Sheikh Ahmed Zuberi, akiongea mjini Dodoma hivi karibuni amesema, hata zile nchi zilizogubikwa na umaskini, matumizi ya kijeshi yameongezeka mno huku watu wakikosa huduma za afya, elimu na zile za kijamii.
Amesema, hiyo ni alama katika alama za kiama. Sheikh Zuber alisema, Mtume (s.a.w.) aliwaambia maswahaba zake kuwa, moja ya dalili za kiama ni kuongezeka kwa askari.
Amezitaja alama nyingine kuwa ni kukata udugu, mauaji ya hovyo, kukithiri kwa rushwa na Qur'an kupuuzwa.
Katika kudhihiri kwa alama hizo Sheikh Zuberi amesema, Waislamu hawana budi kuongeza juhudi kuipigania dini yao huku wakiomba nusra kutoka kwa Mola wao..
Aidha, amewataka wachukue juhudi za makusudi kuamrisha mema na kukataza maovu wakizingatia kuwa athari za maovu hapa duniani zitawaathiri pia.
Wakati huo huo, Waumini wa Kiislamu wametakiwa kwenda kujiandikisha kisha kupiga kura hapo Oktoba 29, kwani hiyo ni nyenzo muhimu kuondoa uongozi usiofaa.
Hayo yamesemwa na Bw. Othman Katunzi mjini hapa hivi karibuni.
"Kupiga kura ndio njia pekee inayoweza kuwang'atua viongozi wabovu, wala rushwa, wasio waadilifu, madhalimu, na wakiritimba wa sheria", alisisitiza Bwana Katunzi akichangia mada katika semina ya siku moja iliyofanyika mjini Dodoma hivi karibuni.
Amewaambia Waislamu wasitumie vibaya nafasi hii ambayo ni muhimu na inayopatikana mara moja kila baada ya miaka mitano. "Kura zenu ndizo zinaweza kutoa mustakabali wa nchi hii katika utekelezaji wa majukumu waliyonayo viongozi kwa raia, hivyo ushabiki na uzembe uepukwe", amesema.
Semina hiyo iliandaliwa ili kuondoa mitazamo potofu ya baadhi ya viongozi wa dini juu ya upigaji kura.
Katika tukio jingine imeripotiwa kuwa, idadi ya wakazi wa Dodoma waliojitokeza katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na mgombea wa CCM, Mhe. Mkapa haikuridhisha.
Mwandishi wetu kutoka mkoani humo anaeleza kuwa minong'ono ya wakazi wa mji huo baada ya mkutano huo imedai kuwa hilo lilikuwa susio la wakazi mji huo dhidi ya CCM.
Dodoma ni mkoa ulioonekana kuwa ngome ya CCM.
Kutoka Sumbawanga hali imeripotiwa kutokumwendea vyema Mhe. Mkapa baada ya wananchi kutojitokeza kwa wingi hali iliyosababisha huzuni kwa viongozi wa mkoa huo.
Mhe. Mkapa jana alitarajiwa kuendelea na kampeni
zake mkoani Mbeya.
ZIKIWA zimebakia siku nne kabla ya kumalizika kwa zoezi la uandikishaji kura, Masheikh jijini wamewahimiza Waislamu kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili wapate fursa ya kupiga kura kuwachagua viongozi wanaofaa.
Akizungumza kupitia gazeti hili, Sheikh Juma Mbukuzi ambaye ni Amiri wa Shura ya Maimamu, amewataka Waislamu kufika kwa wingi vituoni katika wiki hii ya mwisho ya uandikishaji kupiga kura.
Amewataka Maimamu wote nchini kuwahimiza Waumini wajiandikishe ili waweze kupiga kura kuwachagua viongozi watakaoleta maendeleo na kusimamia haki nchini.
"Kila Imamu wa msikiti, sheikh wa mtaa au kijiji abebe dhima hiyo ya kuwahimiza Waislamu na wananchi wengine kwa ujumla wajiandikishe ili waweze kushiriki zoezi hilo muhimu katika jamii", amesema Sheikh Mbukuzi.
Naye Katibu wa Kamati ya kutetea haki za Waislamu, Sheikh Ponda Isa Ponda akikumbushia wajibu huo, amewataka Waislamu kutumia fursa ya kupiga kama upanga kuwakata wasioongoza kwa haki, usawa na uadilifu.
Amesema ufumbuzi wa tatizo la uongozi usiojali unaokiuka sheria katika jamii zisizoongozwa na sheria za Mwenyezi Mungu ni kura.
Kwa hiyo Sheikh Ponda amewasisitiza Waislamu wote kutekeleza juhudi hiyo ya kijamii itakayowaamulia hali ya baadaye.
Akizungumza mara baada ya swala ya Isha, Jumamosi iliyopita, kiongozi wa msikiti wa Ubungo darajani, Bwana Rashid Kadenge aliwataka waumini wa msikiti huo wakumbushane wajibu huo na wale ambao bado hawajajiandikisha wafanye hivyo haraka kabla ya muda kumalizika.
Zoezi la kuandikisha wapiga kura litakamilika
Jumatatu ijayo Agosti 28.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |