Udogma wa Evolution ulivyopigwa kumbo

MWALIMU hasa ni Mwenyezi Mungu, maana Yeye ndiye aliyempa kila mmoja wetu milango ya fahamu na akili inayoipa uwezo wa kufanya kazi katika kiwango cha juu zaidi kuliko ile ya wanyama. Utendaji kazi wa milango ya fahamu ya mwanadamu ni maradufu kuliko ya viumbe wengine.

Ni kweli kwamba wapo baadhi ya wanyama wanaoonekana kukaribiana na binadamu. Viumbe kama vile masokwe na wengineo. Mfano huo umefanywa kuwa kichaka cha maficho ya wale wakaidi wanaofumbia macho ukweli wa kuwepo Mungu Muumba. Wao hudai kuwa kisayansi mwandamu wa sasa ameibuka kutoka mchujiko wa jamii ya manyani.

Madhanifu hao wanatumia sayansi kuficha ububusa (dogma) wa imani yao kwa kisingizio cha utaalam. Wamekuwa wakidai kuwa jamii ya manyani wa Australopithecines, homohabilis, homoeretus ndiyo migongo na mitulinga alimochujikia binadamu wa hivi leo anayeitwa 'homo sapiens''.

Moja ya sifa ambayo ni katika maumbile ya wanadamu ni 'ngurumbili' (bipedalism). Kwa maneno mengine hakuna mnyama aliyetembea kwa miguu miwili isipokuwa binadamu. Upo usemi usemao kuwa 'binadamu hana kibiongo'. Maana yake ni kwamba, pamoja na kutembea kwa miguu miwili, binadamu hutembea wima. Hii ni sifa ambayo jamii ya manyani hawana na hawatakuwa nayo!

Kwa hakika tumemuumba mwanadamu katika umbo lililo bora kabisa. (95:4. Basi uelekeze uso wako katika dini iliyo sawa sawa. Ndilo umbile Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu. Hakuna mabadiliko katika maumbile ya viumbe vya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo dini iliyo ya haki lakini watu wengi hawajui. (30:30)

Haki haifichiki muda wote. Kupitia sayansi, Mwenyezi Mungu anazidi kukichoma moto kichaka cha 'Madogma" . Hakuna mabadiliko ya manyani kuwa masokwe wala masokwe kuwa binadamu! Yanayojulikana na kutopingika ulimwenguni kote ni mabadiliko ya makuzi na kuchakaa kwa viumbe.

Mnakuwaje mnapingana na ukweli wa kuwepo Mwenyezi Mungu? Na hali ya kuwa Yeye amekuumbeni hatua kwa hatua. (71:13-14). Na kwamba Yeye ndiye Afishaye na kuhuisha. Na kwamba Yeye ndiye anayeumba dume na jike. Katika mbegu za uzazi pale zinapomiminwa. (53:44-45)

Umethibiti ukweli wa kisayansi kuwa mafuvu na mifupa ya masokwe yanayohusishwa na mtu wa kwanza yaliyofukuliwa na familia ya Dr. Leakeys hayana mlingano na mtu wa sasa wala wa mwanzo.

Kwa mujibu wa utafiti wa Bwana Tim While, Holy Smith (1994), mtalaamu wa mabaki ya mafuvu na mifupa ya kale wa Kimarekani, ulionukuliwa katika kitabu Evolution Deceit: The scientific collapse of Darwinism and its ideological Background, imethibiti kuwa 'homohabilis' si "homo! (Mtu). Ni masokwe ya kawaida kama yale ya misitu ya Congo .

Na Kumbuka Mola wako alipowaambia malaika. Hakika mimi nitamwumba mtu kwa udongo mkavu, unaotoa sauti, wenye kutokana na matope meusi yaliyovunda. Basi nitakapomkamilisha na kumpulizia roho itokanayo na Mimi, hapo muoneshe heshima ya kumtii. (15:28-29).

Enyi watu! Kama mna mashaka juu ya ufufuo, basi kwa hakika tulikuumbeni kwa udongo. Kisha kwa tone la manii. (22:5). Hakika mfano wa kuumbwa kwa Yesu mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama kuumbwa mtu wa kwanza. Aliumbwa kwa udongo, kisha akaambiwa 'kuwa' akawa. (3:59).

Imeripotiwa katika kitabu Evolution deciet ukurasa wa 63, Mwaka 1994 jopo la wataalamu wa elimu ya maumbile (Anatomy) lilifanya utafiti ulioyapiga kumbo na kuyasukuma nje ya uwanja wa sayansi madai yanayomuhusisha mwanadamu na kizazi cha wanyama.

Dk Harun Yahya ameandika kuwa Bwana Fred Spoor, Bernard Wood na Frans Zonneveld walifanya mlinganisho wa uchambuzi baina ya 'Semi-cercular canals' ndani ya sikio la mtu na wale masokwe.

Utafiti huo ukabainisha kuwa Semi Circular Canals za binadamu anayetembea wima ni tofauti kabisa na masokwe. Kazi ya semi - secular canals ni kuweka insafu (balance).

Insafu ni ile hali ya kutoyumba kama mlevi. Muumbo wa semi Secular , 'homo habilis ni insafu (balance) ya kutembea kwa kutupa mikono na miguu yao. Hivyo mabaki ya mafuvu ya mifupa si ya daraja la 'homo'. (Mtu).

Na yametimia maneno ya Mola wako ya kweli na ya uhakika. Hakuna awezaye kuyabadilisha maneno yake. Na kama ukiwatii wengi katika hawa 'madogmatisti' watakupoteza na njia ya Mwenyezi Mungu. Hawafuati ila dhana tu, na hawana mashiko ila ni wenye kuzua tu. (6:115-116).

Matokeo ya uchambuzi wa viungo vya ndani vya sikio yanaonesha kuwa mlinganisho wa uchambuzi wa sehemu za ndani za sikio la mtu na zile za sikio la masokwe 'homo' habilis, yamefichua kuwa uzushi unaodaiwa kuwa viumbe hivyo vya kisokwe ndivyo mababu wa binadamu ni masokwe ya kawaida! Hakuna ubabu (ancestors) kati ya watu na jamii yoyote ya manyani.

Hakika tumemuumba mwanadamu katika umbo lililo bora kabisa . (95:4). Je! Hatukumpa macho mawili. Na ulimi na midomo miwili! Kwa hakika tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyochanganyika. Na tukamfanya ni mwenye kusikia, mwenye kuona. (90:8-9), (76:2). Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Amemuumba mtu akamfundisha kunena. (55:1-4).

Kuona kwa jicho la binadamu ni kupana sana. Kinyume na wanyama, binadamu huweza kutazama kitu kwa jicho la tafakari. Kwa jicho hilo hilo anamudu kujifunza kwa njia ya utafiti katika kuchungua mambo mbalimbali. Huweza kusoma katika uchunguzi na hatimaye kuthibitikiwa na ukweli wa maumbile baada ya uchambuzi wa kina. Katu uoni wa jicho la mnyama hauna ubavu wa kupiku uoni wa jicho la mwanadamu.

Na amekufundisha Mwenyezi Mungu chungu ya mambo usiyoyajua. Na fadhila za Mola wako zimekuwa nyingi kwako. Na hakika tumewakirimu wanadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini na tumewaruzuku vizuri vizuri. Na tumewatukuza kuliko wengi katika wale tuliowaumba kwa utukufu ulio mkubwa. (17:70).

Leo hii mwanadamu ameikunja dunia, usafiri na mawasiliano vimekuwa rahisi mno. Kuna simu za waya na zisizo za waya, kuna redio na televisheni, kuna Fax, na mtandao wa Internet. Si hivyo tu, binadamu huweza kuruka angani akiwa na shahena ya mizigo akisafiri mamilioni ya kilometa kwa muda mfupi.

Baharini ndio usiseme! Kwa teknolojia aliyofikia, mwanadanu ana uwezo wa kusafirisha kijiji cha watu na yaliyo muhimu kwa mahitajio yao. Aidha, mwanadamu anaweza kuzama katika vina vya bahari na kuyatafiti maisha ya huko. Hakuna anayeshuhudia maajabu yanayodhihirisha kuwepo kwa Muumba.

Mwaka 1983, mtaalamu wa Ufaransa, Captain Jecques Constean amegundua kuwa maji ya kawaida (fresh water) na yale ya chumvi hayachanganyiki! Hutengeneza mikondo ya bahari zenye ladha tofauti japo zinakutana. Kuna samaki wanaostaajabisha. Mfano samaki aina ya Salmon husafiri maili nyingi baharini ili wakatage mayai yao na kurudi tena walikotoka.

Na Mwenyezi Mungu ndiye anayezikutanisha bahari mbili, hii ni tamu inayoondosha kiu, na hii ni yenye chumvi. Na akaweka baina ya hizo kinga na kuzuizi kizuiacho (25:53). Anazikutanisha bahari mbili. Baina yake kuna kizuizi, hayachanganyiki. (55:19-20)

Sikio la binadamu ni sikio la kujifunza. Ni kweli kwamba wanyama kama paka, mbwa, panya na wengineo huweza kujifunza kupitia mlango huu wa fahamu. Lakini kama vile uoni wa jicho la binadamu ulivyo maradufu kuliko viumbe wengine. Kadhalika na usikivu wa sikio lake. Kiwango cha wanyama kujifunza hupitia sikio ni kidogo sana.

Hebu tazama namna mwanadamu anavyoweza kujifunza lugha, mtoto ataweza kusema, kusoma, kuandika na kuhesabu endapo atakuwa mwenye sikio lenye kusikia. Na kama mtoto atazaliwa kiziwi, basi itakuwa ni muhali kwake kujifunza lugha. Vinginevyo atajifunza mambo kupitia ishara zisizokuwa maneno ya kutamkika.

Midomo, meno, ulimi, taya na koo la binadamu vinakazi ya kusaga, kuonja, kugeuza, kuzuia na kumeza chakula. Hata hivyo, viungo hivi vimeumbwa kwa namna ya kutumika katika kufujinza na kuzungumza lugha.

Wanaisimu wanatuambia kuwa kwa kutumia midomo, meno, ulimi na koo, mwanadamu huyadhibiti mawimbi ya sauti yakatamkika maneno fasaha.

Aidha, kazi ya pua si kunusa na kupitisha hewa ndani na nje, ni pamoja na kurahisisha ufasaha wa utamkwaji wa maneno. Ukitaka kuthibitisha, ziba pua kisha utamke,"Nenda, "Ng'oa au "important", kwa ufasaha kama utaweza!

Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Amemuumbia mtu. Akamfundisha kunena (lugha). Amemuumba mtu kwa udongo wa mfinyanzi kama vyombo vya udongo. Basi ni zipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha. (55:1-16). Je! Hatukumjalia macho mawili. Na ulimi na midomo miwili.

Lugha ni ufunguo wa mlango wa elimu. Mtu anayeimudu lugha katika kusema, kusoma, kuandika na kuelewa maana yake inapozungumzwa, atakuwa anamsingi wa kujifunza chungu ya mambo yaliyomo ndani ya utamaduni wa lugha hiyo. Ni kupitia lugha, wanadamu huweza kuwasiliana, kushirikiana na kusaidiana kwa urahisi zaidi.

Maneno yanayotengeneza lugha, yanabeba maana ya vitu na mambo mbalimbali. Uwezo wa akili ya binadamu kutafakari, kuchambua na kujenga hoja hutegemea lugha. Mwanadamu anapofikiri ni kama anazungumza lugha kindanindani. Kwa maneno mengine mtu hutafakari juu ya kitu au jambo kwa kutumia maneno ya lugha iliyomo katika kurasa za ubongo wake.

Kisha husema baada ya kugundua undani wa kuwepo kwake. "Mola wetu! Hukuviumba hivi pasina lengo! Utukufu ni wako. Basi tuepushe na adhabu ya moto. Mola wetu! Hakika wale utakaowaingiza motoni itakuwa umewadhalilisha. Na madhalimu hawatapata msaidizi".

Lugha ni chombo cha kupanua akili na kumuwezesha kupata ujuzi. Mtu huweza kudhihirisha ufahamu wake juu ya jambo au kitu kwa kutaja, kueleza, kutafsiri kwa kusema au kuandika alichojifunza kupitia lugha.

Na Mwenyezi Mungu akamfundisha Adamu majina ya vitu vyote. Kisha akaviweka mbele ya malaika, akasema: "Niambieni majina ya hivi vitu ikiwa mnasema kweli".

Wakasema: Utukufu ni wako! Hatuna ilimu isipokuwa ile uliyotufundisha, bila shaka wewe ndiye mjuzi na ndiye mwenye hekima. Akasema: "Ewe Adamu! Waambie majina yake! Alipowaambia majina yake akasema: "Sikukuambieni ni kwamba Mimi ninajua airi za mbinguni na ardhini. (2:31-33).

Adamu (a.s.) alifundishwa majina ya vitu na baadaye akavitaja majina yake pale alipotakiwa kufanya hivyo. Linalojitokeza hapa ni kwamba binadamu hujifunza kupitia lugha. Lugha ndiyo iliyotoa maneno ya majina ya vitu, ndipo Adamu akavijua kwa undani wake. Hata pale Adamu alipoterezeshwa na Ibilisi, Mwenyezi Mungu akamfundisha maneno ya kutubia.

Basi Adamu akapokea maneno kutoka kwa Mola wake. (2:37). Wakasema: Mola wetu! Hakika tumedhulumu nafsi zetu. Na kama hutusamehe na kuturehemu bila shaka tutakuwa niongoni mwa wenye hasara. (7:23). Na Mola wake akapokea toba yake; Hakika Yeye ni mwingi wa kusamehe na mwingi wa kurehemu. (3:37).

Kwa ujumla, Mwenyezi Mungu ndiye aliyempa na kumfundisha mtu kupitia milango ya fahamu, macho, pua, ngozi, ulimi na midomo vinapewa uwezo wa kupokea masomo yaliyomo ulimwenguni na kuyawasilisha kwenye ubongo kwa ajili ya uchambuzi na uhifadhi wa taswira za masomo yote hupitia milango ya fahamu hadi kwenye ubongo. Mafaili ya taswira hizo huambatana na maneno ya lugha katika mfumo wa majina, vitenzi, viwakilishi, vivumishi, vilezi, viunganishi nakadhalika huleta, maana akili na kujenga dhana za mambo na vitu mbalimbali.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook