Wakati kikao maalum cha Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM kilichokutana Dodoma kujadili majina ya waliowania nafasi ya kugombea Urais kupitia CCM Zanzibar, kikitoa maelezo yake juu ya kuteuliwa bwana Karume katika nafasi hiyo, kilisema huyo ndiye chaguo la Wazanzibari wote!
Kila aliyepata fursa kuongea baada ya mizengwe na pilika pilika za uchaguzi huo wa Halmashauri ya CCM, alisema Karume ndiye kiboko ya wapinzani.
Namna vyombo vya habari vilivyomjenga na kumpa uzito wa namna ya pekee ilikuwa dhahiri Karume kama ilivyodaiwa ndiye Rais mtarajiwa wa Zanzibar.
Kinachoshangaza ni kuona hali inayotisha kuvuruga uchaguzi. Hali inayoonesha kutokujiamini kwa baadhi ya vyama.
Vijana kadhaa kutoka miji ya Dar es Salaam na Tanga wamedaiwa kusafirishwa kwa siri kupelekwa Zanzibar wakajiandikishe kisha shahada zao huchukuliwa na hao waliowatuma.
Wiki mbili zilizopita Kiongozi mmmoja wa chama cha upinzani alitoa taarifa juu ya kundi la vijana lililoonekana katika moja ya meli zilizokuwa zikielekea Zanzibar.
Baadaye ikajafahamika kuwa vijana hao ni miongoni mwa mamaluki wa kura waliopelekwa visiwani.
Jitihada hiyo inakwenda sambasamba na utumiaji wa vyombo vya Dola usiowalazima ambapo tangu zoezi la kujiandikisha kupiga kura lianze wananchi wamekuwa wakipigwa, kutiwa mbaroni na kuzuiliwa kujiandikisha.
Taarifa kutoka maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba zinahuzunisha, kusikitisha na kukasirisha.
Gazeti moja la kila siku juzi katika ukurasa wake wa mbele lilichapisha picha inayomuonesha askari wa FFU akimkwida kanzu mwananchi wa Unguja na kumsukuma kuelekea kwenye Karandinga tayari kumtia mbaroni!
Zaidi ya watu mia moja hadi sasa wameripotiwa kuwekwa rumande wakidaiwa kufanya fujo katika vituo vya kujiandikisha kupiga kura. Mbali ya hao kuna waliokwishajeruhiwa kwa virungu na kumwagiwa biashara zao.
Aidha wanajeshi wa jeshi la wananchi wameripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kupelekwa Zanzibar. Na inasemekana baadhi ya vituo viko katika kambi za jeshi na wananchi hawatakiwi kufika huko!
Hii ni ishara gani kwa Taifa ambalo kila kukicha viongozi wake hudai kuheshimu Katiba na sheria za nchi.
Kama hali hii ya uonevu na ubabe inajitokeza kipindi hiki cha kujiandikisha itakuwaje wakati wa kupiga kura na kutangazwa matokeo? Nadhani kwa mwanzo huu huenda yameandaliwa mazito zaidi, ni vyema wananchi wakajiandaa!
Mwezi mmoja uliopita wakati akizungumza na makamanda wa jeshi la polisi Jijini, Rais Mkapa aliwataka Askari kupambana na kile alichokiita jitihada za baadhi ya watu kutafuata umaarufu kupitia migongo ya askari.
"Katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kitakuwa kigumu kwenu, kwa sababu ni kipindi cha vurugu za kisiasa. Wengine watataka kupata umaarufu kupitia migongo yenu, wangine watawakejeli na wengine watawachokoza. Ninawataka mtumie mamlaka mliyonayo....."
Rais Mkapa aliyatamka hayo akipokewa kwa shangwe na vifijo kutoka kwa maaskari hao wakionekana kuelewa ilikuwa ni kibali rasmi kutoka kwa Rais juu ya utumiaji wa mabavu katika kipindi hiki mpaka oktoba 29.
Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti habari ya kufutwa kwa likizo za polisi mpaka baada ya uchaguzi. Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa jeshi hilo nchini Bwana Omar Mahita.
Wakati ikiripotiwa taarifa hiyo tayari kule Zanzibar kumejazwa maaskari na magari ya deraya yakizunguka mitaani kutisha wapiga kura.
Hata hivyo kiongozi mmoja wa Zanzibar akizungumza juzi alisema utitiri huo wa maaskari uliopelekwa Zanzibar ni kwa ajili ya kulinda amani.
Kwa upande mwingine kiongozi mwingine ameripotiwa kutamka kuwa kwa hali yoyote safari hii chama tawala lazima kipate jimbo kule Pemba!
Wakati hayo yakijiri Tume zote mbili za uchaguzi zinaonekana kupiga kimya hata katika yale yanayoonekana kutaka kuvuruga kabisa uchaguzi wenyewe.
Taarifa za upungufu wa vifaa na uchache wa vituo vya kujiandikishia hazionekani kuwashitua wakuu wa Tume hizo.
Juzi katika kipindi kinachorushwa na DTV, makamu Mwenyekiti amedai kutokuwa na habari juu ya hali hiyo.
Kweli ni uchaguzi huru na wa haki utakaowapatia
watanzania viongozi waliowachagua kwa kura zao wenyewe!
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |