RIWAYA

Joka la Mdimu - 19


DAKTA MIKWALA

HOSPITALI kuu ya Mindule, zamani Prince Edward Hospital, ilikuwa na mchanganyiko wa majengo ya zamani na machache mno ya sasa. Yalijengwa katika uwanja nje kidogo ya jiji. Mandhari yake hayakuvutia.

Kwanza dhahiri aliyechagua mahali hapa hakufikiria ya usoni. Majengo yake yalibakiza nafasi ndogo ya upanuzi. Huku na huku kuizunguka hospitali hiyo kulikuwa na nyumba za kuishi watu. Wazo la kuihamisha hospitali hiyo lisingeyumkinika kutokana na gharama kuu za ujenzi.

Hivyo nyumba zote zilizonyekwa katika nafasi ndogo iliyokuwepo baina ya majengo ya zamani. Miti kadha mikubwa iliyoongezea haiba ya mahali hapo na kufanya kivuli cha wagonjwa, wafanyakazi na wale waliokuja kuwatembelea, ilikatwa kupata nafasi ya kujenga majengo mapya. Bustani zilizokuwa zikipendeza macho nazo zililimwa. Pote pakawa ni msongamano wa majumba. Hapakumvutia daktari, muuguzi, karani, wala mtazamaji wagonjwa. Kwa wale wagonjwa waliokuwa nafuu walichushwa napo na kutapia wapewe ruhusa japo hajawapona barabara.

Kulikuwa na wodi nne au tano mojawapo ikiwa ni ya wagonjwa waliopata ajali. Katika sehemu ya chini ya jengo hilo lililokuwa ghorofa tatu alilala Cheche. Baada ya miezi miwili kupita tangu apate ajali kule kijijini alizidi kudhoofu, akaanza kuwa mweupe. Muda wote alilala chali juu ya kitanda kilichowekwa bao, isipokuwa mara chache mno aligeuzwa kidogo na mwuuguzi. Mazowea yakuwa na wazazi, babu na bibi yake yalimtia unyonge usio mithilika katika upeke huu. Aliwakumbuka ndugu na rafiki zake kule shuleni. Siku za mwanzo wingu la machozi lilimjia katikati na fikra hizo likasonga ndani ya mboni zake na kububujika machozi moto yaliyoweka michirizi mashavuni na kifuani.

Saa kumi na dakika tano, mara tu baada ya lango kuu la hospitali kufunguliwa, Tino na mkewe aliyeshika mfuko uliokuwa na chakula walifika mbele ya kitanda cha Cheche aliyekuwa amekaza macho darini. Hakuyatilia maanani mazungumzo yote yaliyopita baina ya wagonjwa wenye nafuu. Hatua zilipokaribia kitandani aligeuza kichwa. Kuwaona tu wazazi wake alipindua tena kichwa kuangalia darini. Machozi yalijikusanya tena. Kadiri alivyoyazuia akashindwa, ikawa kama ndiyo anayachapuza yamiminike.

"Usilie baba! Utajiumiza", Tino alimwinamia mwanawe akasema huku donge likimpanda na kumsonga kooni. Mkewe alisogea, akaweka mfuko juu ya kimeza, akamwuliza mwanawe, "Walilia nini mwanangu?"

"Naogopa", Cheche alijibu. Wote walikaa kimya.

Tangu azaliwe, Cheche alikuwa hajaona mtu aliyefariki, jana tu, mtoto mmoja karibu na umri wake aliyegongwa na gari na kulazwa karibu naye, alifariki.

"Nataka kurudi nyumbani", alisisitiza katikati ya kwikwi.

"Lakini ngoja upate nafuu".

"Mimi siponi baba!" alisema akilia zaidi. Kimya kizito kilipita. Maneno yake yalipenya katika chembe cha mama yake mithili ya mkuki wa moto. Akaondoka kuelekea dirishani. Huko alikaa kimya akitazama majengo na watu waliokuwa wakipita. Alifikiria mimba ya Cheche, matatizo aliyoyapata na malezi mazuri ya mwanawe, mcheshi, rahimu. Machozi yalimlengalenga, akashindwa kuyamiliki, yakambubujika.

Tino alimaizi nini linatokea kwa mkewe. Kwa muda akapigwa na mzimbao. Maana kuwabembeleza wala kusingeridhisha uchungu wao. Isitoshe naye angechanua jeraha lake la siku zote tangu kuumia kwa mwanawe.

Watu walipita kuwaangalia wagonjwa wao, wakaingia na kutoka. Tino aliwaona kama vivuli tu asipate hata moja ya yale waliyoyazungumza. Uzito ulimlemea moyoni na mwilini akajipweteka katika mfumbati wa kitanda cha mwanaye.

Nusu saa nzima ilipita.

"Mpe chakula mtoto basi", Tino alimtia moyo mkewe.

Alitumia upeto wa khanga akayafuta vizuri machozi yake, akamlisha mwanawe kadiri alivyoweza kula. Kama kawaida yao walibaki hapo hadi kengele ya kuwaondoa waliokuja kuwaona wagonjwa ilipogongwa. Hata hivyo mioyo yao mizito iliwavisha kekee za miguu wasithubutu kutembea.

"Saa imekwisha", waliambiwa na muuguzi aliyejua uchungu wa mwana. "Muacheni rafiki yangu nitazungumza naye", aliendelea.

Ajabu namna maneno yale yalivyokuwa na athari! Ghafla Tino na mkewe walipata nguvu na imani kuwa Cheche yumo mikononi mwa mtu maridhia. Wakaaga na kutoka kimya kimya.

Siku zilikatika, afya ya Tino ikaanza kupungua kwa kasi zaidi na sura yake kufifia. Usiku alijitupa kitandani mapema kuutafuta usingizi japo apunguze fikra zilizokuwa zikisongana na kukipasua kichwa chake. Lakini usingizi ulimtupa mkono ukasimama mbali naye kumdhihaki. Siku nyingine alipata usingizi mapema, kufika usiku wa manane ukakatika lama majogoo ya alfajiri. Alibaki kitandani akijipiga mikambi huku na kule huku akiwa mwangalifu asimwamshe mkewe. Usingizi mchache alioweza kuupata ulizengwa na njozi mbaya za jinamizi. Alipiga kelele, na bila kujua alimwamsha mkewe ambaye alimuuliza kulikoni. Nimeota, lilikuwa ndilo jibu lake, kisha alijikaza kimya kutafakari maana ya njozi zile nuksi.

Asubuhi aliamka dhaifu, macho machungu. Upesi akachukua chai ndani ya chupa kukimbilia vituo vya mabasi hadi hospitalini. Hofu ikimlemea: Vipi mwanangu ameamkaje? Kila hatua aliyopiga kutoka pale langoni hadi wodini kwa Cheche ilichemsha matumbo yake, kumpokonya ujasiri wake, akabaki kama atembeaye hewani. Si mara mbili si mara tatu alipigana vikumbo na watu akasepetuka. Mara nne nusura agongwe na gari. Ama kweli nimekwisha, aliwaza. Maana zamani wachache wangeweza kumpamia bila kusepetuka.

Kutoka hospitali alirejea nyumbani na mawazo yale yale: Mwanangu atapona? Atakufa huyu! Je, nibaki namuangalia tu hivi hivi. Hivyo serikali imeshindwa kumsaidia? Aliwaza kauli ya Dakta Denis Kaya kuwa atapona akipelekwa Glasgow, sio hapa. Sasa, kwa vipi asipelekwe Glasgow? Tafuta mtu unayemjua akufanyie mipango, ndivyo alivyoambiwa. Lakini ni mtu gani huyo?

Kadiri alivyopiga bongo, ndivyo rasi ilivyomdawiri. Hamu ya kula ilimtoka. Badala ya kilo ya ugali alikula nusu kilo tu. Unyonge wa mwili uliathiri utendaji wa kazi yake. Hakumudu tena kukokota kwama lililosheheni mizigo barabara. Mwendo wake ulikuwa si wa kasi tena. Pumzi zilimsonga upesi, akachoka mapema. Hakuwa na baraza na mtu isipokuwa wenzake walimfuata nyumbani kumuulizia hali ya mtoto wake. Jinja Maloni, Amani walikwenda hospitali kumuangalia Cheche kila mara.

Siku moja kiasi cha saa mbili na nusu Amani akapiga hodi nyumbani kwa Tino.

"Karibu shemeji!" mkewe Tino alijibu kwa kuitambua sauti ile.

"Mmeshindaje?"

"Hivyo hivyo tu shemeji, hatujambo", alijibu.

"Huyu bwana nimekumta?"

"Amepumzika ndani".

"Wasemaje Amani!" Tino alijibu huku akishuka kitandani kuelekea pale sebuleni.

"Mbona umelala saa hizi?"

"Aa! najipumzisha tu".

"Sawa!" alijibu huku wakiketi kwenye makochi pale sebuleni.

"Habari ya kutwa?"

"Nzuri!"

"Leo sikuwahi kupita hospitalini. Wamuonaje Cheche?"

Kimya! Halafu Tino alianza kuzungumza akimtazama rafiki yake.

"Tena nilikuwa nakusubiri unipe mawazo".

"Huyu mtoto hawezi kuponea hapa", Tino alisema kwa huzuni kubwa.

"Eee!" Amani alikaa vizuri.

"Kwanini?"

"Hakuna matibabu ya kufaa".

Amani aliangalia chini, akichezea funguo za gari lake kutafakari maneno yale yaliyozama akilini mwake, akasema, "Sasa umefikiri nini, maana ugonjwa huu sio wa miti shamba tukaseme tumtoe mtoto hospitali".

"Siyo hivyo!" Tino alijibu akaendelea.

"Nimekumbuka ushauri wa yule daktari wa nyumbani, unakumbuka?"

"Kwenda Glasgow?"

"Eee!"

Amani alifikiri tena, akasema, "lakini lazima tupate daktari wa kuamua hivyo kwanza, halafu pili serikali ikubali kulipia fedha za matibabu huko Ulaya. Yote yao si rahisi".

Badala ya kukatishwa tamaa na yale maneno ya mwisho akasisitiza, "Naona tujaribu tuone tutashindwa wapi!"

Amani aliitikia kwa kichwa wakaketi tena kimya.

"Wewe humjui daktari anayeweza kutusaidia?" Tino aliinua macho kumuuliza sahibu yake.

"Nafahamiana na wengi, lakini baadhi yao hawahusiki na mambo ya mifupa. Sharti tumpate daktari anayeweza kutoa ushauri ukakubalika.

"Ni kweli!"

Amani alifikiri tena kwa muda mrefu kabla hajasema kwa furaha huku akimpiga Tino pajani kufurahia ugunduzi huu wake. "Ah! wewe pia unamkumbuka yule daktari aliyenitibu nilipovunjika mguu katika ile eksidenti".

"Eee! Ndiyo!" Tino alivuta na kuzikusanya pamoja fahamu zake.

"Namkumbuka", akaangaza, "Aitwa nani vile?"

"Hata mimi jina lake limenitoka".

"Tena jina lake la mzaha hivi".

"Nani! Nani! Nani!" alijipiga piga pajani na usoni kwa gao la mkono wake wa kulia huku funguo zake zikilia che che che ziliposukumwa mbele na nyuma.

"Ewaa! hatimaye akasema kwa furaha.

"Mikwala!"

"Ndiyo Dakta Mikwala!"

Ufumbuzi huo ulileta kicheko cha kweli moyoni na kinywani kwa Tino muda mrefu. Ama kweli kicheko husuuza moyo.

Waliendelea kucheka kwa pamoja kwa muda kisha wakarejea tena katika tatizo lao.

"Sasa mtafute mpange!"

"Hiyo kazi niachie miye! Kesho nitakupa jawabu. Labwa awe hayupo".

"Tuombe Mungu".

"Haya! Ngoja niende!" Amani alisimama.

"Ngojea chakula shemeji!" Mkewe Tino aliingalia.

"Mwenzio anisubiri!" Amani alitania.

"Leo zamu ya mke mkubwa", mkewe Tino alitania kwa dhati. Naye, pia, utani huo uliamsha moyo wake na uchovu wa majonzi ya muda mrefu.

Kwa muda wakaongea namna ya kumnusuru mtoto wao.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook