Msuguano kati ya Waislamu na Nyerere

SIKU ya pili yake serikali ikatoa amri Shariff Hussein afukuzwe nchini pamoja na mdogo wake Mwinyibaba ingawa yeye Shariff Hussein hakuwepo hata kwenye hafla ile ya maulid kwa kuwa alikuwa nje ya Dar es salaam.

Shariff Hussein na Mwinyibaba ikabidi waondoke na kurudi kwao Kenya.

Kwa kauli yake mwenyewe Shariff Hussein alimfahamisha mwandishi kuwa yeye wakati wa uhuru alikuwa akishiriki katika dua nyingi za kumuombea Nyerere mafanikio. Shariff Hussein akasema lakini malipo yake kutoka kwa Nyerere ilikuwa ni kumfukuza nchini.

Lakini ili ieleweke sababu ya kutiwa kizuizini hawa masheikh inabidi turudi nyuma katika mkutano wa mwaka wa EAMWS uliofanyika mwaka 1963.

Jaribio la mwanzo la Nyerere kutaka kuivunja EAMWS lilikuwa mwaka 1963. Lakini jaribio hilo halikufanikiwa kwa sababu ya mpango uliopangwa na Mufti Sheikh Hassan bin Amir na kutekelezwa na Bilali Rehani Waikela, katibu wa EAMWS Tabora.

Mwaka huu wa 1963 EAMWS ilifanya mkutano wake katika ukumbi wa Shule ya wasichana ya Aga Khan. Wajumbe wa mkutano huo walipowasili mjini Dar es Salaam walikuta uvumi kuwa wajumbe wa mkutano wa EAMWS watakamatwa na kuwekwa kizuizini. Chanzo cha uvumi huu hakikufahamika lakini haikuwa vigumu kuhisi.

Baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Wazee wa TANU mwaka ule ilikuwa wazi kuwa Nyerere alikuwa amewatupa mkono washirika wake wa zamani na sasa alikuwa akitafuta wapya ili kujenga upya msingi wake wa siasa. Kutokana na mambo yalivyokuwa yakienda ilikuwa ni dhahiri washirika wake wapya hawatakuwa Waislamu.

Katibu wa EAMWS Tabora, Waikela alipowasili Dar es Salaam kuhudhuria mkutano aliitwa na Sheikh Hassan bin Amir. Mufti Sheikh Hassan bin Amir mbele ya Mzee Ali Comorian, alimfahamisha Waikela kuwa kulikuwa na njama zilizokuwa zikipikwa na Nyerere kumungamiza yeye na Tewa Said Tewa ili kuvunja EAMWS ipatikane nafasi ya kuanzishwa jumuiya ya Kiislamu ya Watanganyika itakayokuwa chini ya wanafiki.

Sheikh Hassan bin Amir alimwambia Waikela kuwa harakati za uhuru zilikuwa zinatekwa nyara na Wakristo kwa manufaa ya makanisa yao.

Sheikh Hassan alimfahamisha Waikela kuwa ni lazima yeye afanye kila linalowezekana ili njama za Nyerere zishindwe. Waikela alimuuliza Sheikh Hassan bin Amir kwa nini amechaguliwa yeye kufanya kazi ile. Sheikh Hassan bin Amir alimuambia kuwa yeye ana imani na uwezo wake.

Baada ya maneno hayo Sheikh Hassan bin Amir alinyanyua mikono yake juu na kumuombea dua Waikela. Nyerere alikuwa anamfahamu Waikela kwa kuwa alikuwa muasisi wa TANU na alikuwa ametoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru.

Nchi nzima hasa sehemu za Waislam kulikuwa mpango wa serikali wa kuwavunja Waislam nguvu na kuwakatisha tamaa.

Waikela, kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine wa EAMWS alikuwa anasuguana na Mkuu wa Mkoa wa Jimbo la Magharibi, Richard Wambura. Kulikuwa na ujeuri kwa upande wa serikali walipokuwa wanashugulikia matatizo ya Waislamu, mbali na mategemeo ya Waislamu waliyokuwanayo kabla ya uhuru. Subira ya Waikela ilifikia kikomo pale Wambura alipowatukana Waislamu katika mkutano wa hadhara.

Baada ya kuhutubia Wambura, Waikela alipanda jukwaani na akaikumbusha serikali isiwe mwizi wa fadhila kwa kusahau jinsi Waislamu walivyojitolea muhanga katika kudai uhuru.

Serikali ikachukulia hotuba ya Waikela kama usaliti na yenye kuwashawishi Waislamu wasiitii serikali.

Ilikuwa katika hali hii Waikela mwanachama shupavu wa TANU alijitoa kwenye chama na akaamua kutumia nguvu zake kuwatumikia Waislamu kupitia EAMWS.

Ilikuwa wazi kuwa Nyerere alikuwa na habari za msuguano kati ya serikali na Waislamu kule Tabora na mtu ambae alikuwa akihusika na msuguano huo.

Siku kabla ya mkutano wa EAMWS, Nyerere aliwaalika wajumbe wa mkutano Government House kwa chakula cha usiku. Hao waalikwa walikuwa wajumbe waliochaguliwa mahsusi. Waikela hakuwa mmoja wa hao waalikwa.

Nyerere alichukua nafasi ile kuwashauri wajumbe wale waanzishe jumuiya ya Waislamu wa Tanganyika ichukue nafasi ya EAMWS. Wajumbe hawa walipoleta katika mkutano hoja ya kuanzisha jumuiya ya Waislamu wa Tanganyika, Waikela alisimama na kuipinga hoja ile. Alizungumza vilevile kuhusu uadui wa serikali kwa Waislam na Uislamu. Waikela alimaliza hotuba yake kwa kutoa changamoto kwa wajumbe wamuite Nyerere kwenye ufunguzi wa mkutano ili aje awaeleze wajumbe msimamo wake kuhusu kadhia hii ya chinichini baina ya serikali na Waislam.

Baada ya kushindwa kwa hoja ya kuivunja EAMWS wajumbe wa mkutano ikaonekana kuwa ingekuwa vyema Nyerere aitwe kufunga mkutano ule na asomewe makubaliano yaliyofikiwa. Nyerere alifika kufunga ule mkutano na akakutana uso kwa uso na Waikela, ambae alimsomea maazimio ya mkutano.

Waikela alimfahamisha Nyerere kuwa umoja kwa Waislamu ni fardh - wajibu wa lazima. Ni kwenda kinyume na maamrisho ya Allah kuwagawa watu.

Baada ya utangulizi huu Waikela huku akimnyooshea Nyerere kidole alieleza uadui unaoonyeshwa na serikali dhidi ya Waislamu. Waikela alimaliza hotuba yake kwa kitisho. Alimwambia Nyerere ikiwa Waislamu watamgeuka kupambanana yeye hatakuwa na uwezo wa kuwashinda. Nyerere alitulia tuli pembeni mwa Rais wa Baraza la Tanganyika la EAMWS Tewa Said Tewa akimsikiliza Waikela. Aliposimama kujibu hotuba ya Waikela Nyerere kwa upole alisisitiza msimamo wa serikali wa kutoa haki na usawa kwa raia wake wote. Kwa kiasi fulani Nyerere alikuwa amefanikiwa kupunguza joto kati ya Waislamu na serikali. Hotuba ya Waikela na ya Nyerere zikapewa umuhimu mkubwa katika radio. Waislam wengi wakajitokeza stesheni ya gari moshi Tabora kuja kumpokea shujaa Waikela. Alipewa heshima ile kwa kuwa na ujasiri wa kuweza kusimama kidete dhidi ya wale waliodhani kuwa wanaweza kuwakalia Waislamu vichwani. Nyerere alihisi ameumbuka na hili lilimchoma moyo sana. Kuanzia hapa Nyerere hakumtazama Sheikh Hassan bin Amir kwa jicho jema. Alingoja nafasi yake ili alipize kisasi. Mwaka ukiofuata, tarehe 20 Januari, 1964 jeshi liliasi. Nyerere alichukua fursa ile kuwatia kizuizini masheikh walioonekana wanapinga serikali na viongozi wa vyama vya wafanyakazi. Waikela alikuwa mmoja wa wale waliokamatwa na kuwekwa kizuizini. 17 Nyerere kwa wakati ule hakuwa na nguvu ya kumgusa Mufti Sheikh Hassan bin Amir.

Viongozi wa EAMWS walitishwa na makachero wa serikali watupe nyaraka na kumbukumbu zote za EAMWS au sivyo serikali itawachukulia hatua. Viongozi wengi walitishika na kuchoma moto majalada yao.

Waikela alihifadhi nyaraka na majalada yake yote hadi yakamfikia mwandishi baada ya zaidi ya miaka ishirini baada ya kufungiwa jumuiya hiyo. Regional Commissioner wa Jimbo la Magharibi wakati ule alikuwa Rashid Heri Baghdelleh yeye alikwenda kuonana na wafungwa wa siasa katika jela ya Uyui akiwa na salamu kutoka kwa Rais Nyerere kuwa wafungwa wa siasa waombe msamaha na yeye atawaacha huru. Waikela alikataa kuomba msamaha na hoja aliyotoa ilikuwa yeye hajatenda kosa lolote kwa hiyo haoni haja ya kuomba msamaha.

Baada ya kutoka kizuizini mwaka 1965, Waikela alikuta ofisi ya EAMWS Tabora imefungwa na Waislam wanatishwa na serikali wasiifungue.

Waikela aliwashawishi Waislamu wakusanye sahihi zao na wamplekee kuomba ofisi ifunguliwe. Hili lilifanyika na ofisi ile ikafunguliwa upya chini ya Waikela na ikaendelea kutoa huduma kwa Waislam kwa miaka mitatu hadi serikali ilipoivunja EAMWS mwaka wa 1968.

Mwaka wa 1963 shughuli za kueneza dini za EAMWS zilikuwa zikienda vizuri sana. Tabligh ilikuwa chini ya Sheikh Amir bin Juma kutoka Tanga na Wakristo wengi walikuwa wakirudi katika Uislamu.

Tabligh ilikuwa ikiongozwa kutoka kwa masheikh wa mikoa na wilaya. Fedha za kufanyia shughuli hizi zilikuwa zikichangwa na Waislamu wenyewe.

Mufti Sheikh Hassan Bin Amir yeye alikuwa akisomesha fikh, mantik, tauhid, na tafsir ya Qur'an katika misikiti mbalimbali ya Dar es Salaam Wakati ule Katibu Mkuu wa EAMWS kwa Afrika ya Mashariki alikuwa V.M. Nazarali.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook