TOLEO la gazeti hili la Julai 28, liliwanukuu Waislamu wa kijiji cha Mnadani wilaya ya Kilombero wakiomba msaada wa walimu wa dini ili kusaidia kuimarisha dini kwenye kijiji hicho.
Kwa mujibu wa Sheikh wa kijiji hicho, Sheikh Hemed Issa Mbeka aliyeongea na mwandishi wa gazeti hili idadi ya waumini katika kijiji hicho imekuwa ndogo kutokana na wengi wao kutokuwa na elimu juu ya Uislamu.
Aidha, alisema, kutokana na kutokuwepo na uhamasishaji juu ya Uislamu watu wengi wamekuwa wakiritadi.
Sheikh Mbeka aliwataka Masheikh na Maustadh waliorundikana mijini kutembelea vijijini ili kuhamasisha dini na kutoa da'awa kwa waumini mbalimbali.
Hali ya ukosefu wa Masheikh na walimu wa dini imejitokeza katika vijiji vingi hapa nchini.
Kama alivyoeleza Sheikh Mbeka vijiji vingi pia vina Waislamu wanaoingia katika dini nyingine kwa sababu ya kutokuwepo na watu wa kuhamasisha dini na kuwafundisha watu elimu ya Uislamu.
Hali imejitokeza wakati mijini kuna Masheikh na Maustadh waliorundikana wengi wao wakiwa hawana kazi.
Kama alivyoeleza Sheikh Mbeka ukosefu wa elimu na watu wa kuhamasisha dini ni tatizo ambalo limezuia kushamiri kwa Uislamu katika maeneo mengi ya nchi.
Kwa mfano, katika kijiji kimoja huko Nzega kulikuwa na tatizo kama hilo. Mwandishi wa habari hizi ambaye alitembelea kijiji hicho mwaka 1994 alikikuta kijiji hicho kikiwa na hali ya kusikitisha wakati huo watu waliokuwa wakifahamika kuwa ni Waislamu walikuwa wanne tu katika kijiji kizima. Hakukuwa na Msikiti wala madrasa na Uislamu ulikuwa hauna nguvu kabisa.
Ilielezwa kuwa baadhi ya Waislamu kwa kutopata elimu ya dini walikuwa hawaujui hata Uislamu wao na walikuwa wakiishi kama Waislamu jina tu. Hakuna kuswali wala kufunga Ramadhani.
Katika hali hiyo ulaji vibudu, ulevi na kushiriki katika imani za kimizimu vilionekana kuwa vitu vya kawaida.
Hata hivyo, Ustadh mmoja aliyetoka wilaya ya Bukoba na kwenda kwenye kijiji hicho kuchimba madini ndiye aliyenusuru hali hiyo.
Ustadh huyo ambaye alisoma elimu ya dini huko Bukoba alishangazwa na hali hiyo na ndipo alipoanzisha harakati za kuujenga Uislamu katika kijiji hicho kwa kutoa da'awa.
Alipofanikiwa kuwavuta watu wengi alianzisha madrasa ya kuwafundisha watoto Qur'an na baadaye aliendesha mchango wa ujenzi wa Msikiti.
Alitembea katika Misikiti ya Nzega kuwaomba waumini wasaidie ujenzi Msikiti wa kijiji hicho wakajitokeza wafadhili mbalimbali kuchangia ujenzi wa Msikiti huo.
Akiilezea hali hiyo, mkazi mmoja wa kijiji hicho alisma kutokana na watu wengi kujaa hamasa ya Uislamu Wakristo wengi walimiminika kwa Ustadh huyo kutaka awasilimishe. Na hivi sasa Msikiti uliojengwa unasaliwa Ijumaa na madrasa imejaa watoto wanaofundishwa Qur'an tukufu.
Jambo jingine alilolieleza ni kuwa uchinjaji ovyo wa nyama za nguruwe na ulaji wa vibudu umeachwa baada ya watu wengi kusilimu.
Kwa mfano huo ni muhimu kuuzingatia wito wa Sheikh Mbeka wa kuwataka Masheikh na Maustadh kwenda katika kijiji ambako dini imezorota ili kutoa da'awa na kuhamasisha Uislamu.
Ni jukumu la Masheikh wetu na Maustadh wa madrasa kutumia elimu zao kueneza na kuimarisha Uislamu mahali popote kwani Uislamu ni elimu waliyonayo ambayo haina budi kunufaisha na wengine.
Ni kweli kuwa hali duni ya kiuchumi imekuwa kikwazo kikubwa kwa Maustadh kwenda vijijni wakitegemea kukaa mijini kupata riziki lakini hatuoni vizuri dini ya Allah ikizorota sehemu fulani kwa sababu ya kiuchumi.
Taasisi za Kiislamu, vyuo na madrasa ambazo hutoa wanafunzi wa Kislamu vingesaidia kuchukua jukumu la kupeleka wanafunzi wao wanaohitimu kwenda kuhamasisha na kutoa elimu ya dini kwenye vijiji kwa utaratibu maalum.
Utaratibu huo ni kwamba mwanafunzi kabla ya kumaliza masomo yake ajitolee angalau kwa miezi sita kwenda kusomesha kwenye kijiji chochote kile atakachopangiwa. Akimaliza kipindi hicho aende mwanafunzi mwingine kuchukua nafasi yake.
Utaratibu huo wa kuwapeleka kwa vipindi maalum Maustadh hao utasaidia kudumisha uhamasishaji wa dini katika vijiji na pia kuwaondolea uchovu Maustadh hao kukaa vijijini kwa muda mrefu.
Ama kuhusu ni nani atagharamia ukazi wa Maustadh hao vijijini, taasisi na vyuo vitakavyotoa Maustadh hao vingepanga mikakati ya kupata fedha ikiwa ni pamoja na kuomba wafadhili wawagharimie.
Kwa mfano utaratibu huo umekuwa ukitumiwa na madrasa Shamsiya na Zahrau za mjini Tanga ambazo hupeleka walimu katika baadhi ya vijiji kufundisha elimu ambapo wanavijiji hao husaidia kuchangia gharama za walimu hao kama posho za matumizi, nyumba na kadhalika.
Utaratibu huo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha dini katika vijiji mbalimbali vya mkoa wa Tanga.
Vyuo na madrasa zingine zilizopo mikoani zinapaswa kuiga mfano huo kwa kuwasiliana na wafadhili na vijiji mbalimbali ambavyo vina matatizo ya walimu.
Jambo hili likifanyiwa mshikamano nchi nzima huenda tatizo la uhaba wa walimu vijijini likapungua kwa kiasi kikubwa.
Wakati umefika kwa taasisi za Kiislamu kuacha kuendesha harakati za Uislamu katika miji tu bali wafikishe huduma zao hadi katika vijiji ambako pia wanahitaji si walimu tu bali hata kujengewa Misikiti na madrasa.
Aidha, Masheikh mbalimbali wanaozunguka mikoani kuendesha mihadhara ya kidini katika Misikiti waende pia vijijini badala ya kuishia mijini kwani waumini wanaohitaji kupewa da'awa hawapo mijini pekee.
Kama Masheikh hao wameweza kujidhamini wenyewe kufanya ziara hizo mjini hawawezi kushindwa kwenda vijijini, kinachohitajika ni dhamiri zao za kuujenga Uislamu na moyo wa kujitolea.
Si vizuri Masheikh na walimu kurundikana mijini
wakati vijijini watu wanakula vibudu kwa kutojua Uislamu.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |