Hakuna Wabara wanaochomewa nyumba Zanzibar -Prof. Lipumba

• Huo ni uchochezi
• Wanaodhibitiwa ni mamluki

Na Mwandishi Wetu

Mgombea urais kupitia chama cha CUF Prof. Ibrahim Lipumba,amesema, ,taarifa kuwa kuna watu wa bara wanaochomewa nyumba zao huko Zanzibar, ni propanda za kichochezi.

Amesema taarifa kama hizo, zinachochea uhasama na chuki kati ya watu wa Bara na Zanzibar ,jambo ambalo ni la hatari.

Akiongea na waandishi wa habari juzi,Prof. Lipumba amewataka waandishi wa habari kutozishabikia taarifa hizo bali wachukue tahadhari na kufanya uchunguzi kabla ya kuparamia habari kama hizo.

"Nendeni mfanye uchunguzi muione hiyo nyumba mthibitishe kweli imechomwa na kwamba imechomwa kwavile mwenyewe ni wa kutoka bara"aliwaasa waandishi wa habari.

Prof. amesema,linalotokea Zanzibar sasa ni kuwadhibiti watu wanaodaiwa kupelekwa visiwani humo kupiga kura wakati wao si wapiga kura halali wa visiwani.Amesema chama chake kimegundua njama hizo na kishawakilisha malalamiko rasmi kwa vyombo mbalimbali kuhusiana na udanganyifu huo.

Lipumba amesema,lengo lao ni kuona uchaguzi unakuwa huru na wa haki.Hata hivyo akasema kuwa,kumekuwa na vitendo vinavyofanywa na vyombo vya dola ambavyo vinaashiria dhamira ya kuvurugwa uchaguzi.

Akitoa mfano amesema,masheha wamekuwa wakiwazuilia wapiga kura halali kujiandikisha na wakati huo huo polisi wakiwa wanawapiga na kuwaweka ndani wanachama wa CUF.Amesema, wanachama wapatao 126 wamewekwa ndani wakiwemo wawakilishi na wale walioteuliwa kugombea ubunge mwaka huu.

Amesema, jambo la kutisha zaidi wanajeshi wengi wamekuwa wakipelekwa Zanzibar pamoja na vifaa vya kijeshi jambo ambalo amesema linawatisha wananchi.Amemuomba Rais Mkapa kuingilia kati kusitisha hali hiyo inayotishia kuvuruga uchaguzi usiwe wa haki na huru.

Wakati huo huo, Rais Benjamin Mkapa amewaonya watu wanaopita wakinunua shahada za kupigia kura.

Ametoa onyo hilo jana wakati akilihutubia Taifa kupitia Radio na televisheni.

Amesema kununua shahada ni kuzuia haki ya mtu ya kidemokrasia kuchagua viongozi watakaoliongoza Taifa lake.

Katika hotuba hiyo Rais pia aliwataka Wananchi wajiandikishe kwa wingi ili waweze kutumia haki hiyo ya kidemikrasia kuchagua viongozi wanaowataka.

Hata hivyo msisitizo wa rais juu ya kujiandikisha kupiga kura umekuja wakati ambapo kuna taarifa Masheha na Waandikishaji mjini Zanzibar wamekuwa wakiwazuia wananchi kujiandikisha kushiriki uchaguzi huo.


Kiwewe cha uchaguzi Chalikumba jiji Dar
Katika hali iliyoelezwa kuwa ni ya kuwa na wasiwasi na uchaguzi,baadhi ya wanachama wa CCM wametuhumiwa kuwatisha wananchi wanaowadhania wanauwezo wa kuwashawishi watu wasiipigie kura.CCM.

Mkazi mmoja wa Sinza jijini ameeleza kuwa,aliendewa na kundi la watu ambao walimtisha wakidai kuwa iwapo ataiangusha tena CCM kama alivyoiangusha wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa watamshughulikia.

"Hakuna cha ujirani safari hii",amedai Bwana huyo kuambiwa na jirani zake ambao ni washabiki wa CCM.

Aidha amedai,mtangazaji mmoja wa televisheni moja jijini,alimjia na kumtahadharisha kuwa ameona jina lake katika orodha ya watu wanaoelezwa kuwa ni hatari wanaotakiwa washughulikiwe.

Amedai,mtangazaji huyo ambaye ni jirani yake, alimtahadharisha aachane na mambo ya CUF.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi mapema wiki hii, Bwana Hassan amesema kuwa ameanza kupata vitisho hivyo baada ya kuwa imara katika kusimamia zoezi la uandikishaji wapiga kura.

Amesema, katika uchaguzi wa serikali za mitaa walisimama imara ambapo CUF ilipata ushindi na kuchukua uongozi katika enea la Sinza Mori.

Katika eneo la Ilala Mchikichini,imeelezwa kuwa kutokana na kuwa na wasiwasi,viongozi wa CCM wamekuwa wakijaribu kuwaorodhesha waliojiandikisha kupiga kura na kujaribu kuona ni wangapi wataipigia CCM.

Taarifa zaidi zimeeleza kuwa, viongozi hao wameshinikizwa kutoka ngazi za juu za chama kila mmoja awe na orodha ya watu wasiopungua 50 ambao wataipigia kura CCM.

Ilikutimiza agizo hilo, imeelezwa kuwa viongozi hao wamekuwa wakiorodhesha majina ya wapiga kura hata kama sio wana CCM.

MWENYEKITI wa serikali ya Mtaa wa Msimbazi Bondeni, Mzee Ngallawa amelalamikiwa na wakazi wake kuwa miongoni mwa watu wanaoendesha sensa isiyo rasmi ili kujua idadi ya waliojiandikisha kupiga kura kwa manufaa ya chama chake cha Mapinduzi (CCM).

Inadaiwa kuwa sensa hiyo iliyofanywa wiki iliyopita na Mwenyekiti huyo, ilifanywa hivyo ili atathimini idadi ya wanachama wake wa CCM ambao imedaiwa kuwa wachache mtaani hapo.

Wakizungumza kwenye ofisi ya gazeti hili baadhi, ya wakazi hao waliofanyiwa sensa, ambayo ilidaiwa na kiongozi huyo kuwa iliagizwa na serikali kuu, walisema kuwa katika sensa hiyo namba zao za shahada za kupigia kura zilichukuliwa .

Wakazi Bi Zainabu Mohamed mwenye shahada namba 09048054 na Shaabani Ngwalera naye shahada yake ina namba 09048009 walisema sensa hiyo ilifanywa nyumba hadi nyumba na Mwenyekiti huyo pamoja na watu wa CCM.

Mmoja wa wajumbe wa serikali ya mtaa huo Bwana Abdallah Seif alithibitisha kufanyika kwa sensa hiyo, lakini alisema ilifanywa na Mwenyekiti wake bila ya wao wajumbe kuhusishwa na wala hawakuelezwa ilikuwa na lengo gani .

"Ni kweli sensa hii ilifanywa na kuna baadhi ya wakazi walitufuata sisi wajumbe kutuuliza kama kweli kuna sensa hii wakati wa kuandikisha kupiga kura na kuwakatalia", alisema mjumbe huyo.

Mwandishi wa habari hizi alipomfuata Mwenyekiti huyo wa Mtaa, Mzee Ngallawa ili kuthibitisha au kukanusha tuhuma hizo, hakuwa tayari kutoa maelezo.


Kinyang’anyiro cha ubunge Dar:
Mnyanga kumvaa Idi Simba Jimbo la Ilala

Na. Mwandishi wetu

Kigogo wa CCM ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ilala na mgombea wa chama hicho jimbo hilo katika uchaguzi mkuu ujao Mzee Idi Simba anakwaana na kijana wa CUF bwana Ahmad Omar Mnyanga katika mchuano ambao huenda ukawa na upinzani mkali.

Mkongwe huyo wa CCM ambaye katika uchaguzi wa mwaka 1995 alipita bila ya jasho jingi, imeelezwa itabidi afanye kazi ya ziada kuweza kutetea kiti hicho.

Upinzani mkubwa baina ya wagombea hao wa CUF na CCM unatokana na umaarufu wao binafsi na vyama vyao katika jimbo hilo.

Kwa upande wake Bwana Idi Simba imeelezwa kushindwa kutekelezwa kwa ahadi alizozitoa kwa baadhi ya "maalwatan" wa jimbo hilo katika maeneo ya Kariakoo na Ilala huenda kumedhoofisha ngome yake mwaka huu.

Hata hivyo bado inaonekana mizizi yake bado ipo japo si kwa kulinganisha na uchaguzi uliopita ambayo huenda ikawapa wakati mgumu wapinzani.

Mgombea wa CUF bwana Ahmad Mnyanga amekuwa gumzo kubwa miongoni mwa wapiga kura wa jimbo hilo hasa kutokana umaarufu wa chama chake miongoni mwa wazee na vijana wa jimbo hilo.

Katika Jimbo la Kawe, baada ya kumalizika "mizengwe" na "kushushuana" ndani ya CCM, mbunge aliyemaliza muda wake jimboni humo Bwana Adamjee ambaye awali alishinda kura za maoni ametupiliwa mbali, badala yake Kamati Kuu ya CCM imemsimamisha bibi Ritha Mlaki kuwa mgombea wa chama hicho jimbo hilo.

Bibi Ritha Mlaki anapambana na kambi ya upinzani ambayo imeelezwa kuwa na mgombea mzito wa chama cha CUF Salum Mandari.

Bwana Mandari ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Fedha Mamlaka ya Bandari (THA), ameelezwa kuwa ni mgombea anaetajwa sana na wapiga kura wa jimbo hilo.

Baadhi ya Wagombea wa majimbo mengine Jijini ni pamoja na Bwana Tambwe Hiza CUF na Bibi Hadija Kusaga CCM (Temeke), Bwana Frank Magoha CUF na Mzee Kitwana Kondo CCM (Kigamboni) na Bwana George Msina CUF (Ukonga).

Wakati huo huo, Kampeni za Urais, Ubunge , Uwakilishi na udiwani zinaanza rasmi kesho nchini kote.

Jijini Dar es Salaam baadhi ya vyama vitazindua kampeni zao kwa mikutano ya hadhara katika viwanja mbali mbali.

Mgombea wa vyama vya CUF na CHADEMA Profesa Ibrahim Lipumba imeelezwa atakuwa katika ukumbi wa Star Light kesho asubuhi kuzungumza na Wazee wa Dar na jioni atakuwa katika Viwanja vya Kidongo Chekundu.

Mgombea wa CCM ambaye pia ni Rais anayemaliza muda wake Mheshimiwa Benjamin Mkapa atazindua kampeni zake Viwanja vya Jangwani siku ya jumapili.

Gazeti hili litachapisha sifa binafsi (CV) za wagombea wote kuanzia toleo la jumanne.


Umaskini chanzo cha ujinga, - Sheikh Mnenge

SHEIKH Yusuf Rajab Mnenge amesema umaskini ndio chanzo cha kukithiri kwa ujinga na maradhi nchini.

Sheikh Mnenge ameyasema hayo Masjid Mujahiduun alipokuwa akizungumza na waumini Ijumaa.ilyopita.

Akifafanua kauli hiyo, Sheikh Mnenge amesema muda ambao wananchi wa kawaida wataendela kugubikwa na wimbi la umaskini watoto wao wataendelea kukosa elimu kwa kushindwa kulipia ada za masomo.

Aidha, Sheikh Mnenge amesema, umaskini huo ndio pia unaomfanya mwananchi wazidi kuteseka kutokana na maradhi mbalimbali.Kinyume cha hivyo, Sheikh Mnenge amesema ikiwa wananchi watakuwa na hali nzuri kimaisha wataweza kuwalipia ada za masomo watoto na pia wataweza kumudu matibabu.

Kwa sababu hiyo, Sheikh Mnenge amesema ni budi kuitumia vizuri fursa ya kupiga kura kwa kuchagua kiongozi mwenye sifa na uwezo wa kuondoa matatizo ya kiuchumi yaliyopo katika jamii .

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook