NAUNGA mkono kauli iliyotolewa na Rais Mkapa wakati akiliaga Bunge kuwa uchumi ndio siasa ya leo.
Kwa kweli, ukiyatazama maisha ya wanaadamu kwa ujumla, unabaini kuwa yana muelekeo mmoja wa kiuchumi.
Mfanyakazi anahangaikia uchumi, mfanyabiashara anahangaiki uchumi, mkulima anahangaikia uchumi. Kimsingi binaadamu wanagawanywa katika makundi haya matatu.
Kwa mantiki hii, siasa ya mfanyikazi ni uchumi, siasa ya mfanyibiashara ni uchumi na siasa ya mkulima ni uchumi.
Hata wale wasiomo katika makundi haya matatu nao pia siasa yao ni uchumi kwani namna moja au nyingine kila mmoja wao ana nia ama ya kuwa mfanyakazi au mkulima au mfanyibishara.
Tunapozungumzia matatizo ya nchi yetu siasa tunayoitumia ni uchumi. Mkulima analalamika kwa kukosa soko la mazao yake au kukopwa mazao yake.
Mfanyibiashara analalamika viwango vya juu vya kodi na ushuru, uhaba wa wateja utokanao na mzunguko finyu wa fedha.
Na wengine nao wanalalamika kwa kukosa ajira, mitaji ya kufanyia biashara na zana za kulimia. Na sote tunalalamika tatizo la rushwa.
Wananchi wote tunaunganishwa na siasa moja tunapozungumzia matatizo yetu. Na siasa hiyo ni uchumi, hata siasa ya mwizi, jambazi na kahaba ni hiyo hiyo ya uchumi.
Hata siasa ya vyama vya upinzani ni hiyo hiyo. Wapinzani wanaikosoa serikali kwa umasikini unaoikabili nchi na kwa uuzaji holela wa mali za umma.
Nayo serikali inapojibu mapigo inatumia siasa hiyo hiyo ya uchumi, ndipo zinaposikika kauli za misamaha ya madeni, uchumi kukuwa kwa asilimia nne, makusanyo ya kodi na kadhalika.
Unaposikia serikali fulani imefanikiwa basi vigezo vya mafanikio yake ni vile vya kiuchumi. Na ukisikia Kiongozi amefeli basi tatizo kuu ni uchumi.
Mvutano mkubwa uliopo baina ya serikali na wananchi ni ule wa kiuchumi. Nguvu ya siasa za upinzani kwa kiasi kikubwa imetokana na mazingira duni ya uchumi.
Hata mivutano kati ya mataifa makubwa na yale madogo ni ya kichumi. Vikao vikubwa vikubwa vinavyoitishwa duniani mara nyingi vinahusu uchumi.
Nchi zinazoitwa kubwa au zilizoendelea zinaitwa hivyo kwa sababu ya uchumi na zile zinazoitwa ndogo zinaitwa hivyo kwa sababu za kiuchumi. Tanzania ni miongoni mwa nchi masikini duniani kwa sababu ya uchumi.
Kilio cha nchi ndogo ni cha kiuchumi. Wadogo wanalia wafutiwe madeni na wakubwa wanaweka masharti kwa maslahi yao kiuchumi.
Sasa basi kwa kuwa siasa ya leo ni uchumi na kwa kuwa nchi yetu inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi, si ushabiki tukisema sasa nchi akabidhiwe mwenye fani yake.
Ni wazi kuwa kama una gari bovu huwezi kulipeleka kwa daktari hospitalini na kama una mgonjwa huwezi kumpeleka kwa makanika.
Zamani tulihitaji zaidi siasa za kidiplomasia kwa ajili ya kufanikisha harakati za ukombozi wa Afrika. Hivi sasa siasa hizo hazina umuhimu kwetu.
Ndio maana hata hadhi ya Taifa letu duniani imeporomoka. Leo Tanzania ni maarufu kwa umasikini sio kwa ukombozi wa Afrika. Hata hadhi ya muasisi wa Taifa letu imefifia mno muda mfupi baada ya kifo chake kwa sababu ya umasikini wa nchi yetu.
Kinyume chake nchi kama Nigeria na Afrika kusini ndizo zinazovuma duniani. Hata viongozi wake wana sauti inayosikika duniani.
Kigezo cha kuheshimiwa kwao ni uchumi ambao ndio siasa ya dunia ya leo.
Ipo hoja kuwa Rais sio lazima awe msomi wa uchumi. Mimi nasema kwa mazingira ya siasa na utawala nchini mwetu, tunahitaji mtaalamu wa uchumi. Hii ni kwa sababu tofauti na nchi zingine ambako, mashauri ya wataalamu yanazingatiwa , hapa kwetu mambo hayako hivyo, ukereketwa ndio unaothaminiwa. Bajeti zinapangwa na kupitishwa kisiasa, kodi zinakusanywa kisiasa, kilimo maneno matupu.
Katika mazingira hayo lazima akae mchumi. Mantiki inatulazimu kuikubali hoja kuwa kuna madaktari wawili wa kutibu, huyu anategemea ushauri wa yule wa pili, na yule anaetegemewa kwa ushauri yu tayari kukutiba, utamchagu yupi? Hivi waweza kuhatarisha maisha yako kwa kumchagua yule anaetegemea ushauri?
Nadhani hiari na kazi wanayo wenyewe wananchi wa Tanzania. Watachagua wampe nani madaraka awatatulie matatizo yao ya kiuchumi.
Batuli Hussein
128 Horton Hill,
Epsom - Surrey,
KT 19 8ST,
UK.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |