RIWAYA

Joka la Mdimu - 22

Siku iliyofuata mazungumzo baina ya Amani na Gray Kwacha yalichukua muda mfupi. Amani alitoka kwenye jengo kuu la Hazina hadi chini ambako aliegesha gari lake. Aliingia ndani akaketi kwa muda kufikiria hatua ifuatayo ambayo hakuwa na hakika nayo. Ujumbe aliokuwa nao kwa Tino ulimuelemea mno akataka autue upesi. Na hata hivyo isingesaidia. Aliamua kumtafuta Tino mwenyewe haraka iwezekanavyo.

Yalikuwa ni majira ya saa tano tu ingawa jua lilikuwa kali. Aliegesha gari lake pole pole kuelekea Sega mkono wa kulia kautoa na kuegemeza juu ya mlango. Lakini wakati bado akiwa njiani aliona anga upande wa Sega inabadilika kuwa njano, akawaza labda jua limepatwa. Mara ghafla akasikia honi kali za gari la kuzima moto likielekea Sega. Alipunguza mwendo na kutoka kabisa nje ya barabara. Wakati anarejea tena barabarani akakabiliwa na Volkswagen Combi ya hospitali inawaka taa ya bluu juu, huku king'ora chake kikilia. Akapunguza tena mwendo, nayo ikampita kasi kama umeme. Mwendo mrefu kidogo akaona mlima mkubwa wa moshi mzito umetanda angani. Akaongeza mwendo.

Moto mkubwa ulikuwa umeanza nyumbani kwa Kashogi, na sasa ndimi zake nyekundu ziliyeyusha mabati, kupasua madebe na mapipa ya petroli, zikateketeza kila kilichofikia. Mabati ya mapaa ya nyumba mbili za Kashogi pamoja na mabanda yake yalifuta ndani baada ya mbao na pau zake kuunguzwa na moto ule. Wafanyakazi wa zima mto walifika hapo saa nzima baada ya moto kuanza na kukuta umerukia katika nyumba za jirani nyuma ukiacha masalia ya makao ya Kashogi yakifuka moshi. Zimamoto walifungua mipira yao mirefu na kutupa maji kwenye miali ile ya moto bila ya mafanikio yoyote. Wazee wenye mikongojo, wanawake na wana wao mikononi na migongoni walikusanyika pembeni kuona vita hivyo baina ya binadamu na moto ambavyo moto uliendelea kushinda dakika hadi dakika. Moto ule uliendelea kwa kiburi ukipepewa na kuzidishwa kasi na upepo mkali uliovuma. Miali yake ilienda huku na huko, halafu ikapaa juu angani ikisindikiza majivu na vitakataka vilivyopeperuka kutoka mabaki ya vitu vilivyoungua. Nguvu ya moto ile ilipungua na kuzimwa baada ya kutokezea kwenye barabara ambazo zilikatisha uwezo wake wa kuendelea. Kuta nyeusi za nyumba zaidi ya kumi zilisimama wima kuomboleza. Amani alitikisa kichwa, akaondoka kumfuata Tino.

Pale Sega barabarani Amani alilikuta kwama la Tino ambaye alikuwa hayupo. Jirani na hapo paliegeshwa teksi bubu, yaani zisizo na leseni. Amani aliegesha gari lake miongoni mwa gari hizo kumsubiri Tino.

Ulipita muda mrefu bila Tino kurejea mpaka Amani akaanza kushikwa na muhuma. Hata alipotaka kupiga gari lake moto kuondoka, Tino alimgusa begani, "Nimekuweka sana?"

"Mno! Ulikwenda wapi"?

"Kuzima moto!

"Umekuwa zima moto?"

"Namsaidia Tajiri wenu Kashogi".

"Hivi amepona?"

Sijui, lakini kuna habari watu kadhaa wameteketezwa. Ule si moto, jahannam".

Wote walibakia kimya. Mwisho Amani akagutuka na kumwambia Tino, "Hebu basi ingia tuzungumze".

Uso wa Tino ulibadilika ghafla na kuonekana mweusi zaidi ya kawaida. Tangu mwanae Cheche aumie uso wake ulilemewa na jitimai, ukaanza kusawajika. Muda wote alikuwa na wasiwasi kama ategemeaye jambo kubwa kumtokea. Alibakia kwenye kiti cha mbele na kumgeukia sahibu yake.

"Bwana nimezungumza na Gray Kwacha".

"Umempata?" Uso wa Tino ukaangaza kwa muda kama radi ya kiangazi na kurejea tena kizani.

"Nimempata".

Amani akaendelea, "Lakini mambo makubwa".

Tino alishusha pumzi kama aliyepigwa ngumi ya kifua. "Ehe?"

"Anataka laki tatu ndipo aidhinishe kutolewa fedha za kigeni".

"Laki tatu?"

"Na siyo hivyo tu. Inabidi ulipie nusu ya gharama za fedha za matibabu huko Ulaya kwa fedha za hapa Tanzania kiasi cha shilingi milioni tatu".

Tino alitikisa kichwa halafu akakiangusha ndani ya magao yake mawili na kuegemea mbele. Alipwelewa mithili ya gunia tupu. Taratibu machozi yalimtiririka. Amani alibaki kimya akiangalia mbele.

"Bradha, nifikishe mjini", abiria mmoja alimgusa kutoka nje.

"Sina mafuta" Amani alimjibu.

Tino alisikia jibu hilo, akajua sio kweli kuwa Amani hakuwa na mafuta. Hakutaka tu amuache peke yake katika ukiwa. Akawaza, dunia hii ya leo, nani atajitoa kwa hali na mali kumsaidia kapuku kama yeye! Nitalipa nini Amani? Moyo ulizidi kumsonga na machozi ambayo yalianza kukatika, yakaendelea kumiminika kupita awali. Robo saa nzima ilipita, ndipo Amani akamgusa begani, "Tino?"

Tino aliitikia bila ya kuinua uso wake.

"Kila kitu kinapangwa na Mungu. Sasa tutafute namna ya kuzipata hizo fedha".

"Tutazipataje?" Tino alikata tamaa.

"Lazima tuzipate".

Msisitizo ule ulichochea ari mpya moyoni mwa Tino. Akainua uso wake, macho mekundu, akaangaza mbele. Taratibu moyo wake uliimarika mithili ya tofari lililotiwa ndani ya tanuri.

Muda ule akili ilimduru mwisho akapata wazo muafaka ila alihofu kumtobolea Amani kwa wakati ule. Akamwambia, "Nimepata wazo. Lakini nitakueleza jioni.

Basi , wakaagana.

Baada ya juma moja, usiku kiasi cha saa tano, Tino alifika nyumbani kwa Amani. Kumaliza kusalimiana kwa muda mfupi Amani alivuta mtoto wa meza akatoa mfuko wa karatasi. Ndani yake akachomoa bastola, akainua macho kumtazama Tino aliyeshusha pumzi akauliza, "Umeipata wapi?"

"Kaniuzia askari jeshi mmoja".

"Umeinunua kabisa?"

"Kwani ulitakaje?"

"Tumrejeshee baada ya shughuli yetu".

"Sawa, lakini alisisitiza niinununue, au asinipe kabisa. Nikawa sina la kufanya".

Tino hakuamini upesi akasema kwa chinichini, "Lakini hatari kukaa na bastola".

"Kila kitu kina hatari. Yategemea matumizi yako. Mimi sina ubaya wa kuwa na bastola. Ubaya ni kuitumia vibaya.

Kuitumai vibaya ndiyo nini? Moyo ulimsonga Tino, ukawa jirani kutokea kinywani mwake. Akawaza lile linalomkabili, kisha akamfikiria Cheche. Pole pole roho yake ikarejea mahali pake.

"Tuyaache hayo!" Amani akasema.

"Kesho tutaanza mazoezi ya kuitumia hii bastola!"

"Lakini si ya kutishia tu?"

"Kama ni hivyo si tungetafuta ya bandia?"

Tino alikazia macho chini, asipate jawabu.

"Sikiliza inaweza kuwa lazima kujitetea, ikibidi basi lazima kuitumia!"

Hata hivyo Tino hakupenda kuyafikisha mawazo yake katika nyanja hizo za kufyatuliana risasi. Bali alikiri, likibidi liwe, basi na liwe.

Siku tatu zilizofuatia walitoka hadi mbali nje ya mji kabisa ambako kulikuwa na mbuga pana. Huko Amani alimfundisha Tino namna ya kutia na kutoa risasi, kulenga shabaha na kupiga shabaha.

Sehemu kubwa iliyosalia ya mpango wenyewe ikawa juu ya Tino mwenyewe.

Usiku Tino alikuwa hapati lepe la usingizi, akili yake ikasukwasukwa na dhoruba za fikra za kutisha. Njozi mbaya zikapanda kichwani mwake na kumshtua hata pale alipodiriki kupata tumba la usingizi. Asubuhi, kamakawaida yao na mkewe walikwenda kumuangalia Cheche hospitalini ambako alizidi kudhofu. Njiani Tino akawaza lazima atekeleze mpango wake haraka.

Wakati mkewe ameelekea nyumbani, Tino alipitia katika maduka ya mitumba pale Sega. Aliingia ndani ya moja, akatokea kwenye jingine hivyo hivyo huku sauti za maboxi zimetangaa angani kunadi biashara zao.

Katika kufanya hivyo zikashindana na honi na miungurumo ya teksi, malori na mabasi yaliyokuwa yanapita katika barabara kuu iendayo Mindule. Huku akiwaepa wasichana, wavulana, wake kwa waume, Tino aliendelea akipita marundo ya nguo zilizotupwa ovyo ovyo juu ya meza.

Watu wenye haraka waliyaingilia matita hayo ya nguo wakipekua chupi, mashati, suruali, sidiria, viguo vya watoto kwa arara mno na kuziacha zimetawanyika vibaya zaidi kuliko awali.

Za juu ziliwekwa kati, za chini zikapelekwa juu. Hivyo hivyo kutwa nzima, huku zikipungua kadri zilivyonunuliwa. Mwisho, alifika kwenye duka moja ambalo kwa nje alining'iniza makoti na suruali. "Karibu Bradha. Mambo yako ndani. Suti mpya kutoka Marekani, Landan, Sweden! Bei poa". Kijana mmoja alimkaribisha. Tino alipitiliza hadi ndani ambako kweli suti aina malimbali zilining'izwa kwenye kamba, za kila rangi, kahawia, kijani, blu nzito na nyepesi, nyeupe, hakuna rangi iliyokosekana.

Yule kijana alimuachia Tino mikononi mwa mwenzake mwingine mle ndani, yeye akarejea tena pale mlangoni kunadi na kuwavutia watu wengine dukani pale. Mle ndani yule kijana mwingine alimsaidia Tino kupekua suti hadi suti.

"Nikutolee faza?" yule kijana alishawishi baada ya kuona Tino kapoteza muda mrefu zaidi kuiangalia suti moja akiipekuapekua.

"Hebu itoe niikague vizuri isije kuwa imechanika".

"Mali safi hii". Haraka yule kijana aliitungua suti ile iliyokuwa kwenye kining'inizo cha makoti. Aliiweka juu ya meza ambapo Tino aliikagua kwa makini mno. Alianzia na suruali akiangalia kiuononi, chini kabisa ya miguu na katikati ya mapaja. Sehemu hizo ndizo zngeonyesha uchakavu wa suruali kwa urahisi. Kuridhika na suruali akajua koti hilo litakuwa bora zaidi, maana suruali huvaliwa na kuchakaa upesi zaidi ya koti. Akaridhika tena na koti lile, akakiinua kizibau cha ndani kwa muda mfupi, akamgeukia yule kijana akiacha macho yake yazungumze kwa niaba ya kinywa chake.

"Alfu kumi".

"Nitakupa saba", Tino alijibu huku akichomoa noti akamhesabia kiasi hicho. Suti ile ilifungwa vizuri ndani ya makaratasi akatoka nayo hadi nyumbani.

Usiku ule ulikuwa mgumu kupita yote maishani mwake. Roho yake ililia na kuomboleza, machozi yake yakapukutikia ndani kwa ndani. Ukali wake ukamchoma mno. Aliomba asubuhi ifike akabiliane na lile alilolikusudia.

Itaendelea Ijumaa.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook