Mtoto wa kigogo wa CCM mgombea Udiwani CUF Moro

CHAMA cha Civic United Front (CUF) Wilaya ya Morogoro kimetangaza rasmi majina ya wagombea Udiwani waliopitishwa na chama hicho akiwemo mtoto aliyekuwa muasisi wa TANU na CCM wilaya ya Morogoro mjini marehemu Mzee Maharagande.

Akiongea na AN-NUUR Jumanne (Agosti 15, 2000) msemaji wa chama hicho Bw. Abdallah Mambo alisema kuwa tayari wagombea hao wameshachukua fomu kwa msimamizi wa uchaguzi

Aliwataja waliopitishwa na kata zao zikiwa kwenye mabano kuwa ni Shaban Saidi Mizambwa (Mzinga), Mhina Abdallah Abdul (Mafiga), Rajab Omary Dendego (Kilakala), Hashim Juma Kiffea (Saba Saba)na Abeid Harubu Mlapakolo (Kiwanja cha Ndege).Wengine ni Mzee Juma Segumba (Kingolwira), Madadi N. Maringo (Mji Mkuu), na Mohamed J. Matokeo (Uwanja wa Taifa).

Wengine ni Mbarala Abdallah Maharagande (Sultan), Bakari Kassim Mbega (Mazimbu), Seng’unda G. Chilosa (Mbuyuni), Ramadhani Hassan Maftaha (Mji Mpya) pamoja na Jafari Thabiti Makala (Mwembesongo)

Aidha, kiongozi huyo alisema kwamba mpaka hivi sasa bado hawajaweka wagombea katika kata sita kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ile ya kuachiana kata na majimbo iliyokubaliwa kati ya Chama cha CUF na CHADEMA.

Pia Bw. Mambo ambaye anashughulikia kitengo cha Hakiza Binadamu ya chama hicho alilieleza gazeti hili kuwa tayari chama chake kimeshamteua mgombea wake wa Ubunge ambaye alimtaja kuwa ni Bw. Athumani Shaaban Maringo.

Wakati huo huo, Chama cha wananchi (CUF) wilaya ya Morogoro kimesema kuwa kumekuwepo na dosari nyingi katika zoezi linaloendelea la kuandikisha wapiga kura za uchaguzi wa udiwani, ubunge na urais

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa chama hicho mwanzoni mwa wiki hii imesema kwamba katika vituo vingine vya kujiandikisha kumekuwepo na upungufu wa vifaa zikiwemo fomu Na 1 hadi 4.

Aidha, wamedai kuwa baadhi ya waandishi wa wapiga kura wamekuwa wakienda kwenye vituo vyao huku wakiwa wamevaa fulana za kukipigia kampeni chama cha CCM.

Wametoa mfano kuwa tukio hilo lilitokea katika kata ya Uwanja wa Taifa ambapo maelezo hayo tayari wameshayapeleka kwa msimamizi wa uchaguzi ambapo wamedai kuwa ameyafanyia kazi baadhi na mengine ameonekana kuyapuuza.

Matatizo mengine waliyoyaorodhesha viongozi hao tangu zoezi la uandikishaji wapiga kura lianze Agosti 8, mwaka huu ni wenyeviti wa serikali za mitaa kuwa na sauti sana kana kwamba wao ndio viongozi wa Tume ya Uchaguzi.

Kasoro nyingine waliyoitaja viongozi hao ilitokea katika kituo cha Nyandira kilichopo kata ya Mazimbu ambapo walidai wakala wa chama cha Mapinduzi (CCM)anaondoka na fomu Na. 2 (kitabu cha orodha ya wapiga kura) jambo ambalo wamedai ni kinyume na utaratibu uliowekwa na Tume ya Uchaguzi.

Gazeti hili lilifika ofisini kwa msimamizi wa uchaguzi jimbo la Morogoro ili kujua kama amepokea madai hayo ya CUF na uamuzi aliochukua. Hata hivyo msimamizi huyo hakuweza kupatikana kwa madai ya wasaidizi wake kuwa anatembelea vituo, nao walipotakiwa kulizungumzia suala hilo wakadai hawako tayari kwa kuwa si wasemaji.


Ilunga atoka hospitali Adakwa na polisi


Ustadh Ilunga ametoka hospitali Jumanne na kulakiwa na polisi waliokuwa wakimsubiri .

Taarifa kutoka Mwanza zimeeleza kuwa,polisi walifika hospitalini Bugando kiasi cha saa nne asubuhi baada ya kupata habari kuwa Ustadh angeruhusiwa siku hiyo.

Polisi hao wapatao 10 walimlaki Ilunga alipotoka tu wodini na kuondoka naye ndani ya landrover 110.

Kuona hivyo,habari zinaeleza,waislamu waliokuwepo walivamia tax kiasi cha 10 zilizo kuwemo hospitalini hapo na kujazana wanne wanne huku wakiwaamrisha madereva wake kufuata gari ya polisi iliyomchukua Ustadh Ilunga.

"Ilikuwa kama maandamano ya tax yakiongozwa na gari ya polisi",amesema Bwana Hamisi na kuongeza kuwa kila magari hayo yalipopita yalizoa waislamu wengine wakiwemo walio fuatilia msafara huo kwa miguu na wale walio kodi magari.

Umati wa waislamu ulifurika kituo cha polisi ambapo polisi walilazimika kuwaomba viongozi wawatulize na kuwaomba waislamu wapungue kwani pasingekuwa na jambo lolote baya.

Mpashaji wetu wa habari anaeleza kuwa,Ustadh Ilunga aliwekwa ndani kwa saa moja kisha akatolewa na kutakiwa aripoti kituoni hapo juzi Jumatano.

Aliwekewa dhamana na watu wawili,Bwana Mohamad Ballah ambaye ni katibu wa Bakwata mkoa pamoja na Bwana Mohamedi Mtole.

Habari zinasema, pamoja na kuwa watu hawakuwa wametangaziwa wafike polisi juzi,lakini kituo kilijikuta kimefurika waislamu wakati zoezi la kumhoji Ustadh Ilunga likiendelea.

Katika zoezi hilo lililoongozwa na kamanda wa polisi upelelezi mkoa, (RCO) Abdallah Waziri Msika,waislamu wawili waliruhusiwa kuwemo kwenye chumba cha mahojiano.

Pamoja na mambo mengi ambayo polisi walitaka kujua katika usaili huo,muhimu walimtuhumu Ustadh kuwa amekuwa akisema kuwa serikali ya Tanzania ni ya kikafiri.

Kwa hilo, imeelezwa kuwa,Ustadh aliwajibu kuwa haoni tatizo katika tamko hilo kwani ni kweli kuwa Tanzania haiongozwi kwa sheria za kiislamu.Habari kutoka ndani ya usaili huo zimeeleza kuwa,Ilunga aliwaambia polisi,mtu kuitwa kafiri sio tusi.Ni sawa na wakatoliki wanavyowaita wasioukubali ukatoliki kuwa ni waprotestanti, yaani wapingaji japo ni wakristo pia.Katika uislamu mpingaji wa uislamu au sheria zake haitwi prostetanti bali kafiri,amewaeleza polisi.

Aidha katika usaili huo ambao ulikuwa ukirekodiwa katika mkanda wa video,imeelezwa Ilunga alihoji mantiki ya polisi kushughulika zaidi kuwakera waislamu katika misikiti yao na ibada zao badala ya kushughulikia maovu ambayo yametapakaa nchini.

Baada ya kuhojiwa kwa masaa kadhaa, Ustadh aliungana na kundi la waislamu waliokuwa wakimsubiri nje na kurejea nyumbani.Hata hivyo kabla ya kuondoka alitakiwa aache namba yake ya simu ili polisi wakimhitaji wamuarifu.

Habari kutoka Mwanza zimeeleza kuwa, ujumbe wa waislamu kutoka Dar es Salaam,Tabora,Bukoba na Shinyanga,umekuwapo mjini hapo kwa wiki moja sasa kufuatilia tukio hilo.

Pamoja na salamu za faraja kutoka kwa waumini, waliowatuma,wajumbe hao wamekuwa wakijadiliana na wenzao wa Mwanza namna ya kukabiliana na tukio hili waliloliita la kutatanisha.

Miongoni mwa masuala ambayo inasemakana wamekuwa wakihoji,kushauriana na kutafuta taawili yake ni hili kwamba mpaka sasa polisi hawajataka kuchukua hatua yoyote kujua kilichotokea.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook