VUMBI limetulia imebaki historia. Wapo wanaodai ni mafanikio makubwa Rais Clinton kutembelea Tanzania. Wao huona fahari kuifanya ziara hiyo jukwaa la kampeni.
"Hata Clinton katusifu kuwa uchumi wetu umekuwa", hunadi.
"Si mchezo, tumefanya makubwa mpaka kakubali tusaini naye makubaliano ya anga huru", wanaendelea kunadi.
Lakini anga hii huru kwa manufaa gani na ya nani? Marekani uwezo wa kuyarusha madege yao ya abiria na hata yale ya kijeshi juu ya anga ya Tanzania wanayo.
Lakini je, Tanzania inayo ndege ya kukatiza bahari ya Atlantiki hadi Marekani? Je, Marekani ikitaka kuitumia anga yetu kuingia Congo? Hayo hayaelekei kuzishughulisha bongo za wengi.
Clinton kasema tumejenga uchumi imara lakini kauli hiyo imebadili hali halisi?
Je, madawa na vifaa muhimu sasa vipo mahospitalini? Je, kila mahali sasa maji safi yapo? Hali ya barabara je! Mashuleni nako je, madeski, vitabu na mishahara ya waalimu inatosheleza!
Yule ambaye alikuwa na shida ya kuwapatia wanae mlo kamili na ada ya shule, hatudhani kauli hiyo ya Clinton imemuondolea shida yake.
Taarifa za shirika la Utangaza la Uingereza BBC jana asubuhi lilitoa tathmini ya kusikitisha.
Lilisema gari la Mhe. Rais wetu Mkapa ilibidi nalo likapekuliwe na mbwa wa Marekani, jambo lililofanya Rais kuduwaa.
Aidha, lilisema ilikuwa kana kwamba usalama wa nchi yetu ulikuwa chini ya wana usalama kutoka Marekani. Hata walinzi wa Marais wengine waliokuwepo hawakuruhusiwa kuingia ndani.
Lakini jingine, mtangazaji wa BBC akasema kuwa Rais Clinton yeye alikuwa akinywa Coca Cola yake kutoka Marekani huku Marais wengine waliohudhuria hafla ya utiaji saini mkataba wa amani Burundi wakinywa maji ya Kilimanjaro.
Maelezo haya yamebeba maswali mengi ambayo pengine kama majibu yake yanapatikana yaweza kujibu swali la msingi: Je, ziara hiyo ni fahari au ya kutudhalilisha na fedheha?
Nini tafsiri ya walinzi wa Rais Clinton kuacha mbwa wao wanuse gari la Mhe. Rais Mkapa! Walituhumu nini. Kwanini walinzi wa Marais Museveni na wenzake wao watiliwe mashaka! Wao ndio kama wenyeji wa Rais Clinton. Vipi mtu aje nyumbani kwako lakini ageuke kuwa kiranja wa kukuelekeza la kufanya.
Asubuhi tu kuamkia usiku alipoondoka Bw. Clinton imeelezwa kuwa mji wa Arusha ulikuwa hauna maji.
Watu walihaha huko na huko kutafuta maji ya kunywa wasiyapate.
Mtangazaji wa BBC alisema, pengine kwa kejeli, kuwa ziara ya Clinton ilikuwa imekausha maji.
Haikuwa kauli bila ya mashiko kwani siku moja kabla ya Clinton kuwasili, magari ya zima moto yalisheheni maji na kuusafisha mji kana kwamba wanapiga deki barabara.
Sisi tunasema, kama uchumi wetu umekuwa wananchi ndio wavaa viatu wanajua wapi kina bana.
Heshima yetu ipo katika kujiamini na kujijengea maendeleo yetu wenyewe na wala sio kwa kusifiwa na watu ambao hata wakija kwetu huja na maji yao ya kunywa na kutupekuwa na mbwa wao.
Wanasiasa wamejijengea sifa moja: Hata akikukuta
watoto wako wamegeuka vibaka, changudoa na wazamiaji kwa kukosa ajira,
atakusifia kuwa uchumi wako umekua na umeongeza ajira nyingi.
--
![]()
|
|