Maoni Yetu

Rithishaneni mali za ukoo sio uongozi, huo ni usultani

KUNA kisa cha dhihaka kinachohusu siasa. Kisa hicho kinaelezea hoja za kuombea kura kwenye kampeni za mgombea Ubunge aliyekuwa akitaka nafasi hiyo kwa mara nyingine tena.

Katika kampeni hizo palikuwepo na mgombea mwingine aliyejitokeza kwa mara ya kwanza kumpinga mgombea aliyekuwa akimaliza kipindi chake cha Ubunge.

Mgombea yule mpya aliwasihi wapiga kura wamchague yeye badala ya yule wa zamani kwa hoja kwamba tangu achaguliwe hakuna maendeleo yoyote aliyowaletea. Kwamba wananchi walikuwa bado wanakabiliwa na shida za ukosefu wa zahanati, shule, maji safi, barabara na ajira wala.Zaidi hapakuwa na msaada wowote wa kuwaendeleza wakulima na wafanyabiashara ndogondogo.

Yule mgombea mpya aliwaambia wapiga kura:

"Msimchague huyu. Hakuna alichokifanya tangu mumchague, isipokuwa kujinufaisha yeye binafsi

na familia yake.

"Kajinunulia ‘shangingi;, kajijengea jumba jipya, kaendeleza mashamba na biashara zake. "Kapeleka watoto wake kusoma Marekani na kuwaacha watoto wenu wakitaabika.

Yeye na familia yake wamekuwa wakitibiwa Uingereza, wakati nyie mliompigia kura hamna uwezo wa kutibu hata malaria", alisema Bwana huyo kwa mujibu wa hicho kisa, na kumalizia, "huyu hawafai kabisa, msimchague".

Kisa hicho kinaendelea kueleza kwamba na yule mgombea aliyekuja kuomba kura kwa mara nyingine alisimama na kujibu:

"Ndugu wananchi, aliyoyasema mwenzangu ni kweli". "Ilibidi kwanza nijiweke sawasawa kwa kujiendeleza mimi na familia yangu".

Kisa hiki huhadithiwa na kuendelea kwa namna mbalimbali kutegemea na mahali, wakati na watu wanaohadithia.

Lakini kuna mafunzo makubwa katika kisa hiki. Mafunzo hayo ni kwamba wapo watu miongoni mwa wale wanaopewa dhamana ya uongozi na wananchi wanaodhani kuwa ni haki yao kutumia nguvu za wananchi kwa ajili ya kujiendeleza wao na familia zao.

Viongozi wa aina hii, ni miongoni mwa wale wanaotafsiri kauli za wananchi wanazozitoa katika ahadi za kujitolea kwa hali na mali kuiendeleza jamii, umma, jimbo au nchi yao ili "watoto na wajukuu zao wasijepata tabu". Wao huelewa vingine. Hivyo wanapokabidhiwa madaraka na wananchi kama vile madaraka ya Ubunge hudhani kuwa ile ahadi na azma ya kushughulikia mandeleo ili "watoto na wajukuu" wasije kupata tabu katika maisha yao, wao huona watoto wao na wajukuu zao waliowazaa wenyewe na sio wale ambao ni sehemu ya wananchi katika jimbo au nchi.

Viongozi wa aina hii ni miongoni mwa wale wasioona haya wala vibaya kutumia madaraka yatokanayo na kura za wananchi, kwa manufaa ya watoto wao, wajukuu zao, shemeji zao, ndugu na jamaa zao kifamilia.

Hawa hujifanya hawajui na hata wakisutwa huwa hawajali kwamba mishahara yao wanayopata zaidi ya milioni kwa mwezi, marupurupu ya vikao, marupurupu ya kamati ndogo, gharama za usafiri na kadhalika ambazo nazo kwa ujumla pengine huzidi milioni kwa mwezi, vinatokana na jasho la wananchi waliowachagua.

Wananchi hutoa malipo hayo kwa njia mbalimbali zikiwemo kodi, michango na kadhalika.

Wakati wananchi wanaweza wakaachwa bila ya maendeleo yoyote kwa miaka mitano, mbunge waliyemchagua anaweza akapata zaidi ya milioni sitini (60,000,000) toka kwenye jumla ya mshahara na marupurupu ya miaka mitano. Na mwisho akaondoka na kiinua mgongo cha shilingi milioni ishirini (20,000,000).

Katika mazingira kama hayo, laiti wananchi wangelikuwa na kauli yenye uwezo wa maamuzi ya muelekeo ya mifumo ya kisiasa, pengine wangelichukua maamuzi makubwa sana ili kujilinda na ubadhirifu wa viongozi wapotofu wanaodhani kuwa maendeleo ya baadaye yenye kuwanufaisha watoto na wajukuu wa jimbo au nchi maana yake ni ya watoto wao na wajukuu zao, binafsi wananchi hao bila shaka wangeliamua badala ya kuchagua mbunge wangeamua kuchukua wenyewe zile milioni zao zaidi ya 80.

Kwa kiasi hicho, wangeliweza kwa kipindi hicho cha miaka mitano kuchimba visima, kujenga zahanati, shule na au kugharamia mambo mengine ya maendeleo yao.

Pamoja na kisa tulichokitaja, tumeyasema hayo kwa kuwa wananchi kadhaa katika maeneo mbalimbali nchini wameanza kujadili kwa uchungu na huzuni mtindo wanaodai umejitokeza wa kupelekewa kwenye majimbo yao watoto wa ‘wakubwa’, mashemeji, ndugu, jamaa na marafiki wa baadhi ya ‘vigogo’ nchini ili wawape kura za Ubunge na Udiwani.

Wananchi hao ambao baadhi yao wameongea na AN-NUUR, katika maoni yao wameonesha kusikitishwa na kitendo hicho. Wananchi hao wameonesha pia kusikitishwa zaidi na kile walichodai kwamba baadhi ya hao walioletwa wala si miongoni mwa vijana waliozaliwa na kukulia kwenye majimbo hayo. Tena inasemekana wazee wao walijaribu kuwapeleka huko walikozaliwa wakakataliwa.

Katika hali hiyo hatuna budi nasi kutoa maoni yetu kwamba kilio cha wananchi hao kisipuuzwe, ingawa wananchi wenyewe bado wana uwezo mkubwa wa kuwakataa wagombea hao kwa kuwanyima kura.

Tunasema masikitiko ya wananchi hao yasipuuzwe kwa sababu yameonesha mwamko wa kuhoji maswali mengi kuhusu maendeleo yao, na ya majimbo yao.

Maana iweje baada ya miaka 40 ya uhuru baadhi ya majimbo nchini yasiwe na wagombea miongoni mwa watoto wao wenye uwezo wa kielimu, hali, mali na uongozi bora mpaka wapelekewe nje ya majimbo yao?

Ni vipi wakubwa hao waweze kusimama mbele ya wananchi kisha kuwasimamisha watoto wao ambao hawakuzaliwa wala kukulia maeneo hayo na kuwatambulisha kwa kusema "nimewaletea kijana wenu", pasipo kujisikia vibaya?

Na tujaalie kwamba watoto wa wakubwa hao wanasifa ya kuwa na elimu ya juu. Lakini elimu hiyo ya juu ni ipi ambayo wakubwa hao walishindwa kuwasomesha watoto wa wakulima na wafanyakazi katika jimbo hilo ila mwanae wa kumzaa yeye tu?

Kwa ‘mkubwa’ yeyote mwenye uchungu na mwenye kuguswa na maendeleo ya wananchi, hawezi kwa mfano, kukaa madarakani kwa kiasi hata cha miaka kumi (10) tu, lakini ashindwe kupeleka maendeleo katika jimbo, maendeleo ya kutoa elimu japo kwa kijana mmoja tu hadi kufikia Chuo Kikuu isipokuwa kwa mtoto aliyemzaa mwenyewe!

Kama hali ndiyo hiyo, kuna hatari ya kila anayepewa uongozi kuendeleza familia yake na baadaye kumpeleka mwanaye mbele ya wananchi na kuwaambia: "huyu hapa kijana, mpeni kura awaongoze".

Tunawaunga mkono wananchi wanaolipinga hilo. Na tunasema bora wachukue uamuzi wautakao maana utasaidia kuondoa dhana ya wale wanaofikiri kuwa watarithishana wapiga kura kama vile wanavyo rithishana mali katika familia zao.

Kuliachia hilo ni sawa na kuruhusu Usultani mambo leo.

Ni kati ya miaka 4-5 kwa kijana aliyemaliza ‘form IV’ kuweza kumaliza shahada ya Chuo Kikuu. Na ni miaka 7-9 kuweza kupata shahada ya juu (PhD). Iweje ‘mkubwa’ awepo madarakani ashindwe kutuonesha kijana mmoja tu aliyemuwezesha kuendelea hivyo kielimu katika jimbo lake?

Tungependa kutumia nafasi hii kutoa pongezi kwa mkongwe mmoja wa siasa nchini ambaye amewahi kushika nyadhifa nyingi za uongozi wa nchi.

Mkongwe huyu ametangaza kustaafu rasmi kugombea Ubunge. Na inasemekana aliwaita wazee wa jimboni kwake na kuwatajia majina ya vijana zaidi ya watatu wenye elimu ya chuo kuuu na kati yao wamo Maprofesa. Vijana wote hao inasemekana ni wazaliwa na waliokulia kwenye jimbo hilo hilo.Watoto wa wakulima wa jimbo hilo na wala siyo wa kuzaa mwenyewe.

Wazee walimshukuru na kupendekeza mmoja wao ambaye ni Profesa kuchukua nafasi aliyoiacha. Hawa ndio wakubwa, wakongwe na vigogo wa kuigwa.

Mkongwe huyu si sawa na yule anayepeleka ‘kimini bus’ kijijini kuwachukua wazee hadi nyumbani kwake kisha kuwakaribisha chai na keki, pilau na mapochopocho mengine kisha akawakabidhi ‘kijana wao’ ambaye wanamjua na walipomuuliza akasema "huyu ni wa kuzaa mwenyewe... shemeji yangu... mtoto wa shangazi na kadhalika".

Hawa hawafai. Hawa ni sawa na wale matajiri wa mashamba na viwanda ambao huwapunja malipo wafanyakazi wao. Lakini wakati wa kutaka Ubunge hujifanya wema wa kutoa mikopo na takrima ili wao au watoto wao wapate kuchaguliwa.

Watanzania tayari wameishaanza kulalamikia matabaka yaliyojitokeza ya madhalimu na wadhulumiwa.Hawawezi kuyaruhusu na yale ya wanafiki wasiowatakia kheri watoto wa wenzao ila watoto wao tu na nafsi zao.

Hawa ni hatari, maana na wao pia ni miongoni mwa madhalimu tena wa kiwango cha juu. Kwa kuwa hawa wanaujua ukweli wa ndugu zao kuhitaji maendeleo lakini hawawapi japo uwezo wa kufanya hivyo wanao, kwa sababu wanataka ‘ndugu zao’ waendelee kuwa vibarua na walinzi wa mashamba yao ili watoto wao wapate kuendelea na kurithi uongozi toka kwa baba zao. Huu ni usultani mamboleo.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook