Mafundisho ya Uislamu

Fiqh

Na Mahmoud A.I. Sameja

FIQHI ni kujua hukumu za sheria zenye kufungamana na matendo ya mwenye kukalifishwa na sheria kwa dalili zake toka katika Qur’an na Sunna, na tanzu zake (Ijmai na Ijitihadi). Marejeo ya Fiqhi ni katika Qur’an na Sunna, Ijmai na Qiyasi.

QUR’AN

Qur’an ni maneno ya Mwenyezi Mungu aliyoteremshiwa Mtume Muhammad ili awatowe watu katika viza vya ukafiri na kuwatiya katika nuru ya Uislamu, nayo yameandikwa katika Msahafu. Ni marejeo makubwa ya hukumu za Fiqhi, yanapotokeya masuala yoyote kwanza hutizamwa Qur’an imesema nini tukikuta masuala yamewekwa wazi tunachukua hukumu yake bila ya kurejea kwingine.

Sunna

Sunna ni kila kilichonakiliwa toka kwa Mtume kuanzia kauli, matendo, na kukiri kwake jambo lililofanywa mbele yake. Sunna ni daraja la pili baada ya Qur’an kwani hurejewa Sunna baada ya Qur’an ima kwa ajili ya kufafanua hukumu iliyo katika aya, au kwa kuwa Qur’an haikuweka wazi hukumu ya masuala fulani.

Dalili ya Sunna ni amri ya Mwenyezi Mungu katika Suratu Nisaa aya ya 65:

"Naapa kwa (haki ya) Mola wako, wao hawawi wenye kuamini (kweli kweli) mpaka wakufanye (wewe ndiye) hakimu (mwamuzi) katika yale waliyokhitalifiana, kisha wasione uzito nyoyoni mwao juu ya hukumu ulyoitoa, na wanyenyekee kabisa.

Na katika Suratul Hashri, aya ya 7: " Na anachokupeni Mtume basi pokeeni, na anachokukatazeni jieopusheni nacho.

IJMAI

Ijmai ni kukubaliana kwa wanazuoni wote wenye sifa za Ijtihadi katika umma wa Mtume Muhammad baada ya kufariki Mtume katika zama fulani katika hukumu ya kisheria ambayo haikuelezwa wazi wazi na Qur’an na Sunna; Kukualiana huko ni kwa kujitahidi katika Qur’an au Sunna.

Ijmai ni daraja la tatu baada ya Qur’an na Sunna katika kutolea hukumu.

Dalili ya nne ni hadithi:

Imepokelewa toka kwa Abi Basrat Al-Ghifariyi kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Nimemwomba Mwenyezi Mungu asiwakusanye (wasikulibaliane jambo la dini) umati wangu katika upotovu". Imam Ahmad katika Musnad (6/386).

QIYASI

Qiyasi ni kuliunganisha jambo moja lisilo tajwa hukumu yake kwa lingine lenye hukumu toka katika Qur’an au Sunna, kwa kulingana sababu.

Qiyasi ni daraja la nne kutolea hukumu baada ya Ijmai.

Dalili ya Qiyasi: Katika suratu Nisaa, Aya ya 56:

"Na kama mkikhitalifiana juu ya jambo lolote basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume.

Na kutokana na Qur’an na Sunnah tumeamrishwa kufanya jitihada ili kulitolea jambo hukumu yake, na kutokana na jitihada hupatikana Qiyasi.

Haya tuliyoyabaini hapa ni kama utangulizi mfupi kwa somo la Fiqhi, kwa hiyo moja kwa moja tutaingia katika somo kwa kuelezea udhu katika toleo lijalo.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook