MAELFU ya wananchi wa Sumbawanga mjini walifurika kwenye mkutano wa kampeni uliofanywa na mgombea Urais kwa tikiti ya chama cha CUF, Prof. Ibrahim Haruna Lipumba.
Mkutano huo ulifanyika katika uwanja wa Reli mjini humo.
Prof. Lipumba ambaye aliongozana na Naibu Mkurugenzi wa Fedha wa chama hicho Bi. Chaurembo, alilakiwa na wananchi na kuongozana nao hadi kwenye ofisi za chama hicho, ngazi ya wilaya na baadaye kwenda kwenye ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga ambapo alitia saini kitabu cha wageni.
Kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara wananchi walimtaka Prof. Lipumba kwenda kushuhudia shehena ya mahindi yao kwenye ghala la mjini humo ambapo walidai kwamba yamekosa soko la kuuzia.
Wananchi hao walimweleza Mgombea huyo kuwa bei ya mahindi mkoani humo imeshuka sana. Walidai serikali haijachukua hatua zozote kuwatafutia soko na badala yake imepiga marufuku kuuza mahindi hayo nje ya mkoa.
Wananchi hao walimweleza Prof. Lipumba kuwa wafanyabiashara wanazuiwa kwenda kununua mahindi hayo ambayo yanatishiwa na hatari ya kuoza.
Baada ya kusikia kilio chao, Prof. Lipumba alisema matatizo wanayoyapata wananchi wa mkoa wa Rukwa yalisababishwa na sera mbovu za serikali ya chama tawala CCM.
Alisema anasikitishwa na kitendo cha serikali kuagiza mahindi kutoka nje ya nchi wakati mahindi hayo hayana soko mkoani Rukwa.
Prof. Lipumba alisema iwapo wananchi watachagua serikali ya CUF atahakikisha mkoa huo unakuwa ni wa hifadhi ya chakula na bei ya kuuzia mazao ya wakulima itawiana na bei ya soko la dunia ambapo mkulima atakuwa na haki ya kuuza mazao yake hata nje ya nchi.
Alisema, mkoa huo una ardhi nzuri hivyo wakulima wana uwezo wa kuzalisha mazao mengi na kuwa washindani wazuri katika masoko ya nje ya nchi.
Aidha, Prof. Lipumba aliwaambia wananchi kwamba sekta ya kilimo itaboreshwa ili kuhakikisha inatoa malighafi viwandani, serikali inapata fedha za kigeni, wananchi wanapata ajira itakayomwezesha kila mtu kupata kipato cha kukidhi mahitaji yake.
Akizungumzia sekta ya elimu, Prof. Lipumba alisema, watoto wenye umri wa kwenda shule milioni tatu hawapati elimu ya msingi kwa kisingizio cha kukosa ada.
Alisema, CUF ikiingia madarakani itakuwa ni marufuku kumfukuza mtoto shule kwa kukosa ada kwani elimu ni haki ya kila mtoto wa Tanzania ambapo wazazi ambao watakuwa hawana uwezo wa kusomesha watoto wao elimu bora ya msingi watalipiwa na serikali.
Prof. Lipumba alisema kuwa nusu ya matumizi ya serikali yake itapelekwa kwenye sekta ya elimu.
Aliongeza kuwa elimu nchini Tanzania imeshuka kulinganisha na nchi jirani ambapo nchini Kenya kati ya watoto 100, 26 wanapata elimu ya sekondari.
Amesema Uganda watoto 12 kati ya 100 wanaojiunga na kidato cha kwanza ambapo nchini kati ya watoto 100, ni watoto 6 tu wanajiunga na kidato cha kwanza.
Akizungumzia serikali inavyofuja rasilimali amesema serikali imekodisha uwanja wa ndege wa kimataifa wa KIA kwa hasara kubwa ambapo inalipwa shilingi 800,000 kwa mwaka, fedha ambayo alidai ni ndogo sana kuliko mtu anayepangisha ubao wa biashara Kariakoo ambapo hulipa shilingi milioni tatu kwa mwaka.
Kuhusu kodi inayotozwa sehemu mbalimbali nchini, Prof. Lipumba alisema, serikali ya CUF itakapoingia madarakani itaondoa msamaha wa kodi kwa makampuni makubwa ili kurahisisha kodi kwa wafanyabiashara ndogondogo.
Alisema kitendo cha serikali kuifutia kodi kampuni kubwa kama ya TCC deni la milioni 500 na kuendelea kuwabana wafanyabiashara wadogo wadogo ni unyanyasaji.
Prof. Lipumba aliondoka Jumamosi kwenda wilaya
ya Mpanda kuendelea na kampeni zake.
WANANCHI wa wilaya ya Rufiji mkoani Pwani wamesema, CCM haina lakuwaambia baada ya kushindwa kutekeleza waliyoahidi mwaka 1995.
Wakiongea na mwandishi wa habari hizi, hivi karibuni huko Rufiji, wananchi hao walidai kuwa makosa waliyofanya mwaka 1995 hawatayarudia tena, na kuahidi kuwaumbua wanaotoa ahadi za uongo.
Bwana Issa Mbonde mkazi wa kijiji cha Mbwela alisema kuwa, katika uchaguzi wa mwaka 1995 mawazo yao bado yalikuwa yamefungwa na walikuwa hawajaelewa madhumuni ya mfumo wa vyama vingi, na kuendelea kuegemea kwenye chama hicho cha CCM.
"Mwaka 1995 tulikuwa bado ni wachanga hatujaelewa vizuri faida ya vyama vingi, lakini leo tumeshafunguliwa macho hivyo hatutafanya tena makosa", alisema Bwana Mbonde.
Alisema kuwa wakati huo walifungwa akili zao na viongozi wa Chama tawala (CCM) kwa kuwaeleza kuwa iwapo wapinzani watapewa nchi kuna hatari ya kutokea vita, na wao wasijue wapi wakimbilie.
Bwana Saidi Omar Mkobokwaa mkazi wa Muhoro alisema kuwa, mwaka 1995 waliamua kukipa kura Chama cha Mapinduzi wakitarajia kuwa kitaendeleza yale ambayo tayari yalishaanzwa na Rais mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi.
Aidha, alisema kuwa walifanya vile wakijua kwa kuwa Rais Mkapa ametoka mikoa hiyo ya kusini, angesimamia vyema ujenzi wa barabara hiyo ili kuwapunguzia wakazi wa mikoa hiyo matatizo ya usafiri.
"Sisi tulitarajia kuwa huyu ndiye atakaye kuwa mwokozi wetu, kumbe badala yake anadai kulipa madeni, alikopa nani?" alihoji kwa mshangao.
Katika kampeni zake za mwaka 1995, Rais Benjamin Mkapa aliwataka wananchi wa mikoa hiyo kuacha kudanganywa na wapinzani kwa kisingizio cha kujengwa barabara kwani chama chake (CCM) kimeshakusanya pesa kwa ajili ya ujenzi wake, kinachosubiriwa ni kupita kwa uchaguzi ili kazi hiyo ianze mara moja.
Akiwahutubia wananchi hao wa vijiji vya Mbwela na Muhoro hivi karibuni, Prof. Lipumba aliwataka wakazi hao waikumbuke ahadi ya Rais Mkapa aliyokuwa ameitoa mwaka 1995 kama ameshaanza kuitekeleza.
"Je ile ahadi ya Rais Mkapa aliyosema atajenga barabara hii Kibiti Lindi ameshafanya hivyo?" alihoji Lipumba kwa masikitiko.
Prof. Lipumba alikuwa anarudia kauli yake kwa kuwaeleza wakazi kuwa umaskini waliokuwa nao siyo laana inayotokana na Mwenyezi Mungu bali ni sera mbovu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ndiyo iliyowafikisha hapo walipo.
Alisema kuwa kabla na baada ya nchi hii kupata uhuru toka kwa wakoloni, Rufiji ilikuwa inang'ara kwa wakazi kuwa na maisha mazuri.
Prof. Lipumba hivi karibuni alikuwa na ziara ya
kutembelea wilaya ya Rufiji, ikiwa ni pamoja na kampeni za kinyang'anyiro
cha Urais unaoendelea hivi sasa, ambapo uchaguzi wake unatazamiwa kufanyika
Oktoba 29, mwaka huu.
WATANZANIA wametakiwa kumchagua Rais mwenye uwezo wa kukabiliana na tatizo la uchumi bila kujali Rais huyo atatoka kwenye chama kipi.
Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Baraza la Vijana wa Chama cha UMD, Bwana Khamis Mattaka wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi mapema wiki hii katika mahojiano maalum yaliyofanyika nyumbani kwake Magomeni jijini Dar es Salaam.
Sheikh Mattaka alisema wananchi wanapaswa kupiga kura kwa mgombea Urais mwenye sifa ya kupambana na tatizo la uchumi badala ya kurubuniwa kwa siasa zisizotekelezeka.
"Rais anayefaa kwa sasa hapa nchini ni yule mwenye taaluma ya uchumi atakayeweza kulikwamua taifa letu kutoka katika matizo ya uchumi na si mwingine", alisema mjumbe huyo wa UMD .
"UMD kwa kauli moja tumeamua kumuunga mkono Prof. Lipumba kwa kumpigia kura za Urais na vile vile kukiunga mkono chama hicho pale kilipo na nguvu kubwa za wagombea wake kwenye nafasi ya Ubunge", alisema Sheikh Mattaka.
Hata hivyo alifafanua kuwa si kama UMD inakiunga mkono chama cha CUF kama ilivyo muungano wao na CHADEMA bali ni kutokana na kuona hakuna mgombea kutoka vyama vya upinzani ambaye anafaa kuliko Lipumba.
"Kati ya wagombea wote wa Urais, kutoka kambi ya upinzani Lipumba anakubalika kutokana na kuwa ni mchumi mwenye uoni juu ya namna ya kuinusuru nchi na umaskini.
Aliongeza kuwa maamuzi ya chama chao kukiunga kujiunga na ushirikiano wa pamoja kati ya CUF na CHADEMA ulifikiwa hivi karibuni baada ya kuona kuwa hayuko mgombea mwenye sifa za kiwango chake.
Wagombea wengine wanaowania Urais ukiwaondoa Rais Mkapa (CCM) na Prof. Lipumba (CUF na CHADEMA) ni Augustine Mrema (TLP) na John Cheyo (UDP).
Uchaguzi wa Rais na Wabunge pamoja na madiwani
nchini kote utafanyika Oktoba 29 mwaka huu na siku ya mwisho ya wananchi
kujiandikisha ilimalizika Jumanne wiki iliyopita.
--
![]()
|
|