LAKINI kile ambacho TANU ilimudu kuwapiku
Waingereza katika mazingira ya kisaikolojia kupitia hotuba za viongozi
wake na propaganda nyinginezo ilikipoteza kwa kukosa gazeti la kuandika
mafanikio hayo. Chini ya ukoloni usambazaji wa habari kwa njia ya uchapishaji
pamoja na njia nyingine za upashanaji habari zilikuwa chini ya ukiritimba
wa serikali na wamishionari.
Kwa namna hii serikali ya kikoloni iliweza kudhibiti habari, ikitoa habari zile ambazo ilifikiria muhimu kwa maslahi yake yenyewe na hivyo zinafaa kusomwa na raia. Idara ya Maendeleo ya Jamii ilikuwa ikichapisha magazeti ya Kiswahili - Mambo Leo, Tazama, Mwangaza na Baragumu.
Wamishonari walikuwa wakichapisha Kiongozi na Lengo, magazeti haya yakimilikiwa na Wakatoliki na Walutheri. Madhehebu ya Ahmadiyya ilikuwa na gazeti lao - Mapenzi ya Mungu lakini gazeti hili halikuwa maarufu na nakala chache sana ndizo zilizokuwa zikiuzwa. Kwa kuwa Waislamu wa madhehebu ya Sunni ndiyo wengi Tanganyika, watu walijiepusha na gazeti hilo wakiliona kama kama chombo cha kufru.
Wakati magazeti ya serikali yakijishughulisha zaidi na kampeni za kufuta ujinga kwa kuchapisha porojo na visa kuwahimiza watu kusoma, Wamishionari walijikita zaidi katika kueneza Biblia na propaganda za kupinga Ukomunisti. Kwa kushirikiana katika nyanja ya vyombo vya habari serikali na Wamishonari waliweza kuyalinda maslahi yao kwa pamoja.
Ramadhani Mashado Plantan alivunja ukiritimba huu baina ya serikali na Wamishionari. Akifuata nyayo za Erika Fiah, Mwafrika wa kwanza kuchapisha gazeti katika Tanganyika, Mashado alianzisha gazeti lake Zuhra.
Mashado alizaliwa mwaka 1900 huko Lourenco Marquis (sasa Maputo) na alikuja Tanganyika akiwa mtoto mdogo mwaka 1905 wakati nchi ipo katika vita vya Maji Maji dhidi ya Wajerumani.
Mwaka 1924 alirudi Msumbiji na alisafiri kwenda Lisbon kwa pasi ya Kireno. Wale waliomfahamu wanasema kwa kiwango cha miaka ya 1950, Mashado Plantan alikuwa mtu mjuzi wa mambo. Alikuwa miongoni mwa wanachama wa mwanzoni wa African Association ilipoanzishwa mwaka 1929 na miongoni mwa wanchama wa awali kujiunga na TANU pale ilipoasisiwa mwaka 1954.
Msimamo wa Zuhra ulikuwa kuwazindua na kuwashirikisha Waafrika kupambana na ukoloni pamoja na ubeberu. Katika tahariri zake nyingi, Mashado alimwonyesha Mwingereza kama mgeni ambae baada ya kukaribishwa sasa anambughudhi mwenyeji wake. Lakini juu ya yote Zuhra lilikuwa gazeti la Kiislamu, likipendwa na halaiki ya watu. Lakini gazeti hilo halikuwa likithaminiwa na wasomi ambao walilidharau na kuliona kama gazeti la Kiswahili tu, lisilokuwa na ujuzi wowote, lililokusudiwa hasa msomaji wa chini asiye na elimu na asiyejua kusoma Kiingereza. Mashado alikuwa akichapisha tafsiri ya Qur'an154 ndani ya gazeti lake. Zuhra kwa ajili hii halikuwavutia sana wasomi kwa kuwa kurasa zake zilitangaza Uislamu.
Mashado, kwa kupitia safu za Zuhra, alikuwa ndiye msemaji wa African Association na kupitia tahariri zake alitangaza na kudhihirisha msimamo wa chama.
Mwaka wa 1955 Mashado alikuwa na umri wa miaka 55. Mtu mzima na mwanasiasa mwenye uzoefu kwa kiwango chochote kile. Mafanikio ya Nyerere katika Umoja wa Mataifa na ile hamasa ya umma katika kudai uhuru kulizua tatizo ambalo halikutarajiwa.
Mafanikio ya TANU yalikuja kwa haraka na hivyo kuwastaajabisha watu wengi. Watu wachache walitambua wakati ule kuwa African Association ilikuwa imepigana vita vile kwa niaba ya TANU kwa hiyo njia ya TANU ilikuwa imekwishasafishwa kiasi cha kufanya kazi iliyobaki iwe ndogo sana. Kwa ajili hiyo sasa ilikuwa rahisi kuwashirikisha watu chini ya TANU kudai uhuru. Baadhi ya vijana katika TANU wakawa hawana subira na wakapumbazwa na mafanikio ya haraka ya harakati. Mashado alikuwa anapokea taarifa nyingi za kukaidi serikali wananchi wakidai kuitambua TANU kama ni mamlaka pekee yenye uwezo wa kutoa haki sawa kwa raia. Mashado aliliona tatizo hili na hatari yake.
Alitumia fursa hiyo kudhibiti hali hiyo ya hatari ambayo kama ingeachiwa kuendelea ingesababisha vurugu na watu kuiasi serikali. Aliandika tahariri muafaka moja katika nyingi, akiwakumbusha Watanganyika hususan wanachama wa TANU kuwa chama hakijachukua majukumu na kazi za serikali. Alisisitiza kwa watu wote kuwa Waingereza walikuwa bado ndiyo watawala na wanahusika na kutunza amani ya nchi. Machafuko miongoni mwa wanachama wa TANU yaliepukwa kabla mambo hayajaharibika.
Mashado alijenga taswira ya TANU na haiba ya Nyerere kama kiongozi wa harakati za kudai uhuru wa Mtanganyika. Kupitia Zuhra Mashado aliwafahamisha wananchi kuhusu masuala mengi ya kisiasa ya siku zile na aliwahimiza wasomaji wake kuyajadili masuala hayo katika kurasa za gazeti lake.
Mafanikio ya TANU katika kuuhamasisha umma yaliathiri serikali ya kikoloni. Mnamo Novemba, 1955 serikali baada ya kuona hali ya hewa na uhasama uliokuwa ukioneshwa na wananchi dhidi ya utawala wa kikoloni, serikali ilirekebisha sheria iliyokuwa ikitumia kujilinda na kile kilichoitwa 'uchochezi', ikawa ni kosa 'kuchapisha na kuuza au katika mkutano wowote wa watu kutoa maelezo yoyote ambayo yataelekea kuzusha chuki na manung'uniko miongoni mwa wakazi wowote nchini'.
Serikali ilifanya marekebisho hayo huku ikiwa na watu kama Mashado na Nyerere katika fikra yake. Kabla ya kuibuka kwa harakati za kudai uhuru, washairi nchini Tanganyika walitunga beti za kuwasifu Wafalme na Malkia wa Uingereza kutoka ukoo wa Windsor pamoja na nasaba yao. Ghafla baada ya kuundwa kwa TANU palitokea mageuzi ya maudhui katika tungo za mashairi na tenzi. Washairi waliacha kumsifu na kumtukuza Mfalme na Malkia wa Uingereza. Wakiongozwa na Saadani Abdu Kandoro walianza kutunga mashairi yenye ujumbe wa kizalendo wakimsifu Nyerere na TANU.
Mara tu baada ya marekebisho hayo ya sheria Mohamed Suleiman, mshairi hodari akijulikana sana kwa jina lake la ushairi la - 'Mtu Chake', alikamatwa, akatiwa ndani na kuhojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kilichokuwa na sifa mbaya ya ukatili. Mtu Chake alikuwa ametunga mashairi ya kuvutia sana kuhusu Nyerere, TANU, utaifa, mshikamano, udugu, upendo na wakati huo huo kuwakejeli Waingereza. Baada ya kuhojiwa Mtu Chake aliachiwa huru bila kufunguliwa mashtaka yoyote. Lengo la kumtia mbaroni lilikuwa kumtisha tu na kumtia msukosuko.
Mashado Plantan aliifanyia kampeni TANU hadi chama kilipoweza kuanzisha gazeti lake lenyewe, Sauti ya TANU mwaka 1956.
Kuanzia hapo Zuhra lilisaidiana na Sauti ya TANU katika juhudi za kuwahamasisha wananchi dhidi ya propaganda za kikoloni. Mashado alimuunga mkono Nyerere hadi mwaka 1958. Baada ya kura tatu na baada ndipo baada ya kuhisi kuwako kwa uroho na tamaa kubwa ya kujinufaisha binafsi na baada ya kuona dalili za kupiga vita Uislam kulikoanza kujitokeza katika uongozi mpya wa TANU ulioibuka, Mashado alijitoa katika chama na kuanzisha chama kipya, All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT). Tutakuja kuona hapo baadae jinsi Mashado alivyotupana mkono na Nyerere.
Wana-propaganda Bantu Group, 1955
TANU ilipoanza juhudi zake za kuushirikisha umma katika harakati za kudai uhuru, hasa baada ya hotuba ya Nyerere mbele ya Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa, chama hakikuwa na chombo chake chenyewe cha propaganda. TANU ilitambua umuhimu wa kuwa na chombo maalum cha propaganda ili kukabiliana na hila za kikoloni.
Katika mwaka 1955, kikundi cha TANU Bantu kiliundwa mahsusi kukabiliana na tatizo la udini kutokana na hisia za baadhi ya Waislam ndani ya TANU. Tangu kuundwa kwa TANU, kulikuwa na hisia ya kupinga Ukristo ndani ya chama.
Tatizo hili la udini lilikuwa likichemka pole pole na chini kwa chini ndani ya TANU. Ilikuwa kazi ya kikundi cha TANU Bantu kuwafichua na kuwapiga vita wanachama wa TANU waliokuwa na hisia kama hizo.
Bantu ilifanikiwa sana katika katika hili hadi
kudiriki kupiga marufuku mamkuzi ya Waislamu ya Asalaam Alaikum
(Amani iwe juu yako) baina ya Waislamu kwa msingi kuwa ilikuwa inawabagua
Wakristo na hivyo inawatenga. Mamkuzi hayo yalipigwa marufuku kwa sababu
kwa mujibu wa Uislamu ni Mwislamu tu ndiyo mwenye haki ya kusalimu na kusalimiwa
kwa namna hiyo. Hii ni kwa sababu maamkuzi hayo yanachukuliwa kama dua;
na kwa mujibu wa mafundisho ya Waislam ni Mwislam tu ndiyo anaweza kumtolea
salam hiyo Mwislam mwingine. Mamkuzi yale ya Kiislamu yalionekana kama
yanakwenda kinyume na imani ya TANU na ilishauriwa kuwa 'salaam aleikum'
ipigwe marafuku isitumike. Ikiwa mathalan kwa kusahau Muislam mmoja atatoa
salaam kwa Muislam mwenzake, kwa kawaida angejibiwa 'Alaikum salaam'
maana yake 'Amani iwe juu yako pia'. Badala ya majibu haya mazuri,
majibu yaliyobuniwa na Bantu yalikuwa - 'Ahlan tabu' maana yake
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |