JINA : Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti wa Taifa wa
Civic United Front (CUF - Chama Cha Wananchi)
P.O. Box 10979
Dar es Salaam, Tanzania.
TAREHE YA KUZALIWA : June 06, 1952
KIJIJI : Ilolangulu
WILAYA : Tabora
MKOA : Tabora
NDOA : Nimeoa
Waheshimiwa Wananchi,
HII ni mara ya pili kuhiari kusimama kuwa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vyama vya CUF na CHADEMA kwa pamoja vimenikabidhi jukumu hilo, kwa imani kwamba nina nia, sababu, na uwezo wa kutoa ushawishi kwa watanzania kuchagua serikali itakayorejesha haki, kuondoa umasikini, na kuharakisha maendeleo yao. Pamoja na kwamba mzigo mzito hupewa Mnyamwezi, hii ni heshima kubwa inayoashiria imani ya wanachama wa vyama hivi na mapenzi yao makubwa kwangu. Kwa kweli sina budi kuwashukuru sana kwa heshima hiyo.
Mwaka 1995 nilikubali kugombea Urais kupitia tiketi ya CUF katika saa za majeruhi kwa sababu mbili kubwa.
Mosi, mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ulikuwa ndio unaanza kufanya kazi katika nchi yetu. Baada ya miaka karibu 35 ya uhuru wa Tanzania maendeleo yetu yalikuwa madogo. Sera za kuondoa ukiritimba wa dola katika uchumi zilizokuwa zikitekelezwa na Rais Mwinyi hazikuungwa mkono kikamilifu na Chama chake.
Baada ya kufanya kazi kama Mshauri wa Uchumi wa Rais Mwinyi, na kushuhudia vizingiti alivyowekewa katika utekelezaji wa sera za kurekebisha uchumi, niliamini kuwa CCM haina uwezo wa kufanya mageuzi ya kimsingi yatakayojenga uchumi imara wenye manufaa kwa wote.
Nilikubali kugombea Urais kwa tiketi ya CUF ili niitumie nafasi hiyo kuwazindua wananchi waelewe kuwa wakiichagua CCM, hali zao za maisha zitaporomoka.
Kwa nini CUF? Nilivutiwa na sera za msingi za Chama cha CUF za "HAKI SAWA KWA WANANCHI WOTE" na itikadi ya UTAJIRISHO yenye madhumuni ya kujenga uchumi imara utakaoleta NEEMA KWA WOTE.
Waheshimiwa wananchi, Je, ni Watanzania wangapi ambao kwa dhati kabisa wanaweza kusema imekuwa ni neema kwao kumchagua Mhe. Mkapa kuwa Rais? Je, hali ya maisha ya wananchi wa kawaida imeboreka au imeporomoka?
Sababu ya pili ilikuwa kujenga umoja wa kitaifa kwa kukiimarisha chama cha CUF Tanzania Bara. Nilikuwa na uhakika kuwa CUF itashinda Zanzibar. Vile vile niliamini kuwa Chama chetu kisingeweza kushinda Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Niliingia katika kugombea Urais kwa nia ya kukiimarisha Chama chetu Bara ili kulinda Umoja wa Kitaifa na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kama chama chetu kingekuwa imara Zanzibar peke yake na kuwa kibovu Tanzania Bara, umoja wa kitaifa ungeathirika. Chama cha CUF sasa kimeimarika sana Tanzania Bara.
Naamini Chama chetu kilishinda uchaguzi mdogo wa Temeke na Ubungo na CCM ikatupokonya kwa mbinu za wizi wa kura. Hivi sasa CUF ni ngangari kweli kweli Bara na Zanzibar.
Waheshimiwa wananchi, kwa mara ya pili katika uhai wangu nimehiari kujitwika mzigo mzito wa kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano.
Sababu kubwa za kuhiari kubeba jukumu hili ni tatu. Mosi, Chama chetu kimeimarika. Sera zake za msingi : Haki sawa kwa wote na ujenzi wa uchumi imara wenye neema kwa wote zinakubaliwa na Watanzania wote. Changamoto wanayoitoa wananchi ni kutafsiri misingi hii kwa vitendo ili kujenga nchi inayoheshimu haki za binadamu, inayoendeshwa kisheria na inayoweka mazingira ya kuboresha hali ya maisha ya wananchi wote mwaka hadi mwaka.
Sababu ya pili ni kwamba baada ya kutawala kwa muda wa miaka 40, CCM imechoka, inanuka rushwa na haina uwezo wa kusimamia maendeleo ya Tanzania.
Uongozi wa CCM wa sasa hauna huruma na hauyajali matatizo yanayomkabili mtu wa kawaida. CCM haina dira. Viongozi wake wanang'ang'ania madaraka kwa manufaa ya watu wachache. Hawana mtazamo wa kujenga demokrasia ya kweli au kutetea maslahi ya wananchi wa kawaida. Viongozi wa CCM hawana haya. Wako tayari kutumia dola na propaganda yeyote ile ili wabaki madarakani. Mbinu hizi zinahatarisha umoja wa kitaifa.
Waheshimiwa wananchi, sababu yangu ya tatu ni ya binafsi. Toka nikiwa kijana mdogo katika shule ya sekondari ya Tabora nilipendelea sana kusoma uchumi na namna nchi zinavyoendelea kiuchumi. Nilipomaliza kidato cha nne nilikuwa katika mchepuo (sub stream) wa sayansi. Masomo niliyofanya vizuri sana yalikuwa Hisabati, Fizikia na Kemia. Kwa kupenda kuelewa maendeleo ya uchumi niliamua kuomba kuchukua masomo ya Hesabu, Uchumi na Jiografia katika kidato cha tano (5). Kwa muda wa miaka thelathini nimekuwa najifunza na kutafiti sababu zinazofanya nchi ziendelee kiuchumi. Shahada zangu zote nne, mbili za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na mbili za Chuo kikuu cha Stanford Marekani ni za uchumi. Miaka 40 baada ya uhuru Tanzania ni miongoni mwa nchi maskini sana duniani. Nahitaji kutumia ujuzi na uzoefu wangu wa maendeleo ya uchumi kushirikiana na Watanzania wenzangu kujenga uchumi imara wenye neema kwa wananchi wote.
Waheshimiwa wananchi, ni vyema tuuelewe vizuri umaskini wa Tanzania. Katika kila Watanzania mia moja, hamsini ni maskini wa kutupwa. Wastani wa pato la Mtanzania ni chini ya nusu ya wastani wa pato la watu wa Bara la Afrika.
Waheshimiwa wananchi, maendeleo hayawezi kupatikana kwenye taifa la wagonjwa. Kwanza kabisa tija ya mtu anayesumbuliwa na maradhi ni ndogo. Pili, fedha nyingi ambazo zingeweza kuelekezwa kwenye maeneo mengine ya huduma za jamii na huduma za kiuchumi itabidi zitumike kugharamia tiba. Katika Tanzania tatizo la afya za wananchi wetu ni kubwa. Huduma za afya ziko katika hali mbaya. Hospitali, vituo vya afya, na zahanati ni chache na zinakabiliwa na matatizo mengi.
Msongamano mkubwa wa wagonjwa, uhaba wa madaktari na wauguzi, uhaba wa vitanda, uhaba wa vifaa vya kazi, uchakavu wa majengo, na zaidi ya yote uhaba mkubwa wa madawa ni baadhi tu ya matatizo haya. Wafanyakazi katika sekta ya afya wanafanya kazi katika mazingira ya hatari yanayoweza kuwaletea maambukizi. Mishahara ni midogo ambayo hailingani kabisa na ugumu wa kazi. Wakilalamika wanaitwa 'wabinafsi' wasiojali 'wito' wa kazi yao na kukumbushwa viapo walivyoapa. Matokeo yake madaktari na wauguzi wamekuwa 'ombaomba' na wagonjwa wasio na chochote cha kutoa wamejikuta wakitelekezwa. Nchi jirani zimekuwa ndiyo kimbilio kubwa la madaktari na wauguzi wetu. Utafiti unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watoto wanaokufa chini ya umri wa miaka mitano hufia majumbani bila kufikiswa hospitali au zahanati alau kwa mara moja. Katika kila watoto 100 wenye umri usiozidi miaka mitano, 44 wana utapiamlo, hawana lishe bora. Watoto wanaokosa lishe bora hawajengi kinga ya mwili na ubongo wao haukuwi vizuri. Wastani wa maisha ya Mtanzania umeteremka toka miaka 52 mwaka 1990 mpaka kufikia miaka 48 mwaka 1997.
Elimu yetu inaendelea kuporomoka. Hivi sasa inakadiriwa kuna watoto 3,000,000 wenye umri wa kuwa shule za msingi ambao hawasomi. Walioko shuleni hawana elimu bora. Mwaka 1998, katika ya kila wanafunzi 100 waliofanya mtihani wa darasa la saba, 70 hawakupata alama za kufaulu. Tanzania ni nchi ya nyuma kuzidi zote ulimwenguni kwa maendeleo ya elimu ya Sekondari. Katika kila vijana mia moja wenye umri wa kuwa shule za sekondari ni sita tu ndio wanasoma sekondari, ukilinganisha na wastani wa 27 katika nchi za Kiafrika kusini mwa jangwa la Sahara.
Waheshimiwa Wananchi, Watanzania ni fukara, lakini Tanzania sio maskini wa mali ya asili. Tuna ardhi ya kutosha, mito mingi na maziwa makubwa. Jiografia ya Tanzania inafanya nchi yetu iwe na majimbo yenye hali ya hewa tofauti. Mazao mbali mbali ya chakula na biashara yanastawi katika ardhi ya Tanzania. Mahindi, mtama, mpunga, ngano, jamii ya kunde, ndizi, mihogo, viazi, karanga, matunda na mbogamboga, hata uyoga vinastawi vizuri katika maeneo mbali mbali. Mazao ya biashara kama kahawa, pamba, chai, katani, korosho, tumbaku, alizeti, ufuta, pareto, minazi, chikichi, na hata maua yanastawi vizuri nchini mwetu. Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao ya chakula na biashara lakini miaka 40 baada ya uhuru Tanzania haijitoshelezi kwa chakula. Uzalishaji wa mazao ya kilimo tunayouza nchi za nje ulipungua kwa kasi kubwa miaka ya 1972 - 85. Ongezeko la mazao hayo katika miaka ya 1986 - 96 haukuwa wa kutosha kuweza kufidia kuanguka kwa uzalishaji miaka ya nyuma. Kilimo cha Tanzania kinategemea jembe la mkono na hakitumii sayansi na teknolojia ya kisasa.
Hakuna kabisa ubunifu wa kuangalia ni mazao gani mapya ya kibiashara yanaweza yakakuzwa. Mathalani, michikichi ni zao ambalo lingeweza likakuzwa kwa mafanikio makubwa katika ukanda wote wa pwani na mkoa wa Kigoma. Mawese yatokanayo na chikichi ndio malighafi kubwa ya takriban mafuta yote ya kula yanayouzwa madukani. Hali kadhalika mawese ni malighafi kubwa kabisa katika utengenezaji wa sabuni za aina zote. Viwanda vya mafuta ya kula na sabuni nchini na katika nchi jirani vinategemea malighafi ya mawese kutoka Malaysia na Indonesia. Zao kama muarobaini linastawi katika ukanda wote wa pwani na katika baadhi ya maeneo mengine ya nchi yetu. Mbegu za muarobaini ni zao kubwa la kibiashara kwani ni malighafi muhimu ya kutengenezea baadhi ya madawa ya kufukuzia baadhi ya wadudu waharibifu mashambani. Kwa kifupi ni kwamba uwezekano wa Tanzania kukuza kilimo chake ni mkubwa sana.
Kwa bahati mbaya sana sera za kilimo za serikali ya CCM tangu uhuru zimekuwa ni za kauli za kisiasa kuliko kuzingatia utafiti, kutoa motisha, ushauri na utaalamu kwa wakulima, na kuwepo kwa mikopo ya zana za kilimo na pembejeo. Wote tutakumbuka matangazo ya 'kilimo cha kufa na kupona' kwenye miaka ya sabini. Wananchi wakahimizwa 'kila mtu alime na alime popote'. Matokeo yake mahindi yakapandwa mpaka katikati ya miji na mapori yanayohifadhi vyanzo vya maji yakafyekwa ili watu wapande viazi! Haikusaidia kitu, zaidi ya uharibifu wa mazingira. Vyanzo vingi vya maji vilikauka na mazalio ya mbu mijini yakaongezeka. Sera zisizotabirika ikiwa ni pamoja na kuvunja vyama vya ushirika vya wakulima wenyewe, operesheni vijiji, operesheni maduka, na mashamba ya mfumaki zimeacha madonda sugu kwa wakulima na sekta ya kilimo kwa ujumla. Nchi yetu haina huduma bora za kilimo cha kisasa. Matumizi ya utafiti na mafunzo kwa wakulima kuongeza tija yametoweka. Barabara na mawasiliano vijijini ni mabaya sana.
Sote tutakumbuka jinsi serikali ya CCM ya awamu ya tatu ilivyoyaanza madaraka kwa pupa. Waziri mkuu, alitoa tishio kwa wakuu wa wilaya kuwa 'Mkuu wa wilaya yoyote ambaye wilaya yake itakumbwa na uhaba wa chakula atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe!' Lakini, Serikali haikuweka mazingira ya kuendeleza kilimo. Zana za kilimo na pembejeo haziwafikii wakulima kabisa na zinapowafikia siyo kwa wakati. Katika miaka mitano ya utawala wa Rais Mkapa, matumizi ya mbolea yamepungua mwaka hadi mwaka. Sababu kubwa ni kupanda kwa bei yake na kutoweka mikopo kwa wakulima. Hata mikopo ya kununulia mazao imekauka kabisa na kusababisha kuanguka kwa bei wanayolipwa wakulima. Tanzania haina dira na sera za kuendeleza kilimo. Miaka arobaini baada ya uhuru wastani wa uzalishaji hapa nchini kwa eka moja ni mdogo kuliko nchi nyingine zote za Kiafrika.
Bahari ya Hindi, visiwa vya Zanzibar na Mafia,
delta ya mto Rufiji, mbuga za wanyama za Serengeti, Ngorongoro, Lake Manyara,
na Selous, Milima Kilimanjaro na Meru na ukarimu wa wananchi wetu na tamaduni
zao, unaifanya Tanzania kuwa nchi ya pekee kwa mapumziko murua kwa wageni
watokao nchi za Ulaya, Marekani na Asia. Gazeti la Financial Times la Uingereza
limeelezea kuwa Tanzania "offers one of the world's most complete holiday
destination." (Ni moja ya nchi inayotoa mapumziko murua yaliyokamilika.).
Hata hivyo hatujatumia urithi wetu wa asili kuinua hali ya maisha ya Watanzania.
--
![]()
|
|