Wazee Dar wamwombea Ujasiri Prof. Lipumba
WAZEE jijini Dar, wamemwombea dua Prof. Lipumba ili awe na ujasiri katika kuwakomboa wananchi kutokana na umasikini na madhila mengine.

"Ewe Mwenyezi mungu muepushie kila la shari kijana huyu. Muepushie na kila balaa.Mpe ujasiri na wape ujasiri wananchi", aliomba mzee mmoja kutoka Temeke.

Wazee hao walikuwa wamejazana katika ukumbi wa mikutano wa Starlight, asubuhi ya Jumamosi kuzungumza na Prof. Lipumba kabla ya uzinduzi wa kampeni za uchaguzi.

Katika hotuba yake, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba amesema, harakati za kukamata uongozi wa nchi ni nzito ambapo nguvu ya kujitoa muhanga ya wananchi na kutegemea msaada wa Mwenyezi Mungu ndiyo silaha yao.

Amesema Vyama vya CUF na CHADEMA havina dola bali vina nguvu inayotokana na kuungwa mkono na wananchi ambao wameazimia kujikomboa kutoka katika dhulma na ukandamizaji.

Amesema, hilo si jambo jepesi kwa kuwa wanayekabiliana naye ana nguvu ya dola kwa hiyo kujitoa muhanga na kutegemea msaada wa Mwenyezi Mungu ndilo jambo la msingi.

Profesa Lipumba alikuwa akizungumza na Wazee wa Dar katika ukumbi wa Star Light ambao walikusanyika kumuombea dua kuzindua rasmi kampeni za Urais, Ubunge, Uwakilishi na udiwani kwa vyama vya CUF na CHADEMA.

Aliwaambia wazee hao kuwa, nchi imefika njia panda hali ya umasikini imekithiri wakati nchi ikiwa inaingia miaka 40 ya uhuru.

Amesema, wananchi wanakandamizwa na kudhulumiwa kwa kukoseshwa huduma muhimu na kunyimwa mafao yao.

"Viongozi walioko madarakani hawaelewi shida za wananchi na wala hawaonekani kuguswa na hali ya dhiki waliyonayo raia wa nchi hii", Profesa Lipumba aliwaambia wazee hao.

Aliwakumbusha kuwa, cheche za harakati za kudai uhuru zilitokana na wakazi wa maeneo ya Pwani na ndio waliokuwa mstari wa mbele kuwaunganisha Watanganyika.

"Ni nyie mliokuwa mkichanga thumni thumni kuimarisha TANU wakati miaka ile sio hawa waliokuja kushika nyadhifa za uongozi", alisema huku akishangiliwa na wazee..

Kuhusu rushwa Mgombea huyo waliwaambia wazee kuwa sio tu ni adui wa haki bali pia ni kikwazo cha maendeleo.

Alisema, rushwa imekithiri nchini kiasi cha mtu ili apate haki yake hana budi kujipapasa.

Alisema, kipimo kizuri cha mizizi ya rushwa nchini ni kura za maoni za chama tawala zilizomalizika hivi karibuni.

Profesa Lipumba alisema, CCM imejijengea utawala wa vitisho na matumizi ya nguvu za dola.

Katika hali hiyoalisema, hata wale walioenguliwa kuwania ubunge kwa tiketi ya chama hicho, wamelazimika kusifu uamuzi huo japo hawakuelezwa sababu za msingi za wao kutupwa nje.

"Kusifu huko ni dalili za kutishwa baada ya hatua hiyo dhidi yao kuchukuliwa", alisema.

Baada ya hotuba hiyo ya Profesa Lipumba, mmoja wa Wazee alisimama na kuanza kuomba dua kwa lugha ya kiswahili.

Sehemu ya dua hiyo ilikuwa "Ewe Mwenyezi Mungu muepushe na kila shari kijana huyu, muepushe na kila balaa, mpe ujasiri na wape ujasiri wananchi".


Cuf yaahidi ajira kwa vijana

MOJA ya mikakati ya chama cha CUF iwapo Wananchi wataipa ridhaa kuongoza nchi oktoba 29, utakuwa kujenga viwanda vipya na kuboresha vilivyopo ili kutoa ajira kwa vijana waweze kujikimu kimaisha.

Aidha amesema, Serikali hiyo itaboresha Sekta ya Kilimo kwa ajili ya mazao ya chakula na biashara, kufufua Viwanda na kuongeza Tija.

Ili kuleta ufanisi Prof. Lipumba amesema, CUF na CHADEMA wataunda serikali ndogo isiyozidi wizara 15, watapunguza matumizi yasiyo lazima ya safari za mara kwa mara nje ya nchi na kuondoa kabisa ukarabati wa kila mwaka wa Ikulu.

Hayo aliyazungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za vyama hivyo uliofanyika uwanja wa Kidongo Chekundu Jijini jumamosi iliyopita.

"Mkituchagua tutaongeza tija kwa wananchi, tutainua sekta ya viwanda ili kuongeza ajira. Tutaimarisha sekta ya kilimo na kuongeza pato la fedha za kigeni", Profesa Lipumba aliuambia umati mkubwa wa wananchi uliohudhuria mkutano huo.

Aliahidi kuboresha Kilimo ili nchi ijitosheleze kwa chakula na mazao ya biashara hali ambayo amesema itachangia maendeleo ya kila sekta.

Aliikosoa serikali inayomaliza muda wake kwa kupuuza Kilimo na kutowajali wakulima ambapo alisema wazalishaji wa zao la kahawa Bukoba wanaishi maisha ya dhiki huku wakizalisha zao hilo la biashara.

Alisema Wakulima wa kahawa wa Bukoba Tanzania ni wa mwisho kimapato katika wazalishaji wa zao hilo duniani.

Kuhusu tatizo la ajira kwa vijana wengi alisema, serikali yake itahakikisha kila kijana mwenye uwezo wa kufanya kazi anapata ajira ili kumuwezesha kujikimu kimaisha.

Juu ya suala la elimu, Profesa Lipumba alisema, serikali yake itahakikisha elimu ya lazima inakuwa bure kwa watoto wote.

Alisema sasa hivi vijana milioni 3 wenye uwezo wa kwenda shule hawapo mashuleni. Na kila mwaka wanaongezeka.

"Tukiingia madarakani itakuwa marufuku kufukuza mwanafunzi eti hajalipa ada", alisema Profesa huku akishangiliwa na halaiki ya wananchi waliokuwa kimsikiliza.

Aidha aliahidi kuwa serikali yake itatilia mkazo elimu ikiwa ni pamoja na kuwalipa vizuri waalimu sambamba na kuinua elimu ya msingi na sekondari ambayo amesema hivi sasa imeshuka kwa kiwango kikubwa.

Kuhusiana na afya mgombea huyo alisema serikali yake itahakikisha kila mwananchi anapata matatibu na zaidi itashughulikia kinga za maradhi mbali mbali.

Akizungumzia hali mbaya ya usafiri iliyopo nchini hivi sasa, Profesa alisema ubovu wa barabara umekwamisha mawasiliano hali iliyosababisha baadhi ya mikoa ionekane kama si sehemu ya Tanzania.

"Hivi sasa ukitaka kwenda Bukoba lazima uwe na Passport unalazimika kupitia Kenya au Uganda", alisema na kusisitiza "tukiingia madarakani tutatengeneza barabara za Dar es Salaam mpaka Mwanza na ile ya Lindi".

Juu ya suala la ukusanyaji na ulipaji wa kodi, alisema kodi inayokusanywa sasa na serikali haichangii maendeleo ya nchi bali inawanyanyasa wananchi wa chini.

"Tukiingia madarakani kodi zinazoitwa za maendeleo tutazifuta. Hizi ni kodi za manyanyaso. CCM inawatoza watu wa chini kodi na kuwasamehe watu wa juu. Kodi za manyanyaso zinaingiza fedha chache mno ikilinganishwa na kodi zinazosamehewa watu wa daraja la juu", alisema.

Kampeni za kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano, Zanzibar, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani, zilianza rasmi jumamosi ambapo vyama mbali mbali vilifanya mikutano ya hadhara kuwatambulisha wagombea wa nafasi hizo.

Vyama vya CUF na CCM vilifanya mikutano yao siku ya jumamosi katika viwanja vya Jangwani na Kidongo Chekundu.

Chama cha TLP kilifanya mkutano wake wa hadhara siku ya jumapili katika uwanja wa Kidongo Chekundu na kumtambulisha mgombea wake wa Urais Bwana Agustino Mrema.


Moro wawalaani polisi Mwanza

WAISLAMU mjini hapa wamelaani vikali hatua ya polisi Mwanza kuonesha chuki za wazi dhidi ya Waislamu kufuatia polisi kutochunguza tukio la kuvamiwa na kukatwa kwa mapanga Ustadh Ilunga Hassan Kapungu

Wakiongea na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni wamesema,polisi kutokuona umuhimu wa kuchunguza tukio hilo,ni ushahidi mwingine kuonyesha jinsi waislamu wanavyonyanyaswa nchini hapa.

"Hii nayo inaweza kutupa wawasi kwamba huenda yaliyomkuta ustadh ni jambo la kupangwa", alisema Ustadh Juma Mohamed mswaliji wa Msikiti wa Mafiga 'A'.

Aliendelea kusema Ustadh huyo kuwa huu ni ushaidi mwingine wa kisayansi kwa Rais Mkapa kwamba hakuna uadilifu na kwamba watu wananyanyaswa kwa ajili ya dini zao..

Mwingine aliyelaani kitendo hicho ni Mwalimu Ally Issa ambaye alisema kwamba sasa imekuwa ni kawaida kwa viongozi wa serikali kuwapelekea Waislamu misiba kutokana na jinsi wanavyoshughulikia matatizo yanayowahusu.

"Kwa kweli mimi kilio changu bado kipo kwa serikali kutokana na kufumbia macho unyanyasaji unaofanywa na vyombo vyake vya dola dhidi ya Waislamu, ambapo tukio la Ustadh Ilunga lingemtokea mtu wa Kanisa, sidhani kama dola ingempuuza na kudai kuwa mtu huyo walikuwa wakimtafuta sana", alisema.


Mkapa jukwaa moja na Mtopea

Mgombea urais kupitia CCM, Mh. Benjamin William Mkapa amesema, ameongoza kwa haki, uwazi, ukweli na uadilifu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Mh. Mkapa ameyasema hayo alipokuwa akizindua kampeni za uchaguzi katika viwanja vya Jangwani Jumamosi.

Aidha katika mkutano huo, mtu mmoja aliyeitwa sheikh Mtopea alisoma aya aliyodai ni ya Qur'ani lakini isiyopatikana popote katika msahafu.

Mtopea alisoma aya hiyo, akiwashambulia waislamu huku akitiwa mori na wana CCM walionadi, "waambie hao" na wengine wakipiga takbira za kejeli.

Akiwa jukwaani alimokuwa Mh. Mkapa na Rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi, Mtopea alisema, "INNA LLAHA LA YUGHAYYIRU NIIMATIHI, HATTA YUGHAYYIRU MA BIANFUSIKUM"

Mashekh mbalimbali walioongea na gazeti hili wamesema, hakuna 'aya'.kama hiyo katika msahafu.

Labda "wakati Rais Mkapa akizindua kampeni za chama chake, sheikh Mtopea alikuwa akizindua Qur'an yake", amesema sheikh Bassaleh katika taarifa yake ya maandishi.

Kuhusu Takbiira zilizopigwa, imewashangaza waislamu wengi, kuhusu hatua hiyo ya wana CCM kushabikia kufanyiwa kejeli Qur'an.

"Haiwezi kuwa hiyo ilikuwa ni akili ya Mtopea pekee.Ulikuwa mkakati wa CCM kuikejeli Qur'an.Mbona walikuwa wajuzi kama Mzee Mwinyi na hawakumkemea",amehoji Mzee Uwesu wa Mburahati.

Mzee Uwesu alinukuu aya isemayo:"Naye amekwisha kuteremshieni katika kitabu hiki ya kwamba mnaposikia aya za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na zinafanyiwa kejeli,basi msikae pamoja nao, mpaka waingie katika mazungumzo mengine.(Mtakapokaa) mtakuwa mfano wao. Hakika Mwenye zi Mungu atawakusanya wanafiki na makafiri wote pamoja katika Jahannamu".(Annisai 4:140).

"Walikuwepo waislamu wanaozijua aya hizi, lakini wakaweka mbele ushabiki wa CCM yao na kuhiyari Qur'an ikejeliwe",amesema Ustadh Salimu.

Mh. Rais Mkapa akiongea alisema, amesimamia vizuri mshikamano na umoja wa Watanzania hali iliyopeleka kudumishwa kwa amani na utulivu.

Aidha alisema dalili kuwa amefanikiwa katika utendaji wake wa kazi ni kuja nchini kwa Rais Bill Clinton.

Mkisikia Rais Clinton wa Marekani anakuja Tanzania, mjue tumefanya kazi kweli", Mhe. Mkapa aliwaambia wana CCM waliofurika katika viwanja vya Jangwani.

Aidha alisema, amelinda uhuru na kutetea umoja wa taifa, ni kwa sababu hiyo Rais Mstaafu wa awamu ya pili aliyemkabidhi madaraka ametoa ruhsa aendelee..

Kuhusiana na kero ya rushwa alisema, CCM imeendelea kupiga vita rushwa na kwamba tayari imeshawafikisha wengi mahakamani na wengine kustaafishwa kwa manufaa ya uma kutokana na kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Aliwatahadharisha WanaCCM kuwa wasipojizatiti Wapinzani watawapokonya uongozi wa nchi na hasa Ubunge katika mikoa mbalimbali likiwemo Jiji la Dar es Salaam.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook