Polisi wasaidie wananchi
Ndugu Mhariri
NIMEKUWA nikifuatilia utendaji wa kazi wa jeshi la polisi kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu sasa.
Nimelazimika kufanya shughuli hii kwa vile kwa kipindi hicho nimekuwa nafanyakazi ya polisi ya kulinda usalama wa raia wa mtaani kwetu pamoja na mali zao nikiwa kama mlinzi wa sungusungu.
Kwa kipindi hicho ambacho nimekuwa nikifanya kazi hiyo ya polisi bila mshahara nimegundua kuwa polisi wanapenda sana kazi za mezani za kuandika RB tu!
Kipindi hicho chote ambacho mimi na wenzangu tumekuwa tukifanya kazi hiyo katika mazingira magumu na silaha duni imekuwa vigumu kupata msaada wa polisi.
Polisi wamekuwa wepesi kutoa visingizio kila unapohitaji msaada Tunashukuru kuwa Mwenyezi Mungu amekuwa akitulinda na kutupa moyo wa kuendelea na kazi hiyo.
Polisi pamoja na mafunzo yao na silaha zao hawaipendi kazi ya kwenda mtaani kulinda usalama wa raia mali zao. Kwa mfano utawapelekea taarifa ya mwizi aliyemwibia mwananchi na kuwaelekeza anakopatikana watakuambia umkamate wewe mwenyewe halafu uwapelekee wafungue RB!
Utawapatia taarifa ya mtu aliyebaka na mahali alipo, watakuambia umkamate uwapeleke wao ofisini wakafungue RB!
Utawapigia simu polisi kuwa kuna majambazi wanavunja nyumba ya raia waje wawakamate, polisi wenye SMG zenye risasi thelathini watakuambia hawana usafiri au wako wachache kituoni.
Wahalifu wote waliokamatwa mtaani kwetu wamekamatwa na raia wenyewe na sio polisi.
Inapotokea polisi wakawakamata wale wanaohisiwa ni wahalifu, ni kwa ajili ya kutafuta "Takrima" tu hasa ukitilia maanani kuwa sasa CCM imeruhusu kutoa na kupokea "takrima".
Polisi wa nchi hii hawana msaada kwa raia zaidi ya kuwapiga virungu kwenye mikutano ya siasa na wakati wa kujiandikisha kupiga kura.
Kwa kumalizia natoa pongezi za dhati kwa kikosi cha zimamoto kwa jinsi wanavyojituma.
Pamoja na kutelekezwa na wizara yao ikiwa ni pamoja na kukosa vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi, askari wa zimamoto huwa anaitikia wito muda wowote wanapohitajika hata kama ni saa nane za usiku.
Huwa hawatoi visingizio vya kukosa hiki na kile, Mchapa kazi mzuri ni yule anayetumia nyenzo alizonazo kufanyakazi anayotakiwa afanye na sio yule ambaye ni bingwa wa kutoa visingizio.
Stanley Mathew,
S.L.P. 2544,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
TUNAWASHUKURU sana viongozi wa vyama vya siasa Tanzania hasa vya CCM, TLP na UDP kwa kutufahamisha wazi maana halisi ya neno udini.
Neno hili lilikuwa ni kitendawili kisichoteguka na fumbo lisilofumbuka ila wale waliolifumba hilo wamelifumbua.
Cha kufurahisha ni kwamba waliokitega ndio waliokitegua na aliefumba fumbo ndiye aliyelifumbua. Kwa hiyo bila shaka ukweli umebainika.
Wanaposema udini maana yake halisi ni Uislamu na Waislamu, kwa hiyo kila Muislamu ni mdini. Atende dini asitende dini akubali hilo au asikubali hiyo ni juu yake.
Makusudio halisi ya tamko hilo ni kwamba mwenye kuhusishwa na hilo tamko hastahili kuwa kiongozi wa nchi hata awe ana uwezo wa kuogoza au hana ana elimu ama hana maadamu ni Muislamu ni mdini. Lake ni kupiga debe viongozi wa Kikristo tu.
Bali ninachoshauri mimi kwa hili ni kwamba kama kufuata chama ambacho kiongozi wake ni Muislamu ni udini, basi ni bora tuwe wadini kuliko kuendelea kufuata vyama ambavyo vimeshatangaza uadui na Waislamu.
Qudra Al-Hassan,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
KUNA haja ya makusudi kabisa kuzindua umma huu wa Kiislamu kuweza kujua juhudi za makusudi zilizofanywa na Wamisheni na zinazoendelea kufanywa na serikali iliyopo madarakani kuhakikisha kwamba maeneo ambayo yana idadi kubwa kabisa ya Waislamu nchini yananyimwa mianya endelevu ya maendeleo ili Waislamu wazidi kubaki nyuma huku Wakristo wakipeta.
Ushahidi ni mikoa ya Tanga, Tabora na mingineyo ambapo Tanga ndiyo uliokuwa mji wa pili kwa kuwa na viwanda vingi nyuma ya Dar es Salaam, hivyo ulikuwa na ustaarabu mkubwa kabisa kwani walimu wa kwanza wengi Watanzania walitoka mkoa huu wa Tanga ikawa Manispaa ya kwanza.
Hivi sasa mambo ni kinyume kwani ndiyo miji ya mwisho kimaendeleo kwa serikali kuifanya "mark-time" kwa sera zisizo rasmi za udini. Ujumbe wangu ni kubadilisha mwelekeo.
Shime zindukeni wananchi msizugwe.
A. Kihama,
S.L.P 47,
Pangani, TANGA.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |