Jibuni madai ya Waislamu msiwatukanie dini yao

WAISLAMU kadhaa nchini wameelezea kukasirishwa kwao na kitendo cha Mpiga debe wa CCM, Sheikh Mtopea kuwashambulia Waislamu.

Waislamu hao wamedai kwamba, Sheikh huyo wa CCM aliparaganya aya za Qur'an na kuunda apendavyo kisha akazitumia katika hotuba yake ya kuwashambulia Waisalmu ili kutaka ionekane kuwa Qur'an inamuunga mkono mgombea wa CCM.

Kitendo cha Sheikh huyo kimedaiwa na Waislamu hao kuwa ni cha kuichezea Qur'an, kumshirikisha na kumfukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuwafurahisha viongozi wa CCM. Aidha, Waislamu wamedai kwamba kitendo hicho hakikubaliki katika Uislamu.

Akizungumzia suala hili,Bwana Ahmad amesema, anavyofahamu yeye, katika ulingo wa siasa kama hizi za kumnadi mgombea ili wananchi wampe kura zao,kinachotarajiwa na wananchi toka kwa wagombea na wapambe wao, ni kuzungumzia matatizo yanayowakabili wananchi na nini chama na mgombea wake watakachokifanya kutatua matatizo hayo pindi watakapochaguliwa.

"Sisi waislamu hatuna tatizo na CCM kujitafutia Sheikh wao na kumfanya mpiga debe katika kampeni, wala hatuna tatizo lolote kwa CCM au chama chochote kile kujikusanyia idadi watakayo kuwatumia katika kampeni zao nchini.

La muhimu ni kuwa wapiga debe hao wajue kuwa wananchi wanasubiri kusikia mnayachambua vipi matatizo yao na mna sera gani za kutatua matatizo hayo",amesema..

Kuacha au kukwepa kuzungumzia matatizo ya wananchi,amesema Bwana Ahmad, na badala yake kumsimamisha mpambe wa chama awakejeli watu na dini yao, ama ni dalili za kukosa uwezo wa kuyatambua matatizo yao na ufumbuzi wake, au ni mbinu ya kutaka kupotosha mawazo ya wananchi wakose kufuatilia hoja za wagombea katika kampeni.

Naye bwana Hashimu Rajab wa Mbagala amesema, kama wagombea au wapambe wao wanadhani kuwa yapo malalamiko na madai ya wananchi dhidi yao na chama chao, dawa siyo kuwashambulia wananchi. .Amesema, katika awamu ya tatu, wananchi walipiga kura kwa ahadi za kuondolewa rushwa, umaskini, ujinga na maradhi. Kura za maoni zimeonesha kukithiri zaidi kwa rushwa siyo tu nchini bali hata ndani ya Chama kilichounda serikali kwa ahadi ya kuondoa rushwa.

Bwana Hashimu amesema, umaskini pia umekithiri kiasi cha watu 45 kuripotiwa kufa kwa njaa wilayani Ulanga, na hadi sasa njaa imetanda nchini. Pamoja na hayo amesema, vijana wengi hawana ajira na wananchi kwa ujumla hali zao za maisha zimekuwa ngumu sana Amesema maradhi pia ni hivyo hivyo. Hospitali hazitoshi, zilizopo hazina dawa za kutosha, na penye dawa chache wananchi hawana uwezo wa kulipia matibabu.

"Hivyo wananchi wanapohoji kulikoni kwa wakusanyao kodi kwa wingi kushindwa kuyatatua matatizo hayo, msiwashambulie kwa maneno makali au kuwapuuza,na kuwakusanyia watu waikejeli dini yao",amesema. Mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Bibi Hafsa amesema, wananchi wasiondolewe haki. yao ya kujibiwa hoja na madai yoyote waliyonayo dhidi ya chama cha CCM na serikali yake na wala isiwe sababu ya kutukanwa kwenye majukwaa.

Yapo mambo mengi Wananchi wangependa kupata maelezo,amesema Bi Hafsa.Akitoa mfano alisema, wakulima wa kahawa nchini wangefurahi kupata maelezo ni kwa nini kahawa bora ya Tanzania iuzwe kwenye soko la kimataifa kwa bei ndogo kuliko ile ya wenzao itokayo nchi nyingine za Afrika au Amerika ya kusini.

Wananchi shida yao si kusomewa aya za kughushi katika majukwaa ya kisiasa,bali kupewa maelezo namna ya kutatua matatizo ya bei ndogo ya mazao yao,amesema.

Amesema kwa upande wa wafanyakazi, wangependa kujua kwa nini haki yao ya kidemokrasia ya kujiundia vyama huru vya kutetea maslahi yao nchini ni nzito kutekelezeka.

"Hivyo ni haki yao wote hao kujibiwa kwa usahihi wake na wala siyo kushambuliwa kwa namna yoyote ile.

Wala si sahihi kwa wenye madai yao kupuuzwa na kunyimwa majibu yanayostahili na badala yake kushambuliwa binafsi",amesisitiza..

"Hatudhani kuwa ni vizuri na sahihi baada ya kuona wananchi hawakubaliani nanyi kuanza kuwaandamana kwa dini zao.Kama Wakatoliki wanadai na kuhoji kama wananchi masuala ya siasa au ya seirkali na uongozi wa nchi yao, wajibuni kwa uananchi wao na siyo kama Wakatoliki",amesema ustadh Mussa.

Akasema, kama.Kwa mfano wakihoji uadilifu wa chama wakidai kuwa kinaonekana kuwa kichaka cha majambazi, wanahaki kutoshelezwa kwa hoja juu ya ukweli au upotofu wa madai hayo.kama wananchi.

Utadh Mussa amesema, si sahihi kuanza kuwashambulia wao kwa dini yao na kwa kupopotoa aya za Biblia za Wakorintho au Wagalatia ili kujenga hoja ya kuhalalisha mashambulizi dhidi yao.

Vivyo hivyo kwa Waislamu.amesema, Waislamu wana madai yao kadhaaa dhidi ya serikali ya CCM. Pamoja na madai hayo wanayo yale ya kuvamiwa Msikitini, kupigwa na baadhi yao kuuawa.

Amesema, Waislamu bado wanadai tume ya kuchunguza mauaji ya Mwembechai na pia kukamatwa na kufikishwa mahakamani polisi walioua.

"Sasa kama majibu hayapo au wanaotakiwa kujibu wanaona kuuliwa waislamu si suala la kuwashughulisha, basi si vyema kuwakodia watu wa kuwashambulia kwa aya za kuunganishwa kijuujuu",amesema.


Kilwa wasusa uchaguzi

WANACHAMA 1,248 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kilwa kusini mkoani Lindi, wamerudisha shahada zao za kupigia kura kwenye ofisi ya Kata ya Chama hicho, iliyopo kata ya Kivinje, kufuatia hatua ya Halmashauri yake kuu (NEC) kuliengua jina la Bwana Athumani Ghullam Dewji, ambaye walimchagua kuwania jimbo hilo.

Wakizungumza kwa jazba mara baada ya kikao chao kilichoketi kwenye ofisi ya kata ya chama hicho, wanachama hao walidai kusikitishwa na maamuzi ya NEC kulieungua jina la Dewji, ambaye aliongoza katika kura za maoni baada ya kupata kura 770 dhidi ya 559 za Mbunge anaemalia muda wake Bwana Omari Mwenda.

Hivi karibuni Halmashauri Kuu ya CCM iliketi mjini Dodoma kupitia maombi ya wanachama wake, waliotaka kugombea Ubunge.

Katika panga hilo majina kadhaa yakiwemo mapya na ya zamani yalikatwa kwa madai kuwa katika upigaji wa kura hizo za maoni kulitawaliwa zaidi na rushwa.

Mwanachama Omari Issa Chuwa alisema kuwa kitendo kilichofanywa na Halmashauri kuu kulikataa jina la Bwana Dewji ni cha uonevu kwa wanachama hao kwa kile walichokieleza kuwa hilo ndilo changu lao.

"Mimi ninashangazwa na hii NEC, kama ni madai ya rushwa jimbo letu halikupeleka lalamiko lolote, leo vipi sisi watunyime haki yetu?" Alihoji kwa masikitiko Bwana Chuwa.

Akiungwa mkono na mwanachama mwenziwe Bi. Hidaya Juma yeye alisema ni bora kuacha kabisa kupiga kura kuliko kumpigia mgombea ambaye siyo chaguo lao, na kuongeza kuwa mgombea huyo tayari alishashindwa kuwatumikia wananchi wakati alipokuwa Mbunge wa jimbo hilo.

Katibu wa CCM wa kata hiyo Bwana Mohammed Muhidini, amewasifu wanachama hao, kwa kile alichokiita kuwa wameitumia demokrasia yao, na kuongeza kuwa endapo NEC haikubaliki, maamuzi yake kwa jimbo hilo, kuna hatari ya kulipoteza kwa wapinzani mwaka huu.

Muhidini aliendelea kusema kuwa ni heri Halmashauri hiyo ingeangalia zaidi katika majimbo ambayo yamepeleka malalamiko yake na kuyaacha yale ambayo hayakutuma shutuma zake kwenye Halmashauri hiyo.

Katika kuonyesha kuchukizwa kwao, wanachama na wakereketwa 1,248 wa chama hicho, wamerudisha shahada zao za kupigia kura, huku wengine ambao bado hawajarejesha wametishia kupigia upinzani, endapo Halmashauri hiyo haitabadili maamuzi yake, ya kutolirudisha jina la Bwana Dewji.

Katibu wa CCM wilaya ya Kilwa, Luteni M.Y. Kupwata pwata alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi, kutoa ufafanuzi juu ya sakata hilo, alisema kuwa hana la kuzungumza kwa kile alichokieleza kuwa kutingwa na kazi nyingi.

"Sina la kukueleza ndugu yangu kwa hivi sasa kwani nimetingwa na kazi, si unafahamu kuwa tupo katika hekaheka za uchaguzi", alimaliza kusema kusema.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook