Mkimchagua Karume Zanzibar imekwenda


WAZANZIBARI wametakiwa kuipenda nchi yao na kutokuruhusu ifanywe mkoa.

Maalim Seif Shariff Hamad ametoa nasaha hizo akidai kuwa, upo mpango wa kuifanya Zanibar mkoa kupitia kwa mgombea wa Urais Zanzibar kupitia CCM, Amani Abeid Karume.

Maalim Seif anayegombea Urais Zanzibar kupitia CUF, aliyasema hayo juzi akifungua kampeni za uchaguzi kwenye viwanja vya Malindi.

"Uchaguzi wa mwaka huu ni wa kuamua hatima ya Zanzibar", amesema Maalim Seif na kuonya kuwa, iwapo Wazanzibari watamchagua mgombea wa CCM atawapeleka kwenye serikali moja.

Aliwaambia waonyeshe mapenzi yao kwa Zanzibar kwa kumchagua yeye ili washirikiane kuijenga Zanzibar.

Mgombea huyo wa Urais aliwataka Wazanzibar wajiulize ni kwanini Rais Mkapa anambeba Bwana Aman hadi anaingilia suala la mishahara ambalo ni tatizo lililokuwepo muda mrefu.

Aidha, akahoji "itakuwaje uchaguzi wa Wazanzibari ulete meli kwa meli (za wananchi wa bara na askari) halafu Mzanzibari mwenye haki afukuzwe na virungu asijiandikishe".

Maalim Seif ameahidi kuwa, katika siku za awali za uongozi wake iwapo atachaguliwa ataondoa tatizo la ukosefu wa madawa mahospitalini.

Amesema, pato la Zanzibar linatosha kufuta kabisa tatizo la maji na kuboresha elimu ya bure kwa wote.

Maalim Seif amesema, tatizo lililokuwepo ni viongozi wa CCM kuwa wabinafsi wenye kujali maslahi yao binafsi.

Ameahidi kuifanya Zanzibar kuwa kituo muhimu cha biashara kwa kuifanya Bandari huru.

Aidha, amesema, ataboresha kilimo na sekta ya uvuvi ambapo wakulima zaidi ya kupewa pembejeo na kutafutiwa masoko watapewa elimu. Amesema,Wizara ya kilimo itakuwa na kitengo cha kuwaelimisha wakulima.

Amesema, wavuvi watapatiwa nyenzo na mashine za kuvulia.

Akizungumzia hali ilivyo Zanzibar hivi leo amesema, Zanzibar haikuwa na wezi, changudoa wala ombaomba.

Lakini leo mtu akijenga nyumba huifanya jela. Analazimika kuweka magrili kujihami na wezi.

Aidha, akasema, ni jambo la aibu kuwa leo Zanzibar wapo ombaomba.

Matendo yote haya ya aibu amesema, ni matokeo ya utawala wa CCM. Akasema, CCM isitoe ahadi leo bali ieleze ilichofanya.

Mkutano huo wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika juzi ulifurika umati wa watu kiasi kwamba wengine walikosa sehemu za kukaa.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook