KATIKA toleo Na. 273 la gazeti hili ilitolewa makala iliyopewa kichwa cha habari "Rais Mugabe aheshimu katiba na sheria". Katika makala hiyo mwandishi alijaribu kutoa ufafanuzi wa jinsi ambavyo mgogoro wa ardhi Zimbabwe kati ya Wazungu na wapiganaji wa Uhuru wa Zimbabwe wanaoonekana kuungwa mkono na serikali ya Rais Robert Mugabe unavyohatarisha kuanguka kwa uchumi wa nchi hiyo, iliyo kusini mwa Afrika.
Mwandishi wa makala hiyo ameonesha kutoridhishwa na namna ambavyo Rais Mugabe anavyolishughulikia tatizo la mgogoro wa ardhi nchi mwake.
Katika makala hiyo mwandishi katoa wito kwa wananchi na serikali ya Mugabe kufuata na kuheshimu sheria na katiba ili kuleta mustakbali mzuri wa nchi.
Kama kichwa cha habari cha makala yangu hii kinavyojieleza, mimi nadhani kuheshmu sheria na katiba pekee si hakikisho la nchi kuwa na utawala wa haki.
Nimelazimika kuandika haya kuwatanabahisha wote wanaodhani kuwa kuheshimu sheria na katiba kwa serikali na vyombo vyake ndiyo ufumbuzi wa wananchi kuwa na haki mbele ya utawala, bila ya kuangalia sheria zenyewe.
Zimbabwe kama ilivyo Tanzania ilikuwa ni koloni la Waingereza. Kwa hiyo ukiacha sheria chache zilizotungwa baada ya uhuru, sheria nyingine zote zinazotumika katika nchi hiyo zilitungwa na wakoloni wakati wa utawala wao ili kulinda na kuhifadhi maslahi yao. Sheria hizo hazikujali maslahi ya Wazimbabwe hata kidogo. Sheria ya ardhi ya Zimbabwe ni mojawapo ya sheria hizo.
Kwa kutumia nguvu na sheria walizozitunga wakoloni waliwanyang’anya milki ya ardhi wananchi wa Zimbabwe. Mashamba yao yenye rutuba waliyagawa kwa Wazungu walowezi wachache (Setters).
Kwa hiyo wanachofanya maveterani hao wa vita wa Zimbabwe ni kuirudisha haki yao iliyoporwa na wakoloni waliotunga na kuheshimu sheria za ukandamizaji na ubaguzi.
Maveterani au wapiganaji uhuru wa Zimbabwe wameamua kuvamia mashamba yanayomilikiwa na Wazungu, sio kwa sababu sheria hazipo, ila ni kwa sababu sheria zilizopo zinawakandamiza na kuamua kuzitumia katika kudai haki ya milki ya mashamba hayo ni sawa na kuridhia kukosa ardhi ya kuendesha maisha yao.
Kupigania kwao uhuru hakukumaanisha tu kutaka kutawaliwa na Mwafrika mwenzao bali ni pamoja na kumiliki njia kuu za uchumi kwa haki, usawa, na kwa faida ya wote katika misingi ya kibinadamu kwa wote. Kuheshimu sheria hakutakuwa na maana yoyote iwapo asilimia kubwa ya wananchi hawana ardhi.
Hivyo basi, tatizo sio serikali kuheshimu sheria na katiba bali ni sheria gani zinazojenga huo utawala ili kudumisha haki, usawa na ustawi wa jamii, unaojenga umoja wa kitaifa wenye kuheshimu utu, heshima na hadhi ya kila mwananchi.
Zipo sheria na katiba zinazotoa haki sawa kwa wote na zipo pia zinazolenga na kujenga ubaguzi, uonevu na unyanyasaji kwa raia katika misingi ya jinsia, rangi, kabila na dini. Sheria zote hizo zipo na zinaongoza jamii mbalimbali ulimwenguni.
Mfano wa sheria mbaya ni sheria za ubaguzi Afrika Kusini wakati wa utawala wa makaburu, sheria za Manazi nchini Ujerumani wakati wa Hitler, na sheria za ukandamizaji, ubaguzi na uonevu kwa Wapalestina chini ya utawala wa Mayahudi Israel.
Tawala zote hizo zilikuwa na nyingine bado zinaendeleza uonevu na ukandamizaji kwa raia kwa kufuatilia kwa makini na kwa ukaribu utekelezaji wa sheria zao bila kuacha mwanya kwa watu kuzivunja. Kwa hakika tawala hizo zinaheshimu na kufuata sheria zake.
Hapa kwetu Tanzania, pamoja na kuwa na katiba inayolinda na kuheshimu haki za raia bado wananchi wananyimwa haki hizo pasipo na sababu yoyote, kwa sababu serikali na vyombo vyake vinaheshimu baadhi ya sheria onevu na za ukandamizaji zinazokwenda kinyume na haki za binadamu zilizoainishwa ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kwa Mfano Ibara ya 9 )f) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inafafanua malengo ya katiba na utekelezaji wa mamlaka ya nchi kwa kuzingatia kwamba, heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu.
Isitoshe kuanzia ibara ya 12 mpaka Ibara ya 24 katiba hiyo inatoa na kufafanua haki za msingi za binadamu, kama vile, haki ya usawa, haki ya kuwa huru, haki ya hifadhi ya maisha na mali, kutembea, haki ya kutoa mawazo, kuabudu, kushirikiana na wengine, haki ya kufanya kazi na kadhalika.
Lakini haki zote hizo zilizoainishwa kwenye katiba katika Ibara tulizozitaja hapo juu ni sawa na kama vile hazipo, kwa sababu katiba hiyo hiyo inatoa uwezo (Powers) kwa mamlaka za serikali kama vile polisi, magereza, Rais, Mawaziri, na taasisi mbalimbali, kutumia sheria nyingine zilizopo kutoa amri, kama vile kuruhusu au kutoruhusu jambo fulani lifanyike au lisifanyike. Japo jambo hilo linaweza kuwa limeruhusiwa na Ibara za Katiba kama tulivyozitaja hapo juu.
Nguvu (powers) hizo ambazo nyingi ni "Subjective" au "Too discretionary" zinafuta kabisa uhuru wa wananchi kufaidi (enjoy) haki zao za msingi.
Pamoja na katiba inaheshimu haki ya mtu ya kuishi, lakini watu wanaweza kuuliwa na polisi, mfano Mwembechai na polisi au serikali ikakataa kufanya uchunguzi wa vifo hivyo. Kwa kisingizio cha polisi kuwa hawakufanya kosa kwa sababu walichokifanya kinaruhusiwa chini ya sheria ya usalama wa nchi na sheria za polisi. Hapo serikali inadai kuheshimu sheria zake!
Basi, kama kuheshimu sheria ndio utekelezwaji na utoaji wa haki basi serikali ya Tanzania ingekuwa ya kwanza katika kutoa haki. Kwa sababu "Subjective powers" na "discretionary powers" tulizozitaja hapo mwanzo zinaheshmiwa na serikali na zinatumiwa vilivyo kuminya na kuzuia haki za raia zinazotambuliwa na katiba waliyokula kiapo kuilinda. Haki za wananchi zinavunjwa kwa kisingizio cha kuheshimu ya kulinda sheria za nchi!
Kukamatwa ovyo kwa Masheikh na kuingiliwa kwa uhuru wa kuabudu kwa Waislamu kunatokana na serikali na vyombo vyake, kama vile polisi, kuheshimu sheria zake zinazokandamiza uhuru na haki za raia.
Kupigwa marufuku kwa kitabu cha Mwembechai pia kunatokana na Rais kuheshimu sheria ya Newspaper Act, inayokandamiza uhuru wa raia kutoa mawazo na maoni yao, ili hali kitabu hicho kama kinavyosomeka kwenye Internet hakina lolote zaidi ya kueleza ukweli wa mauaji ya polisi.
Kwa hiyo ili kulinda haki sio tu serikali iheshimu sheria zake, isipokuwa kwanza ni lazima seriakli iongozwe na sheria zinazolinda haki kwa raia wote bila ubaguzi, hapo ndipo suala la umuhimu wa kuziheshimu utafuata. Haki sio tu itendeke bali pia ionekane kuwa inatendeka.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |