TAHARIRI

Wananchi wasiingiliwe uhuru wao

Jumamosi jioni, halikuwepo gari lililothubutu kukatiza Jangwani.Labda lililokuwa likipepea bendera ya C C M.

Aliyekuwa akiwahi Muhimbili kumpelekea mgonjwa wake chakula, akitokea Kimara, Ubungo Manzese na kwingineko kupitia Magomeni, alilazimika ama kupitia Kigogo hadi Ilala au atembee kwa miguu kuanzia Magomeni.

Wengi walioamua kupitia Kigogo, walijikuta wakichelewa kufika Muhimbili ndani ya wakati unaoruhusiwa kuona wagonjwa.

Foleni ilikuwa kubwa kukiwa na msongamano wa magari kuanzia makutano ya barabara ya Uhuru na Kawawa.Walioamua kutembea kwa miguu nao walifika wakiwa hoi.

Ni kwanini barabara hiyo ilifungwa bila kujali usumbufu ambao wangepata wananchi,hatujui. Na wala polisi waliokuwa wakizuia magari kupita, hawakuwa na maelezo zaidi ya kuhakikisha kuwa gari ambayo haikuwa inakwenda Jangwani kwenye mkutano wa CCM, haikatizi.

Waliokwama kufika Muhimbili kwa wakati kuwapelekea wagonjwa wao chakula na dawa, ni wananchi ambao ni wapiga kura.Pamoja nao,walikuwepo pia ambao kutokana na shida za aina tofauti, walikuwa wakienda maeneo mbalimbali jijini kupitia Magomeni -Jangwani.

Japo ilikuwa siku ya ufunguzi wa kampeni,ni wazi si wote ambao wangekuwa na fursa ya kwenda Jangwani au Kidongo chekundu.Kuwepo kwa mikutano ya kisiasa katika viwanja hivyo,haina maana kila kitu katika harakati za maisha kimesimama kutoa fursa kwa mikutano hiyo.

Ni kwanini basi wananchi wakwazwe katika shughuli zao, ni suala ambalo linatatiza.Pengine tujiulize,mkutano wa Jangwani ungeathirika vipi kwa magari kuendelea kupita barabarani kuelekea mjini? Je ni tatizo la kiusalama kwa vile Mh.Rais alikuwepo jangwani ?Kama ni suala la kiusalama ,mbona magari kutokea mjini yaliruhusiwa kupita?

Japo polisi wenyewe hawakusema kitu,lakini inasemekana barabara ilifungwa baada ya magari mengi,daladala,pick-ups na hata molori yaliyojaa wananchi yakiwa na bendera za CUF,kufululiza kuelekea Kidongo chekundu.

Kama chanzo ni hicho,kuna tatizo gani watu kwenda kwenye mkutano wao?.Si wananchi wana uhuru wa kuchagua chama halikadhalika ule wa kukusanyika?.

Je, ilitakiwa wananchi wote waishie Jangwani?.Ule uhuru wao wa kujiunga na vyama vya siasa utakuwa wapi sasa! Je, kufunga barabara hiyo ilikuwa ni kuwaadhibu wale ambao hawakutaka kwenda Jangwani?.

Tunadhani maadhali nchi imeamua kuingia katika mfumo wa vyama vingi, watu waachiwe uhuru .wao wa kujiunga na vyama wavitakavyo na kuhudhuria mikutano waitakayo.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook