Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Tabora, Bwana Ally Kondela amesema, tukio hilo lilitokea Ijumaa ya wiki iliyopita.
"libidi swala ya Ijumaa ya hapa Msikiti wa Gongoni icheleweshwe kidogo ili kuwapa muda wale walio swali nje ya Msikiti huu wapate kufika na kupata maelezo juu ya tukio lilompata", alieleza Bwana Ally.
Jumla ya Misikiti minne ya Ijumaa mjini hapo, waumini wake walikusanyika katika Msikti wa Gongoni.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Sheikh Ilunga aliwaeleza waumini waliofurika Msikitini hapo jinsi tukio zima lilivyotokea, kuwa watu waliomvamia walidhamiria kumuua kwa madai kuwa amezidi mdomo.
"Nimezidisha mdomo wanadai kwa maana nazungumzia sana Uislamu na haswa kuwataka Waislamu kusimama kidete kudai haki zao", ilieleza taarifa hiyo iliyomnukuu Sheikh Ilunga.
Aidha, mpashaji habari huyo ameeleza kuwa waumini wengi walibubujikwa na machozi Msikitini hapo kutokana na mawaidha ya Sheikh Ilunga, na baada ya kumuona jinsi alivyojeruhiwa.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa Sheikh Ilunga ameapa kwa waumini hao kuwa ataendela kutetea Uislamu na Waislamu kwa ujumla. Pia alitoa shukrani kwa Waislamu hao wa Tabora walivyomfariji.
Sheikh Ilunga ni mzaliwa wa mjini Tabora hivyo alifika hapo kama nyumbani na kupata fursa ya kuongea na Waislamu.
Sheikh Ilunga alivamiwa hivi karibuni usiku nyumbani
kwake na watu wanaodaiwa ni majambazi na kukatwa mapanga hali iliyopelekea
alazwe katika hospitali ya Bugando Mwanza. Aliwekwa chini ya ulinzi wa
polisi akiwa hospitalini.
CHAMA cha Wananchi (CUF) kata ya Makange, wilayani Kondoa kimeitaka serikali kurejesha fedha za wananchi walizochangishwa kwa ajili ya kugharimia uzinduzi wa kampeni za CCM wilayani humo.
Kwa mujibu wa barua yenye kumb. Na. CUF/KM/026/08/2000 na kusainiwa na Katibu wa CUF kata ya Makange, Bwana Hamadi Nyange, kwenda kwa mkuu wa wilaya hiyo, imesema kwamba serikali imewachangisha wananchi ili kugharimia mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM huku ikifahamu kuwa CCM ndio iliyopaswa kugharimia shughuli hiyo.
Kila kijiji kililazimishwa kuchangia shilingi elfu ishirini na viongozi wa vijiji husika walisimamia uchangishaji huo, kata ya Makange ina jumla ya vijiji vitano hivyo kiasi cha shilingi laki moja zilikusanywa.
Chama cha Mapinduzi kilifanya uzinduzi wa kampeni zake kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wilayani Kondoa katika kata ya Makange jimbo la Kondoa Kaskazini siku ya Agosti 22, mwaka huu na kuhutubiwa na mgombea mwenza wa kiti cha Urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Omar Ali Juma.
Sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa Agosti 32, 2000 inasema kuwa CUF inapinga kitendo hicho cha kuwachangisha wananchi kwa ajili ya kampeni za CCM, huku ikifahamu wazi kuwa miongoni mwa wananchi hao wapo ambao sio wana CCM.
Barua hiyo ambayo nakala yake imepelekwa kwa mgombea Ubunge kwa tiketi ya CUF jimboni humo Bwana Othman Omari Dunga, imeeleza, "kwa barua hii tunaitaka serikali kuzirejesha fedha za wananchi hao haraka iwezekanavyo".
Nae mgombea huyo amewahakikisha wananchi wa jimbo hilo kuwa sera za CUF zinatekelezeka tofauti na sera za CCM ambazo hata Mwenyekiti wake alikiri wazi kuwa hazitekelezeki.
Bwana Dunga amesema, kutotekelezeka kwa sera za CCM kumedhihirishwa jimboni humo kwani pamoja na mbunge wa CCM anayemaliza muda wake Bwana Khalidi Suru kuahidi mambo mengi mwaka 1995 hajatekeleza hata moja.
Bwana Dunga ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika moja lisilo la kiserikali linalojishughulisha na huduma za kijamii, amesema katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika Kondoa mjini kuwa endapo wananchi wa jimbo hilo watamchagua atahakikisha kero zote zinazowakabili wananchi jimboni humo zinatoweka.
Bwana Dunga (31) amewaeleza wananchi waliofurika
kumsikiliza kuwa ubovu wa barabara, ukosefu wa huduma nzuri za afya na
elimu duni ni miongoni mwa mambo ambayo atahakikisha yanaondoka mara atakapochaguliwa
kuwa mbunge wa jimbo hilo.
--
![]()
|
|