Joka la Mdimu - 23
USIKU ule ulikuwa mgumu kupita yote maishani mwake. Roho yake ililia na kuomboleza, machozi yake yakapukutikia ndani kwa ndani. Ukali wake ukamchoma mno. Aliomba asubuhi ifike akabiliane na lile alilolikusudia.
"Mimi leo sitakwenda hostali asubuhi", alimweleza mkewe ambaye aliamka kabla yake kutayarisha chai ya Cheche. Mkewe alishtuka, akauliza kulikoni.
Tino alichukua muda mrefu kujibu akiwaza nimwambie, nisimwambie? Hatimaye alisema: "Ngoja nitakueleza nikitoka kuoga".
Alivundumka kwenda kuoga. Aliporejea alimkuta mkewe kaketi kitini kashika tama.
"Mbona hivyo mama Cheche?"
Mkewe aliguna, bila ya kujibu, kisha akavuta pumzi na kutunisha kifua chake kidogo kwa muda mrefu kabla ya kupumua kwa nguvu. Tino aliacha kuchana nywele, akamgeukia. Alimtazama kwa muda mrefu sana. Kisha alikwenda akachomoa mfuko wa karatasi chini ya kabati la nguo akamkabidhi mkewe.
"Nini?" aliuliza kwa mastaajabu.
"Fungua", Tino alimwelekeza.
Mkewe alifanya hivyo kwa hadhari. Alipoona kilichokuwa ndani aliinua tena macho yake kumtazama mumewe.
"Hesabu".
Mkewe alivihesabu vichangata vya noti zilizokuwa mle, hatimaye akasema; "laki moja".
"Sasa sikiliza mke wangu", Tino alisema kwa utulivu mno.
"Sikiliza kwa makini".
Kimya tena, akaendelea, "Fedha hizo akiba yako na watoto endapo sitarudi".
Kidogo mkewe aanguke, akashindwa hata kuuliza kitu. Hivyo Tino akamtobolea. "Ninakwenda kutafuta fedha za kumpeleka Cheche akatibiwe Ulaya".
"Sasa ndiyo hurudi?"
"Kwa bahati mbaya yakitokea matatizo".
"Lakini..."
"Nini!" Tino aliinua mikono kumkatisha, akaendelea sawia. "Nenda hospitali, nisalimie sana Cheche".
Mkewe alitoka akifuta machozi, nyuma Tino akavalia ile suti ya mistari, na tai, kisha akachukua kofia ya pama nyeusi akaivaaa. Halafu alitia risasi kumi ndani ya bastola yake na kuichomeka kwenye mfuko wa ndani wa koti. Alitoka kupitia kwa Amani.
"Barabara". Amani alipomwona. "Tena uchukue na huu mfuko!" Akatoa mfuko wa kuwekea vitabu kutoka chini ya meza na kumkabidhi.
Basi walikaa hapo wakisikiliza muziki, mara moja moja wakizunguma, kusubui saa muafaka.
"Lazima tufike pale wakati watu wamepungua kabisa, karibu na kufunga benki".
Kufika saa saba na nusu Amani alimpa Tino ndevu za bandia, akazivaa. Waliondoka ndani ya Peogeot 504 ambayo Amani aliiazima kwa rafiki yake, akaipachika namba za bandia.
Mbele ya Tawi la Standard Bank jijini Mindule Amani aliegesha gari lake, kisha alimgeukia Tino. Moyo wa Tino ulikwenda kasi mno hata karibu apooze. Lakini kama radi fikra zake zikarejea kitandani kwa Cheche aliyesawajibika kwa maumivu makali na kulala kwa zaidi ya miezi miwili. Akapata faraja ghafla kwa tendo lililomkabili. Hata Amani aliporudi, moyo wake Tino ulikwishageuka jabali. Aliipapasa vizuri bastola yake, akatoka huku kashika ule mkoba mkono wa kushoto.
"Nisubiri", akasema kwa sauti nzito.
Pale nje ya Benki palikuwa na askari mmoja akilinda kashika sub-machine gun. Alitembea huku na kule kwa hatua fupi fupi. Mara moja aliinua mkono wake kuangalia saa kwa uchovu wa kusimama tangu asubuhi.
Amani alimuangalia Tino akitoweka ndani ya Benki. Alipiga moto gari na kuliacha likiunguruma kimya kimya tayari kwa kuondoka.
Mle ndani mlikuwa na watu wachache mno. Bila ya kupoteza muda Tino alikwenda kunako kaunta ya karibu na mlango. Mrembo nyuma ya kaunta aliinamia mabunda ya noti alizokuwa akihesabu. Kivuli cha Tino kilipomsogelea aliinua macho. Tino aliuweka mkono wakae juu ya kaunta. Akaufungua kama atayae kutoa fedha. Badala yake akachomoa kikaratasi kilichoandikwa TIA MILIONI TANO UPESI SANA.
Yule msichana alibenua midomo yake kwa dharau kumtazama Tino akakuta uso wa chuma, ndevu kama beberu la kafara, mkononi ameshika bastola iliyomuelekea kifuani pake. Ndoto au nini? Yule binti alitaka kugeuka na kupiga kelele, akahofia maisha yake.
Ndoto si ndoto tena. Upesi aliyatoa yale mabunda ya noti kumkabidhi Tino ambaye aliyapanga chapuchapu. Upesi aliufungua mkoba ule huku akirejea kinyumenyume. Halafu akaongeza hatua hizo upesi. Nyuma yake ikasikika sauti iliyopasua anga, "mwizi! Mwizi!
Lakini Tino alikuwa amekwishachapukia upande wa pili wa barabara.
Amani alimfungulia mlango wa nyuma akaingia. Katika mtafaruku ule ilikuwa vigumu kuelewana. Hatimaye watu walitoka nje wakionesha kidole lile gari la Amani. Yule askari pale nje aliinua bunduki kutaka kupiga lakini Tino alimpiga risasi ya tumboni. Gari likatokomea kwa kasi kubwa huku watu wakimkimbilia yule askari aliyelala chini akitapia roho yake.
KATIKA wadi ya daraja la kwanza ya Hospitali ya Rufani ya Mindule, Gray Kwacha alikuwa amelala kwenye chumba cha pekee. Aliletwa hapo jumamoja lililopita taabani baada ya kuziba mkojo kwa siku mbili nzima.
Asubuhi nesi mmoja alipita chumbani mwake kupiga deki na kuacha harufu kali ya Detrol. Gray Kwacha alikuwa amekwishaamka lakini bado kalala chali kajifunika shuka nyeupe kutoka dole gumba hadi kifuani. Si mbali na kitanda chake palikuwa na meza yenye dawati, juu yake paliwekwa chupa ya chai, madafu mawili na riwaya tano za waandishi mbalimbali wa lugha ya Kiingereza. Juu kabisa ilikuwa ile ya Fredrick, Day of the Jackal, ambayo aliisoma na kuirudia tena mara zisizo hesabu.
Punde si punde aliingia muuguzi mwanamume akiwa na gazeti la kila siku, Times. Upesi Gray Kwacha alilichukua gazeti hilo akapekua kurasa hadi kurasa kwanza akisoma vichwa vya habari. Alipofika ukurasa wa tatu moyo ulimpasuka aliposoma:
"Wabunge wadai maelezo kuhusu Meli ya Mafuta". Habari ziliendelea: "Wabunge wamemtaka Waziri wa Fedha atoe maelezo kamili kwa nini serikali imeshindwa kulipatia taifa mafuta ya petroli na dizeli kwa muda mrefu. Aidha, wamedai waelezwe kwanini meli iliyoleta mafuta imeondoka bila ya kuyapakua. Na wamemtaka Waziri huyo awasilishe bungeni mahesabu kamili ya mapato na matumizi ya fedha za kigeni kabla ya mwisho wa kikao hiki cha Bunge".
Gazeti hilo lilitetemeka mikononi pake kama tanga la jahazi katika kusi, asiweze kulizuia likamponyoka mikononi hadi kifuani pake. Akawa atweta kupita aliyekimbia mbali. Huku na kule alitumbatumba kutafuta kama yupo aliyemfaidi katika mtafaruku ule. Kuona hakuna mtu machoni wala jirani, alijikusuru kuliokota tena lile gazeti, huku akipuna jasho juu ya paji lake la uso, akaendelea kusoma makala yake fupi. Punde alihisi tumbo likimsonga, asiweze kuendelea tena! Alifumba macho akiwaza, picha mbalimbali zikiyumba akilini mwake.
Muda mfupi kupita daktari na wenzake walimfikia na kukizunguka kitanda chake.
"Habari ya asubuhi Bwana Kwacha", alisabahi nesi mrefu, kavaa gauni jeupe, kama wafanyavyo manesi wote, tepe mbili za bluu zikiwa zimetua juu ya mabega yake. Kabla hajajibu yule daktari naye akamsogelea karibu zaidi na kumuuliza, "unaendeleaje?"
"Sijambo", alijibu. Daktari alimuangalia vizuri machoni, akawageukia wale wanafunzi wa uganga kuzungumza nao kabla hajamuashiria yule nesi kumfunua shuka Gray Kwacha.
"Utatuwia radhi kidogo", Daktari alimueleza Kwacha aliyekuwa hana la kufanya. Tangu amefika hapo jambo hilo lilikuwa ndio ibada, mwisho wauguzi na wanafunzi wote wataniona uchi wangu, alikasirika. Lakini mficha uchi hazai!
"Utaendelea na dawa zao na usiache kunywa maji mengi ya madafu". Daktari alimsisitizia Gray Kwacha. Lakini Kwacha alikuwa ameshafikiria mambo mengi katika kipindi kile kifupi, akamwita daktari, ninaomba tuzungumze faragha mimi na wewe".
"Sasa hivi?" Daktari yule, mtu wa makamu, alimgeukia akamsogelea.
"Kama inawezekana".
Daktari alitabasamu akamuangalia, "vyema. Ngoja tumalize wagonjwa wengine katika wadi hii, nitakuja".
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |