VIJANA mkoani Tanga, wameonesha mwamko mkubwa wa kisiasa katika uchaguzi wa mwaka huu kwa kuwa mstari wa mbele katika zoezi la kujiandikisha kupiga kura.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa gazeti hili katika vituo mbalimbali vya uandikishaji wapiga kura, umeonesha kuwa vijana ndio wamekuwa mstari wa mbele katika kujiandikisha.
Kuhamasika huko kwa vijana, kumekuwa tofauti na chaguzi zilizopita ambapo waliokuwa wakijitokeza zaidi katika uchaguzi walikuwa wazee.
Pengine mwamko huo wa vijana unafuatia kujitokeza kwa mijadala mingi ya kisiasa katika baadhi ya mabaraza na maskani za vijana wakizungumzia haja yakuwa na taifa litakalowajali vijana.
Uchunguzi huo umeonesha kuwa katika kipindi hiki cha mabaraza na maskani nyingi za vijana zilizopo katika kona mbalimbali za mji gumzo kubwa limehusu siasa.
Katika mijadala yao, vijana wameonesha nia ya kutaka mabadiliko zaidi ili kuinua hali zao zinazoelekea kuzorota kila kukicha.
Baadhi ya waandikishaji wapiga kura, wamethibitisha
kujitokeza kwa wingi vijana kujiandikisha.
WAFANYABIASHARA ndogo ndogo maarufu, Wamachinga wanaofanya shughuli zao mataa wa Msimbazi, wamewekeana mikakati ya kujiandikisha kupiga kura kwa kile kilichoelezwa kujaribu kuondoa adha wanazozipata.
Wakiongea na mwandishi wa habari hizi mapema wiki hii, Wamachinga hao wamesema, kilichowasukuma zaidi kuhakikisha kuwa kila mfanyabiashara wa eneo hilo anajiandikisha ni maonevu wanayoendelea kufanyiwa na serikali iliyopo madarakani.
"Karibu kila siku tunaulizana wangapi wamejiandikisha na wale ambao bado tunawahimiza kufanya hivyo na wakati mwingine tunawashikia biashara zao, kwani safari hii hatutaki kufanya makosa ya mwaka 1995", alisema mmoja wa Wamachinga hao aliyejitambulisha kuwa anaitwa Aloyce Kondo.
Akifafanua makosa waliyoyafanya wakati wa uchaguzi huo wa mwaka 1995, Bw. Kondo alisema kuwa vijana wenzake wengi walikuwa wanashabikia siasa bila ya kujua lengo na kushiriki kuwabeba viongozi wa siasa.
Kosa lingine alililodai walilifanya ni vijana wengi kushindwa kujiandikisha na hatimaye kushindwa kupiga kura.
"Sasa hivi kila kijana inabidi aoneshe karatasi yake ya kupigia kura kwa sababu tumedhamiria kukomesha kunyanyaswa na dola, si umeona mwenyewe tulivyofukuzwa na mgambo wa Jiji kana kwamba sisi wakimbizi", alisema mfanyabiashara huyo huku akiwa na shahada yake.
Mwingine aliyezungumza na mwandishi wa habari hizi ni Bw. Ally Wandwi ambaye alidai wapo watu waliowafuata na kudai wawauzie shahada zao na wengine wakipigia kampeni vyama vyao, lakini amedai wameelimika, hawanunuliki wala kuuza haki yao.
Aidha, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika maeneo ya wapiga debe wa Kariakoo wamebaini kuwa wengi wao mpaka hivi sasa hawajajiandikisha kupiga kura kutokaan na sababu mbalimbali.
Wakiongea na gazeti hili wapiga kura hao wengi wao wakiwa vijana walisema kwamba wamebanwa sana na muda wa kutafuta riziki ambao wengi wao wanatoka majumbani mwao asubuhi sana na kurejea usiku, hivyo kukosa muda wa kushiriki zoezi hilo la kujiandikisha.
"Sisi sote tunapenda kushiriki kupiga kura, lakini muda hatuna kwani ukichelewa tu kufika kituoni wenzio wanakupiga 'bao', hivyo unaweza ukalala njaa kutokana na kuchelewa kufika kituoni", alisema mpiga debe mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mahimbo.
Pia uchunguzi umebaini kuwa wengi wa wapiga debe hao wamekosa mwamko wa suala zima la uchaguzi ambapo wengine wameonesha wazi kutoona umuhimu wa kushiriki kwa madai kwamba wakijiandikisha wasijiandikishe viongozi watakaokuwepo madarakani ni wale wale.
Vile vile gazeti hili lilitembelea baadhi ya vituo
vya kujiandikisha na kushuhudia waandishi hao wa wapiga kura muda mwingi
wakiwa wamepumzika kwa kusoma magazeti au kuongea na mawakala wa vyama
vya siasa kufuatia kutojitokeza watu wa kujiandikisha.
RAIA mmoja wa kizungu kutoka nchi ya Denmark Bw. Brown (45) aliyekuwa muumni wa dini ya Kikristo ,alisilimu jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Mzungu huyo ambaye kwa sasa atajulikaka kwa jina la Omar Brown alisilimishwa katika Msikiti wa Kwa Mtoro kabla ya swala ya Ijumaa iliyoswaliwa Msikitini hapo.
Akiwa kavaa kanzu nyeupe na kofia , raia huyo wa Denmark ambaye yupo nchini kikazi, alioneshwa mbele ya waumini baada ya swala na kupokelewa kwa takbiir .
Katika mahojiano mafupi na gazeti hili, Mzungu huyo alisema ameamua kusilimu kwa hiari yake baada ya kugundua kuwa Uislamu ndio dini ya haki na ukweli inayoendana na maumbile ya mwanadamu.
"Uislamu ndio dini ya haki na yenye ukweli juu ya imani na hili nimeligundua baada ya kufanya uchunguzi na kujifunza kutoka kwa Masheikh niliokuwa nao karibu na huyu aliyenisilimisha", alisema Bwana Omar.
Alisema awali yeye alikuwa muumini wa dhehebu la Anglikana ambalo ni miongoni mwa madhehebu ya Kiprotestant na alijikuta akijutia muda wake alioupoteza ndani ya Ukristo.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |