Chapa mamba kuinyoa CUF - Karume

MGOMBEA Urais Zanzibar kupitia Chama cha CCM, Mhe. Amani Karume jana aliibukia Kibanda Maiti na kusema CCM itashinda kwa kishindo mwaka huu.

Bwana Karume amesema, wembe ulioinyoa CUF 1995, ulikuwa butu, lakini zamu hii watainyoa kwa wembe wa chapa mamba.

Karume ambaye alikuwa akizindua kampeni zake mjini Unguja jana , amesema CCM wanaomba kuendelea kutawala ili kudumisha sera ya amani.

Kabla ya kuanza hutuba yake, Karume aliwataka waliohudhuria kukaa dakika moja kuwakumbuka wazee waliotangulia mbele yake ya haki.

Watu waliguna pale alipomtanguliza hayati Mwalimu Nyerere kisha kukomea kwa Sheikh Idrisa Abdulwakil.

Mgombea huyo wa CCM alisema, aliyokusudia kuwaeleza wananchi wameshayasikia kwani alishayasema huko Pemba.

Akimtambulisha mgombea huyo, Rais wa Zanzibar Salmin Amour alisema wapinzani lao ni kutaka kukata wenzao pua zao na mashikio yao.

Akawaambia wana CCM washikamane na chama chao chenye amani.

"Wakitaka (wapinzani) wakate mashikio yao", alisema.

Akiwataka wananchi wampe Karume kura, amesema, Karume ni kijana maridadi, mwerevu, aliyetuli na mwenye mwelekeo".


Karani wa kura akataa kuandikisha wanafunzi wa Ubungo
WAKATI Mheshimiwa Kingunge Ngombale Mwiru na viongozi wengine wa kitaifa wakiwahimiza wananchi wajiandikishe kupiga kura, Wanafunzi kadhaa wa shule ya Sekondari ya Kiislamu ya Ubungo hadi jana waliendelea kuzuiliwa kujiandikisha katika kituo cha shule ya msingi ubungo Kisiwani kilicho jirani na shule hiyo.

Kwa mujibu wa kiongozi wa vijana hao aliyejitambulisha kwa jina la Adamu, zaidi ya wanafunzi 43 walio bweni katika shule hiyo wamezuiliwa kujiandikisha ili kutumia haki yao hiyo ya kikatiba.

Adam amesema walipomtaka mwandishi wa kituo hicho aeleza kwa nini anakataa kuwaandikisha, mwandishi huyo hakutoa sababu ya msingi zaidi ya kung'ang'ania apelekewe orodha ya wanafunzi wote wa shule hiyo.

Walipomtaka atoe maandishi kuthibitisha msimamo wake huo alikataa kata kata akidai suala hilo akaulizwe msimamizi wa jimbo.

Aliposhinikizwa awaandikishe wanafunzi hao kwa kuwa hakuwa na sababu za msingi na wala hakuwa tayari kutoa maandishi, mwandishi huyo alikusanya vitabu vyake kutaka kuondoka, muda huo ilikuwa saa tisa alasiri.

Kuzuiliwa kwa wananfunzi wa shule hiyo kumewashangaza watu wengi kwa kuwa wanafunzi wa shule zote Jijini walio bweni imeelezwa wamekuwa wakijiandikisha katika vituo vilivyojirani na shule zao.

Baadhi ya watu wametuhumu hatua ya mwandishi huyo kuwa huenda inatokana na maelekezo maalum kutoka ngazi fulani au ushawishi wa wagombea fulani.

Wanafunzi hao wamesema watahakikisha wanapewa haki yao hiyo kwa jitihada zote.

Aidha wameahidi kwenda tena katika kituo hicho leo hii na wamewataka viongozi wa Tume kumtupia macho mwandishi huyo kabla hajasababisha kizaa zaa.


Swahiba wa Kingunge ajiengua CCM

MPIGA debe maarufu wa Waziri wa Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa, Kingunge Ngombale Mwiru, Bw. Hassan Mnyika (76) amejiengua kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kilwa mkoa wa Lindi na kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF).

Bw. Mnyika alifikia hatua hiyo hivi karibuni baada ya kuanza kuona sera za Chama hicho zinaweza kutekelezeka, kufuatia uongozi mpya wa kijiji cha Njia Nne chini ya Chama cha CUF kufuta kodi ya maendeleo kwa wakazi wake.

Katika uchaguzi wa serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, Chama cha CUF kimeweza kutwaa uongozi wote wa kijiji hicho cha Njia Nne wilayani Kilwa.

Akitangaza rasmi kukihama chama hicho hivi karibuni, kwenye mkutano wa hadhara uliokuwa umefanyika kwenye viwanja vya Sokoni mjini Masoko, Bw. Mnyika amesema kuwa ameamua kukifuata chama alichokiita kimeanza kuonesha mwelekeo kwa wananchi wake.

"Ndugu zangu nimeanza kuona ukweli na sasa ninaamua rasmi kukihama Chama cha CCM na kujiunga na CUF", alisema Bwana Mnyika.

Bwana Mnyika ambaye alikuwa amempigia debe mkongwe huyo wa siasa hapa nchini, na hatimaye akaibuka mshindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 19, 1995, alidai kuwa amefanya hivyo baada ya kuanza kuona matunda yaliyoanza kuoneshwa na chama hicho.

Aidha, aliendelea kudai kuwa, mwaka 1995 alifanya kazi hiyo ya kukipigia debe Chama cha Mapinduzi (CCM) akiamini kuwa huenda kingebadilisha hali ya maisha kwa watu waliokuwa wa hali ya chini, lakini badala yake alidai kuwa kimezidi kuwakandamiza walalahoi.

Naye Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Kilwa Bwana Selemani S. Bungara alidai kuwa huo ndio mwanzo na pindi chama hicho kitapata ushindi katika uchaguzi ujao, wataondoa kero zote, ikiwemo kufuta ada za shule, uchangiaji wa huduma za afya na kodi ya maendeleo.

Kijiji cha Njia Nne kilichopo wilayani Kilwa, chini ya uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kimeamua kuwafutia kulipa kodi ya maendeleo wanakijiji wake, kwa madai yakuwa kijiji hicho kina uwezo wa kuwalipia bila ya kuwatoza kutoka mifukoni mwao.

Bungara alidai kuwa uwezo wa kuwafanya watu wawe matajiri katika nchi yao upo, lakini kinachokosekana ni sera na uongozi mzuri unaojali maslahi ya watu wake.

"Kama mnavyotusikia tukisema siku zote, sera zetu ni haki sawa kwa wote na Utajirisho", alisema Bungara.

Katika mkutano huo jumla ya watu 250 walichukua kadi za CUF ili kujiunga na chama hicho, wakiwemo wa kutoka vyama vya CCM, TLP, UDP na NCCR-Mageuzi.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook