Mpaka hii leo Wasomali wamo katika mapambano ya wenyewe kwa wenyewe hali iliyosababisha nchi hiyo isiwe na serikali moja inayotambulika kitaifa. Mwandishi A. HUSSEIN anaelezea zaidi.
Pamoja na hivyo kitu kimoja ambacho wameweza kuifundisha dunia ni kule kuujali utaifa wao, haki yao kuwa huru, mila na desturi zao. Ni kwa ajili hiyo waliweza kuweka pembeni tofauti zao wakaungana kushambulia Taifa la Marekani lililotaka kutumia fursa hiyo kupenyeza mirija yake. Kwa umoja huo waliweza kuwang’oa wavamizi kutoka nchini mwao kwa masiku machache.
Hapakuwepo hata kundi moja miongoni mwa makundi yanayopingana lililokuwa tayari kumuunga mkono Mmarekani. Waliiona mapema hatari ya kuwepo Taifa hilo kubwa nchini mwao, wakakubaliana kuweka pembeni kwa muda tofauti zao, wakaafikiana kumpiga vita mvamizi adui yao wote.
Ukiachilia mbali Somalia, zipo nchi kadhaa hivi sasa za Kiafrika zinazofukuta migogoro ya ndani ambayo kwa sababu hii au ile hazijaweza kuitatua, wakati huo huo zikinyemelewa na hatari kubwa zaidi kutoka nje ya mipaka.
Kwa muda mrefu inaelezwa Wazanzibari wamejengeana uhasama miongoni mwao. Kama maelezo hayo ni sahihi uhasama wenyewe ni ule wa kisiasa ambao kiasili hautokani na Wazanzibari wenyewe. Uhasama uliopandikizwa na wachache kwa maslahi yao wakishirikiana na nguvu kutoka nje yenye agenda ya kukalia visiwa hivyo kwa mlango wa nyuma.
Tangu kuasisiwa ulioitwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Visiwa hivyo vimeshindwa kuwa na maamuzi yake kama nchi, kwa sababu hiyo wazanzibari kwa umoja wao wamekuwa wakilalamika kukoseshwa haki ya uananchi ya kujiamulia mambo yao kwa mujibu wa sheria za nchi yao. Wanaona wanaingiliwa na kushinikizwa na mamlaka fulani iliyo juu kutoka nje ya nchi yao.
Ikiwa chini ya mamlaka hayo wanadai Zanzibar inaonekana kama mkoa tu unaoongeza idadi ya mikoa ya nchi jirani.
Kibaya zaidi Wazanzibari hawana haki ya kuamua nani awe Rais wao bila ya kibali cha nguvu ambayo sehemu kubwa ya wajumbe wake si wananchi wa nchi hiyo!
Kwa ajili hiyo Zanzibar kama nchi huonekana ni kauli za kisiasa na za kuipaka mafuta kwa mgongo wa chupa kwa sababu Kiongozi wake mkuu hulazimika kutekeleza hata yasiyo na maslahi kwa nchi yake ilimradi yawe ni katika sera au maamuzi ya chama.
Mfano mmojawapo ni pale Zanzibar ilipotaka kuwa na bandari huru na alipotaka kujiunga na OIC kwa sababu za kiuchumi, uamuzi huo ukachukuliwa na mamlaka kuu kuwa ni uvunjaji usiovumilika wa katiba ya Jamhuri ya Muungano, "uhaini" ambao nusura umng’oe madarakani Rais wa Visiwa hivyo. Wazanzibari tujiulize iko wapi mamlaka ya Zanzibar hapa!
Ni mpaka lini hali hii watadumu nayo Wazanzibari, ni swali zito kujibika linalohitaji tafakuri iliyohuru na isiyozugwa na msimamo au ukereketwa.
Awe Muunguja au Mpemba, kila mwananchi wa Zanzibar afahamu anakabiliwa na hatari ya siasa za kushinikizwa ambazo kilele chake huenda ikawa kufutwa kimya kimya Taifa la Zanzibar huru katika ramani ya Dunia.
Kama ilivyokuwa kwa Wasomali, Wazanzibari hawana budi kuiona na kuipiga vita kwa umoja na nguvu zote hatari hiyo wakiweka kando tofauti ambazo tangu hapo hazitokani na wao wenyewe.
Wasimame kama Wazanzibar kwanza kutetea sasa katika mitaa ya Unguja na Pemba.
Wale wakereketwa wachache wa maskani ambao mtazamo wao unakomea kumuona mgombea wao anakamata usukani, waanze kutanabahi.
Rais ambaye kuingia kwake madarakani hakutatokana na kura za wananchi wenyewe ni wazi hatakuwa kwa maslahi ya waliopiga kura.
Wazanzibari hawana budi kuweka pembeni tofauti zao wakasimama kama Wazanzibari kupigania maslahi ya nchi yao.
Rais wa Zanzibari awe yule atakayesimamia maslahi ya nchi hiyo akidumisha mashirikiano na nchi nyingine kwa taratibu au mikataba itakayotambua mamlaka kamili ya Zanzibar.
Zanzibar ilijikomboa ikiwa kama Taifa linaloundwa na visiwa viwili vya Unguja na Pemba. Asitokee kidudumtu au jinamizi kutaka kukamua na kunyonya damu Wazanzibari kwa kuwatumia Wazanzibari wenyewe kwa manufaa yake binafsi au itikadiyake. Hili lingepaswa kuwekwa kwenye mazingatio na kila Mzanzibari aliyehai hivi sasa!
Kila mzalendo wa Zanzibar ingefaa autazame uchaguzi wa mwaka huu kama fursa pekee itakayowezesha kubadili mfumo kandamizi kwa njia ya amani.
Wazanzibari wanawajibika kuiweka wazi agenda ya siri dhidi ya nchi yao inayolenga kumfanya Mzanzibari asijinasibu kwa utaifa, mila na desturi zake ndani ya nchi yake.
Kusimamisha, kutetea na kudumisha haki na usawa
Wazanzibari wote ni jukumu la kila Mzanzibari. Hasa kwa wale wenye uwezo
wa hali na mali. Ni makosa kuridhia dhulma na uonevu. Fitna inayosukwa
dhidi ya Zanzibar ni kubwa. Ni bora mtu afe kishujaa akipigania haki.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |