Mikutano ya hadhara ya TANU 1954-1961

Mikutano ya TANU ya siku za mwanzo ilikuwa ikifanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja mbele ya Princess Hotel.

Kwenye jukwaa lililojengwa kwa miti walikuwa wakikaa wale viongozi wa mstari wa mbele ndani ya TANU - Nyerere rais wa TANU, Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU, Bibi Titi Mohamed, John Rupia na Clement Mtamila.

Sahani ya santuri ilikuwa ikipigwa katika gramafoni kupitia kipaaza sauti.

Mwimbo uliokuwa ukipigwa ulikuwa wa Frank Humplink. Frank alikuwa kijana wa Kichagga kutoka Moshi. Baba yake alikuwa Mzungu. Hamplink alikuwa mwimbaji na mpiga gitaa maarufu sana wakati ule akipiga muziki wake na dada zake wawili Maria na Regina Humplink.

Katika nyimbo zake nyingi Frank alikuwa akiimba pamoja na dada zake. Mwimbo uliopendwa sana na TANU na ndiyo uliokuwa ukipigwa katika kila mikutano yake yote na uliosisimua wananchi ulikuwa na mashairi yafuatayo, 'Uganda nayo iende, Tanganyika ikichangamka, Kenya na Nyasa zitaumana'.

Mwimbo huu ulikuwa na ujumbe wa kisiasa kwa Waafrika wa Tanganyika. Ujumbe katika wimbo huo ulikuwa kuwa, Tanganyika itakapoamka, kutakuwa vilevile na mapambano nchini Uganda, Kenya na Nyasaland.

Ulikuwa ukivuma toka kwenye vipaza sauti mfululizo kabla ya mkutano huku watu wakikusanyika viwanjani. Haikupita muda mrefu serikali ya kikoloni ilipata maana halisi ya wimbo huo. Mara moja mwimbo huo ukapigwa marufuku na serikali.

Serikali ya kikoloni iliamuru kwamba mashairi ya wimbo huo yanachochea watu kuasi. Lakini kabla ya mwimbo huo kupigwa marufuku ulipendwa sana na ukwa ukiombwa na wasikilizaji na kupigwa katika kituo cha radio 'Sauti ya Dar es Salaam'. Kituo hicho cha radio kikaacha kupiga nyimbo hiyo.

Huenda huu ulikuwa wimbo wa kwanza kupigwa marufuku katika historia ya utangazaji Tanganyika. Kwa muda mrefu sana mwimbo huu ulikuwa kama nyimbo rasmi ya TANU. Inaelekea uzalendo na shauku ya uhuru ndiyo vitu vilivyomtia hamasa Humplink hata akatunga na kuimba nyimbo hiyo.

Katika mikutano ya TANU katika zile siku za mwanzo, kabla Nyerere au Bibi Titi kuhutubia umma, Sheikh Suleiman Takadir alikuwa akisimama na kuomba dua. Kwa kawaida alikuwa akisoma ghaibu Surat Fatihah, sura ya kwanza katika Qur'an Tukufu:

"Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu. Kila sifa njema ni milki yake Mwenyezi Mungu, Mola wa Ulimwengu wote. Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu. Mfalme wa siku ya Hukumu. Wewe tu ndiyo tunayekuabudu na wewe tu ndiyo tunakuomba msaada. Tuongoze katika njia iliyonyooka, njia ambayo umewaongoza wale uliowaneemesha, si ya wale uliowaghadhibikia wala ya wale waliopotea".

Hii ni dua ambayo kwa kawaida husomwa na Waislam kabla ya kuanza jambo lolote la kheri. Wakati Sheikh Takadir akisoma dua hii watu walikuwa wima mikono yao juu wakimshukuru Allah. Baada ya hapo Nyerere au Bibi Titi, kutegemea na ujumbe maalum uliotaka kutolewa katika siku hiyo, alikuwa akisimama na kuhutubia.

Bibi Titi alikuwa akijulikana kwa maneno yake makali wakati Nyerere alikuwa bingwa wa fikra tulivu na utoaji wa ujumbe mzito. Sheikh Suleiman Takadir mwenyewe, vilevile alikuwa msemaji mzuri sana. Ilikuwa kwa sababu hii na umri wake mkubwa ndiyo alipewa heshima na wazee wa mji ya kuzungumza kwanza kabla ya yoyote hajasema na kuomba dua, kisha kumtambulisha Nyerere kwa wananchi.

Katika siku hizo Nyerere alikuwa akivaa kaptura na soksi ndefu, mavazi yaliyopendwa na walimu wa shule na hasa kivazi kilichopendwa na wale waliojiona wameelimika, hususan watu wenye asili ya bara. Nyerere amenukuliwa akisema kuwa ilikuwa Dossa Aziz ndiye aliyemtahadharisha kuwa maadam sasa anachanganyika na wazee haitakuwa vyema kwake kuonekana amevaa kaptura.

Hotuba hii aliyotoa Nyerere siku ile pale Mnazi Mmoja ambapo aliwaeleza watu kuhusu safari yake kwenda Umoja wa Mataifa ilikuwa ndiyo mwanzo hasa wa historia mpya ya Tanganyika. Kabla ya hapo Waafrika wa Tanganyika hawakupata kuonyesha shauku na matumaini katika mustakbali wao.

Katika viwanja vya Mnazi Mmoja Nyerere aliwaeleza halaiki ya watu wenye furaha na waliokuwa wakimsikiliza kwa makini kuwa miongoni mwa mataifa kumi na mbili yanayounda Baraza la Udhamini saba kati yao yalitoa idhini kuwa muda wa utawala wa ndani wa Tanganyika utakapowadia, Waafrika lazima wapewe nchi yao.

Katika hotuba yake Nyerere alitilia mkazo sera ya TANU kuhusu mahusiano mema baina ya Waafrika na watu wa mataifa mengine na aliwaonya wanachama wa TANU ambao walikuwa wameanza kuwabagua watu wa rangi tofauti kuwaambia kuwa hivyo haikuwa sawa. Alisisitiza juu ya umoja miongoni mwa wananachi na hatimaye aliwadhihaki wasikilizaji kwa kuwauliza ikiwa wangesubiri kwa miaka ishirini na tano kuwa huru.

Halaiki hiyo ya watu kwa pamoja ilipiga kelele, 'hapana'. Wananachi kwa pamoja walijibu kwa sauti kubwa wakisema walitaka uhuru kesho au kesho kutwa.

Nyerere ambaye alikuwa akiogopa kuchukua uongozi wa TANU tangu 1953 alikuwa amefarajika sana na mshikamano huu ulioonyeshwa na wananchi.

Sasa ilikuwa dhahiri kwake kwamba rafiki yake Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz, Rupia na uongozi mzima wa TANU pamoja na lile Baraza la Wazee lilikuwa limemsafishia njia kuongoza harakati kwa niaba yao. Lakini Padri Walsh na Wamishionari katika shule ya Mtakatifu Francis, Pugu, walitazama harakati hizi kwa mtazamo mwingine kabisa. Wamishionari hawakuweza tena kumvumilia Nyerere kuwa mmoja wa walimu katika shule yao.

Hatima ile ile iliyowasibu wazalendo wengine kabla yake sasa ilimkabili Nyerere. Aliambiwa ama abakie mtumishi mtiifu wa kanisa au ajiuzulu; Kanisa halikuweza kukaa kimya na kumuangalia Nyerere akiwatumikia mabwana wawili.

Nyerere alilipeleka tatizo hili kwa Clement Mtamila, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya TANU. Mtamila aliitisha mkutano wa kamati kuu nyumbani kwake mtaa wa Kipata na TANU ilijadili tatizo hilo. Miongoni mwa wajumbe wa kamati ile mbali na Rupia na Kambona walikuwa Bibi Titi Mohamed na Bibi Tatu bint Mzee.

Kamati Kuu ya TANU ilimshauri Nyerere ajiuzulu. Tafrani hii ilitokea wiki chache tu baada ya kurudi kutoka Umoja wa Mataifa katika wiki za mwisho za mwezi Machi. Tarehe 23 Machi, 1955 Nyerere alijiuzulu ualimu. Ilikuwa adhuhuri Nyerere alipokuja Dar es Salaam kutoka Pugu, akiwa si mwalimu wa shule tena.

Inasemekana aliposhuka tu kwenye basi alikwenda moja kwa moja ofisini kwa Abdulwahid katika soko la Kariakoo kumpasha habari rafiki yake. Nyerere alikaa na Abdulwahid katika nyumba yake namba 78 Mtaa wa Stanley. Baadaye kidogo Nyerere alirudi kijijini kwake huko Musoma. John Hatch alipokuja Dar es Salaam kwa mwaliko wa TANU Nyerere alikuwa kwao kijijini.

Tutaona hapo baadae kidogo jinsi mgeni huyu Mwingereza alivyomgutusha Schneider Abdillah Plantan kuhusu TANU kuwashirikisha wanawake katika harakati za kudai uhuru.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook