BARUA

Wanahabari vipi?

Ndugu Mhariri,

Kwa muda wa miezi miwili kabla ya kampeni kuanza inasemekana ziliandaliwa semina kadhaa kwa wanahabari wetu.

Mapesa mengi yametumika ikilengwa kuwakumbusha wanahabari hao yale wanayoyajua katika uwanja huo na zaidi namna ya kuripoti habari zinazohusiana na uchaguzi mkuu wa vyama vingi ambao utafanyika mwezi oktoba.

Nimeelezwa na baadhi ya walioshiriki semina hizo kuwa, ilisisitizwa wapiga kura wapewe taarifa zitakazowaelekeza kufanya maamuzi huria juu ya nani anayefaa kuongoza jahazi hili kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Inasemekana wanahabari waliambiwa kutoa nafasi sawa kwa vyama vyote, kutoa habari sahihi na zilizokamilika, na kutoa mwanga kwa wapiga kura kwa kuchapisha hotuba makini zinazoonekana kujali hali na maslahi ya wapiga kura na nchi kwa ujumla.

Vyombo vya habari vya serikali kama Radio na Televisheni vilitakiwa kutoa habari zisizopendelea chama fulani kwa sababu vinaendeshwa na walipa kodi ambao ni wananchi wote bila ya kujali uanachama wa chama tawala au Upinzani. Na vilitakiwa kutoa nafasi na muda ulio sawa kwa vyama , wagombea na mikutano yao hadhara.

Aidha vile vya binafsi vilitakiwa kutokushinikizwa na serikali, wachapishaji au chama tawala kuvuruga mikutano, kuficha ukweli na kuvipa picha isiyo ya kweli vyama vya upinzani na wagombea wao.

Kinachosikitisha baada ya semina hizo ni kusoma au kusikia habari za upande mmoja tu. Nadhani vyombo vya habari vimedhamiria kukibeba chama tawala.

Mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu bara inadhihirisha dhamira hiyo ya vyombo vyetu vya habari. Kana kwamba uchaguzi huu ni wa chama kimoja, vyombo hivyo hasa Radio ya Taifa, vimeng'ang'ana kuripoti kampeni za CCM peke yake.

Wakati wa ufunguzi wa kampeni hizo siku ya jumamosi, mikutano ya vyama viwili ilifanyika Jijini, cha kusikitisha magazeti yote yalichapisha habari juu ya kuwepo mkutano wa CCM Jangwani. Habari za mkutano wa Kidongo Chekundu zikawekwa katika namna ya kitendawili! Na hata vilipokuja kuripoti siku iliyofuata kana kwamba hapakuwa na chochote Kidongo Chekundu, mkutano wa CCM Jangwani ndio uliopewa nafasi ya juu katika magazeti yote.

Kwa makusudi kabisa vyombo vyetu vya habari vilipotosha taarifa juu ya mkutano wa CUF.

Vyombo hivyo, kimoja kiliripoti kuwa mkutano huo usingekuwepo, kingine kikaripoti mkutano huo ungefanyika sehemu nyingine. Mbaya zaidi Radio moja iliendelea kuripoti kutokuwepo mkutano huo hata baada ya maelfu ya watu wakiwa wameshakusanyika Kidongo Chekundu, mahali ambapo si hatua nyingi kutoka ilipo radio hiyo!

Hata hivyo wananchi walipuuza taarifa za vyombo hivyo badala yake hawakuonekana kuelekea kule walikodanganywa kuwa kungefanyika mkutano huo wala kuamini kuwa mkutano huo usingefanyika, wakamiminika kwa wingi eneo walikofahamishana nyumba kwa nyumba na mtu kwa mtu.

Wanahabari wetu chonde chonde, tuko katika kipindi ambacho nchi iko chini ya Milki ya wananchi wenyewe. Wananchi wanajiandaa kutoa maamuzi ya nani wamkabidhi nchi kwa niaba yao kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Katika hali hiyo umakini na kujali kwenu maslahi ya nchi na watu wote, utachangia kupatikana Kiongozi bora atakayelivusha jahazi hili kutoka katika wimbi zito linaloekelekea kuzamisha nchi kama nyambizi ya Urusi. Kinyume chake mtakuwa mmechangia kuwadumisha Watanzania katika siasa za ubabaishaji, umasikini, ujinga na maradhi ndani ya kapu la "amani na utulivu".

Mwamshindo Shaha
Ilala,
D' Salaam


RTD yahimiza kuchanganya siasa na dini

Ndugu Mhariri

KUPITIA Redio ya Taifa (RTD) saa sita kasoro kumi kila siku usiku huwa kuna vipindi vya dua kwa Waislamu na Wakristo ili kumuomba Mungu walale na waamke kwa salama na amani.

Kama wiki mbili hivi zilizopita katika kipindi hicho kilianza na dua kutoka kwa Waislamu na mawaidha mafupi wakati tunapotaka kulala nayo yalitolewa na Sheikh Gorogosi.

Baadaye ikawa ni dua kutoka kwa Wakristu. Cha kushangaza kilichotolewa si dua bali ni kuwahimiza Wakristu kuepukana na propaganda ya kutochanganya dini na siasa.

Msemaji huyo alisema amekuwa akiwasikia Wakristo wakizungumza wao kwa wao kutochanganya dini na siasa. Kwamba siasa mbali na dini mbali akaendelea kusema na kuwatahadharisha waondokane na propaganda hiyo kwa kuviweka hivyo vyote pamoja na kuvihusisha na maisha yao ya kila siku.

Na mwisho katika kumalizia msemaji huyo aliwahamasisha Wakristo wenzake kwenda kujiandikisha kupiga kura ili wawachague viongozi walio bora.

Mimi binafsi sistaajabu kuhamasisha watu kuchanganya dini na siasa. Kinachonishangaza ni uhamasishaji wa msemaji huyo kuchanganya dini na siasa kupitia Redio ya serikali ambayo serikali hiyo inaimba kila leo na kuwatuma vibaraka wake kuwataka watu wasichanganye dini na siasa.

Na vile vile kuona kwamba mambo ya siasa yanahamasishwa katika kipindi kilichotengwa kwa ajili ya dua.

Kwa upande mwinigne ni vigumu kuamini ujasiri wa muhamasishaji huyo kupitia chombo cha serikali na kusema hayo aliyoyasema, lakini hata hivyo inatubidi tuamini tu kwa sababu kanisa limejikita katika serikali na siasa ya Tanzania kiasi kwamba utendaji na utekelezaji wa vyombo mbalimbali vya serikali umekwa wa mkondo Kristo.

Mwisho napenda kuwaasa Waislamu wenzangu na wale wapendao haki tusitishike na mifumo "Katoliki" tufanye juhudi kujikwamua na zaidi kujiandikisha kupiga kura ili tusipoteze haki zetu za kikatiba.

Ngoi K. Ibrahim,
S.L.P. 3075,
Mwanza.


Mgombea Ubunge kwa tiketi ya CUF Handeni ashitakiwe

Ndugu Mhariri

KWANZA ni kitendo cha kinyama sana kwa ndugu yetu ambaye alikuwa mgombea ubunge kwa kutumia tiketi ya CUF Handeni mashariki.

Sisi wanachama wa Chama cha CUF tunasikitika sana kwa kijana mwenzetu toka mwaka 1995 tulikuwa tunauliza ni nani ambaye anaweza kutusaidia kimawazo.

Hasa katika mfumo huu wa vyama vingi. Lakushangaza ni kwamba eti kachelewa kurudisha fomu. Katuibia mawazo yetu na mwelekeo wetu sasa tupo gizani kabisa tena totoro hatujui twende wapi. Maana sisi watu wa vijiji hivi vifuatavyo CCM imetuchoka. Vijiji vyenyewe ni ni hivi: Kwasunga, Kwangange, Kwagunda, Kwandunga na Pozo hali ya wananchi waishio vijiji hivi wanatia huruma utafikiri kwamba hawapo Tanzania.

Kwanza barabara haipitiki, usafiri wao hutumia matrekta toka Pangani hadi Maono. Pili, maji ya kunywa kutoka kijijini mpaka huko yanakopatikana maji ya kisima ni maili 12.

Mwanamke akitoka nyumbani saa 11 alfajiri anarudi saa 5 asubuhi au saa sita mchana.

Na akitoka huko ndoo ya maji ni moja tu haya kuoga wapi, kupikia wapi kuoshea vyombo wapi kufulia wapi.

Kwa upande wa hospitali hakuna toka Mbunge Kigoda alivyojenga hilo boma la nyumba mwaka 1995 hapo Kwasunga mpaka 2000 bado analipigia kampeni anasema nipeni kura nimalizie. Nyumba moja inapigiwa kampeni miaka 10.

Miaka arobaini (40) ya CCM haijaboresha maisha ya vijiji hivi.

Tunaomba watu wanaoomba ubunge halafu wanawaibia wananchi mawazo yao halafu wananunuliwa dakika za majeruhi ni sawa na dereva wa gai la mafuta katumwa Dar hadi Arusha kabla hajafikikisha akauza mafuta yote kufika Wami akatosa na gari mtoni.

M.M. Bolli,
Kwasunga,
HANDENI.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook