Kampeni za CUF, CCM Zanzibar:
Piga mawe, FFU kimya
MSAFARA wa magari yapatayo 200 juzi ulipigwa mawe na kuwekewa vizuizi barabarani. Msafara huo ulikuwa ukielekea Makunduchi katika mkutano wa kampeni wa CUF.

Wapiga mawe hao wanaodhaniwa kuwa wakereketwa wa CCM walisababisha gari moja kupata ajali.

Watu 15 walijeruhiwa ambapo hadi jana wanne walikuwa bado hospitalini.

Gali hilo lilipata ajali wakati likikwepa mawe ambayo yalikuwa yamepangwa barabarani kama vizuizi.

Watu wengine walijeruhiwa katika eneo la Taveta ambapo wafuasi hao wa CCM wamedaiwa kuyavurumishia mawe magari ya CUF.

Polisi wakiwemo wale wa FFU waliokuwa wakifuatilia msafara huo wameelezwa kutochukua hatua zozote kuwafuatilia na kuwakamata waliokuwa wakirusha mawe hayo.

Hata hivyo, kutokana na umati mkubwa uliokuwa umefurika Makunduchi, polisi walikuwa wamechukua tahadhari kubwa kutwa nzima.

Polisi wengi walimwagwa mitaani wakiwa tayari kukabiliana na tafrani yoyote ambayo ingeweza kutokea.

Katika tukio moja ilibidi wafanye kazi ya ziada kumnusuru Waziri Abdissalami Khatib na gari lake.

Naibu Waziri huyo wa Fedha wa serikali ya Muungano amedaiwa kuwa alilivurumisha gari lake katika umati wa watu.

Walioshuhudia tukio hilo wameeleza kuwa watu walikimbia ovyo kulipisha gari hilo.

Hata hivyo, hakuna taarifa za majeruhi.

Aidha, imeelezwa kuwa kwa hasira watu walilishambulia gari hilo kwa mawe, polisi wakalazimika kumnusuru na kumuondosha.

Mhe. Abdisallaam ni mgombea Ubunge katika jimbo hilo la Makunduchi kupitia CCM.

Taarifa kutoka Zanzibar zinaeleza kuwa kutokana na msafara wa CUF kuwa na magari mengi polisi ilibidi wakati wa kurudi iyazuie kiasi maili 10 kabla ya kuingia mjini.

Magari hayo yalikuwa yakiruhusiwa kuingia mjini kidogo kidogo ili kuepusha msongamano.

"Ilibidi polisi waruhusu magari kumi, kumi kuingia mjini juzi jioni vinginevyo ingekuwa vurugu mjini", amesema mpashaji habari wetu.

Mkutano huo wa juzi ni moja ya mikutano ya kampeni ya Maalim Seif Sharif Hamad kugombea Urais Zanzibar.

Katika hali isiyo ya kawaida mitaa na vichochoro vyote vya Unguja vimejaa mabango ya wagombea wa CCM, wakati hakuna hata moja la CUF.

Picha za Mhe. Mkapa, Karume na wagombea Ubunge kupitia CCM zimetanda kila mahali huku ikiwa haionekani hata moja ya Maalim Seif au Lipumba.

Wananchikadhaa walioongea na mwandishi wa habari hizi wamesema hata wanachama wa CUF wamelazimika kubadika picha za Karume na Mkapa ili kuepusha shari ya polkisi.

Taarifa nyingine zinaeleza kuwa chama cha CUF chenyewe hakijatoa mabango na kuwataka wafuasi wakee wabandike.


CCM hatutoki, lakini kura No
WANA-CCM wa Kilwa kusini wamedai kuwa CCM hawatoki, lakini hawamtaki mgombea Ubunge aliyepitishwa na CCM.

Taarifa kutoka kijiji cha Lihimaliyao zimedai kuwa wana-CCM wamekuwa wakinadi ujumbe huo kila mahali.

Lihimaliyao ndipo anapotoka Bw. Omar Mwenda aliyepitishwa na NEC ya CCM kugombea Ubunge japo alishindwa na Bw. Athuman Gullam Dewji (Sinani) katika kura za maoni.

Wananchi kadhaa walioongea na mwandishi wa habari hizi wamesema, wao bado chama wanakipenda, lakini maadhali kimewapuuza hawatampigia kura mgombea waliyeteuliwa.

Hata hivyo, wamesema, iwapo Mhe. Rais Mkapa aliye Mwenyekiti wa CCM naye hatawapa maelezo ya kuridhisha watalazimika kumkabidhi kadi zao za CCM ikimaanisha wametoka chama.

"Tumerejesha shahada za kupigia kura bado kadi tutamkabidhi Mwenyekiti (Mkapa) atakapokuja iwapo hat awala ziara yake.

Viongozi kadhaa wa CCM na wajumbe rasmi wamejaribu kutatua mgogoro huo lakini hawakufanikiwa.

Akiwa Mikumi hivi karibuni Rais Mkapa amewaonya wanaotaka kukihujumu chama kwa vile watu wao wameenguliwa na NEC watoke CCM yenyewe.

Alisema ni bora watu hao watoke CCM kuliko kubaki huku wakiwaunga mkono wagombea kutoka upinzani.

Katika hatua nyingine Mkapa alimpongeza Bw. Aziz Abood kwa kuheshimu maamuzi ya chama.

Akiwa Morogoro mjini katika kampeni zake, alisema amefurahishwa kwa uamuzi wa Abood kubakia katika chama na kukipigia debe.

Amewataka walioenguliwa wawe na nidhamu katika chama na wawaunge mkono wenzao.

Akijinadi kutaka achaguliwe tena kuiongoza nchi Mkapa alisema, wapinzani hawajakomaa. Wengine hawana hata katiba, alidai.

Naye mgombea wa Urais Zanzibar kupitia CCM Bw. Amani Karume ameahidi kutengeneza bandari ya Wete iwapo ataingia Ikulu.

Aidha, amesema atatengeneza barabara toka Wete hadi Gando yenye umbali wa km 11 ambayo hivi sasa ina hali mbaya.

Karume alikuwa katika mikutano ya kampeni jimbo la Gando juzi.


'CCM wana picha, CUF wana watu'

"CUF wana watu, CCM wana picha na wapigao kura ni watu".

Huo ni usemi wa Bwana Tambwe Hiza alipokuwa akijinadi huko Temeke mwishoni mwa wiki iliyopita.

Bw. Tambwe anayegombea Ubunge Jimbo la Temeke amesema, tofauti na chama tawala chenye kuendesha kampeni zake kwa mapesa, wao kampeni zao zinakwenda kwa nguvu ya wananchi.

Amesema wakati mikutano ya CUF inafurika wananchi, CCM wamekazana kulipamba jiji kwa picha za wagombea wake.

Bwana Tambwe ambaye pia ni Mwenyekit wa CUF wilaya ya Temeke amesema, wananchi wanaofurika mikutano ya CUF wanakodisha magari kwa fedha zao wenyewe na wengine kutembea masafa marefu kwa miguu.

Ameitaka Tume ya Uchaguzi kuwa makini na kutenda kazi zake kwa uadilifu isijezusha vurugu.

Awali Bw. Tambwe akijinadi kwa wananchi alisema, wao (CUF) wameingia katika upinzani kwa lengo la kutatua matatizo ya wananchi.

"Tumeingia katika shughuli hii sio kujifurahisha, tuna lengo la kuchukua serikali ili kutatua matatizo ya Watanzania", alisema.

Aidha, aliwaeleza wananchi kuwa watakapoichagua CCM, hali itazidi kuwa ngumu zaidi.

Alisema, CCM imeua viwanda muhimu na hali imezidi kuwa ngumu kwa wananchi, si tu wale waliopunguzwa kazi, bali hali hiyo imeathiri wananchi kwa ujumla.

Alieleza kuwa, athari hiyo imesababisha wauza vitumbua kuwa wengi mitaani, na kufanya wanunuzi kupungua.

Naye mgombea Udiwani wa Chama hicho Bw. Haji katika mkutano huo aliwaeleza wananchi kuwa wamekosa maendeleo kwa muda mrefu bila sababu yoyote kwa maana wilaya hiyo ni moja ya wilaya za jiji zenye utajiri.

"Kura ni mkataba, unapompa mtu kura, alete maendeleo. Akikusanya kodi atoe huduma za jamii, elimu, maji na afya (hospitali), asipofanya baadhi ya hayo amevunja mkataba", alisema Bw. Haji.

Akijinadi aliahidi atakapochaguliwa atahakikisha barabara ya Temeke Yombo inapitika tofauti na sasa barabara hiyo inapitika kwa tabu.

Wakati huo huo, mgombea Ubunge Jimbo la Temeke (CCM), Bibi Khadija Kusaga amesema, iwapo atakipata kiti hicho atashughulikia elimu na haki za wanawake. Naye Dkt. Mahanga Milton Makongoro Mahanga, mgombea wa Ubunge kupitia CCM jimbo la Ukonga ameahidi kujenga shule mbili za sekondari jimboni humo.

Ahadi hizo zimetolewa na wagombea hao katika mikutano yao ya kampeni iliyofanyika majimboni kwao juzi.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook