa awali ni katika hili kamati ambayo kuundwa kwake hakuko wazi. Na ikiwa hiyo kamati kweli imeshatoa mapendekezo yake, basi si kweli kuwa Tanzania inatarajia kujiunga na OIC, kwa sababu Rais Mkapa mapema mwaka huu alisema kuhusu suala hili, ya kuwa hawezi kupuuza maoni ya wasiokuwa Waislamu.
Wakristo wengi wamekuwa wakifanya kampeni kwa njia mbalimbali kuona kuwa Tanzania haijiungi na OIC. Sasa Karume ana dalili zipi za Tanzaina kujiunga na umoja huo?
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |