MUFTI wa Bakwata amedai kuwa watu wamemtenga ambapo wengine wanadiriki kukataa hata kumuuzia vitu.
Aidha amekanusha kwamba yeye si mpiga debe wa CCM kama baadhi ya watu wanavyodhani.
Amesema wale wanaodai kuwa amekuwa akiinadi CCM mikoani walikuwa wakieneza mawazo potofu.
Mufti huyo wa Bakwata alitamka hayo wakati akizungumza na Waislamu wa mjini Tanga jumamosi iliyopita.
Amesema chuki iliyopandikizwa dhidi yake imeshamiri miongoni mwa Waislamu kiasi kwamba imefikia yeye kukataliwa hata kuuziwa shamba mjini Mang'ula mkoa Morogoro.
Akihadithia tukio hilo la kunyimwa shamba, Hemed alisema ilikuwa wamekubaliana na mtu mmoja wilayani humo kuwa angeuziwa shamba kwa gharama ya shilingi laki tatu, lakini alipokwenda kukamilisha maafikiano hayo mtu huyo alibadili mawazo.
Mzee Hemed alidai kuwa mtu huyo alimweleza kuwa kama angeendelea na mpango huo wa kumuuzia shamba Mufti wa Bakwata wanakijiji wenziwe wangemtenga.
Alimwambia kuwa hayo yalikuwa ni maamuzi ya Waislamu wa Mang'ula ambao wakati wa kujadili suala hilo kuna waliomuelezea Mufti kuwa ni adui wa Waislamu kwa hiyo ni kharamu kushirikiana naye.
Mufti wa Bakwata Hemed bin Juma amedai ziara yake mikoani haikuwa na lengo la kisiasa bali kuhimiza mshikamano, amani na utulivu nchini.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na mkuu wa mkoa, Bwana George Mkuchika na mkuu wa wilaya Bwana Said Mack, Mufti wa Bakwata alirejea kauli yake kuwa Waislamu hawawezi kushika nafasi za uongozi wa nchi kwa kuwa hawana elimu.
Aidha alikemea kauli ya baadhi ya viongozi wa dini wanaowahimiza waumini wao kuwa wawachague wachaMungu kwa mujibu wa dini zao.
Alisema hali hiyo inaweza kuifikisha nchi mahali pabaya ambapo iwapoWakristo watataka kuwachagua Wakristo wenzao basi na Waislamu nao watahimizana wachaguane wenyewe hivyo kuigawa nchi katika misingi ya dini.
Hotuba ya Mufti imetafsiriwa na wakazi wengi wa
mjini hapa kuwa ni jaribio la kutaka kujikosha baada ya zoezi lake la hivi
karibuni mikoani kukinadi chama tawala kugonga mwamba.
MENEJA wa Kampeni za CCM, Abdul Rahamani Kinana amekishutumu chama cha CUF kwa kile alichodai kuzua kuwa Zanzibar itamezwa iwapo wananchi wa huko wataichgua CCM kwa mara nyingine.
Bwana Kinana amesema CUF wamekuwa wakiwatisha Wazanzibar kuwa upo mpango wa kuimeza Zanzibar,
Amesema wanatumia hadaa hiyo kuwataka Wazanzibar wasiipe CCM kura.
Akiongea na waandishi wa habari jana katika ofisi za CCM Lumumba amesema mpango huo haupo bali Zanzibar ina uhuru zaidi kuliko Bara.
Bwana Kinana amedai kuwa Zanzibar wana Rais wao na hata Bunge lao na mambo mengi wanayojiamulia wenyewe ukiacha yale machache ya Muungano.
Hata hivyo hakufafanua ni kwa nini Zanzibar ipewe uhuru huo tofauti na bara.
Mheshimiwa Kinana amedai CUF wanatumia hadaa hiyo baada ya kukosa cha kuwaeleza wananchi.
"CUF inasikitisha sana kwa kusema CCM ina mpango wa kuimeza Zanzibar, hao ni wanasiasa waliofilisika na ndiyo maana wanaingiza sera za ukabila na udini", alisema na kuongeza kuwa kama kuna kitu wazanzibari wanaweza kujivunia katika Muungano ni kuwa na uhuru mkubwa kuliko wabara.
Alisema jambo la msingi linalotakiwa litazamwe ni jinsi gani Taifa linaweza kuyatatua matatizo ya Muungano.
Amedai hoja nyingi zinazotolewa na wapinzani hazina msingi kwa vile wamekuwa mabingwa wa ulalamishi.
Katika mazungumzo yake, Mheshimiwa Kinana hakugusia
chochote kuhusiana na maelezo ya Profesa Lipumba juu ya Takwimu za elimu.watahadharishana
WANACHAMA WA CCM katika wilaya ya Temeke wamewatahadharisha wagombea wa chama hicho na wapiga debe wao kuwa tabia ya kuwauliza wananchi wanaojitokeza kwenye mikutano yao ya kampeni kuwa wangapi ni wapinzani itakigharimu chama hicho.
Wakizungumza na gazeti hili mara baada ya mkutano wa kampeni wa chama hicho katika viwanja vya Mwembeyanga Temeke juzi, wanachama hao wamedai kuwa tabia hiyo inawapunguzia nguvu wanachama wa chama hicho kwa kuwa hudhidhirisha kuwa wengi wanaojitokeza kwenye mikutano hiyo ni wapinzani.
Akizungumza na wananchi katika mkutano huo mgombea udiwani wa kata ya Tandika Bw. Abushiri Kilungo aliuliza umati uliofurika kwenye mkutano huo kuwa wangapi walikuwa wanachama wa NCCR mageuzi ambapo hakukuwa na mtu aliyenyosha kidole na alipouliza wangapi walikuwa TLP walionyoosha vidole walikuwa tisa, alipouliza wangapi walikuwa CUF umati wote uliitikia kwa sauti "tupoo", isipokuwa wachache waliokuwa katikati ya uwanja.
Huko Mbagala nako hali ilikuwa kama hiyo ambapo mheshimiwa Kingunge Ngombare Mwilu alipouliza swali kama hilo takribani wananchi wote waliokuwepo hapo waliitikia kwa pamoja kuwa wao ni CUF.
Hata hivyo, wanachama wa CCM wamekuwa wakijigamba kuwa si lazima mikutano yao ihudhuriwe na watu wengi, wamedai wao hushinda uchaguzi kwa idadi kubwa ya kura kwa kutumia mbinu nyingine.
"Si uliona mwaka 95, mikutano ya Mrema ilikuwa na watu kibao kuliko sisi lakini tukashinda", alijigamba mmoja wa wanachama hao aliyejitambulisha kwa jina la Jakson.
Akizungumza katika mkutano huo, mgombea ubunge wa chama hicho jimbo la Temeke Hadija Kusaga aliwaomba wakazi Waislamu wa jimbo hilo kumpigia kura, huku akidai kuwa Uislamu hauruhusu wanawake kuwa viongozi.
Wakati huo huo, chama cha Mapinduzi wilayani Temeke kimefuta mkutano wa kampeni uliokuwa ufanyike katika viwanja vya Zakheem jana, bila taarifa yoyote.
Kwa mujibu wa ratiba ya mikutano ya kampeni katika
jimbo la Kigamboni, mkutano huo ilikuwa mgeni rasmi awe mgombea Urais wa
CCM Bw. Benjamin Mkapa.
--
![]()
|
|