KUTOKA MAGAZETI YA ZAMANI

Chama cha Waislamu kingali imara wala hakitishiki - Kwikima

BARAZA, Alhamisi Desemba 19, 1968

WATU pekee wanaoweza kusahihisha makosa katika chama cha Waislamu - East Africa Muslim Welfare Society - cha Tanzania, iwapo yapo kweli makosa, ni wanachama wa chama hiki, wala si mtu mwingine.

Katibu wa ile tume ya uchunguzi iliyoundwa hivi majuzi kusuluhisha mgogoro uliomo kwenye chama hiki, Bw. Mussa Kwikima, amesema majuzi katika makao makuu ya chama, mjini Dar es Salaam,

Alikuwa akijibu madai yaliyofanywa na chama kipya kilichoundwa majuzi - National Muslim Council of Tanzania - kwamba "chama cha Waislamu cha zamani kimekufa"

Chama cha Waislamu cha zamani kingaliko, na hakuna mtu anayeweza kukisitisha isipokuwa tu wanachama wake, sheria na serikali, lakini "sio watu binafsi" alidai Bw. Kwikima.

East Africa Muslim Society ni mali ya Waislamu wenyewe na asiye mwanachama wake hana cha kutamka kwa chama hiki ila wanachama wake tu, aliendelea mbele Bw. Kwikima.

Hata kama matawi yote 17 yaliyomo chamani yaliamua kujitenga na chama, haingejalisha kitu kwani kuwako kwa chama hakutegemei matawi hayo - bali ni wanachama wake - Waislamu wenyewe ndio wanaotegemewa, alisema.

Kulingana na katiba ya chama, hakiwezi kuvunjiliwa mbali isipokuwa tu mwandikishaji vyama akigundua kuwa chama kimeacha kutimiza wajibu wake, Bw. Kwikima alisema.

Pia chaweza kuvunjiliwa mbali kwa amri ya Rais. Lakini chama chenyewe kingali imara na chaendesha wajibu wake sawa, alimaliza Bw. Kwikima.


Msako wa Mini-skati tayari

BARAZA, Alhamisi Desemba 19, 1968

INGAWA vijana wengine wamo kwenye maandamano kupinga upigaji marufuku wa mavazi mafupi mjini Dar es Salaam, mipango yasonga mbele kupambana vikali na mavazi haya, nywele za kubandika, rangi za midomo, dawa za kugeuza ngozi, suruale za kubana hata za kucha ndefu, kokote nchini Tanzania.

Mwenyekiti wa TANU Yusi Ligi, Bw. Sijaona, majuzi aliuambia mkutano wa hadhara mjini Arusha.

Alisema mipango kamili ingetolewa kwa taifa mapema wiki hii. Vijana wa TANU Yusi Ligi wenyewe ndiyo wamepewa uwezo wa kupambana na jambo hili. Wajulikana kama "Operation vijana".

Akitilia mkazo jambo hili, Bw. Sijaona aliwatoa makosa wale wenye "mafikira ya kigeni" wanaong'ang'ania mambo haya kwamba sheria ya kupiga marufuku mini skati, ipitishwe kwanza bungeni.

Bunge lilikuwa na kazi ngumu za heshma, si kushughulikia mambo ya upuuzi kama haya, alidai.

Akielezea zile nywele za bandia kama "nywele za wafu", Bw. Sijaona alisema kuwa hizo zilikuwa hila za wabeberu kutaka kumaliza jadi na utamaduni wa Kiafrika.

"Katika nchi zilizoanzisha mini skati, wanaume walikuwa wakioa wanaume wenzao kanisani, kondoo kugeuzwa wanaume kuingizwa nchini kugeuzwa wanaume", jambo ambalo wabeberu walitaka kuingiza nchini Tanzania, alidai Bw. Sijaona.

Aliwahakikishia wananchi wapatao 6,000 kuwa kwa mara nyingine wabeberu wangeshindwa tena kwenye shughuli zao kutaka kuingiza sumu katika Tanzania.

Alitumaini kwamba vijana wote Watanzania wangekuwa macho kupambana na jambo hili kiume.


Kenyatta kiongozi shujaa Afrika - Swai

BARAZA, Alhamisi Desemba 19, 1968

RAIS KENYATTA wa Kenya, majuzi alitajwa na Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia mipango ya upimaji na kazi za starehe, Bw. A.Z. Nsilo Swai kama kiongozi Mwafrika shupavu.

Bw. Swai alisema hayo alipohutubia wageni kwenye karamu iliyotayarishwa mjini Arusha, kusherehekea mwaka wa tano tangu Kenya kujinyakulia uhuru wake, mwishoni mwa wiki.

Alisema kuwa Afrika ilikuwa na bahati kubwa kuwa na kiongozi mkubwa kama Rais Kenyatta, akiongoza si mashauri ya Wakenya tu bali kwa mipango yote ya Mwafrika.

Alikumbusha wasikilizaji wake kuwa yeye akiwa mmojawapo wa wanachama wa Kilimanjaro Citizens' Union yapata miaka 22 iliyopita, chama chake kilikuwa mara kwa mara kikimwendea Mzee Kenyatta kwa mashauri fulani.

Akimjulisha Bw. Nsilo kwa wageni kama mgeni wa heshima katika karamu hiyo, Waziri wa Jumuiya anayeshughulikia mipango ya Hazina na Utawala, Bw. Odero Jowi, alisema kuwa Rais Kenyatta angekumbukwa katika historia kama shujaa, milele.

Watu wengine walifikiria Kenya ingekuwa na matata mara tu baada ya uhuru, lakini kwa ajili ya uongozi bora wa Rais Kenyatta, nchi ilikuwa ikijipatia nguvu mwaka baada ya mwingine, alisema.

Bw. Odero - Jowi aliwaombea maisha marefu Marais watatu wa Afrika Mashariki ili kubakia uongozini zaidi.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook