Baraza la Wazee wa TANU na Safari ya Nyerere Kwenda Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa, New York, 1954.
Mara tu baada ya kuundwa kwa TANU, baraza la wazee liliundwa katika makao makuu, Dar es Salaam ambalo lilikuwa na takriban wajumbe mia moja na sabini.
Ilikuwa ni kamati ya wazee ambayo wajumbe wake wote walikuwa Waislam. Sheikh Suleiman Takadir ndiye alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Baraza la Wazee wa TANU.
Kamati kama hiyo iliundwa vilevile Tabora mwaka 1956, na Mzee Fundi Muhindi mwanasiasa mkongwe, muasisi wa African Association Tabora mwaka 1945 na muasisi wa TANU mwaka 1954 Jimbo la Magharibi alichaguliwa mwenyekiti wake wa kwanza.
Baada ya kuundwa kwa TANU uongozi ulianza kushugulikia mpango wa kupeleka madai yake mbele ya Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa kudai uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Waingereza. Hii ilikuwa mara ya pili Waafrika wa Tanganyika wanafikisha madai yao Umoja wa Mataifa. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1952 wakati Japhet Kirilo alipokwenda Umoja wa Mataifa kuwakilisha madai ya mgogoro wa ardhi ya Wameru.
TANU ilikuja kutambua kuwa taarifa za ujumbe za wa Umoja wa Mataifa zilikuwa na athari ndogo sana kwa Uingereza. Ikijifunza kutokana na uzoefu uliopata wa Japhet Kirilo katika Umoja wa Mataifa, kuanzia mwaka 1952 TAA ikawa inashughulikia kumpeleka mjumbe wake mwenyewe kwenda Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa kudai uhuru wa Tanganyika. Katika safari ya Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa ndipo tunakutana na Idd Faiz Mafongo.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba Idd Faiz Mafongo alihudhuria mkutano wa uzinduzi wa TANU katika Ukumbi wa Arnautoglu.
Haifahamiki kwa hakika hasa ni lini Idd Faiz alijiunga na TANU kwa sababu kadi yake ya kwanza ya uanachama ilipotea na alipewa kadi nyingine iliyokuwa na namba 915 iliyotolewa tarehe 28 Agosti, 1954. Lakini kwa kukisia tu kutokana na kadi ambayo Idd Faiz mwenyewe aliitoa kwa kaka yake Idd Tosiri ambayo ni kadi namba 25 na yenye saini yake kama afisa aliyetoa kadi hiyo, inaweza kuchukuliwa kwa uhakika kuwa Idd Faiz alikuwa miongoni mwa wale watu wa mwanzo kabisa kuingia TANU na huenda akawa miongoni mwa wanachama ishirini wa mwanzo.
Ukichukua katika fikra ukweli kwamba Ali Mwinyi Tambwe aliyekuwa katibu wa Al Jamiatul Islamiyya aliingizwa TANU na Mtemvu katikati ya mwezi Agosti, 1955 huenda Ally Mwinyi kama katibu wa Al Jamiatul Islamiyya na Idd Faiz akiwa mweka hazina, wote wawili waliingia TANU wakati mmoja.
Idd Faiz na nduguye Idd Tosiri, muasisi wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika, walikuwa Wakusu, moja ya makabila ya Kimanyema, kwa upande wa baba yao; na Wabwali kwa upande wa mama yao. Wote wawili walikuwa katika Batetera Union (Congo Association) chama kilichokuwa kikiwaunganisha Wamanyema wa Tanganyika.
Mzee bin Sudi alikuwa rais muasisi wa chama hicho na baada ya kifo chake Sheikh Hussein Juma alichaguliwa kushika nafasi hiyo. Batetera Union kilikuwa chama kilichoshikamana na chenye nguvu sana miongoni mwa vyama vya kikabila. Wamanyema ni kabila la Waislam watupu na kwa sababu hii hakukuwa na pingamizi katika kuunga mkono TANU.
Batetera Union ilikuwa na nguvu sana kiuchumi kwa kuwa kilikuwa katika wafuasi wake, watu waliomiliki majumba na walihodhi takriban nusu ya nyumba zilizojengwa mjini Dar es Salaam kati ya vita kuu mbili za dunia.
Uwezo huu wa kiuchumu uliwafanya Wamanyema kuwa wapinzani wagumu wa serikali ya kikoloni na uliwanyanyua hadi kufikia kuwa mbele katika siasa mjini Dar es Salaam na katika miji mingine ya Tanganyika. Umoja wa Wamanyema ndiyo uliojenga msikiti maarufu wa Wamanyema mwaka 1912 uliokuwa karibu na makao makuu ya African Association.
Wamanyema wanajulikana kama watu wenye damu ya kali na wana sifa ya ushujaa. Mmanyema anaweza kuulipia fedha ugomvi ili na yeye awemo, na kadri mpinzani anavyokuwa na nguvu na hodari, ndivyo Mmanyema anavyofaidi ugomvi wake. Katika siku hizo Wamanyema walikuwa wameshikwa katika magomvi.
Katika mwaka 1941 ilihitaji serikali, maimamu na masheikh wa msikiti mingine mjini Dar es Salaam kuingilia kati ili kuamua ugomvi uliowakumba Wamanyema kuhusu msikiti wa Manyema. Wamanyema hawakumstahi mtu yeyote, waligombana hata wenyewe kwa wenyewe. Hamaki hizi zilipoelekezwa kwa serikali ya kikoloni zilikuja kuwa na manufaa sana. Kwa kuwa walikuwa ni kabila la Waislam watupu, Wamanyema hawakuweza kufaidika na elimu iliyokuwa ipo mokononi mwa wamishionari. Hata hivyo Wamanyema walipiga hatua kubwa katika elimu ya dini yao na hii ndiyo sababu kuwa hadi leo utamaduni wa Kiislamu umeenea katika kila familia ya Mmanyema iwe nyumbani Kigoma au huko pwani. Mmanyema hayupo mbali sana na utamaduni wa Kiislam. Wamanyema, Warufiji na Wadigo ni katika makabila ambayo ni tabu sana kumpata Mkristo.
Idd Faiz alikuwa Mmanyema. Hadhi yake iliongezeka zaidi kwa kuwa alikuwa mweka hazina wa TANU. Idd Faiz aliifanyia kampeni TANU, akifuatana na Nyerere katika safari za awali za kukitangaza chama, akihutubia mikutano jukwaa moja na Nyerere.
Ilikuwa ni Idd Faiz na kaka yake Idd Tosiri ndiyo waliompeleka na kumtambulisha Nyerere kwa binamu yao Sheikh Mohamed Ramia wa Bagamoyo. Ilikuwa baada ya utambulisho huu kwa Sheikh Ramia ndipo urafiki ukajengeka kati ya Sheikh Ramia na Nyerere na ndiyo ndiyo Nyerere akakubalika Bagamoyo.
Sheikh Ramia akiwa khalifa wa tariqa ya Qadiriya alikuwa na murid wengi waliomfuata kama kiongozi wao. Sheikh Ramia alikuwa miongoni mwa wanachuoni walioheshimiwa sana. Hakuna kilichoweza kusimama na kuota mizizi Bagamoyo bila kupata ridhaa ya Sheikh Mohamed Ramia.
Akiwa khalifa wa tariqa ya Qadiriya ambayo ilianzishwa na kustawishwa Bagamoya na baba yake, Sheikh Yahya Ramia, mwanzoni mwa karne ya ishirini, nguvu za Sheikh Ramia zilikuwa hazisemeki. Anachosema sheikh ndicho hicho kitafuatwa.
Baraza la Wazee iliyachukua mafanikio ya safari ya Nyerere kuwa ni jukumu lao binafsi. Sehemu ya kwanza ya maandalizi ilitakiwa ifanyike kwa siri sana. Uongozi wa TANU ulikabidhi Idd Faiz kazi ya kuandaa, kukusanya na kusimamia mfuko wa safari ya rais wa TANU kwenda Umoja wa Mataifa, New York. Safari ilikuwa ifanyike mwezi Februari, 1955.
Mwaka 1953 Idd Faiz alikuwa na umri wa miaka arobaini na tatu, mwenye ari na nguvu tele. Alipokuwa katika kamati kuu ya ya TANU mwaka 1959 aliteuliwa kuwa mweka hazina wa taifa wa TANU pamoja na kuwa mjumbe wa kamati kuu. Idd Faiz alikuwa mmoja wa viongozi wa chama walioanzisha TANU Press iliyokuwa katika njia panda ya Mtaa wa Mchikichi na Livingstone mjini Dar es Salaam.
TANU Press ndiyo ilikuwa ikichapisha na kusambaza jarida la TANU, Sauti ya TANU lililohaririwa na rais wa chama, Julius Nyerere, na baadae kuchapisha Mwafrika chini ya uhariri wa Rashid Heri Baghdelleh na Robert Makange. Kampuni hiyo ya kupiga chapa ilimilikiwa na Mwananchi Development Corporation na TANU ilimteua Abdul Faraj kuongoza kampuni hiyo.
TANU ilihitaji takriban shilingi elfu kumi na mbili kumwezesha Nyerere kusafiri kwenda Umoja wa Mataifa, New York. Kamati ya Abdu Kandoro, Japhet Kirilo na Abbas Sykes ilikuwa imekusanya kiasi cha fedha kutoka majimboni ambacho kilitumika katika ile safari ya Ally na Phombeah kwenda kwenye Pan African Congress mjini Lusaka. Kilichosalia hakikutosha kumpeleka Rais wa TANU, Nyerere Amerika. Ilibidi fedha za ziada zitafutwe kutoka kwa wananchi ili kumwezesha Nyerere kufanya safari hiyo.
John Rupia alichangia zaidi ya theluthi moja ya fedha iliyotakiwa. Wanachama wengine walichangia kwa uwezo wao wote lakini TANU katika siku zile ikiwa bado changa ilikuwa maskini, kiasi hicho kilikuwa bado kiko nje ya uwezo wake kukipata.
Ikitambua ule upungufu katika fedha za safari ya Nyerere, Idd Faiz aliombwa na uongozi wa Al Jamiatul Islamiyya kutoa fedha katika mfuko wa Al Jamiatul Islamiyya na kuzitia katika hazina ya TANU ili chama kiweze kumpeleka Nyerere New York.
Hata pamoja na fedha zile kutoka Al Jamiatul Islamiyya bado fedha hizo hazikuweza kukidhi haja. Al Jamiatul Islamiyya haikuwa na jingine isipokuwa kumuomba Idd Faiz asafiri kwenda Tanga na kupata fedha zaidi kutoka huko. Mwalimu Kihere alikuwa tayari amekusanya fedha hizo na alikuwa anasubiri tu zije zichukuliwe na kupelekwa makao makuu.
TANU ilipata habari kwamba yeyote atakaekwenda Tanga kuchukua fedha hizo kwa ajili ya safari ya Nyerere atakamatwa. Kabla ya kuondoka, Oscar Kambona, Katibu Mkuu wa TANU, na John Rupia, Makamo wa Rais wa TANU, walikwenda kuonana na Idd Faiz nyumbani kwake Ilala kumuaga, kumtakia safari njema na kumpa maelezo kwa ufupi.
Safari ya kwenda Tanga haikuwa na tatizo lolote, lakini katika wakati wa kurudi basi ambalo Idd Faiz alikuwamo lilisimamishwa njiani Turiani na Special Branch. Idd Faiz alikamatwa, akavuliwa nguo na kupekuliwa, lakini hakukutwa na fedha. Hili lilimshangaza na kumchanganya yule afisa wa aliyemkamata kwa sababu walikuwa na taarifa kwamba Idd Faiz alikuwa amechukua fedha kutoka kwa Mwalimu Kihere kule Tanga. Idd Faiz aliwekwa chini ya ulinzi na kupelekwa Dar es Salaam kwa usaili zaidi wakati wote akiwa analindwa na askari wenye silaha. Baadae Idd Faiz aliachiwa huru. Zile fedha za TANU zilifika makao makuu ya TANU Dar es Salaam, salama salimini. Fedha zile alikuwa amepewa kubeba msichana mdogo ambae alikuwa abiria ndani ya basi lile alimokuwa Idd Faiz.
Mnamo tarehe 17 Februari, 1955 Nyerere aliondoka kwenda New York kuhutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa. Nyerere aliiweka wazi nia ya TANU kuwa alikuwa ametumwa na wananchi wa Tangayika kuwasilisha ujumbe ufuatao:
…kuona kanuni ya uchaguzi ikianzishwa na Waafrika wanajiwakilisha katika taasisi zote za umma... Hii tunaamini, ni kwa mujibu wa masharti ya Makubaliano ya Udhamini na Ibara ya 76 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
TANU mbele ya Umoja wa Mataifa haikuwa ikidhihirisha tamko lolote jipya, yale yote yaliyowasilishwa pale yalikuwa ni maoni ya kamati ndogo ya siasa ya TAA yaliyowakilishwa kwa Constitutional Development Committee ya Gavana Edward Twining mwaka 1950.
Gavana Edward Twining aliyapuuza mapendekezo ya TAA na badala yake aliendelea na mipango yake ya kuwa na wawakilishi wa rangi zote katika Baraza la Kutunga Sheria.
Ili kuupa msukumo msimamo wake huo serikali ilituma ujumbe wake Umoja wa Mataifa kuipinga TANU uliowakilishwa na I. C. Chopra, Mwasia; Sir Charles Phillips, Mzungu na Liwali Yustino Mponda, mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria wa Newala.
Nyerere alirudi kutoka New York Jumamosi, tarehe 19 Machi, 1955 na alipokelewa uwanja wa ndege na halaiki ya watu. Dossa Aziz anakumbuka kuwa aliruhusiwa pale uwanja wa ndege kuingiza gari yake hadi ndani ya uwanja chini ya ndege ili kumrahisishia Nyerere kuingia ndani ya gari lake kuepuka msongamano wa watu.
Dossa Aziz anasema kama isingekuwa kwa msaada huu Nyerere angesongwa sana na watu. Watu walikuwa kila mahali wakisukumana na kusongamana wakijaribu angalau kumtia Nyerere machoni. Watu walikuwa wakiimba na kucheza ‘mganda’, ngoma ya Kizaramo, wakiimba: ‘Baba Kabwela Yuno’. Jambo la kushangaza ni kwamba hakuna mtu aliyewahi kuusikia wimbo huu kabla ya siku ile na hakuna ajuaye lini ulitungwa. Ile gari ya Dossa Aziz aliyopanda Nyerere ilisukumwa kutoka uwanja wa ndege hadi nyumbani kwa Nyerere, Magomeni Majumba Sita, kiasi cha kama kilomita ishirini.
Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili. TANU ilifanya mkutano wa hadhara Mnazi Mmoja ambao ulihudhuriwa na umati ambao kamwe haukupata kuonekana Dar es Salaam. Inakisiwa zaidi ya watu 40,000 walikuja kutoka kila upande wa mji kumsikiliza Nyerere. Hakuna mtu aliyekuwa na raha ya kuandika kuhusu mkutano ule na safari ya kihistoria ya Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa kuliko Mashado Plantan katika gazeti lake Zuhra. Mtambo wa gazeti wa Mashado uliokuwa Mtaa wa Ndanda, Mission Quarters ulichapisha nakala za ziada za gazeti hilo na toleo lote liliuzika.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |