TAHARIRI

Waacheni Wazanzibari wajiamulie mambo yao

Muungano wowote wa hiyari hadumu kwa ridhaa ya pande zote zilizoungana. Ulaghai, hadaa vitisho na maguvu ya aina yoyote ile huwa havisaidii kuudumisha.

Nchi nyingi zimewahi kuungana na kubwagana. Malysia na Singapore waliwahi kuungana. Hakuna vitimbi vyovyote vilivyoweza kuwaimarisha au kuwalazimisha waendelee kinyume cha ridhaa ya pande zote. Hatimaye walibwagana. Wamebaki kuwa majirani wanaoheshimiana kama zamani.

Vilevile nchi mbili zinapoungana kwa hiyari, hiyari ile huwa si ya viongozi tu. Wananchi pia hutakiwa kuthibitisha ridhaa yao. Ridhaa hiyo pia huwa haitafuwi kwa ulaghai wala vitisho.

Katika hali hiyo, kwa nini wananchi wa Zanzibar hawajengewi mazingira yaliyohuru na ya haki katika kuamua mambo yao ili ridhaa yao katika muungano ionekane na kuthibitika kuwa ni hiyari?

Wazanzibari wamekuwa wakidai kwamba kuna juhudi za kuifanya nchi yao kuwa mkoa. Wanadai kuwa kauli za chama tawala kwamba Muungano huu wa serikali mbili kuelekea serikali moja unawakilisha tamaa ya upande mmoja wa bara kutaka kumeza mwingine, wazanzibar.

Mabadiliko ya vifungu vya 11 na 13 vya katiba ya muungano wa Tanzania vimelalamikiwa zaidi na Wazanzibari kuwa vinakwenda kinyume na mkataba wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uliosainiwa mwaka 1964.

Alhaj Abou Jumbe, amesema katika kitabu chake The Partner-ship kwamba kwa mujibu wa maelezo ya mkataba huo, wala haioneshi kuwa palikusudiwa pawepo na serikali mbili. Na kama zipo mbili, basi ni kuelekea kwenye serikali tatu, hizo ndizo zilizokusudiwa.

Mzee Jumbe pia ameeleza kwenye kitabu chake kuwa, marehemu Karume alitia saini mkataba wa muungano huku akiamini kuwa maslahi ya Zanzibar yangaliendelea kuamuliwa na Wazanzibari. Katika kitabu chake hicho, ametoa mfano wa mgogoro wa balozi za Kijerumani. Wakati huo Jerumani zilikuwa mbili, ya mashariki na magharibi. Ya kwanza ilikuwa na ubalozi wake Zanzibar, ya pili ilikuwa na ubalozi Dar es Salaam. Baada ya muungano Ujerumani magharibi ilitaka Tanzania ifunge ubalozi wa Ujerumani mashariki Zanzibar. Ingawa masuala ya mambo ya nje yalikuwa ya muungano, na hayati Nyerere alikubali ubalozi wa Ujerumani mashariki ufungwe Zanzibar. Mzee Karume alimkatalia Mwalimu Nyerere kwa hoja kuwa ubalozi ule ulikuwepo Zanzibar kwa manufaa na maslahi ya Wazanzibari.

Mfano mwingine maarufu ni pale Tanzania ilipopitisha Azimio la Arusha mwaka 1967. Mzee Karume inasemekana baada ya kuona Azimio hilo halikuwa na maslahi yoyote kwa Wazanzibari, alisema, "Azimio hilo liishie Chumbe", yaani lisiende Zanzibar. Liishie kwenye eneo la kisiwa cha Chumbe kilichopo mpakani mwa Tanganyika (Tanzania bara) na Zanzibar.

Ni katika mazingira kama hayo, wananchi wengi wa Zanzibar wanadai kuwa wazee wao hawakumwaga damu ya mapinduzi mwaka 1964, ili wapate kuwaachia nchi ya wao kuja kuikabidhi 'Chimwaga'.

Tunaamini kuwa muungano huu haukuundwa kwa hadaa yoyote wala hautarajiwi kudumishwa kwa vitisho na mabavu. Na kwa imani hiyo, ni vyema basi Wazanzibar wakaachia mazingira ya kujiamulia mambo yao hususan katika masuala kama haya ya uchaguzi mkuu.

Lakini inasikitisha kusikia Wazanzibari wanalalamika na kudai kuwa wakati baadhi yao wanazuiliwa kujiandikisha kupiga kura Zanzibar, wapo baadhi ya watu, polisi na wanajeshi wasiokuwa Wazanzibari, walipelekwa kujiandikisha kupiga kura kama moja ya mbinu ya kumsaidia mgombea wa CCM kushinda uchaguzi ujao kiti cha Urais.

Kama madai hayo ni kweli hatudhani kuwa juhudi hizo zinakusudio jema kwa Wazanzibar.

Pamoja na hivyo, Wazanzibari wanadai na kulalamika kwamba wakati baadhi yao kisiwani humo wamekuwa wakiandamwa na virungu vya polisi, jeshi la wananchi limepeleka wanajeshi wengi na vifaa vya kijeshi , ambavyo wanadhani vimepelekwa kisiwani humo kwa mara ya kwanza tena katika kipindi hiki cha uchaguzi ili kuwajaza khofu.

Kwa kuwa madai na malalamiko ya Wazanzibari sasa yamezidi na yameanza kuzungumzwa kwa sauti kubwa na ya juu kwenye hadhara za majukwaa ya siasa, tunadhani ni vizuri Watanzania wakaanza kuona umuhimu wa kuwa na muungano utakaodumu kwa ridhaa ya pande zote mbili. Si vizuri kutaka muungano huu kuonesha kuwa Wazanzibari hawana haki ya kushiriki na kujiamulia mambo hata yale yaliyokubalika kwenye katiba yao.

Ni vizuri vile vile tukajifunza toka kwa wenzetu sehemu mbalimbali za Afrika ambao hivi sasa wamekumbwa na migogoro pamoja na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Waburundi wanakutana Arusha wiki ijayo. Wasingefika Arusha ila baada ya kupoteza fursa ya kuheshimiwa kama binadamu na wananchi wenye haki sawa katika nchi yao. Wamepoteza fursa hiyo baada ya kunyimana fursa hiyo baada ya kunyimana haki ya kikatiba na ya kidemokrasia ya kujiamulia mambo yao wenyewe, ndani ya nchi yao.

Kosa lao hilo limewasababishia aibu ya kulazimika kuamuliwa mambo yao na akina Clinton watu ambao hawana nasaba nao ya lugha, ukoo wala utamaduni.

Mwaka 1993 walifanyiwa khiana. Waliwanyima wenzao haki ya kumchagua Rais wamtake. Wakamuua Rais Melechior Ndadaye kwa kuwa tu, alichaguliwa na watu ambao hawakutakiwa kuwa na haki ya kuamua mambo yao. Imechukua miaka 7 na mauaji mengi ya kikatili kabla ya akina Clinton kuingilia. Na wala hatujui kama watafanikiwa au itakuwa kama Somalia na kwingineko ambako maafa yanaendelea.

Tunayo haki ya kuwashukuru wapatanishi. Lakini wengine kati yao wamekuwa kama washenga wa ajali. Hawaji mpaka kwanza muuane, tena kwa malaki. Mauaji kama yale ya Mwembechai kwao wao si tatizo.

Hamtawasikia wakiuliza wangapi waliuliwa, kwanini waliuliwa na hata kutaka tu kujua kwanini kitabu kinachoelezea mauaji hayo kimepigwa marufuku.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook